Utangulizi
Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume, Makamu Mwenyekiti
wa CCM na Rais Mstaafu
wa Zanzibar;
Ndugu Pius Msekwa, Makamu Mwenykiti wa CCM wa Bara;
Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Ndugu Benjamin William Mkapa;
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Waziri Mkuu;
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ;
Viongozi Wakuu Wastaafu;
Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Wilson Mukama;
Ndugu Wajumbe wa Mkutano
Mkuu wa Taifa wa CCM;
Wageni wetu waalikwa kutoka vyama rafiki,
Ndugu zetu wa Vyama vya Siasa Nchini;
Waheshimiwa Mabalozi,
Viongozi wa Dini,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana;
Kama ilivyo ada, naomba tuanze kwa kumshukuru
Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana
hapa Dodoma, siku ya leo, kwenye Mkutano Mkuu wa Nane wa Chama cha Mapinduzi.
Ndugu
Wajumbe;
Karibuni
Dodoma. Karibuni Mkutanoni. Nawapeni pole kwa safari. Tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufika
salama na tuombe turejee makwetu salama. Kwa niaba yenu, niruhusuni niwashukuru
wenyeji wetu, yaani wana-CCM na wananchi wote wa Dodoma, wakiongozwa na Alhaji Adam
Kimbisa, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Mkoa Dkt. Rehema Nchimbi,
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa. Tunawashukuru
kwa kutupokea vizuri na kwa ukarimu wao unaotufanya tujisikie tuko nyumbani katika
huu mji ambao ndiyo Makao Makuu ya nchi yetu na Chama chetu.
Ndugu
Wajumbe;
Napenda
kuchukua nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Halmashauri Kuu ya Taifa kwa
matayarisho mazuri ya Mkutano huu wa Nane wa Taifa wa CCM. Natoa pongezi maalum kwa Sekretarieti ya
Halmashauri Kuu ya Taifa chini ya uongozi mahiri wa Katibu Mkuu Ndugu Wilson
Mukama na Kamati zote za Maandalizi ya
Mkutano kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya ya kuwezesha Mkutano huu
kufanyika. Kwenu nyote nasema hongereni
na asanteni sana.
Ndugu
Wajumbe;
Karibuni tena Kizota. Nasikitika kwamba matumaini yangu ya kufanya
Mkutano Mkuu katika ukumbi wetu wenyewe hayakutimia. Hii ni kwa sababu kazi ya matayarisho imechukua
muda mrefu kuliko nilivyotazamia.
Tumechelewa kupata kiwanja kilichokidhi mahitaji yetu na matazamio
yetu. Kwanza tulipata kiwanja nyuma ya
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Lakini
tukaona ni mbali mno na walipo wananchi.
Tukaja kupata kiwanja kingine juu ya Kilimani Club ambacho hakikuwa
kikubwa cha kutosha. Mapema mwaka huu ndipo
tulipopata kiwanja eneo la Makulu ambacho kinakidhi sifa za kuwa kikubwa cha
kutosha na kuwa karibu na katikati ya mji wa Dodoma. Tumekiafiki
na matayarisho ya kuanza ujenzi yamekamilika. Leo asubuhi tumeweka jiwe la msingi kuzindua
ujenzi wa Ukumbi wa Mkutano (Dodoma Convention Centre). Baadae utafuta ujenzi wa jengo la Makao Makuu
ya CCM na jengo la Hoteli ya Kisasa.
Wageni Karibuni
Ndugu
Wajumbe;
Kama
mjuavyo Chama cha Mapinduzi kina marafiki wengi Afrika na kwingineko
duniani. Tumekuwa na mazoea ya kualikana
katika mikutano mikuu yetu. Safari hii
tumefanya hivyo tena. Kwa niaba yenu
niruhusuni niwashukuru sana wageni wetu wote wa kutoka vyama rafiki Afrika na duniani
kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kujumuika nasi siku ya leo. Kuwepo kwao ni
kielelezo tosha cha udugu na urafiki uliopo baina ya vyama vyetu na nchi zetu
ambao hatuna budi kuudumisha, kuuendeleza na kuukuza. Hali
kadhalika, nawashukuru Mabalozi wa Nchi za Nje na Wawakilishi wa Mashirika ya
Kimataifa walioweza kuja kushiriki nasi katika sherehe za ufunguzi wa Mkutano
wetu.
Ndugu
Wajumbe;
Tunawakaribisha
kwa furaha na upendo mkubwa viongozi na wawakilishi wa vyama vya siasa vya hapa
nchini kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Taifa wa
CCM siku ya leo. Tunawashukuru kwa moyo wao wa uungwana kwani
tofauti za vyama si uadui.
Wamethibitisha jinsi demokrasia ya vyama vingi inavyozidi kustawi na
kukomaa hapa nchini.
Nawashukuru
sana pia, viongozi wetu wa dini na wananchi mbalimbali waliojumuika nasi. Kuwepo kwao ni jambo la faraja kubwa. Dua za viongozi wa dini zitasaidia kuponya na
kuupa baraka mkutano wetu uende salama, uwe wa mafanikio na kuwafanya wale wote wasiokiombea mema
Chama chetu watahayari na kufadhaika.
Karibuni
Diaspora
Ndugu
Wajumbe;
Napenda
kuwatambua na kuwakaribisha viongozi na wananchama wa Chama chetu waliopo nje,
Marekani, Italia, India na Uingereza. Ndugu zetu hawa kwa upenzi wao kwa Chama
wamesafiri masafa marefu kuja kushiriki nasi.
Hawa wanastahili pongezi maalum kwa jinsi wanavyopeperusha bendera ya
CCM na kueneza sera zake. Naomba tuwape makofi ya nguvu.
Agenda ya Mkutano
Ndugu
Wajumbe;
Agenda ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa
Nane wa Chama cha Mapinduzi ina mambo makuu manne. Kwanza kufanya marekebisho ya Katiba ya Chama
cha Mapinduzi. Mengi ya marekebisho hayo
yanatokana na uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa katika kikao chake cha trehe
11 – 12 Aprili 2011 wa kufanya mageuzi ndani ya Chama. Miongoni mwa matunda ya mageuzi hayo ni kuundwa
kwa Baraza la Ushauri na Wajumbe wa NEC kuchaguliwa Wilayani badala ya
Mikoani.
Kwa
mujibu wa Katiba ya CCM, Halmashauri Kuu ya Taifa ina mamlaka ya kufanya
marekebisho ya Katiba na marekebisho hayo kutumika. Hata hivyo, marekebisho hayo hayana budi
kuletwa katika Mkutano Mkuu wa Taifa ili yaingizwe rasmi kwenye Katiba.
Ndugu
Wajumbe;
Jambo
la pili litakuwa ni kwa Serikali zetu mbili kutoa taarifa za maendeleo ya
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2010 – 2015 tangu baada ya uchaguzi mkuu
hadi sasa. Vile vile, tutapokea Taarifa
ya Halmashauri Kuu ya Chama kuhusu kazi za Chama kwa miaka mitano iliyopita. Jambo la nne na la mwisho ni kufanya uchaguzi
wa Mwenyekiti, Makamu wake wawili na Wajumbe wa NEC wa Kundi la Zanzibar na
Tanzania Bara.
Ndugu
Wajumbe;
Tofauti
na mikutano iliyopita, Halmashauri Kuu ya Taifa inapendekeza kuwa wajumbe wa
Mkutano Mkuu wajigawe katika makundi matano
kujadili taarifa ya kazi za Chama na zile za utekelezaji wa Ilani. Kisha kila kikundi kitatoa taarifa ya maoni
na mapendekezo yake. NEC ilifikiria iwe hivyo
ili kutoa muda wa kutosha kwa wajumbe kujadili taarifa hizo muhimu katika utaratibu
wa zamani wa mtu mmoja kila mkoa kuitwa kusoma, wajumbe hawapati fursa ya
kutosha ya kuzijadili taarifa zinazotolewa.
Kuimarisha Chama Kazi
Endelevu
Ndugu
Wajumbe;
Katika hotuba yangu ya kushukuru baada ya
kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwenye
Mkutano Mkuu wa Taifa Maalum wa tarehe 25 Juni, 2006, pamoja na kuzungumzia
mambo mengine, nilisisitiza umuhimu wa kuimarisha Chama chetu. Nilitoa maoni yangu kwa upana kiasi kuhusu
mambo ya kuzingatia. Leo tena, katika
ufunguzi wa Mkutano Mkuu huu narudia kusisitiza jambo hili. Nafanya hivyo kwa sababu hilo ndiyo jukumu la
kudumu na jukumu la kwanza na la msingi kwa kila kiongozi na kila mwanachamawa
CCM. Isitoshe, kwa hali ilivyo sasa,
kuimarisha Chama cha Mapinduzi lazima iwe agenda kuu ya kila mmoja wetu. Ni ukweli ulio wazi kuwa ustawi na uhai wa
Chama unategemea viongozi na wanachama kufanya kazi ya ziada kuimarisha Chama
chao.
Ndugu
Wajumbe;
Bahati
nzuri, chini ya uongozi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Lt. Yusuf Rajab
Makamba tarehe 19 Desemba, 2006 ulianzishwa Mradi wa Kuimarisha Chama. Mradi huo ndiyo uliokuwa dira na mwongozo
wetu wa kufanya kazi za Chama tangu wakati huo mpaka leo. Wajibu wa kila kiongozi na kila mwanachama na
kila kikao cha kila ngazi vimeainishwa vizuri.
Pia, uliwekwa utaratibu mzuri wa kufuatilia utekelezaji wake. Bila ya
shaka mtakumbuka kuwa utaratibu maalum uliwekwa wa kutoa tuzo kwa Mikoa
iliyofanya vizuri katika utekelezaji wa vipengele mbalimbali vya uimarishaji wa
Chama kwa mujibu wa Mradi huo.
Ndugu
Wajumbe;
Kazi
ya kuimarisha Chama chetu ni jukumu endelevu kwa kila mwanachama wa CCM, kila
kiongozi wa CCM na kila mtumishi wa CCM.
Kwa sababu hiyo, Mradi wa Kuimarisha Chama ni mchakato usiokuwa na
ukomo. Ni kazi ya kudumu na wala siyo
tukio lililoanzishwa na Katibu Mkuu Lt. Yusufu Rajabu Makamba na kukoma siku alipostaafu.
Tuongeze
Wanachama
Kazi ya kuingiza wanachama wapya ni ya
kudumu katika uhai wa Chama cha Mapinduzi.
Hii siyo kazi ya msimu wa uchaguzi wa ndani ya Chama au wakati wa kura
za maoni na hivyo kugeuzwa kuwa ni kwa ajili ya kuwapigia debe watu wanaotafuta
vyeo. Lazima wakati wote tuwe tunaingiza
wanachama wapya lakini pia lazima tuzingatie utaratibu ulioelekezwa na Katiba
ya CCM. Hatuna budi kuhakikisha kuwa
tuna wanachama walio waumini wa kweli na wapenzi wa dhati wa CCM, itikadi yake
na sera zake na zile za Serikali zake.
Ndugu
Wajumbe;
Wanachama
ndiyo nguvu kuu ya uhai na ushindi wa CCM.
Lazima Chama chetu kiwe na Jeshi
kubwa la wanachama walio tayari kukijenga, kukisemea na kukipigania. Kuwa na Wanachama wengi ambao ni waumini wa
kweli wa Chama chetu ina maana ya kuwa na kura nyingi za msingi za kuanzia
katika uchaguzi wa dola. Pia wanachama ni
nyenzo muhimu ya CCM kupata kuungwa mkono na wananchi hasa pale ambapo
wanachama wataifanya ipasavyo kazi ya Chama ndani ya umma. Kila mwanachama akifanya kwa mafanikio kazi
ya kushawishi wananchi kupigia kura wagombea wagombea wa CCM tutapata kura
nyingi za uhakika.
Tuwe na Viongozi
Wazuri
Ndugu
Wajumbe;
Kazi ya kuhakikisha kuwa Chama cha
Mapinduzi kina viongozi wazuri ni ya kudumu na wala siyo ya msimu wa kuchuja
majina ya wagombea. Lazima Chama chetu
kiwe na viongozi ambao ni waumini wa dhati wa itikadi yetu na wanaozijua vyema
sera za Chama cha Mapinduzi na Serikali zake.
Wao ndio wanaotarajiwa kuonesha njia kwa kuelimisha wanachama na wananchi. Viongozi wa CCM lazima wawe hodari wa
kufafanua sera na masuala mbalimbali yahusuyo Chama chetu na Serikali zake. Hawataweza kufanya hivyo kama wao wenyewe ni
maamuma. Kiongozi mzuri wa Chama cha
Mapinduzi ni yule ambaye ni jasiri kukitetea Chama cha Mapinduzi na kama hapana
budi yuko tayari kujitolea muhanga. Kuwa
na kiongozi ambaye haguswi wala kusikitishwa na hali mbaya ndani ya Chama au
hujuma dhidi ya Chama ni sawa na kutokuwa na kiongozi. Bora asiwepo.
Na kuwa na kiongozi ambaye yeye mwenyewe anafanya vitendo viovu dhidi ya
CCM na Serikali zake ni kuwa na nyoka ndani ya nyumba. Ni jambo hatari lisilokubalika na halistahili
kuvumilika. Tukiwajua tuwaseme,
tuwashughulikie, wachague wanapotaka kwenda.
Ndugu
Wajumbe;
Kiongozi
mzuri wa CCM lazima awe muaminifu na muadilifu na lazima wanachama na jamii
imuone hivyo. Chama chetu kinashindania
kushinda akili na mioyo ya Watanzania na hiyo ndiyo kazi tunayomtarajia
kiongozi wetu afanye katika jamii. Hii ndiyo
hasa kazi ya Chama ndani ya umma.
Lakini, ili kiongozi wetu aweze kuifanya kwa mafanikio taswira yake
mbele ya jamii ni kitu muhimu. Awe na
taswira nzuri mbele ya wananchi. Kama
jamii inamuona kuwa si mtu muadilifu itakuwa taabu sana kwake kufanikisha
jukumu la msingi la Chama chetu. Hivyo
ndugu zangu, lazima tuhakikishe kuwa viongozi wetu wanakuwa waadilifu ili
wasigeuke kuwa balaa na hasara kwa Chama.
Ndugu
Wajumbe;
Baada ya kukamilisha mchakato wa
uchaguzi ngazi ya taifa, tutatengeneza na kutekeleza programu maalum ya kutoa
mafunzo kwa viongozi wa Chama kuanzia ngazi ya Tawi hadi Taifa. Hali kadhalika, tutaendeleza na kukamilisha
kazi ya ukarabati na upanuzi wa Chuo cha Ihemi ili kiwe kitovu cha kutoa
mafunzo ya siasa kwa makada na viongozi wa Chama na Jumuiya zake kama
ilivyokuwa inafanywa katika Chuo cha CCM cha Kivukoni na vyuo vyake vya kanda.
Ndugu
Wajumbe;
Bahati
nzuri vyama vya ukombozi vya nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika
vimekubaliana kuwa Chuo cha Ihemi kiwe Chuo cha Mafunzo ya siasa kwa makada wa
vyama vyao pia. Ni heshima kubwa kwa
CCM, lakini pia inakipa Chama chetu wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa Chuo
hicho kinawekwa katika viwango vya kimataifa.
Tuko tayari na tutajipanga ipasavyo kutimiza wajibu wetu huo wa
kihistoria.
Vikao Vifanyike
Ipasavyo
Ndugu
Wajumbe;
Ni
kazi endelevu kwetu sote, wanachama na viongozi, kuhakikisha kuwa vikao
vinafanyika kwa wakati na kwamba mikutano inaendeshwa vizuri na ina agenda
zenye maslahi ya kujenga Chama na kuendesha nchi. Pia, ni muhimu kuhakikisha kuwa kinachoamuliwa
kinatekelezwa ipasavyo. Naamini kwamba
mafunzo tutakayotoa kwa viongozi na watendaji wa Chama kuhusu wajibu wao na
jinsi ya kuutekeleza yatasaidia sana kuimarisha CCM.
Watendaji
Mahiri
Ndugu
Wajumbe;
Kwa
Chama chetu kuwa na watendaji wazuri ni jambo lisilokuwa na mjadala. Lazima tuwe na watendaji ambao ni makada
wazuri na watu mahiri kwa kazi zao. Wawe
ni watu ambao wana uelewa mzuri wa sera za Chama na kwamba wanaweza
kuzifafanua, kuzieneza na kuzitetea. Pia,
wawe ni watu wanaojua vyema kazi yao ya utendaji, kwa mujibu wa shughuli zao wanazozifanya. Ni vyema kwa kazi za kitaalamu tukapata watu
wataalamu wa kazi hizo. Ni muhimu sana
tukayazingatia haya kwani utendaji mzuri katika Chama ni nguvu muhimu sana ya
kukifanya Chama chetu kuwa imara. Chama chetu
kiwe na mipango thabiti ya kuwaendeleza watumishi wake na kama hapana budi
kuwadhamini wakasome. Tufanye hivyo.
Bila
ya shaka mtakumbuka kuwa tarehe 3 Novemba, 2007, pale Kizota, niliahidi kuwa
tutaboresha maslahi ya watumishi wa Chama.
Tumetimiza ahadi hiyo. Leo nasema
kuwa tutajitahidi kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi wetu kadri uwezo
utakavyoruhusu.
Tujitegemee
Ndugu
Wajumbe;
Lazima
Chama chetu kiwe na uwezo wake chenyewe wa kujisimamia na kujiendesha. Kiwe na fedha za kutosha na vitendea
kazi. Hivi sasa hatuko hivyo. Hatuna budi kuongeza maarifa na juhudi za
kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kujitegemea kifedha bila ya kujali kama kuna
ruzuku au hakuna. Jambo hili sasa liwe
ni la kufa na kupona kwetu kuhakikisha linakuwa. Iwe agenda kuu ya Chama katika
ngazi zote. Kila mmoja afikirie nini cha
kufanya na kifanywe. Jambo la kuzingatia
ni kufanya shughuli halali. Fursa zipo
tuzitumie. Tusikubali kushindwa kwenye
azma kwani hiyo itakuwa maangamizi wa CCM.
Lazima tushinde.
Ndugu
Wajumbe;
Mtakumbuka
pia kwamba niliahidi kuimarisha usafiri ndani ya Chama. Ahadi hiyo tumeitimiza. Kila Mkoa na kila Wilaya imepata gari mpya
tena gari nzuri na imara. Gari hizi tukizitunza
vizuri zitatuwezesha katika uchaguzi
ujao bila ya taabu. Kwa Mikoa na Wilaya
mpya mipango ya kuwapatia magari iko mbioni. Kila Jumuiya tuliipatia magari
yasiyopungua matatu.
Jumuiya
za Chama
Ni
wajibu wa kudumu wa Chama chetu kuhakikisha kuwa Jumuiya zake zinaimarika na
kutimiza ipasavyo wajibu wake. Jumuiya
ndiyo mkono mrefu wa Chama cha Mapinduzi kuufikia umma mpana wa Watanzania hasa
wale ambao si wanachama. Jukumu letu ni
kuhakikisha kuwa watu hao wanakuwa wanachama au wapenzi na marafiki wa
CCM. Kwa hiyo, kuwepo kwa Jumuiya ni
fursa nzuri kwa Chama cha Mapinduzi kuungwa mkono na watu wengi ili wakati wa
uchaguzi tuweze kupigiwa kura na kupata ushindi. Jumuiya lazima zihakikishe kuwa zinatimiza
ipasavyo wajibu wake ili wasiipotezee CCM fursa hii adhimu.
Ndugu
Wajumbe;
Kwa
muhtasari, hayo ndiyo baadhi ya mambo ya msingi ya mradi wa kuimarisha
Chama. Mtakubaliana nami kuwa haya yote
ndiyo kazi na wajibu wa kila mmoja kufanya.
Ni kazi endelevu isiyokuwa na ukomo.
Tupo kwa ajili hiyo na rai yangu kwenu ni kuhakikisha kuwa kila
mwanachama na kila kiongozi anatimiza ipasavyo wajibu wake.
Mageuzi Ndani ya
Chama
Ndugu Wajumbe;
Kwa dhamira ya kuendelea kukiimarisha
zaidi, Chama cha Mapinduzi, katika mkutano wake wa tarehe 11-12 April, 2011,
Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua kuanzisha mchakato na kufanya mageuzi ndani ya
Chama. Lengo kuu la uamuzi huo ni
kukiwezesha Chama chetu kuwa na taswira inayovutia katika mitazamo na hisia za
wanachama wake na wananchi.
Kimsingi
NEC inataka tukiwezeshe Chama cha Mapinduzi kiendelee kupendwa na kuaminiwa na
wananchi wote wa Tanzania. Tunataka
wanawake na wanaume, wadogo na wakubwa, maskini na matajiri, wanyonge na wenye
nguvu waone kuwa CCM ndiyo kimbilio lao.
Ndugu
Wajumbe;
Kwa ajili hiyo mageuzi ya ndani ya Chama yamejengeka
juu ya misingi ifuatayo:-
1.
Kukiwezesha Chama cha
Mapinduzi kuwa na makada na viongozi mahiri, waadilifu na waaminifu kwa Chama
chao;
2.
Kukiwezesha Chama
kuwa na sera zinazojali maslahi ya wengi na kusukuma mbele kwa kasi maendeleo
ya taifa letu;
3.
Kukiwezesha Chama
kuwa na muundo na mfumo wa uendeshaji ulio nyumbulifu na unaokifanya kuwa
karibu na wanachama na wananchi;
4.
Kukiwezesha Chama
kujitegemea kimapato na kiuchumi ili kiweze kuendesha shughuli zake kwa uhakika,
uhuru na heshima;
5.
Kukiwezesha Chama
kuwa na watu hodari wa kazi na Makada wazuri ambao wanalipwa vizuri na
kuwezeshwa kutekeleza majukumu yao;
6.
Kukiwezesha Chama
kuwasiliana na umma kwa urahisi na kupambana na propaganda chafu za vyama vya
siasa; na
7.
Kukiwezesha Chama cha
Mapinduzi kupambana na maovu ndani ya Chama na katika jamii likiwemo tatizo la
rushwa na mengineyo.
Ndugu
Wajumbe;
Katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya
Taifa iliamuliwa kuwa kutokana na umuhimu wa hoja na haja ya kufanya mageuzi
ndani ya Chama utekelezaji wa mageuzi uanze mara moja. Aidha, pawepo na progamu ya utekelezaji
unayoainisha nini kinafanyika lini na mhusika ni nani! Bila ya shaka mtakumbuka kuwa katika kikao
kile, tuliunda upya Kamati Kuu na kuteua Sekretarieti mpya. Vile vile iliamuliwa kuwa tufanye marekebisho
katika muundo wa Chama na moja ya matokeo
yake ni Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kuchaguliwa kutoka wilayani. Nafasi za NEC za mikoa zikafutwa na zile za
taifa zikapunguzwa. Aidha, limeundwa
Baraza la Taifa la Ushauri ambalo wajumbe wake ni viongozi wakuu wa Chama
wastaafu. Wanapata fursa ya kukaa na
kutoa ushauri kwa Chama na viongozi wake.
Ndugu
Wajumbe;
Tuliamua, pia, kuunganisha chaguzi za
Chama na Jumuiya zifanyike mwaka mmoja.
Shabaha ya uamuzi huo ni kutaka kujipa muda wa kutosha wa kujenga Chama
na Jumuiya zake na kujiandaa kwa chaguzi za dola. Uamuzi huo umeokoa takriban mwaka mzima ambao
tulikuwa tunautumia kwa uchaguzi. Vile
vile Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua kwamba mgao wa fedha unatokana na mapato
Chama zinazopelekwa kwenye Matawi na Mashina uongezwe. Lengo ni kuziwezesha ngazi hizi muhimu za
Chama kufanya kazi vizuri zaidi.
Ndugu
Wajumbe;
Suala la nidhamu na maadili ya
viongozi na wanachama lilisisitizwa sana kwa sababu ya umuhimu wake kwa taswira
ya Chama chetu mbele ya jamii na wanachama wake. Pia, kutokana na ukweli kwamba ni kilio cha
wanachama na wananchi cha kutaka tuiondowe taswira mbaya dhidi ya Chama iliyopo
katika jamii kuwa ni Chama kisichokerwa na rushwa. Hicho ni kilio cha dhati kwa watu wenye nia
njema na CCM: Chama chao, wanachokipenda
na kukiamini. Chama ambacho bado hakina
badala yake wa kuiongoza vyema nchi yetu na watu wake.
Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua mambo
mawili yafanyike. La kwanza, mfumo mzima
wa kushughulikia masuala ya usalama na maadili katika Chama utazamwe upya na uimarishwe. Pili, Chama kichukue hatua na lazima
kionekane kinachukua hatua dhidi ya viongozi na wanachama wasiokuwa waadilifu
na waaminifu wanaofanya sura ya Chama ichafuke mbele ya jamii. NEC iliagiza wenyewe wajipime na kuamua na
wasipofanya hivyo vikao husika katika Chama vichukue hatua.
Ndugu
Wajumbe;
Hayo ni baadhi tu ya mambo muhimu yaliyoamuliwa
yafanyike katika kufanya Mageuzi Ndani ya Chama. Utekelezaji wake umeanza. Yapo yaliyokamilika na yapo yanayoendelea
kutekelezwa. Yapo mambo mengi ambayo ni
endelevu kama vile mapambano dhidi ya rushwa.
Hatuna budi kuendelea kulikemea na kusimama kidete kupambana na tatizo
hili mpaka likomeshwe. Ni kwa maslahi na
heshima ya Chama chetu kuendesha mapambano haya bila ya woga mpaka
tushinde. Tukishindwa itakuwa hatari kwa
uhai wa Chama chetu.
Umoja ni Ushindi
Ndugu
Wajumbe;
Mara ya mwisho tulipokutana tarehe 11
Julai, 2010, tulikuwa tunajipanga kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2010. Mliniteua mimi na Dkt. Mohamed
Ghalib Billal kupeperusha bendera ya CCM kwa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia
tulipitisha Ilani ya Uchaguzi ya 2010-2015.
Siku moja kabla ya Mkutano Mkuu, Halmashari Kuu ya Taifa ilikuwa
imemteua Dkt. Ali Mohamed Shein kupeperusha bendera yetu kwa nafasi ya Rais wa
Zanzibar.
Bahati
nzuri tumepata ushindi kwa nafasi zote hizo za juu za uongozi wa taifa
letu. Pia tulifanikiwa kupata Wabunge na
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wengi zaidi kuliko vyama vya upinzani. Kwa sababu hiyo, tumeunda Serikali zote mbili
za nchi yetu na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi unaendelea vizuri.
Ndugu
Wajumbe;
Kwa upande wa Zanzibar, tuna Serikali
ya Umoja wa Kitaifa na mambo yanakwenda vizuri.
Tuzidi kuunga mkono na kuwatakia heri Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein,
Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa
Rais, Balozi Seif Ali Idd. Tunawapongeza
sana kwa mafanikio yaliyopatikana.
Zanzibar ina amani na umoja unaozidi kuimarika. Tunatakiwa tuendelee kuiunga mkono Serikali
ya Umoja wa Kitaifa ili ifanikiwe zaidi.
Ndugu
Wajumbe;
Uchaguzi uliopita kwa upande wa
Tanzania Bara ulikuwa na changamoto nyingi ambazo hatukuzizoea wala kujiandaa
nazo. Zinaelezea matokeo tuliyoyapata
jambo ambalo linatulazimu kuwa makini zaidi katika uchaguzi ujao. Tusikubali kushtukizwa tena. Lakini, jambo moja lililo dhahiri ni kwamba
umoja na mshikamano miongoni mwa wana-CCM ndiyo uliotuwezesha kukabili
changamoto hizo na kupata ushindi tulioupata.
Bila ya hivyo, mbinu hasi zilizotumika zingetufanya tushindwe.
Napenda
ukweli huu uwepo katika vichwa na mioyo ya wana-CCM na sisi viongozi wao
tuliochaguliwa hivi majuzi na watakaochaguliwa katika Mkutano huu. Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere
alisema: Umoja ni Nguvu, ni kweli
kabisa na sisi ni mashahidi. Nami napenda
kuongeza kwa kusema kuwa Umoja ni
Ushindi.
Ndugu
Wajumbe;
Nawaomba wakati wote wa mkutano na
baada ya mkutano tukumbuke na kuzingatia Umoja.
Tuishikilie kamba ya Umoja isituponyoke.
Tuimbe Umoja kimoyo moyo na tubainishe wazi wazi kwa kauli na matendo yetu
kuwa: Umoja ni Nguvu Utengano ni Udhaifu!
Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi!. Napenda kuona kuwa tunatoka hapa tukiwa kitu
kimoja, tukiwa watu tunaopendana na tulioshikamana. Nataka
tuondoke katika Mkutano sote tukivuta kamba upande mmoja badala ya kuvutana. Nataka tuazimie kukabiliana na kauli, matendo
au watu wanaopandikiza chuki na kuhatarisha umoja ndani ya Chama chetu na
miongoni mwetu. Nataka kaulimbiu ya ujumbe
wa Mkutano huu uwe Umoja ni Ushindi!
Umoja na Ushindi! Tukiendelea kuwa
watu tunaovutana na kuhasimiana hatutaweza kukijenga Chama chetu wala
kuwatafutia ushindi wagombea wa Chama chetu.
Tutakuwa sawa na ule msemo wa Kiswahili usemao: “vita vya panzi furaha ya kunguru”
Tusijigeuze panzi na wala tusikifikishe Chama chetu kiwe hivyo.
Ndugu
Wajumbe;
Mtakubaliana nami kuwa harakati za
kutafuta uongozi ndani ya Chama au uteuzi wa kugombea katika chaguzi za dola
imekuwa ndiyo chanzo kikuu kinacholeta mifarakano na kuvuruga umoja ndani ya
Chama chetu. Hili ndugu zangu siyo sawa
hata kidogo. Kugombea uongozi ni haki ya
msingi ya mwanachama na raia wa Tanzania.
Kwa nini mtu achukiwe au aonekane adui kwa kuamua kuitumia haki yake
hiyo? Kwa nini afanyiwe vitimbi, vitendo
viovu au njama za kuhujumiwa? Nani mwenye
haki zaidi ya mwanachama ama raia mwenzake?
Ni ubabe na jeuri ya pesa isiyokuwa na msingi. Ni ubinafsi na uchu wa madaraka uliopitiliza
mipaka. Watu wa namna hiyo ni hatari
sana kwani wanaweza hata kuua au kukivuruga Chama chetu kizuri kama tamaa zao
zisipokidhiwa.
Ndugu
Wajumbe;
Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi
wale wote wanaochukiana kwa sababu ya kugombea watakafakari upya misimamo yao. Wafanyayo siyo sahihi, wanaathiri nguvu na uhai
wa Chama chetu. Naomba Kamati za Siasa
za ngazi zote ziwatambue watu hao na kuwaita kuwapatanisha. Naomba wahusika watoe ushirikiano wao. Hata wale wanaohisi kuwa hawakutendewa haki
katika uchaguzi, walidhulimiwa au hata kushindwa kwa sababu ya vitendo vya
rushwa, wakumbuke kuwa Chama chetu kina utaratibu wa kushughulikia malalamiko
yao. Wautumie utaratibu huo badala ya
kufanya vitendo vinavyokigawa na kukivuruga Chama chetu. Kulalamika katika vyombo vya habari, kufanya
ghasia au kuchochea migawanyiko hakutaleta ufumbuzi.
Ndugu
Wajumbe;
Niruhusuni nitumie nafasi hii kuwasihi
wale wote wenye tamaa ya kugombea uteuzi ndani ya Chama wasituulie Chama
chetu. Kuwa na tamaa ya kugombea Urais,
Ubunge na Udiwani si kosa ni haki ya mwanachama na ni haki ya raia wa nchi
hii. Jambo ambalo halikubaliki na gumu
kulivumilia ni kufanya vitendo vya kuwagawa wanachama na Chama chetu. Kuwalazimisha au kuwashinikiza kujiunga na
kundi fulani siyo sawa. Kumchukia mtu
kwa sababu naye anagombea au amekataa kukuunga mkono au kumuunga mkono umpendae
ni jambo baya. Unaifanya demokrasia iwe
haina maana au kichekesho. Na, lililo
baya kupita kiasi ni kutumia fedha kushawishi, kuwarubuni au kuwanunua watu kukuunga
mkono au kumuunga mkono mgombea wako au kujiunga na makundi. Hili ni jambo haramu na ni utovu wa maadili
usiokubalika ambao lazima tuukatae, tuukemee na tuupige vita kwa nguvu zetu
zote. Naomba wote tushirikiane katika
mapambano haya kwa heshima ya Chama chetu.
Utekelezaji wa Ilani
ya Uchaguzi
Ndugu Wajumbe;
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya
mwaka 2010 unakwenda vizuri kwa Serikali zetu zote mbili. Taarifa zitakazotolewa na Waziri Mku,
Mheshimiwa Mizengo Pinda, kwa upande wa Serikali ya Muungano na Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd kwa upande wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, zitathibitisha ukweli huu.
Niruhusuni nichukue muda wenu kidogo nizungumzie baadhi ya mambo
yahusuyo shughuli za Serikali.
Nchi Iko Salama
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuanza kwa kuwahakikishia kuwa
Tanzania iko salama pamoja na kuwepo matukio ya hapa na pale. Mipaka yetu iko salama. Hakuna tishio lo lote la kiusalama la
kutufanya tuhamanike. Hata mpaka wetu na
Malawi uko salama pamoja na kuwepo kwa maneno maneno yahusuyo nchi zetu mbili
kutofautiana wapi ulipo mpaka halali.
Hakuna jambo lo lote linalofanywa upande wa wenzetu ambalo linatufanya
tuwe na mashaka ya usalama wa nchi yetu kuwa hatarini. Kwa sababu hiyo hatujaiona haja ya kusogeza
Majeshi yetu mpakani na anayesema tumefanya hivyo ni muongo. Apuuzwe na kushushuliwa.
Ndugu
Wajumbe;
Tumeendelea
na juhudi za kuimarisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kuwajengea
uwezo, zana na vifaa vya kisasa vya kivita.
Lengo letu ni kukuza nguvu ya kimapigano ya Jeshi letu na kuimarisha
utayari wake kivita. Hali kadhalika, tumeendelea
kuboresha maslahi ya wanajeshi na mazingira yao ya kufanyia kazi na ya kuishi. Kwa upande wa usalama wa raia, yaani maisha na
mali zao, matukio ya uhalifu yanaendelea kupungua. Hali hii inaashiria kuwa Jeshi la Polisi linafanya
kazi nzuri. Kama tufanyavyo kwa JWTZ, tutaendeleza
juhudi za kuimarisha Jeshi la Polisi kwa watu, zana na vifaa vya kisasa vya
kufanyia kazi. Tutaendelea kuboresha
maslahi na mazingira ya kufanyia kazi na ya kuishi ya Jeshi la Polisi na vyombo
vingine vya usalama.
Ndugu
Wajumbe;
Pamoja na kutokuwepo kwa tishio lililo
dhahiri la shambulio la kigaidi, wakati wote vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viko katika
hali ya tahadhari kuepuka kushtukizwa.
Kama mnavyokumbuka mwaka 1998 Ubalozi wa Marekani hapa nchini
ulishambuliwa na ndugu zetu 11 walipoteza maisha. Hivyo basi, kuchukua tahadhari ni jambo la
busara kufanya. Aidha, tuko katika hali
ya tahadhari dhidi ya uharamia wa kuteka meli katika Bahari Kuu ya Hindi. Takriban mwaka mzima umepita bila ya matukio
ya kutekwa nyara meli katika bahari yetu .
Hata hivyo hatuachi kuchukua tahadhari.
Ndugu
Wajumbe;
Matukio
ya hivi karibuni ya vurugu zenye mwelekeo wa kidini yanasikitisha na kusononesha. Ni mambo ambayo hayafanani na sifa ya nchi
yetu ya kuheshimiana na kuvumiliana pamoja na kuwepo tofauti zetu za dini, kabila rangi au maeneo tutokako.
Vitendo hivyo havikubaliki na Serikali haitawavumilia au kuwaonea muhali wale
wote wanaohusika na kuchochea vurugu hizo.
Tumechukua hatua na tutaendelea kuchukua hatua bila ya ajizi. Ombi langu na wito wangu kwa viongozi na
wafuasi wa dini nchini kuhubiri dini zao huku wakitambua na kuzingatia umuhimu
wa kuheshimu imani za wengine na kuvumiliana.
Tusipofanya hivyo nchi yetu tutaingiza kwenye matatizo yasiyostahili kuwepo.
Ndugu
Wajumbe;
Inatia moyo kuona kuwa watu wenye nia
njema na nchi yao ni wengi. Kwa sababu
hiyo pamoja na jitihada za baadhi ya watu wasiyoitakia mema nchi yetu
hawajafanikiwa kuwagawa na kuwafarakanisha Watanzania. Nawaomba Watanzania wenzangu tuwe na moyo huo
huo na sisi katika Serikali tutaendelea kumchukulia hatua mtu ye yote anayetaka
kutuvurugia amani na utulivu wa nchi yetu na watu wake.
Ndugu
Wajumbe;
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali
haitamuonea mtu ye yote asiyehusika.
Tutaendelea kuidumisha sifa yetu ya kuendeleza utawala bora, kuheshimu
haki za binadamu na kuzingatia utawala wa sheria. Kadhalika tutaendelea kuheshimu mgawano wa
madaraka miongoni mwa mihimili mikuu ya dola.
