Baadhi ya Waandishi wa Habari kutoka Vyombo na Mashirika mbalimbali ya Habari hapa nchini wakimsiliza kwa makini Mhe. Waziri Membe. |
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikino wa Kimataifa, Bw. John M. Haule (aliyesimama) wakati akimkaribisha Mhe. Waziri Membe kuzungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani). |
Mmoja wa Wanahabari Bw. Florian Kaijage akiuliza swali wakati wa mkutano wao na Mhe. Waziri Membe. |
Mhe. Waziri Membe akifafanua kwa Waandishi wa Habari kuwa mpaka katika ramani ya Tanzania umepita katikati ya Ziwa Nyasa na si ufukweni kama inavyodaiwa na Malawi. |
Wageni waalikwa na baadhi ya waandishi wakimsikiliza Mhe. Waziri Membe. |
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) amewambia waandishi wa habari kuwa Malawi haiwezi kuipeleka Tanzania
katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ili iamue mgogoro wa mpaka
kwenye Ziwa Nyasa unaozozaniwa baina ya nchi hizi mbili.
Mhe. Membe alibainisha hayo mbele ya Waandishi wa
Habari jijini Dar es Slaam siku ya Jumamosi tarehe 06 Oktoba, 2012.
“Tanzania ni mjumbe wa ICJ lakini bado haijatambua Mamlaka ya Mahakama
hiyo, hivyo Malawi haiwezi kuipeleka Tanzania ICJ isipokuwa Tanzania
inaweza kuipeleka Malawi”, alisema Mhe. Membe.
Mhe. Waziri aliitolea wito Malawi irudi katika meza
ya majadiliano na kuiomba Serikali ya nchi hiyo kutuma wawakilishi katika
kikao walichokubaliana kufanyika Dar es Salaam kuanzia tarehe 07 - 10
Oktoba, 2012.
Kikao hicho kinakusudia kupendekeza msuluhishi ambaye
atakubalika na pande zote baada ya kubainika kuwa Tanzania na Malawi
zenyewe hazitaweza kusuluhisha mzozo huo.
Mhe. Waziri aliwafahamisha waandishi kuwa alipokea
kwa mshtuko taarifa kwamba Malawi haitashiriki katika kikao kilichopangwa
kufanyika Dar es Salaam kwa hoja kuwa lazima Serikali ya Tanzania itoe
maelezo ya kina kuhusu boti ya kijeshi iliyoonekana kufanya doria kwenye
Ziwa Nyasa ambayo inasemekana kuwaletea hofu kubwa wakazi wa maeneo
ya Ziwa kwa upande wa Malawi.
Aidha, Malawi inataka kupatiwa maelezo
kuhusu toleo jipya la Ramani ya Tanzania lililotolewa na Mamlaka za
Tanzania ambayo inaonyesha mpaka baina ya nchi hizo mbili umepita katikati
ya Ziwa Nyasa.
Akitolea ufafanuzi masuala hayo, Mhe. Membe alisema
kuwa toleo hilo jipya lilikuwa na lengo la kuionyesha Mikoa mipya minne
na Wilaya mpya 19 katika ramani ya nchi, na kuonyesha mpaka kupita katikati
ya Ziwa, hilo si jambo jipya kwani ndivyo ramani ya nchi yetu ilivyokuwa
katika matoleo yote manne yaliyotolewa na Serikali kabla na baada ya
uhuru.
Kuhusu boti ya kijeshi kufanya doria kwenye Ziwa
Nyasa, Mhe. Waziri alisema taarifa hizo sio sahihi, ila kinachofanyika
ni doria ya kawaida ambayo inaendeshwa na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo
na Uvuvi kuwasaka wavuvi haramu na wale wanaotumia zana za uvuvi zilizopigwa
marufuku.
Mhe. Waziri aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali
ya Tanzania inapenda kuona mgogoro huo unamalizika katika kipindi cha
Serikali ya Awamu ya Nne inayongozwa na Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete
na kitendo cha Malawi kutishia kugomea majadiliano hakitarudisha nyuma
dhamira ya Serikali.
Alisema Serikali imejipanga vyema kuhakikisha kuwa
inakuwa na hoja za kisayansi na kisheria ili ishinde katika mgogoro
huo. Moja ya mikakati ya Serikali imeunda Kamati tatu ambazo zimeshaanza
kazi na kazi yao inaendelea vizuri. Kamati hizo moja inahusika na utafutaji
wa nyaraka kuhusu Ziwa Nyasa, ya pili inahusika na masuala ya kisheria
na ya tatu inahusika na masuala ya majadiliano.
Alidokeza kuwa katika kufuatilia kesi zilizohukumiwa
na ICJ hakuna nchi iliyodai umiliki wa ziwa lote au mto uliopo mpakani
baina ya nchi mbili ilishinda kesi. Hivyo, aliwataka Watanzania wasiwe
na wasiwasi kwani Serikali yao itaibuka mshindi katika mgogoro huo.
Alihitimisha mazungumzo yake kwa kuwataka Wananchi
wanaoishi kando ya Ziwa Nyasa kufanya shughuli zao kama kawaida pasi
na kuhofia chochote kwani hakuna tishio la vita kabisa baina ya Tanzania
na Malawi.
No comments:
Post a Comment