Waziri Mkuu Mizengo Pinda akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mara mara ya kuongoza mkutano maalum wa Mpango wa kukuza kilimo kusini mwa Tanzania (SAGCOT), akizungumzia umuhimu wa uwekezaji katika sekta ya kilimo, kulia ni Waziri wan chi Ofisi ya waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu na Kushoto ni Waziri wa Kilimo, Bw. Christopher Chiza.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania imesisitiza kuwa itaendelea kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi na wadau wengine ili kufikia mapinduzi ya kilimo hapa nchini na hivyo kupatikana usalama wa chakula na maendeleo.
Msimamo huo umetolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokuwa akifungua mkutano mkubwa wa kilimo unaofanyika jijini Dar es Salaam leo.
Mkutano huo wa siku mbili umetayarishwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu na Kituo cha mpango maalum wa uendelezaji kilimo katika ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Mkutano huo unalenga kuvutia wawekezaji katika maeneo ya kilimo, biashara na miradi ya maendeleo kijamii na kiuchumi katika eneo la SAGCOT.
“Ushirikiano uliopo kati ya serikali, sekta binafsi, wadau wa maendeleo, wakulima na wadau wengine wa kilimo umesaidia kuendeleza sekta hii hapa nchini,” alisema.
Waziri Mkuu aliyashukuru makampuni 20 ambayo tayari yameshatoa ahadi ya kuwekeza katika sekta ya kilimo Tanzania katika miaka ijayo na wakati huo huo akaitaka sekta binafsi kufanya uamuzi zaidi wa kuwekeza zaidi katika sekta hiyo.
Hata hivyo alisisitiza kwamba wawekezaji wote katika ukanda wa SAGCOT watapewa kipaumbele pale ambapo uwekezaji wao unalenga pia kushirikisha wakulima wadogowadogo..
“Ni muhimu kusisitiza kwamba tunahitaji zaidi uwekezaji ambao utajali kushirikiana na wakulima wadogo na wajasiriamali wadogo na wa kati,” alisema.
Alisisitiza kwamba hata mapendekezo ya sera za uwekezaji katika kilimo zitoe kipaumbele kueleza jinsi wakulima wadogo na watanzania wa kawaida watakavyofaidika na uwekezaji katika ukanda wa SAGCOT.
Waziri Mkuu aliwahakikishia wawekezaji kwamba kupitia sheria mbalimbali Tanzania inatoa vivutio vingi na vizuri kulinganisha na nchi nyingine za Afrika.
“Kuwekeza Tanzania pia kunawahakikishia soko la uhakika katika eneo hili la Afrika,” alisema.
Alisema Tanzania imesaini mikataba mbalimbali ya kimataifa inayohakikisha usalama wa wawekezaji.
Akitoa mada katika mkutano huo, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza alitaja baadhi ya maeneo yanayolengwa katika uwekezaji SAGCOT kama kilimo cha miwa, matunda, ufugaji, nafaka na mazao ya misitu.
Katika siku ya pili ya mkutano huo wawekezaji watapata fursa ya kutembelea maeneo maalum ya miradi pamoja na kuangalia miradi ya kuimarisha miundombinu katika ukanda huo wa SAGCOT.
SAGCOT ni mpango unaoshirikisha sekta binafsi na ya umma unaotegemewa kuleta mapinduzi makubwa katika usalama wa chakula nchini kwa kushirikisha pia wakulima wadogo wadogo katika mazingira endelevu.
No comments:
Post a Comment