Monday, September 3, 2012

KAIMU MKURUGENZI MKUU MPYA WA MAKUMBUSHO YA TAIFA AKUTANA NA WAFANYAKAZI WA MAKUMBUSHO NA NYUMBA YA UTAMADUNI JIJINI DAR

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Bi Eliwasa Maro akiongea na Wafanyakazi wa Makumbusho zilizopo Dar es Salaam, pembeni yake ni Mkurugenzi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dkt Paul Msemwa.
Mtawala Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Bw Fredrick Mwakalebela, akiongea na Baadhi ya Wafanyakazi wa Makumbusho ya Taifa Dar es Salaam wakati wa kumkaribisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu aweze kongea na wafanyakazi hao.
Pichani wapili kutoka kushoto ni Dkt Amandus Kweka akufafanua jambo juu ya Mifupa ya Mijusi (Dinosaur) iliyopo Nchini Ujerumani, wengine ni wafanyakazi wa Kijiji cha Makumbusho na wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam.

Na Sixmund J. Begashe wa Makumbusho ya Taifa.

Wafanyakazi wa Makumbusho ya Taifa Nchini wameshauriwa kufanya kazi kwa bidii kwa maendeleo ya Taasisi.

Hayo yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Nchini Bi, Eliwasa Maro alipokutana na wafanyakazi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam na wale wa Kijiji cha Mkumbusho kwa lengo la kujitambulisha kwao na kuwafahamu wafanyakazi wa Makumbusho hayo.

Bi Maro alisisitiza kuwa ushirikiano, uadilifu na uchapakazi utaisaidia Taasisi kupiga hatua kubwa kufikia malengo yaliyo wekwa. Ili kufikia malengo ya Taasisi kila mfanyakazi anapaswa kuitumikia nafasi yake vyema kwa kutumia ujuzi wa ziada ambapo ana amini kuwa kila mfanyakazi anauwezo wa kufanya hivyo.

Katika suala zima la Mawasiliano, Bi Maro aliwataka wafanyakazi wote wafuate taratibu zinazo stahili za kimawasiliano. Alisisitiza ngazi stahili zifuatwe na wahusika wakuu watatue matatizo yaliyo chini ya uwezo wao.

Pia aliwakumbushia wafanyakazi maagizo ya Waziri wa Malihasili na Utalii Mh Khamis Suedi Kagasheki (MB) aliyoitoa Bungeni wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara kwamba si vyema kwa mfanyakazi kuvujisha siri za ofisi kwa lengo la kutaka kutatua matatizo ya Taasisi ama tatizo binafsi bila kuangalia ukubwa wa madhara yanayo weza kutokea.

Hivyo, Bi Maro alisisitiza umuhimu wa kila mmoja kutathmini maana ya methali “Mvunja nchi ni Mwananchi” katika utendaji wake.

Akizungumzia suala la Masalia ya Mijusi yaliyo hifadhiwa Nchini Ujerumani, Bi Maro aliwaomba wataalam wa Makumbusho kutoa elimu ya kutosha kwa jamii kuhusu masalia ya Mjusi huyo kwani kuna ukweli kuwa watanzania wengi wana ufahamu mdogo. Alisema kuwa suala hili linahitaji kufanyiwa kazi kwa kina.

Akitoa mfano wa ugumu alioupata kusafirisha masalia ya mifupa yenye umri mdogo wa chini ya miaka milioni mbili toka Nairobi, Mkuu wa Idara ya Mikusanyo wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam Dkt Amandus Kweka alisema, “Masalia hayo ni mifupa Mawe (Fossil Bones) ya zaidi ya miaka milioni 200 hivyo usafirishaji wake unahitaji uangalifu mkubwa kwani ikipata nyufa au kupasuka ni vigumu kuirekebisha na kuwa kwenye hali yake ya awali” Dkt Kweka pia alisema katika kukamilisha umbo la mjusi huyo vimeongezwa vipande vya mifupa ya kutengenezwa.

Wakizungumza kwa nyakati tofati, baadhi ya wafanyakazi walioudhuria mkutano huo walimshukuru Kaimu Mkurugenzi Mkuu kwa kukutana nao na kubadilishana uzoefu na kwa namna alivyoanza kushughulikia matatizo machache makubwa kwa muda mfupi tangu ateuliwe kukaimu nafasi hiyo.

“Nimefurahi sana kuona sasa kuna mapinduzi ya kiuongozi katika Makumbusho ya Taifa kwani ni mara ya kwanza tangu makumbusho yaanzishwe nafasi hii ya Juu kushikwa na Mwanamke, akina mama tunaweza, si unaona ni muda mfupi sana tangu Mama Maro ashike nafasi hii na ameleta mabadiliko na wafanyakazi sasa wana ari ya kazi” alisema Afisa Elimu wa kwanza mwanamke wa Makumbusho Tanzania,Bibi Lusina Shayo.

Makumbusho ya Taifa ni Shirika la Serikali lenye wajibu wa kutafiti, kukusanya, kuhifadhi na kuielimisha jamii juu ya mambo yote yanayo thaminiwa na jamii.

No comments: