Tuesday, September 11, 2012

WATANZANIA TUNA MENGI YA KUJIFUNZA KUTOKA MASHINDANO YA VILEMA –PARALIMPIKI 2012

Na Freddy Macha
Mkuu wa msafara wa wanamichezo walemavu, bwana Johnson Meela amesema ingawa hatukushinda medali yeyote lakini tumepata elimu na maarifa mengi kutokana na tukio hili la majuma mawili, mjini London.
Timu ya Tanzania iliwakilishwa na Zaharani Mwenemti aliyeshiriki katika utupaji kisahani (discus) na tufe (shot-put). Mwenemti aliyezaliwa Dar es Salaam alifuatana na kocha wake, wote wawili walemavu wa mguu mmoja, John Ndumbaro na katibu mkuu wa Paralimpiki Tanzania, Iddi Kibwana.
Meela mwenye ulemavu wa miguu yote miwili aliendelea:
“Mashindano ya London mwaka huu yametangazwa na kutoa mwamko mkubwa sana kuliko yeyte yale ya miaka ya nyuma. Mashindano haya yalikuwa ya kusisimua. Wahudhuriaji wengi sana wamejaza viwanja kila siku ya michezo. Hii imedhihirisha kuamka kwa mtazamo wa mamilioni ya wanadamu na kuwaelewa walemavu. Sisi Watanzania tuna mengi ya kujifunza. Uingereza imesifiwa sana kutokana na juhudi zake.”
Mashindano ya walemavu (Paralimpiki) mwaka huu yalivutia wanamichezo na watazamaji wengi kuzidi yote toka ilipoanzishwa rasmi mwaka 1960. Vyombo vya habari vilitangaza zaidi ya watu milioni saba walioingia viwanjani.
Neno “paralympic” ni muungano wa “paralyse” (kupooza viungo au mwili) na “olympic”lilianza kutumika rasmi wakati wa michezo ya Los Angeles mwaka 1984...Uuandaji huu wa maneno unaitwa “portmanteau” na hutumika katika lugha mbalimbali. Katika Kiswahili mathalan tuna “lele” na “mama” (lelemama); “rununu” (sauti kutoka mbali) na “maninga” (macho yaonayo mbali) kuunda “runinga” (televisheni) na “Tanzania” (Tanganyika na Zanzibar).
Toka 1988, (Seoul, Korea Kusini) michezo ya ulemavu imefanywa sambamba na Olimpiki na kuongezeka ki-dadi. Mwaka 1960 mashindano ya Italia yalikuwa na wanariadha 400 toka nchi 23; Atlanta (1996) wanariadha vilema walikuwa 3,500 (mataifa 104) na mwaka huu idadi imefikia 4,294 (nchi 104).
Shughuli hii ilianzishwa na mganga wa Kiyahudi, Profesa Ludwig Guttman kusaidia kurejesha hali ya walemavu hasa waliopooza uti wa mgongo, mwaka 1948. Kadri miaka ilivyokwenda shabaha hiyo imepanuka zaidi. Wahusika wa michezo walitangaza mwaka 1996 kwamba nia ya “paralympic” ni kujenga mwamko kuhusu vilema, usawa na uwezo wa walemavu.
“Ushindani wa michezo unafuta makovu kuhusu ulemavu na kuonyesha uwezekano wa hali ya juu,” walisema.
Bwana Johnson Meela alimalizia kusema kwamba uwekezaji zaidi unatakiwa kusaidia mustakabal wa wanamichezo walemavu na kuonya kwamba nchi zilizofanya vizuri London ni zile zilizokuwa na uchumi mzuri. Alitaja nchi Afrika Kusini, Tunisia, Morocco, Misri and Algeria, barani Afrika na Uingereza, Marekani na China kama mifano ya mataifa yaliyoongoza na kufanikiwa duniani kutokana na uwekezaji huo.

http://www.freddymacha.com

 Iddi Kibwana-Afisa Utawala
 Mwandishi nikiwa na Meela
 Vipofu toka Argentina walioshiriki katika soka wakiwa na kochja wao-katikat
 Watazamaji wa mataifa mbalimbali wakielekea viwanjani kushangilia walemavu
Zaharani Mwememti akiwa na wasaidizi wakujitolea Olimpiki ya London 
Johnson Meela akiwa na wahudumu waalioichangamkia Tanzania toka Kongo na Nigeria. Picha zote na Freddy Macha

No comments: