Wednesday, January 9, 2013

Wanachuo Kipawa sasa kulipa ada kwa M-Pesa


Mkuu wa chuo cha VETA kipawa, Jijini Dar es Salaam, Eng. Lucius Luteganya, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa ulipaji ada kwa wanafunzi wa chuo hicho kupitia huduma ya M – Pesa. Kufuatia ushirikiano kati ya chuo hicho na Vodacom Tanzania. Kushoto ni Mkuu wa ukuzaji biashara – M - PESA Jackson Kiswaga.
Meneja mawasiliano wa Vodacom Tanzania Rukia Mtingwa, akimuelezea jambo Mkuu wa Chuo cha Veta Kipawa, Eng. Lucius Lutenganya wakati wa uzinduzi wa ulipaji ada kupitia huduma ya M – pesa kwa wanafunzi wa chuo hicho. Katikati ni Mkuu wa Ukuzaji Biashara – M - PESA, Jackson Kiswaga.

Wanachuo wa Chuo cha VETA Kipawa Dar es Salaam kuanzia sasa wataanza kulipa ada kupitia huduma ya M-Pesa baada ya chuo hicho kufikia makubaliano na Kampuni ya Simu za mikononi ya Vodacom kuwezesha huduma hiyo.

Chuo hicho ni miongoni mwa Shule na Vyuo vingine kadhaa ambavyo vipo katika hatua za mwisho za mazungumzo na Vodacom ya kuviwezesha kutumia huduma ya M-pesa katika ulipaji wa karo ada nynegine katiika taasiis hizo za elimu nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo eneo la Kipawa kilipo chuo hicho Dar es Salaam, Mkuu wa Ukuzaji Biashara; M-Pesa Jackson Kiswaga amesema kuanza kwa huduma hiyo ni mwendelezo wa azima ya Vodacom ya kuyaleta maisha ya watanzania kiganjani kupitia teknolojia ya simu za mkononi.

Amesema katika mipango ya kuwezesha malipo ya karo kwa M-pesa Vodacom imeanza na VETA kipawa kinachotoa elimu zaidi ya masula ya teknolojia ingawa mipango ni kufikisha huduma hiyo kwa vyuo vyote vya VETA nchini pamoja na vyuo vingine na shule.

"Tunajivunia ushirikiano huu unaoleta mapinduzi mengine ya kiteknolojia na kimfumo wa jinsi tunavyoendesha biashara zetu na hata maisha yetu, na ni matarajio ya Vodacom kwmaba huduma hii itakuwa na mafanikio makubwa katika kukidhi mahitaji ya wanachuo.” anasema Kiswaga.

Aidha, Kiswaga anaeleza kuwa ushirikiano huo utatoa njia mbadala katika malipo ya ada, na kusisitiza kuwa huduma ya M-Pesa ni salama, haraka na ya uhakika, kwa kuwa imeleta mapinduzi katika huduma mbalimbali za kifedha tangu kuanzishwa kwake miaka minne iliyopita.

Kwa upande wake, Mkuu wa chuo hicho, Lucius Luteganya, amesema uongozi na jumuiya nzima ya chuo cha Veta Kipawa wameupokea mfumo wa huduma hiyo katika mtazamo chanya, kwa kuzingatia hali halisi ya muktadha wa teknolojia ya sasa na vipaumbele vyake.

"Ukweli wanafunzi walio wengi wanapopewa fedha za karo na wazazi wao hawazifikishi na hata wakizifikisha zinafika zikiwa pungufu, sasa kupitia huduma ya M-Pesa wazazi watapata fursa ya kulipa ada moja moja wakiwa nyumbani, na kupiga simu kuthibitisha badala ya kuwapatia wanafunzi mikononi." anasema Luteganya.

Amesema suala la wanafunzi kupanga foleni au kuchukua muda mrefu wakati wa ulipaji wa karo sasa limepatiwa ufumbuzi, kwani adha hiyo imekuwa ikizorotesha shughuli nyengine chuoni hapo hasa kwa idara zinazohusika na malipo, kuwapotezea muda mwingi wananfunzi na kujikuta wakichelewa vipindi darasani na hivyo kupunguza ufanisi wao kimasomo.

Aidha, Luteganya anasema pamoja na mambo mengine, vyuo vya Veta nchini ni wadau wakubwa wa masuala ya teknohama, hivyo wanaona fahari kuwa mfano wa kuigwa kwa wao kuwa sehemu ya teknolojia zenye manufaa zinazoibuliwa ndani ya jamii za kitaifa na kimataifa.

Huduma ya M-Pesa ya Vodacom Tanzania ina mawakala zaidi ya elfu 40,000 nchini kote, na ni pekee ambayo inaongoza kwa kuwa na wabia wengi w akibishara katika kila Nyanja na hivyo kutoa wigo mpana zaidi wa wananchi kunfaika nayo katika kulipia huduma mbalimbali pamoja na kuhifadhi, kutuma na kupokea fedha.

Kupitia M-pesa mteja wa Vodacom anaweza kulipia tiketi za ndege, huduma za maji, umeme na ving’amuzi, kulipia manunuzi ya bidhaa katika baadhi ya maduka makubwa – Super Markets, kulipia bima, kulipia michango katika baadhi ya mifuko ya hifadhi ya jamii na sasa karo katika chuo cha VETA kipawa.

No comments: