Mimi nimefuatana na Mch. Dr. Emmanuel
Kandusi ambaye ni mwaathirika, muhanga na manusura wa saratani ya tezi dume
(prostate cancer) ili niongee nanyi machache. Dr. Kandusi baada ya kuugua
gonjwa hilo, gonjwa linalowasibu wanaume tu, akiwajali wanaume wenzake, aliona
kukaa kimya si faida “alivunja ukimya”
na kuanza kutoa elimu na kuwasaidia wanaume wenzake katika kukabiliana na
saratani ya tezi dume. Saratani ni gonjwa ambalo limepamba moto dunia nzima
lakini sisi huku Afrika tunaathirika sana. Zipo aina zaidi ya 100 za saratani,
lakini saratani ya tezi dume ndio saratani hatari sana inayowapata wanaume tu
na hasa kuanzia hata miaka 40 na kuendelea.
Kati
ya nukta ninazoweza kuzitaja kwa haraka haraka ni hizi:
·
Katika wanaume 5, mmoja atapata saratani
ya tezi dume;
·
Kila dakika 5 wanaume
wawili wanagunduliwa wana saratani ya tezi dume;
·
Katika wanaume 100
wanaogundulika na saratani za aina mbali mbali, 25 wanakuwa na saratani ya tezi
dume;
·
Mtu ambaye ana ndugu wa
karibu (baba, babu, kaka etc) yuko katika hali hatarishi kupata saratani ya
tezi dume;
·
Saratani ya tezi dume
inaua mtu mmoja kila dakika 13;
·
Mbaya zaidi saratani ya
tezi dume huwezi kuigundua mwanzoni. Inachukua miaka zaidi ya 8 ndipo dalili
zinmapoanza kujitokeza.
Kwa
uchache ukiangalia haya niliyogusia utaona kuna umuhimu mkubwa kutoa elimu kwa
jamii ili akina baba na hata akina mama wajue hali hatarishi, dalili za
saratani ya tezi dume na hasa umuhimu
wa kufanya uchunguzi wa tezi dume kwa wanaume wote ikibidi kuanzia miaka 40.
Kama ilivyo kwa saratani nyingi, saratani ya tezi dume ikigundulika mapema inatibika kwa urahisi zaidi.
Sisi wa MAN
Magazine, gazeti linalochapisha maswala mengi yanayomhusu mwanaume,
tulivutiwa tokea mwanzo wa Tanzania 50 Plus Campaign na tukaona wadau wa kampeini hii na
wadau wa MAN Magazine ni wamoja – WANAUME. Tumekuwa mstari wa mbele kuchapisha
makala nyingi toka Tanzania 50 Plus Campaign na wasomaji wetu wame-appreciate
sana elimu hiyo. Pia tumekuwa kila tunapoweza kuchangia Tanzania 50 Plus Campaign
katika hali na mali.
Namalizia kwa kutoa changamoto kwa wenzangu waandishi wa
habari, lishikieni bango gonjwa hili – saratani na hususani saratani ya tezi
dume. Serikali iweke mikakati mtambuka kuhusu saratani na kuitekeleza kwa
vitendo. Wafanyabiashara na makampuni mbalimbali yaunge mkono kampeini zote za
saratani – za matiti, shingo ya uzazi, ngozi nk na pia saratani ya tezi dume
inayoendeshwa na Tanzania 50 Plus Campaign. Gonjwa hili si la kitabaka, leo
kwangu kesho kwako !
Ahsanteni kwa kunisikiliza !
Dismus Massawe
Mkurugenzi
Mtendaji
MAN
Magazine
September
28, 2012 AD
No comments:
Post a Comment