Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha,Mrakibu Mwandamizi wa Polisi,Gilles Muroto akiongea na wananchi wa Mtaa wa Sanawari (hawapo pichani) uliopo kata ya Sekei halmashauri ya jiji la Arusha juu ya uanzishaji wa vikundi vya ulinzi shirikishi
Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha,Mrakibu Mwandamizi wa Polisi,Gilles Muroto (wa tatu kulia) akimtambulisha Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha,Mrakibu wa Polisi (SP),Mary Lugola pamoja na askari wengine wa kitengo hicho mkoani Arusha. (Picha na mahmoud ahmad).
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Gilles Muroto amewaambia wakazi wa Mtaa wa Sanawari waliopo Kata ya Sekei iliyopo halmashauri ya jiji la Arusha waunganishe nguvu zao pamoja ili waweze kuushinda uhalifu.
Hayo aliyasema jana katika mkutano kati jeshi la Polisi na wananchi hao uliofanyika katika uwanja wa wazi uliopo mtaani hapo ikiwa ni muendelezo wa mkakati wa jeshi hilo juu ya utoaji wa elimu ya polisi jamii kuanzia ngazi ya mtaa na vitongoji vya Mkoa huu wa Arusha.
Mkuu huyo wa Polisi wilaya alisema kitendo cha watu wachache kujitokeza kuhudhuria katika mkutano huo ambao ulikuwa unajadili mambo mbalimbali ya maendeleo ya mtaa pamoja na masuala ya ulinzi ni dalili tosha kwamba baadhi ya wakazi wa eneo hilo hawana umoja.
“Hii inashangaza yaani mkutano ambao umetangazwa karibu kila nyumba na una lengo la kujadili maendeleo ya mtaa ambao umehudhuriwa na viongozi wa mtaa pamoja na Diwani wa kata lakini watu wachache, hii ni hatari na hamtaweza kusonga mbele.” Alionya Mkuu huyo wa Polisi wilaya.
Alisema hali hiyo ya utengano ndio inayotoa mwanya kwa wahalifu kufanya uhalifu kwani mpaka hivi sasa mtaa huo hauna vikundi vya ulinzi shirikishi kwa kuwa wananchi hawahudhurii katika mikutano ili waweze kushirikiana na jeshi la Polisi kujadili suala hilo.
Mrakibu huyo Mwandamizi wa Polisi alisema kwamba, suala la ulinzi si la kiitikadi za kisiasa bali watu wa vyama vyote wanatakiwa washiriki kwani mhalifu anapovamia sehemu hamuulizi mwenye mali kama ni kiongozi, mwanachama au shabiki wa chama gani bali anaangalia kile anachokiihitaji.
Aliwataka wananchi wa Mtaa huo kuanza kuchukua hatua za kupambana na wahalifu kwa kuanzisha kikundi cha ulinzi shirikishi ambacho kitaendeshwa kwa michango ya kila mkazi ambaye atapaswa kufanya hivyo kwa ajili ya kuwalipa posho walinzi pamoja na ununuzi wa vifaa kama vile tochi, sare na kadhalika.
Aliongeza kwa kusema ili kikundi kikamilike inatakiwa wawe na silaha ya moto ambayo itawasaidia katika shughuli za doria badala ya kutumia marungu pekee. Alisema kikundi hicho kitakuwa kinafanya kazi hiyo kwa kushirikiana na jeshi la polisi ambapo pale wanapoona kuna matatizo watakuwa wanawasiliana na yeye au viongozi wengine wa jeshi hilo moja kwa moja ili waongezewe nguvu.
Mkutano huo uliohudhuriwa na Diwani wa Kata ya Sekei Mh. Chrispin Tarimo, Mwenyekiti wa mtaa huo Godfrey Mollel, Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi Mary Lugola, Polisi Tarafa ya Themi Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Zuhura na askari wengine toka kitengo hicho ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Mkuu huyo wa Polisi wilaya kwa wenyeviti wa mitaa ya halmashauri ya jiji Arusha ya kufanya mikutano na wananchi ili kuimarisha ulinzi ndani ya wilaya ya Arusha.
No comments:
Post a Comment