Jamal Malinzi, wakili wake (kushoto) na wakili wa mpinzani wake Peter Heller wakati rufaa yake ilikpokuwa inasikilizwa juzi |
ALIYEKUWA mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais Michael Wambura ametoa siku tatu kwa Shirikisho la Soka Tanzania kuhakikisha inamrejesha madarakani mgombea wa nafasi ya urais Jamali Malinzi.
Wambura alisema kuwa ifikapo Jumatatu kama TFF haijatoa jibu la kueleweka na kumrejesha
kwenye kinyang'anyiro Malinzi basi ataenda mahakamani kusaka haki ya msingi ya kikatiba ambayo
alidai TFF wameikiuka.
Akizungumza na waaandishi wa habari kwenye ukumbi wa idara ya Habari Maelezo leo, Wambura
alisema kuwa hajali kuenguliwa kwake kwani hata kamati ya uchaguzi chini ya Deogratius Lyato
ilishamuengua na kudai kuwa kamati ya rufaa iliyomuengua Malinzi ni batili na maamuzi yote
yaliyotolewa na kamati hiyo chini ya wakili Idd Mtiginjola ni batili.
"Kwa mujibu wa katiba mpya ambayo mimi naiita sio halali ibara ya 76 katiba hiyo imeanza
kutumika Desemba 15 mwaka jana na Kanuni za uchaguzi zimeanza kutumika Januari 7 mwaka
huu kanuni hizi na katiba yake ndio zilizotumika kuitisha uchaguzi huu, na mbaya zaidi Tenga
amesaini na akamwambia msajili alifanya mkutano mkuu Desemba 15 na kupitisha marekebisho
na yalianza kutumika siku hiyo hiyo wakati ukweli ni kuwa hakuna mkutano mkuu uliotishwa
badala yake mabadiliko yalifanywa kwa njia isiyo halali ya waraka.
"Cha kushangaza Kanuni za uchaguzi za TFF zilipitishwa na kusainiwa na Tenga na katibu wake
Angetile Osiah January 7 mwaka huu wakati Katiba ya TFF ilisajiliwa na kugongwa mhuri wa
msajili Januari 10 siku tatu baada ya kanuni ya kusainiwa, cha kujiuliza hizi kanuni zilitungwa kwa
mujibu wa katiba gani?"alisema kwa kuhoji na kuongeza:
"Baada ya kupitisha katiba na kuanza kutumika TFF ilipaswa kuunda Kamati mpya ya uchaguzi kwa mujibu wa katiba ya TFF ibara ya 49(4) ambayo inasema mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi anapaswa kuwa na taaluma ya Sheria sifa ambayo mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi Deogratius
Lyato hana......:
"Kwa kuwa hana sifa hiyo ushiriki wake kwa mujibu wa katiba ya TFF ni batili na mchakato wote
wa uchaguzi ni batili hivyo ufutwe na kuteua kamati mpya ili mchakato uanze upya.
"Namshauri Tenga kwa kuwa katiba sio sahahi afute mchakato mzima wa uchaguzi na uanze upya kwa kutumia katiba ya zamani, na pia atengue na kuvunja kamati ya rufaa maamuzi yatumike ya Lyato ingawa mimi hayanisaidii kwani hata kamati ya Lyato ilishaniengua kwa kufanya hivyo itajenga muktasari mzuri wa uchaguzi.
"Kwa mantiki hii Kanuni za uchaguzi ni batili na katiba ni batili kisheria, naishauri TFF kuondoa uwezekano wa kuingiza TFF kwenye mgogoro wa kisheria uamuzi ambao ni wa busara ni kuachana na katiba batili.
Aidha Wambura alisema kuwa kitendo cha kamati ya rufaa kumuengua Malinzi kuna mkono wa TFF kwa madai kuwa ilianza kumpiga zengwe toka mwaka 2008 alipojitosa kuwania nafasi ya urais sambamba na rais anayemaliza muda wake Leodegar Tenga pale walipomuengua kwa kigezo cha kukosa uzoefu wa miaka mitano sababu ambazo pia zimetolewa na Agape Fue aliyemkatia Malinzi pingamizi kwenye kinyang'anyiro hicho.
"Agape Fue ni wa kufikirika na mpango wa kumuondoa Malinzi ulianza mapema na ulifanywa na
kambi ya mgombea mmoja ambaye kwa kiasi kikubwa alishiriki kusigina katiba na kuunda kamati ya rufaa ya uchaguzi ambayo sehemu kubwa imejaa marafiki wa mgombea huyo.
"Mwenyekiti wa kamati ya rufaa Mtiginjola ninamfahamu aliwahi kuwa kwenye kamati moja za
DRFA wakati Nyamlani ni Katibu, baadae alihamishwa TFF kwenye kamati ya nidhamu na usuluhishi,hakuna ubishi anafahamiana viuzri na mgombea Nyamlani, kisheria Mtiginjola alipaswa kujiondoa wakati wa rufaa ya Malinzi kwa kuwa asingeweza kuwa na mikono misafi ya kutekeleza haki ya msingi 'Natural Justice' kwani sheria inataka si tu haki itendeke lakini ionekane imetendeka.
"Kulikuwa na mgongano wa kimaslahi kwenye uamuzi wa juu ya rufani ya Malinzi, Katiba ya TFF
(2006) ibara ya 36 (3) inatamka mjumbe wa kamati ya utendaji kutoa tamko kama ana maslahi na mjadala wowote na kujiondoa kwenye mjadala kama kushiriki kwake kutaleta mgongano wa kimaslahi.
"Hivi ni kweli Mtiginjola na wenzake hawakulijua hili au uwepo wao katika kamati hii ulikuwa wa kimkakati zaidi huku wakisimamiwa na TFF ili majina ya Malinzi na Wambura yaondolewe?
Kanuni za uchaguzi ibara 2 (1) inazungumzia demokrasia ya mgawanyo wa madarka katika uwazi bila kuacha kitu katika mchakato wa uchaguzi wa TFF je urafiki wa hila, ghilba ndio uwazi huo? alihoji.
Mapema wiki hii kamati ya uchaguzi ilitangaza kumuondoa kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi
Jamali Malinzi kwa madai ya kukosa uzoefu wa miaka mitano pamoja na uadilifu kwa madai ya
kupinga utekelezaji wa mabadiliko ya katiba ya TFF.
Hata hivyo tayari Malinzi alishatoa msimamo wake wa kutokubaliana na kuenguliwa kwake na kumtaka rais Tenga kuingilia kati sakata hilo kwa kumrejesha kwenye kinyang'anyiro huku wanachama wa klabu za Simba na Yanga nao wakichimba mkwara kwenda kusimamisha uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Februari 24 Mahakamani iwapo Malinzi hatorejeshwa kwenye mchakato.
No comments:
Post a Comment