Wednesday, November 21, 2012

campus night UDOM 2012


MKUU WA MKOA Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi amewataka wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu walioko katika mkoa huo kujihoji nafsi zao na kutathimini matendo yao kama kweli ni ya kumpendeza Mungu kwa vile ndiyo yanachangia wao kutotambua umuhimu wa nafasi walizonazo.


Dk. Nchimbi ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akihutubia maelfu ya wanavyuo waliohudhuria Jumuiko la Wanavyuo wa Dodoma (Dodoma Campus Night) lililoambatana na mkesha wa kusifu na kuabudu uliofanyika kwenye ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma.

Jumuiko hilo lilihudhuriwa na wanafunzi zaidi ya 3,500 wa dini mbalimbali kutoka vyuo vikuu vya Dodoma (UDOM), St. John’s, Vyuo vya Mipango, Madini, Mirembe, Hombolo, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na vyuo vya ualimu vya Mtumba na Capital.

Dk. Nchimbi alisema wanavyuo wengi ambao walifaulu kidato cha sita kwa alama za juu (first class) huwa wanaporomoka kimasomo wanapoingia kwenye vyuo vya elimu ya juu kwa sababu hawajiweki sawa kwenye mahusiano yao na Mungu aliyewaumba. “Wanaharibikiwa kwa sababu hawajiweki sawa na Mungu... hawakai pale ambapo Mungu anataka wawe (their right position),” alisema.

“Tunzeni nafasi zenu ambazo Mungu amewapatia... wingi wenu huu katika usiku wa leo hauna maana kama hatutakuwa na uhusiano mwema na Mungu kwani hata shetani ana watu wake na huwa anawapatia mahitaji yote... kila mmoja wenu aanze upya na Mungu”, alisema.

“Tumfikirie Mungu, tuangalie mahusiano yetu na Mungu wetu yakoje na tumuombe atusaidie katika yote tuyatendayo, naye atatujibu kwa sababu Mungu huwa hawekezi kwa hasara bali huwekeza kwa faida,” alisema huku akishangiliwa na wanafunzi waliokuwa wamefurika kwenye ukumbi huo.

Alisema idadi kubwa ya wanavyuo wakishapata fedha za mkopo hutumbua maisha kwenye vilabu vya muziki ambavyo ni maarufu mjini humo kama vile Club 84, Club La Aziz na Maisha Club na hawarudi vyuoni hadi fedha yote imekwisha.

“Mungu alipofanya uumbaji alisema kila alichokifanya ni chema sana. Sasa kama wewe ni kiumbe chema wa Mungu iweje uende kwenye hizo club kuponda maisha, iweje unywe pombe, iweje ufanye uzinzi na uasherati badala ya kukaa chuoni ukasoma, iweje ugome kufanya mtihani hadi upate ‘kibuti’?, alihoji huku akishangiliwa na wanavyuo hao.

Alisema yeye kama mzazi analazimika kuyasema hayo kwa sababu anatambua kuwa watoto wa leo wamezungukwa na mitego mingi. “Hatutaki shetani awachezee, ndiyo maana tunawaonya,” alisisitiza.

Alisema katika kundi kubwa kama hilo wamo viongozi wa kesho na kwamba wasipojihadhari na kuweka mahusiano yao sawa na Mungu kuanzia sasa, watajikuta wanafanana na baadhi ya viongozi nchini ambao wamekabidhiwa dhamana lakini wanakengeuka na kufanya kinyume na matarajio ya wengi.

Akitoa mfano alisema: “Nchi hii wako wasomi wengi lakini wamekaa kiwiziwizi tu, fedha za barabara zikitolewa haziendi kufanya kazi iliyopangwa, wakurugenzi wakipewa fedha za kujenga shule, mabweni au nyumba za walimu, unakuta zinakamilika lakini ziko chini ya kiwango, madaktari nao wanaiba dawa za hospitali kwa kutumia magari ya kubebea wagonjwa.”

“Kama viongozi hawa wangesimama kwenye nafasi zao (right position) haya mambo yangetoka wapi? Mambo ya mikataba mibovu yangetoka wapi? Mnadhani nchi hii ingekuwa maskini? Haiwezekani!” alisisitiza huku akishangiliwa na wanavyuo hao.

Aliwasihi wanavyuo wote watambue nafasi zao na wazitunze nafasi hizo ili wasimkosee Mungu. “Tunzeni nafasi zenu mlizopewa na Mungu na wakati wote jitahidini kusikiliza sauti yake, muone jinsi atakavyowashindia”, alisema.

Mapema, akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kuzungumza na wanafunzi hao, Mchungaji Gerald ole Nguyaine wa Kanisa la ICC –TAG Dodoma alisema wanafunzi walio katika vyuo hivyo ni wababa na wamama wa kesho hivyo hawana budi kumtanguliza Mungu katika yote wayafanyayo.

Naye Mchungaji Gavin Walker kutoka Kanisa la Calvary Christian Fellowship lililoko Columbus, Ohio, Marekani ambaye alikuwa mnenaji mkuu katika mkesha huo, aliwasihi wanavyuo kutambua makusudi ya Mungu ambayo ameyaweka juu yao. “Mungu amekuumba wewe kwa kusudi maalum hivyo ni lazima ujue hilo kusudi”, alisema.

Alisema kwa kutotambua kusudi la Mungu katika maisha yao, wako watu ambao wamejikuta wakitaka kufanana na wengine bila kujua ni kwa nini watu hao wamekuwa hivyo. “Wanatamani nafasi za wengine kwa sababu tu wao ni maarufu, ni waigizaji, ni wacheza sinema ama wasanii...  hapana! Kila mmoja anatakiwa kujua kusudi ka Mungu katika maisha yake,” alisisitiza.

Alisema duniani kuna wakazi zaidi ya bilioni saba lakini wengi kati ya hao wanaishi maisha yasiyotimilika kwa sababu hawamjui Mungu. “Hakuna kitu ambacho Mungu hawezi kukifanya maishani mwetu, tunachotakiwa ni kumuomba tu! Kama ni masomo soma kwa bidii huku ukimtumaini Mungu, nawe utashinda sababu Mungu yuko upande wako,” alisisitiza.

Aliwaasa wawe wavumilivu wawapo vyuoni. “Katika maisha ya chuo jifunze kuwa na saburi. Ukijenga saburi sasa hivi tangu uko chuoni, itakusaidia kuvumilia mengi katika maisha ya mbele baada ya kuhitimu Chuo Kikuu au chuo chochote unachosoma sasa,” alisisitiza. 

No comments: