Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete anaanza
ziara rasmi ya Kiserikali ya siku nne katika Taifa la Kifalme la Oman, ikiwa ni
ziara ya kwanza ya Kiserikali kufanywa na Rais wa Tanzania katika nchi hiyo.
Rais
Kikwete na ujumbe wake ameondoka mjini Dar es Salaam asubuhi ya leo, Jumatatu,
Oktoba 15, 2012, kwenda Oman kuanza ziara hiyo inayofanyika kwa mwaliko wa
Kiongozi wa Ufalme wa Oman, Mfalme Qaboos bin Said, ambaye atakuwa mwenyeji
wake kwa siku zote nne.
Kwenye
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muscat, Rais Kikwete anatarajiwa kulakiwa na Waziri
wa Mambo ya Nje wa Oman, Mheshimiwa Yousef
bin Abdullah bin Alawi ambaye ataandamana naye hadi Jumba la Muscat Gate
ambako Rais atapokelewa na Mfalme Qaboos. Kutoka hapo wataandamana hadi Kasri
ya Kifalme ya Al Alam ambako atapokelewa rasmi kwa heshima zote za Kiserikali.
Shughuli
kubwa ya jioni ya leo ya Mheshimiwa Rais itakuwa ni kufanya mazungumzo rasmi ya
Kiserikali kati ya Serikali za Tanzania na Ufalme wa Oman na pia kuhudhuria
dhifa rasmi ambayo Mfalme Qaboos atamwandalia mgeni wake kwenye Kasri ya Al
Alam.
Kesho,
Jumanne, Oktoba 16, 2012, Rais Kikwete atatembelea Jumba la Makumbusho la
Majeshi ya Ulinzi ya Oman, atafungua Mkutano wa Wafanyabiashara wa Tanzania na
Oman, atashuhudia utiaji saini makubaliano ya mikataba miwili kati ya nchi hizo
mbili, ukiwamo ule wa kuundwa kwa Baraza la Biashara la Tanzania na Oman na ule
wa Kuendeleza na Kulinda Uwekezaji katika nchi hizo mbili.
Jioni,
Rais Kikwete atatunukiwa nishani ya juu kabisa ambayo Ufalme wa Oman hutoa kwa
viongozi wa nchi za nje ya First Order Medal kwenye Chakula
Maalum cha Usiku kitakachoandaliwa na Mfalme Qaboos kwa heshima ya Rais
Kikwete.
Rais
Kikwete na ujumbe wake pia utakutana na kuzungumza na Watanzania wanaoishi Oman
katika mkutano utakaofanyika kwenye Hoteli ya Kifalme ya Al Bustan.
Hii
itakuwa mara ya pili kwa Mheshimiwa Kikwete kutembelea Oman. Aliitembelea nchi
hiyo mara ya kwanza mwaka 1998, wakati huo akiwa ni Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
15
Oktoba, 2012
No comments:
Post a Comment