Nafurahi kwamba mpaka sasa mambo yanakwenda vizuri.
Muungano Imara
Ndugu Wajumbe;
Muungano wetu ni imara pamoja na
kuwepo vitendo vyenye lengo la kuudhoofisha vinavyofanywa na baadhi ya viongozi
wa siasa na wa dini hasa kule Zanzibar.
Jambo linalosikitisha ni watu hao kutumia njia za vitisho na ghasia ili kuwalazimisha
watu kuwaunga mkono. Njia hizo
hazikubaliki na wala hazitavumiliwa.
Inastaajabisha
mambo hayo kufanyika hivi sasa wakati kuna Tume ya Katiba. Kama mtu ana maoni yo yote kuhusu Muungano
ayafikishe tu, yatapokelewa na kupimwa. Vile
vile Kamati ya Pamoja ya Serikali zote mbili inayowakutanisha Waziri Mkuu na
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar chini
ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano imekuwa inafanya kazi
nzuri kutatua kero za Muungano. Kama mtu
analo jambo analotaka lipatiwe jawabu awasilishe kwa wahusika litashughulikiwa.
Hali ya Uchumi
Ndugu Wajumbe;
Katika Mkutano Mkuu Maalum wa Julai, 2010 hapa Kizota,
nilielezea mafanikio tuliyoyapata na changamoto tulizokumbana nazo katika
kukuza uchumi wa nchi yetu na kupunguza umasikini. Nilieleza pia nia yetu ya
kuendelea kupambana na changamoto zilizokuwa mbele yetu pamoja na ugumu
unaotokana na hali ya kuyumba kwa uchumi wa dunia ambamo na sisi pia tumo. Kwa ajili hiyo mwaka 2011 tulizindua Mpango
wa Maendeleo wa Miaka Mitano(2011/12 – 2015/16).
Mpango huu ni wa kwanza kati ya mitatu katika safari
yetu ya kutekeleza Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025. Kwa mujibu wa Dira yetu hiyo, tunatarajia ifikapo
mwaka 2025 nchi yetu itaondoka katika kundi la nchi maskini sana duniani na
kuwa nchi ya uchumi wa kati. Yaani
tunataka pato la wastani la Watanzania litoke kwenye dola za Kimarekani 545 za sasa hadi kufikia dola
za Kimarekani 3,000. Lengo hilo ni kubwa linalohitaji mipango
thabiti na uwekezaji makini wa Serikali na sekta binafsi. Pia inahitaji kuwepo kwa nidhamu ya dhati ya
viongozi na wananchi wa Tanzania.
Ndugu Wajumbe;
Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo umekwishaanza. Lengo la jumla katika Mpango wa kwanza ni Kufungulia fursa kwa ukuaji wa uchumi;
wa pili ni Ujenzi wa mazingira ya
maendeleo ya viwanda; na wa tatu ni Kuimarisha ubunifu na ushindani kimataifa. Tayari miradi ya kimkakati imekwishaainishwa
na inapewa kipaumbele katika bajeti ya Serikali na ubia baina ya sekta binafsi
na sekta ya umma. Katika kila hatua suala la kukuza ajira limepewa umuhimu
mkubwa kwani lengo letu ni kuwa na ukuaji wa uchumi unaojumuisha maisha ya
watu. Vijana ni walengwa wakubwa.
Mwelekeo wa
uchumi wetu ni mzuri. Kasi ya ukuaji wa
uchumi iliyokuwa asilimia 6.4 mwaka wa jana inatarajiwa kufikia asilimia 7
mwaka huu. Mauzo yetu ya nje yanazidi
kukua na kuongezeka. Kwa mfano mwaka 2005
ilikuwa dola za Kimarekani milioni
2,945.5 na sasa ni milioni 7,461.2. Akiba yetu ya fedha ya kigeni nayo ni nzuri. Hivi sasa ni dola za Kimarekani bilioni 4.1 inatuwezesha kuagiza bidhaa
kutoka nje kwa miezi 3.8.
Ndugu Wajumbe;
Changamoto kubwa katika uchumi ni mfumuko wa bei. Ni kweli umepungua kutoka asilimia 19.8
Desemba, 2011 hadi asilimia 13.5 Septemba, 2012, hata hivyo kupungua huko ni
kidogo mno. Tunaendelea kuchukua hatua za
kudhibiti na kupunguza zaidi mfumuko wa bei.
Kwa vile moja ya sababu ni kupanda kwa bei za mafuta. Tumeipa dhamana
EWURA kusimamia kwa karibu uagizaji na upangaji wa bei ya mafuta.
Kwa kuwa bei
za vyakula hasa mchele na sukari navyo huchangia kupanda kwa mfumuko wa bei na
kuongeza gharama ya maisha mamlaka husika zimeagizwa kuhakikisha kuwa
wafanyabiashara wanawezeshwa kuagiza bidhaa hizo kwa wingi kutoka kwa nje kwa
kuwapatia nafuu ya baadhi ya kodi.
Pamoja na hayo jawabu la kudumu lipo katika kuendeleza mageuzi ya kilimo
ili nchi yetu ijitosheleze kwa chakula na kupata ziada kubwa ya kuuza nje. Hayo ndiyo malengo na hatua zinazochukuliwa katika
ASDP, Kilimo Kwanza na SAGCOT. Ndiyo
maana tutaendelea kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima, kuimarisha masoko na
miundombinu vijijini.
Mapato na Matumizi ya Serikali
Ndugu Wajumbe,
Tunazidi kupata
mafanikio ya kutia moyo kwa upande wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Makusanyo ya mapato ya kodi Mwezi Agosti
2012, kwa mfano, yalifikia shilingi bilioni
554.8 ikilinganishwa na makusanyo ya
shilingi bilioni 147 mwezi Desemba 2005. Mafanikio haya yametokana na juhudi za
dhati za Serikali katika kusimamia mabadiliko ya sera na kuimarisha mifumo na
taasisi za ukusanyaji wa mapato ya kodi na mengineyo.
Kwa sababu ya kuongezeka
huko kwa mapato, bajeti ya Serikali nayo imeongezeka kutoka shilingi trilioni 4.13 mwaka 2005/06
hadi shilingi trilioni 15.12 mwaka
huu. Jambo linaloleta faraja ni kuwa
mchango wa Serikali kutokana na bajeti hiyo nao umeongezeka kutoka shilingi trilioni 2.1 mwaka 2005 hadi trilioni 8.8 mwaka huu. Utegemezi wa wahisani nao unaendelea kupungua
kutoka asilimia 44 mwaka 2005/6 hadi
21.
Ndugu Wajumbe;
Sambamba na kuongeza
mapato, nidhamu, udhibiti wa matumizi ya fedha na mali za umma vinazidi kuimarika. Hii ni kutokana na kuimarika kwa mifumo na kada
ya uhasibu katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Pia ni matokeo ya kazi nzuri inayoendelea
kufanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Mamlaka ya
Udhibiti wa Manunuzi ya Umma. Hati Chafu
katika idara za Serikali zinaendelea kupungua katika taarifa ya ukaguzi kila
mwaka. Hivi sasa tunaelekeza nguvu zetu
katika kuhakiki thamani ya fedha zilizotumika na kazi iliyofanyika au huduma
iliyotolewa.
Uwekezaji
Ndugu Wajumbe,
Serikali imechukua hatua
kadhaa kuboresha mazingira ya uwekezaji na ya kufanya biashara hapa
nchini. Lengo letu ni kuvutia wawekezaji
wa ndani na nje kuongeza vitega uchumi nchini na kupanua biashara ndani ya nchi
na kati ya nchi yetu na nchi nyingine duniani.
Tunafanya hayo kwa kutambua ukweli kwamba uchumi unakua na kuongezeka
pale ambapo uwekezaji unaongezeka. Takwimu
zinaonyesha kwamba uwekezaji umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka katika sekta
ya utalii, viwanda, kilimo, madini, fedha, ujenzi na sasa kwenye utafutaji wa gesi na
mafuta. Tumepata mafanikio makubwa katika
utafutaji wa gesi na nchi yetu itakuwa moja ya mzalishaji mkubwa wa gesi. Mwaka 2011, kwa mfano, kulikuwa na jumla ya miradi 826 yenye thamani ya dola za
Kimarekani milioni 7,177 itakayozalisha
ajira ya watu 79,000. Haya ni mafanikio madogo lakini tunaweza
kufanya vizuri zaidi.
Tutaendelea kutumia
fursa ya kijiografia ya nchi yetu kuvutia uwekezaji na kuifanya Tanzania kuwa
lango kuu la biashara na usafirishaji kwa nchi za Afrika ya Mashariki na
Kati. Ili kufanikisha hayo, tutaendelea
kuboresha miundombinu ya barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege na
teknohama.
Miundombinu
Ndugu
wajumbe;
Moja ya vipaumbele vya juu vya Serikali
ya CCM ninayoiongoza ni kuboresha miundombinu ya usafiri wa ardhini, majini na
angani nchini. Tumethibitisha hayo kwa mgao wa fedha za bajeti ya Serikali
ambapo miundombinu ni ya pili baada ya elimu.
Mwaka huu ni shilingi trilioni 2.4,
ambayo ni asilimia 16 ya bajeti ya Serikali
ukilinganisha na elimu yenye trilioni
3.6 ambayo ni sawa na asilimia 24,
na afya yenye shilingi trilioni 1.5
sawa na asilimia 10 ya bajeti ya
Serikali. Tunafanya hivyo kwa kutambua mchango muhimu wa sekta ya usafiri kwa
maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Usafiri unapokuwa bora na wa uhakika,
gharama za usafirishaji zinapungua, shughuli za uzalishaji viwandani na kilimo
zinaimarika. Ni kichocheo kikubwa cha
kuibuka kwa fursa mbalimbali za uchumi na kuongeza kasi ya maendeleo na kukuza
kipato cha Watanzania waliopo mijini na vijijini.
Ndugu
Wajumbe;
Tunafanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi
wa barabara kuliko wakati mwingine wo wote katika historia ya nchi yetu. Hivi sasa barabara zenye urefu wa kilometa 11,154 zinajengwa kwa kiwango cha lami katika sehemu
mbalimbali nchini. Tulijipa lengo la
kuunganisha mikoa yote kwa barabara za
lami na barabara zote kuu ziwe za lami.
Nafurahi
kusema kuwa utekelezaji wake unakwenda vizuri.
Tumeanza kufanikiwa kuifikia ile mikoa ambayo kwa muda mrefu ilikuwa haifikiki
kwa urahisi kwa kukosa barabara za lami.
Katika hotuba yangu ya tarehe 25 Juni, 2006 niliwaambia Wajumbe wa Mikoa
ya Ruvuma, Rukwa, Mtwara, Kigoma na Tabora kuwa kilio chao tumekisikia. Niliahidi kuwa ujenzi wa barabara katika
Mikoa hiyo tutaipa kipaumbele.
Tumetimiza ahadi hiyo na kazi inaendelea kwa kasi na hata wenyewe ni
mashahidi. Karibu tunafikia ndoto yetu ya
kwamba hakuna mkoa utakaoachwa nyuma.
Ndugu
Wajumbe;
Inafurahisha
zaidi kuona kuwa zaidi ya asilimia 60 ya gharama za ujenzi wa
barabara tunazojenga nchini ni fedha zetu wenyewe. Aidha, uwezo wa Mfuko wa Barabara (Road Fund) nao umeongezeka
sana kutoka shilingi bilioni 58
mwaka 2005 hadi shillingi bilioni 430.
Hali hiyo imeongeza uwezo wetu wa kujenga na kukarabati barabara mbalimbali
nchini. Kwa ajili hiyo tumeongeza bajeti
ya barabara kwenye Halmashauri zote nchini.
Ndugu
Wajumbe;
Pamoja
na barabara, tunaendelea kuimarisha viwanja vya ndege, bandari na usafiri wa
reli. Changamoto
mbalimbali zinajitokeza katika utekelezaji wa lengo letu na kubwa zaidi ikiwa ni
ile ya gharama za ujenzi na ukarabati wa miundombinu kuwa kubwa mno
ikilinganishwa na uwezo wetu. Tunaendelea
kuchukua hatua mbalimbali kuzikabili changamoto hizo hatua kwa hatua na
tunazipunguza.
Elimu
Ndugu
wajumbe;
Tumefanikiwa
kupanua sana fursa za kuwapatia elimu vijana wetu katika ngazi zote. Kuna watoto
wengi katika elimu ya awali, na kwa elimu ya msingi asilimia 97 ya watoto wenye umri wa kwenda shule wamejiandikisha.
Kwa kiwango hicho, tuko mahali pazuri kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2015 kama ilvyoagiwa katika Malengo ya
Milenia ya Umoja wa Mataifa. Kuhusu elimu ya Sekondari, wananchi na wadau
wengine wameitikia wito wa Serikali wa kila Kata kuwa na shule ya sekondari. Kwa
sababu hiyo idadi ya shule 3,165
zimejengwa kati ya 2005 na hivi sasa na idadi ya wanafunzi katika shule za
sekondari imeongezeka kutoka 524,325
mwaka 2005 hadi 1,884,272 mwaka
huu.
Tumepanua
sana mafunzo ya ufundi na elimu ya juu. Hivi
sasa nchi yetu ina vyuo vikuu 27 na wanafunzi
waliopo vyuoni humo ni zaidi ya 166,484 ikilinganishwa
na 40,719 wa mwaka 2005. Ili kutoa fursa sawa kwa wanafunzi wote
tumeongeza sana uwezo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili iwape wanafunzi wengi mikopo ya elimu. Bajeti ya Bodi hiyo imeongezeka kutoka
shilingi bilioni 56.1 mwaka 2005
hadi shilingi bilioni 306.0 mwaka
huu. Wanafunzi wanaopata mikopo wapo 93,176 ukilinganisha na 16,345 mwaka 2005. Tutaendelea kuongeza fedha ili tuwafikie
wanafunzi wengi kadri inavyowezekana.
Ndugu
Wajumbe;
Upanuzi
mkubwa wa elimu katika ngazi zote nchini umezua
changamoto mbalimbali kuhusu
ubora wa elimu. Tunazitambua changamoto
hizo kuwa ni pamoja na zile za upungufu wa walimu, hususan wa sayansi; upungufu
wa vifaa vya maabara, vitabu na nyumba za walimu hasa kwenye maeneo ya
vijijini. Tumejipanga vyema kuzitafutia
ufumbuzi na tumeanza kufanya hivyo. Tumeongeza
vyuo vinavyotoa mafunzo ya ualimu ili kuongeza idadi ya waalimu. Bajeti ya elimu ni kubwa kuliko zote ili
kusaidia kutatua tatizo la upungufu wa vitabu, maabara, vifaa vya kufundishia
na nyumba za walimu na mahitaji mengineyo.
Hivi karibuni nilipokuwa Mkoani Singida nimewaagiza Wakuu wa Mikoa na
Wilaya zote nchini kuhakikisha kuwa shule zote za sekondari katika maeneo yao
zinakuwa na maabara ya sayansi katika miaka miwili ijayo.
Afya
Ndugu
wajumbe;
Suala
la afya ya Watanzania tunalipa umuhimu mkubwa sana. Tumeongeza bajeti ya afya
kutoka shilingi bilioni 271 mwaka
2005 hadi shilingi trilioni 1.5 mwaka
huu. Nyongeza hii ndiyo iliyotuwezesha
kutekeleza Sera mpya ya Afya (2007) na Mpango wa Miaka Kumi wa Maendeleo ya
Afya ya Msingi (MMAM) wa kuitekeleza vyema Sera hiyo. Lengo kuu la sera na MMAM
ni kuwapatia Watanzania huduma ya afya iliyo bora katika umbali usiozidi
kilometa tano. Vile vile, ni kuimarisha huduma zinazotolewa katika hospitali za
Wilaya, Mikoa, Kanda na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Katika
mpango huu pia tumeazimia kukabili tatizo la upungufu wa madaktari, wauguzi na
wataalamu wengi. Tunaendelea kupanua
mafunzo ya wataalamu hao katika vyuo vyetu hapa nchini na hata nje ya nchi. Tumejenga na tutaendelea kujenga vyuo vipya, wakati
huo huo tukipanua vilivyopo. Tumeendelea
kujenga uwezo wa kupambana na maradhi makubwa yanayoua watu wengi. Tumeelekeza nguvu zetu kwenye maradhi
yanayoambukiza kama vile malaria, UKIMWI na kifua kikuu na yale yasiyoambukiza kama vile saratani, moyo,
shinikizo la damu na vifo vya kina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa
miaka mitano.
Ndugu
Wajumbe;
Kwa
maradhi yote mafanikio ya dhahiri yanaendelea kupatikana. Maambukizi ya virusi vya UKIMWI yanapungua
kutoka asilimia 8 hadi asilimia 5.7, vifo kutokana na malaria vimepungua kwa asilimia 40 kwa Tanzania Bara na kwa Zanzibar tunakaribia kutangaza
kufutika kwa maradhi hayo. Tumepanua
uwezo wa kutibu maradhi ya moyo ikiwa ni pamoja na kufanya upasuaji wa
moyo. Tumepanua uwezo wa kuchunguza na
kutibu maradhi ya kansa. Tunaendelea
kujenga uwezo wa ndani kwa maradhi tunayopeleka wagonjwa wengi nje na mafanikio
yanaaza kuonekana. Safari ni hatua,
naamini tutafika kwani mwelekeo wetu ni mzuri.
Umeme
na Maji
Ndugu
wajumbe;
Tunaendelea
kupanua uwezo wetu wa kuzalisha na kusambaza umeme nchini. Tumeanza safari ya uhakika ya kupunguza
kutegemea mno umeme wa nguvu ya maji.
Tunapanua umeme utokanao na vyanzo vingine hasa gesi asilia na makaa ya
mawe. Mipango ya kutumia upepo na mionzi
ya jua nayo iko mbioni. Pamoja na hayo
tunayo mikakati ya kupunguza umeme unaozalishwa kwa kutumia mafuta kwa kubadili
mitambo hiyo iweze kutumia gesi asilia.
Hivi
majuzi tu nilizindua ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es
Salaam. Litakapokamilika nchi yetu
itakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati
3,000 na kuung’oa mzizi wa fitina wa mgao na upungufu wa umeme nchini. Tumeendelea kuwekeza katika usambazaji wa
umeme nchini jambo ambalo limetuwezesha kuwapatia umeme kwa asilimia 18.4 Watanzania kutoka asilimia 10 mwaka 2005. Kwa kasi hii naamini tutafikia lengo la asilimia 30 ifikapo 2015.
Kwa
upande wa maji, jitihada za kuwapatia wananchi maji safi na salama zinaendelea
vizuri. Eneo hili lina changamoto kuu mbili.
Kwanza ni ule ukweli kwamba kuna baadhi ya maeneo ya nchi yetu hayana
vyanzo vya maji karibu au hayapati mvua za kutosha au yana ukame. Katika maeneo
ya aina hii upatikanaji wa maji huwa wa shida sana na hivyo kutulazimisha
kujenga miradi ya maji ya bomba kutoka masafa marefu. Changamoto yetu ya pili ni ule uwezo mdogo wa
kifedha kwa miradi mingi inayohitaji pesa nyingi. Mwaka 2006
tulianzisha Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Kufuatia utekelezaji ulio makini wa programu ya sekta ya maji, asilimia 60 ya watu wa vijijini na asilimia 86 ya watu wa mijini wanaopata
maji safi na salama. Ni matumaini yangu kuwa
tutafikia lengo letu la asilimia 65 la
upatikanaji maji kwa vijijini na asilimia
90 kwa mijini ifikapo 2015. Bahati nzuri tunayo miradi ya maji inayoendelea
kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini na itapokamilika tutafikia lengo
letu au hata kulivuka.
Pongezi
kwa Kuchaguliwa
Ndugu
Wajumbe;
Katika Mkutano huu, Ndugu Amani Abeid
Karume, Makamu Mwenyekiti wa Zanzibar na Ndugu Pius Msekwa, Makamu wa
Mwenyekiti wa CCM kwa upande wa Tanzania Bara watastaafu. Ndiyo maana NEC imeamua kuwapendekeza kwenu Dkt.
Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Ndugu
Philip Mangula kuchukua nafasi zao. Napenda kuchukua nafasi hii kwashukuru kwa dhati
Rais Amani Abeid Karume na Mzee Msekwa kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya
kunisaidia kuongoza Chama chetu. Wamekifanyia
Chama chetu mambo mengi mazuri ambayo hatuna budi kuwapongeza na kuwashukuru. Waliendelea kuwa walimu wangu na washauri
wangu kwa mambo mengi ya Chama na nchi.
Nawashukuru sana. Sote tuwatakie
afya njema na maisha marefu. Na tumuombe
Mzee Msekwa asichoke kuandika vitabu ili hazina yake kubwa ya uzoefu na maarifa
iwanufaishe wengi kwa miaka mingi ijayo.
Kwa
viongozi wa Mikoa, Wilaya na Jumuiya pamoja na Wajumbe, nirudie kuwapongeza
nyote kwa kuchaguliwa kwenu. Poleni kwa
magumu ya uchaguzi mliyokumbana nayo.
Sasa uchaguzi umeisha, fanyeni kazi ya kujenga Chama. Tibuni majeraha ya uchaguzi na hasa fanyeni
kila muwezalo kuziba nyufa za uchaguzi na migawanyiko miongoni mwa wanachama na
viongozi. Kumbukeni wosia wa Baba wa
Taifa “Umoja ni Nguvu” Kumbukeni kaulimbiu ya Mkutano wetu huu ya Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi! Kajengeni umoja katika maeneo yenu ya uongozi
kwa maslahi ya Chama chetu na nchi yetu.
Hitimisho
Ndugu
Wana-CCM;
Kwa kuhitimisha naomba nirudie kusema
kuwa tumepata mafanikio ya kutia moyo katika ujenzi wa Chama na utekelezaji wa
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 – 2015.
Bado kazi kubwa iko mbele yetu kwa mambo yote hayo mawili. Tunaitambua na tunayo mipango thabiti ya kutekeleza
majukumu yetu. Nina imani tutafanikiwa
kwa kiasi kikubwa katika kufikia malengo yetu.
Tukiendelea kushirikiana tutafika.
Umoja ni Ushindi! Umoja na
Ushindi!
Baada ya hotuba yangu naomba sasa
nitamke kuwa Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM umefunguliwa rasmi.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki
Tanzania!
Kidumu Chama cha Mapinduzi
Asanteni sana kwa Kunisikiliza
No comments:
Post a Comment