ZIARA YA KIKAZI YA KAMATI YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA(NUU) UMOJA WA MATAIFA
Na Mwandishi Maalum
Wabunge wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wameanza ziara yao ya kikazi na mafunzo hapa Umoja wa Mataifa. New York
Wabunge hao watano wakiongozwa na mwenyekiti wa Kamati, Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Edward Lowassa ( Mb), waliwasili Jijini New York siku ya Alhamisi, ambapo siku ya Ijumaa walianza ziara yao kwa kuutembelea Ubalozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Wabunge hao ni Mhe. Beatrice Shelukindo, Mhe. Rachel Masishanga, Mhe. Khalifa Khalifa na Mhe. Vita Kawawa.
Akielezea madhumuni ya ziara hiyo, baada ya kutakiwa kufanya hivyo na mwenyekiti wa Kamati. Mhe. Beatrice Shelukindo aliwaeleza maafisa wa Ubalozi kwamba, ziara yao ilikuwa inalenga pamoja na mambo mengine, kujifunza na kupata uelewa wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na Balozi za Tanzania nje ya nchi.
Aidha akasema ziara hii ni ya kwanza ya aina yake kufanywa na kamati hiyo na kwamba itawapa fursa ya, siyo tu kufahamu kazi zinazofanywa na Balozi, lakini pia namna bora ya kuishauri serikali hususani katika kuangalia ni kwa namna gani bora zaidi ambapo balozi za Tanzania zinaweza kuchangia katika kukuza pato la taifa, lakini pia kutekeleza kwa ufanisi na tija sera ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi.
Halikadhalika wabunge hao, kupitia ziara hiyo wanataka kujifunza mafanikio ya yatokanayo na kazi za kila siku zinazofanywa na Balozi hizo, changamoto wanazokabiliana nazo, na maeneo gani yanayotakiwa kutiliwa mkazo au kutafutiwa ufumbuzi.
Wabunge wakiwa hapa New York watapata pia fursa ya kutembelea na kukagua majengo yanayomilikiwa na serikali
Wakiwa ubalozini hapa, walipata fursa ya kuwasikiliza maafisa wa Ubalozi wanaosimamia Kamati Sita za Balaza Kuu la Umoja wa Mataifa. Wakiongozwa na Kaimu Balozi, Dkt. Justin Seruhere kila mmoja alitoa muhtasari wa kamati anayoifanyia kazi, akielezea mafanikio na changamoto wanazokabiliana zao wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Baada ya kipindi cha maswali na majibu, wabunge hao pia walipata fursa ya kwenda Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ambapo walihudhuria majadiliano ya mikutano miwili mikubwa inayoendelea kwa sasa hapa Umoja wa Mataifa.
Mikutano waliyohudhuria wabunge hao ni ule wa mchakato wa maandalizi ya Mkataba wa Biashara ya Silaha ( ATT), na Mkutano wa Baraza la Umoja wa Mataifa linalohusika na Masuala ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii ( ECOSOC). Mikutano hii imeanza mwanzoni mwa wiki hii.
Wakiwa katika ukumbi wa mkutano wa majaliano ya ATT, wabunge waliweza kujionea na kufuatilia namna ambavyo majadiliano yalivyokuwa yakifanyika, huku kila nchi ilivyokuwa ikiwasilisha hoja huku zikiteteza misimamo na maslahi ya nchi zao.
Mkutano wa nchi wanachama kuhusu Mkataba wa Biashara ya Silaha Duniani, ambao Tanzania inashiriki kikamilifu na kufuatilia kwa karibu masuala ya udhibiti wa silaha ndogo ndogo na za kati . Silaha ambazo zimekuwa na madhara mkubwa kwa maisha na uhai wa watu barani Afrika.
Mkutano huu ambao ni na nyeti dhumuni na lengo lake kuu ni kuandaa Mkataba wa kisheria utakaoratibu na kudhibiti biashara ya silaha Duniani.
Tanzania katika mkutano huu ukiacha maafisa wa ubalozi, inawakilishwa na ujumbe mzito wa wataalamu kutoka, Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambao ni Brigedia Generali Dkt. Charles Muzanila, na Brigedia Generali Venance Mabeyo, kutoka Jeshi la Polisi ni Kamishina Msaidizi, Esaka Mugasa, Bw. Theobald Kazora kutoka Ofisi ya Rais ( Ikulu) na Bw. John Kinuno, wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa Upande wa Mkutano wa katika mkutano wa ECOSOC ambao ajenda yake kuu ni uhuishaji na uchagiaji wa ajira kwa vijana ujumbe wake unaongozwa na Mhe. Gaudentia Kabaka(Mb) Waziri wa Kazi na Ajira, ujumbe ambao unaojumuisha pia wawakilishi kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
----------------------------------------------------------
Wabunge wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ( NUU) ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamemuelezea Naibu Katibu Mkuu Dkt. Asha- Rose Migiro, ambaye amemaliza muda wake wa utumishi UN kama hazina ambayo Tanzania na watanzania wanatakiwa kuiezi na kuitumia.
Hayo yameelezwa kwa nyakati tofauti na wabunge wa kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati , Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Edward Lowassa wakati walipokutana na kufanya mazungumzo na Dkt. Asha- Rose Migiro jijini New York siku ya Ijumaa.
Wabunge hao ambao ni Mhe. Khalifa Khalifa, Mhe. Vita Kawawa, Mhe. Beatrice Shelukindo na Mhe. Rachel Masishanga, wapo Jijini New York kwa ziara ya kikazi na mafunzo .
Wabunge wakabainisha kwamba litakuwa jambo la ajabu na la kushangaza kama watanzania watashindwa siyo tu kutambua mchango mkubwa wa Asha- Rose Migiro bali hata kuchota na kumtumia kupitia uzefu na utalamu aliojipatia akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja.
Aidha Wabunge hao walitumia nafasi ya mazungumzo hayo kumpongeza Asha-Rose Migiro, kwa kumaliza salama jukumu hilo zito na kwamba ameiwakilisha vema Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla.
“ Kwa niaba ya wajumbe wa Kamati yangu, tukupongeze kwa kumaliza salama jukumu hili zito na kubwa, kwa hakika umetuwakilisha na umeipeperusha vema bendera ya Tanzania na umeliwakilisha vema Bara la Afrika na waafrika” akasema Mhe. Lowassa.
Wakasema kwamba ni matarajio yao kuwa ushirikiano ambao dkt. Migiro alikuwa akiutoa wakati akiwa Naibu Katibu Mkuu atauendeleza na maslahi ya taifa na nasa sasa baada ya kumaliza wadhifa huo na kurejea nyumbani.
Kwa upande wake, Dkt. Migiro amewashukuru wabunge hao kwa pongezi zao na kwamba kama mtanzania daima atakuwa tayari kutoa mchango wake pale atakapohitajika kufanya hivyo.
Aidha amesema amefurahishwa na uamuzi wa Kamati hiyo wa kufanya ziara za kikazi na mafunzo katika Balozi za Tanzania nje ya nchi.
Akasema ziara hizo si tu zinawapatia uzoefu na utambuzi ya kile kinachojiri katika ngazi ya kimataifa, lakini inaweka katika nafasi nzuri ya kuwa wachangiaji wazuri linapokuja suala la uhusiano wa kimataifa, ulinzi na usalama.
Aidha amewashuri wabunge wa Kamati hiyo kujijengea utaratibu wa kuhuhudhuria mikutano na mijadala ya wazi inayofanyika hapa Umoja wa Mataifa hasa ile inayohusu masuala ya ulinzi na usalama.
Amewataka pia wabunge wa kamati hiyo, kujijengea uwezo na ufahamu kuhusu ushiriki wa Tanzani katika Operesheni za Kulinda Amani zinazosimamiwa na Umoja wa Mataifa.
Akabainisha kwamba wabunge wa Kamati hiyo wanapashwa pia kufahamu nini kinachoendelea katika operesheni hizo, hali ya wanajeshi wa Tanzania waliomo katika opereshi hizo wakiwamo Polisi na Askari Magereza na kubwa zaidi kujifunza manufaa makubwa ya kiulinzi na kiuzoefu yanayotokana na wanajeshi wa Tanzania kushiriki operesheni hizo.’
Akawaeleza wabunge hao kwamba ingawa Tanzania imeingia katika siku za hivi karibuni katika operesheni za ulinzi wa amani , lakini wanajeshi wake, jeshi la polisi na askari magereza wamejizolea sifa kemkem kutokana na uhodari, nidhamu na utendaji wao makini katika jukumu hilo.
Akielezea nini ambazo amejifunza katika utumishi wake wa miaka mitano na nusu akiwa naibu katibu mkuu . Migiro alikuwa na haya ya kusema.
“ Yapo mengi ambayo nimejifunza, lakini kwa ufupi tu niseme nimejifunza, uadilifu, uwajibikaji, kujituma, uzalendo, utii, kujiamini, matumizi sahihi ya yenye tija ya raslimali, kuthamini muda wa kazi, ushirikiano wa pamoja na maelewano”.
No comments:
Post a Comment