Wednesday, January 23, 2013

Wadau wa maendeleo waiwezesha WAMA kuwasaidia wanawake na watoto

Na Anna Nkinda - Paris

Ushirikiano wa pamoja baina ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) na wadau wa maendeleo nchini umeiwezesha taasisi hiyo kuwasaidia na kuwainua wanawake kiuchumi ambao wameweza kujishughulisha na kazi za ujasiriamali na hivyo kujikwamua na hali ngumu ya maisha.

Pia Taasisi hiyo imeweza kutoa ufadhili wa masomo kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi jambo ambalo limewafanya watoto hao wapate elimu sawa watoto wengine wenye wazazi na kuimarisha afya za mama wajawazito na watoto.

Hayo yamesemwa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati alipotembelea Taasisi inayoshughulika na masuala ya watoto (France Parrainages) kiliyopo mjini Paris ambacho kinafanya kazi na Kituo cha Ufaransa cha kuwaangalia watoto kwa kushirikiana na Taasisi ya Partage Tanzania inayohudumia watoto yatima katika mkoa wa Kagera.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAMA alisema kuwa Taasisi hiyo imeweza kujenga shule ya Sekondari ya WAMA – NAKAYAMA iliyopo Rufiji Mkoani Pwani ambayo ina wanafunzi 247 ambao ni watoto yatima na matarajio ya baadaye ni kuwa na wanafunzi 780.

“Katika mkoa wa Lindi tumejenga mabweni ya wanafunzi wa sekondari wa kike, tunagharamia masomo ya Sekondari kwa wanafunzi 250 na wanafunzi 16 wa elimu ya juu kutoka mikoa yote nchini”, alisema Mama Kikwete.

Aliendelea kusema kuwa Taasisi hiyo imeweza kuwasaidia wanawake kiuchumi na kuwafanya waweze kuongeza kipato cha familia zao, kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vikundi vidogo vidogo ambavyo vinaweza kutengeneza bidhaa za kusindika za vyakula na kuziuza.

Kwa upande wake Charline Flauge’re ambaye ni msimamizi wa Programu za Kituo cha Ufaransa cha kuwaangalia watoto upande wa Afrika alisema kuwa Taasisi ya Partage Tanzania ambayo inahudumiwa na kituo hicho inafanya kazi nchini katika mkoa wa Kagera ambayo ni moja ya nchi tatu muhimu kutokana na idadi ya watoto wanaowahudumia kufikia 10000.

Alisema kuwa watoto hao yatima wanaishi vijijini na familia zao zinajishughulisha na kazi za ukulima mdogo wa kahawa na migomba wao wanatoa ufadhili ambao unawasaidia waweze kuishi na familia zao na kupata upendo wa ndugu bila ya kuishi katika vituo vya kulelea watoto yatima.

Flauge’re alisema, “Tunashukuru kwa kuwahudumia watoto hawa ambao wameweza kukua wenyewe ndani ya familia zao za mama, kaka au dada, ufadhili huu umeweza kumsaidia mzazi aliyebaki hai, bibi na babu zao kuwaangalia na hivyo kukua katika afya njema na mazingira yao waliyozaliwa.

Alimalizia kwa kusema kuwa ufadhili huo hautoi fedha na vitu peke yake bali pia unajenga mahusiano baina ya watoto na wafadhili wao ambao wanaishi nchini Ufaransa kwani watoto wanawaandikia wafadhili barua na kuwasiliana nao na wakati mwingine wanakuja kuwasalimiana nchini Tanzania na hivyo kujifunza mila na desturi za pande zote mbili.

Taasisi ya WAMA ilianzishwa mwaka 2006 ikiwa na malengo ya kutoa ufadhili wa masomo kwa watoto wa kike ambao hawakupata nafasi ya kusoma, kuimarisha afya ya mama wajawazito na watoto, kuwainua wanawake kiuchumi na kuwasaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.

No comments: