Na Mashaka Mhando,Horohoro
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Luteni (Mstaafu) Chiku Gallawa, amemkamata na kumweka ndani Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mwakijembe kilichopo mpakani mwa Kenya na Tanzania, Francis Mtiambo, kwa madai ya kushindwa kulinda rasilimali za Taifa.
Mkuu huyo wa mkoa wakati akimkamata mwenyekiti huyo alisema ana mweka ndanikwa kushindwa kusimamia na kutekeleza agizo lake la kuzuia agizo lake la kusimamisha uvunaji wa miti na uchomaji mkaa alilolitoa Julai mwaka huu kufuatia baadhio ya watu kuiharibu misitu hasa katika wilaya za Handeni na Kilindi kwa kisingizio cha kuandaa mashamba.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, anatuhumiwa kwamba ameshindwa kusimamia zoezi la ukataji wa miti aina ya mipingo ambayo imekuwa ikikatwa kwa wingi katika kijiji hicho na kuchongwa vinyago vinavyouzwa nchi jirani ya Kenya pamoja na ukataji wa miti ya mikarambati na mikumbulu ambayo inachomwa mkaa na kuuzwa huko nje ya nchi.
Mkuu huyo wa mkoa alifanya ziara ya ghafla na kamati yake ya ulinzi na usalama kwenye wilaya Mkinga kukagua shughuli za uchomaji mkaa unaofanywa mpakani ambapo alipita katika wilaya ya Kwale iliyopo nchini Kenya alipopewa askari wawili wa Kenya aliongozana nao hadi katika kijiji hicho cha Mwakijembe baada ya kukagua mawe yanayotenganisha mpaka wa nchi hizio.
Akiwa mpakani huko mkuu huyo wa mkoa alikagua jiwe lililoandikwa namba T13-3K na jingine T17-1K, pia alisikitishwa na uharibifu mkubwa uliofanywa wa ukataji wa miti na uchomaji wa mkaa katika eneo la mpaka wa Tanzania huku miti ya sehemu ya Kenya ikiwa haijaguswa hatua ambayo inaonekana kwamba Watazania wanahujumu miti upande wao lakini wenzao wa Kenya wanatii sheria ya utunzaji wa maziongira.
Pia alishuhudia baadhi ya magari ya Kenya yakiwa yamesheheni magunia ya mkaa yakitokea upande wa Tanzania hatua ambayo ilimsikitisha ikiwemo kushindwa kuyakamata na asakri wa Tanzania kwa kuwa aliyakuta yakiwa nchini Kenya ikiwemo kushuhudia makambi yanayotumika kuchoma mkaa na kusafirishwa nchini humo.
mmoja ya wananchi wa kijiji cha Magojoni kilichopo wilaya Kwale nchini Kenya Bw. Rumba Dunya alimweleza Mkuu wa mkoa kwamba wananunua magunia ya mkaa katika kijiji hicho cha Mwakijembe kati ya sh. 400 na sh. 450 za Kenya ambazo ni sawa na shilingi 8,500 za Tanzania huku kijiji kikipata ushuru wa sh. 30 za Kenya pindi wanaponunua magunia hayo ya mkaa.
Diwani wa kata hiyo Bw. Ramadhani Madika alipopulizwa na mkuu wa mkoa ni kwanini wanashindwa kuzuia ukataji huo na kuacha rasilimali ya Taifa ikiendelea kuhujumiwa, alisema kwamba hawawezi kuzuia uhalifu huo wa ukataji wa miti na uchomaji, kutokana na woga waliokuwa nao wa kuuwawa na watu wanaojishughulisha na uchomaji huo.
"Mheshimiwa mkuu wa mkoa, siwezi kuzungumza hapa kutokana na mazingira haya, hii ni kamati yenu ya ulinzi na usalma na hapa pana watu wengi, lakini tunaogopa kuuwawaa mimi siwezi kufa kwa kulinda suala hili waacheni wakate miti, tunaogopa kufa," alisema diwani huyo alisema.
Baada ya kueleza maelezo hayo mkuu huyo wa mkoa alisema "Kama diwani unaogopa kufa huwezi kuwa kiongozi jiuzulu basi utoe nafasi kwa watu wengine wasiogopa kufa kwa kulinda rasilimali za Taifa, ni bora tuitishe uchaguzi mwingine lakini si wewe uliyeapa kwamba utailinda nchini hii halafu unasema unaogopa kufa, tena unasema huoni aibu," alisema Mkuu huyo wa mkoa.
Wakati Tanzania msitu huo wa Mwakijembe ukiwa unahudhunisha kwa kuvunwa miti na kupelekwa Kenya kwa ajili ya mkaa na kuchongea vinyago ikiwamo kusafirishwa magogo nje,msitu huo huo kwa upande wa Kenya msitu unapendeza kutokana na kuwa na miti yote ya asili na sababu iliyoelezwa ni kwamba kuna sheria kali ya kulinda maliasili hiyo.
Akiwa upande wa Kenya,Raia wan chi hiyo walimweleza Mkuu huyo wa Mkoa kwamba, hawathubutu hata kukata mti mmoja kwenye ardhi yao kwa sababu ya kuogopa sheria kali badala yake wanaingia Tanzania kuvuna kwa fujo miti na mkaa na kuuvusha nchini kwao.
Mmoja wa raia hao wa Kenya ambaye ni dalali wa mkaa unaovunwa katika msitu wa Mwakijembe upande wa Tanzania,Rumba Dunya alimweleza Mkuu huyo wa Mkoa kwamba uvunaji kwa msitu huo unafanikishwa kwa kiasi kikubwa na viongozi wa vijiji vilivyopo Kata ya Mwakijembe ambao hutoa vibali vya uvunaji.
Dunya ambaye anaishi Kijiji cha Kitongoji cha Mwerere Wilaya ya Kwale nchini Kenya alisema ndani yam situ huo wa Mwakijembe kuna kambi nyingi za uvinaji wa magogo ya kuchongea vinyago na mkaa ambazo zinafadhiliwa na wafanyabiashara waliopo Mombasa.
“Kazi kubwa ya uvunaji wa miti katika msitu wa Mwakijembe inafanywa na wananchi wa Tanzania ambao baada ya kuvuna hutayarisha kwa ajili ya wafanyabiashara kutoka Mombasa kwenda kuchukua shehena kwa shehena na kisha kuivusha”alisema Naomi Nzuma mkazi wa Kijiji cha Kitwamba Wilaya ya Kwale.
Wakazi hao wa Kenya walisema kuwa mkaa unaofikishwa Mombasa hutumika kwa matumizi ya majumbani lakini shehena nyingi husafirishwa katika nchi za nje huku magogo yakipelekwa nchi za Uarabuni na Ulaya.
Walisema gunia moja la mkaa likiwa porini hapo huuzwa kwa bei y ash 6,660 lakini ukifikishwa katika mji wa Mombasa unauzwa sh 21,600.
“Huku kwetu Kenya kuna sheria kali ya kutuzuia kuvuna msitu,ndiyo maana hakuna anayethubutu kukata miti lakini kwa sababu upande wa Tanzania hakuna sheria ndiyo maana wengi wanakimbilia huko”alisema Naomi
Mkuu huyo wa Mkoa na msafara wake walisafiri mwendo wa zaidi ya kilomita 300 msituni kukagua yalikowekwa mawe ya kuonyesha alama ya mpaka kati ya Tanzania na Kenya pamoja na makambi ya kuchomea mkaa na mawe ya mipaka ambapo pia alikamata maroli yaliyokuwa yakisafirisha bidhaa hizo za maliasili.
Kufuatia taarifa alizopata kutoka kwa wakazi wa vijiji vilivyopo upande wa Kenya ,Gallawa aliamuru kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mwakijembe,Francis Mtiambo kutokana na kukaidi amri iliyotolewa na Mkuu huyo wa Mkoa miezi miwili iliyopia ya kupiga mafuruku utoaji wa vibali vya kuvuna na kusafirisha mkaa na bidhaa zote za malisili ya misitu.
Askari polisi wa Kenya waliokuwa kwenye msafara huo wa mkuu wa mkoa wa Tanga aliyekwenda kukagua hali ya uvunaji wa miti na uchomaji wa mkaa.
gari aina ya fuso mistubishi lenye namba KBH 985 J likiwa limesheheni mkaa kutoka Tanzania likipelekwa Mombasa Kenya.
Mkuu wa mkoa Chiku Gallawa akiwa na kamati yake ya ulinzi na usalama wakitazama jiwe linalotenganishwa mpaka wa Kenya na Tanzania.
Mkuu wa mkoa wa Mkoa wa Tanga Chiku Gallawa akitazama gunia za mkaa zikiwa zimewekwa kwenye maguni tayari kusafirishwa kupelekwa nchini Kenya hasa katika mji wa Mombasa. |
Mkuu wa mkoa Chiku Gallawa akitazama jiwe ambalo lipo katika mpaka lakini eneo hilo kuna majani mengi. Kushoto ni Mwandishi wa habari hizi
Gari lililosheheni mkaa likiwa limekamatwa na askari polisi
Askari polisi wakimsindikiza kwenda kuaga kwa mkewe Mwenyekiti wa kijiji cha Mwakijembe Bw. Francis Mtiambo aliyekamatwa na Mkuu wa mkoa wa Tanga, Luteni (mstaafu) Chiku Gallawa kufuatia kumtuhumu kushindwa kusimamia rasilimali ya Taifa.
No comments:
Post a Comment