Sunday, July 1, 2012

HOTUBA YA MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA WANANCHI, TAREHE 30 JUNI, 2012

Ndugu Wananchi,

          Kama ilivyo ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza nusu ya kwanza ya mwaka 2012 salama.  Kwa kutumia utaratibu wetu wa kuzungumza nanyi kila mwisho wa mwezi, leo napenda kuzungumzia mambo mawili. Jambo la kwanza ni suala la usafirishaji haramu wa binadamu nchini na la pili ni la mgomo wa madaktari. 
Usafirishaji Haramu wa Binadamu Nchini
Ndugu Wananchi;
          Bila ya shaka mtakuwa mmezisikia taarifa za tukio la kushtusha na kuhuzunisha la kukutwa maiti 43 za watu wasiojulikana, zilizotupwa katika kichaka kilichopo kijiji cha Chitego, Wilayani Kongwa, Mkoa wa Dodoma tarehe 26 Juni, 2012.  Pamoja na maiti hao, walipatikana watu 84 wakiwa hai lakini wote wakiwa wamedhoofu na baadhi yao wakiwa mahututi.  Hatua za haraka zilichukuliwa kuwasafirisha watu hao hadi Dodoma ambapo wale waliokuwa mahututi walifikishwa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu na wengine walihifadhiwa katika Kituo cha Kati cha Polisi, Dodoma.  Maiti 22 zilipelekwa Dodoma na 21 zilipelekwa Morogoro kuhifadhiwa.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa wale walionusurika zimebainisha kuwa watu hao ni raia wa Ethiopia ambao walikuwa safarini kwenda Malawi na baadaye Afrika ya Kusini ambako wangetengenezewa utaratibu wa kwenda kuishi Marekani na Ulaya.  Kwa mujibu wa maelezo yao, safari yao ilianza miezi mitano iliyopita.  Mwezi mmoja waliutumia Ethiopia na miezi minne waliitumia Kenya kabla ya kuletwa Arusha ambako walipakiwa kwenye lori na kuanza safari ya kuelekea Malawi lakini ikaishia Chitego.  Lori walilopanda lilikuwa limezibwa kabisa na hivyo kusababisha vifo kwa kukosa hewa.
Tukio la Chitego, Dodoma la wahamiaji haramu kukamatwa na wengine kukutwa wamekufa si la kwanza kutokea hapa nchini.  Kwa jumla, katika kipindi cha takriban miaka 10 sasa kumekuwepo na tatizo kubwa la wahamiaji haramu kuingia nchini.  Kwa mfano, kati ya mwaka 2005 na hivi sasa jumla ya wahamiaji haramu 19,683 wamekamatwa.  Karibu wote wameshaondoshwa nchini na hivi sasa wapo karibu watu 1,500 tu magerezani wanaotumikia adhabu na kusubiri kurejeshwa makwao.  Wengi wa watu hao wanatoka Ethiopia na Somalia na baadhi kutoka Pakistan na Bangladesh.
Wahamiaji haramu wamekuwa wanaingia nchini kwa kupitia njia zisizo rasmi.  Wapo wanaotumia nchi kavu hasa kupitia mikoa ya Mara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.  Na, wapo wanaopitia baharini kwa kutumia fukwe za Pemba, Unguja na za mikoa ya ukanda wa Pwani ya Tanzania Bara yaani Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa kauli zao, watu hao wamekuwa wanaeleza kuwa hawaji nchini kuhamia bali wao ni wapita njia tu.  Wanaelekea Afrika ya Kusini ambako wameahidiwa kuwa watatengenezewa mipango ya kuhamia Marekani na Ulaya.  Watu hao pia wamethibitisha kuwepo kwa watu maalum wanaojihusisha na usafiri wao tangu nchi watokako na zote wanazopitia mpaka kule waendako.  Aidha, wamesema kuwa wao wanawalipa watu hao ili wawasafirishe na hakika si kiwango kidogo.  Kwa jumla ni kwamba hili si suala la uhamiaji haramu bali ni la biashara haramu ya kusafirisha binadamu.
Ndugu Wananchi;
Kufuatia vyombo vyetu vya usalama kuwa makini na watu wengi kukamatwa ndipo wasafirishaji walipobuni njia za kuwasafirisha kama mizigo.  Makontena, malori yaliyofunikwa nyuma na matenki ya mafuta na ya maji yamekuwa yanatumika kwa ajili hiyo.  Usafiri wa aina hiyo ndiyo uliosababisha vifo vilivyotokea Dodoma tarehe 26 Juni, 2012 na vya watu 21 vilivyotokea mwezi Desemba, 2011 Mkoani Morogoro, na vile vya watu 12 vilivyotokea katika matukio mawili ya Mkoa wa Mbeya, mwezi Mei, 2012.
Ndugu Wananchi;
Tarehe 27 Juni, 2012 nilikutana na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini kuzungumzia tukio la Chitego na suala zima la biashara hii haramu na hasa mbinu mpya inayotumiwa na wasafarishaji.  Nilitoa pongezi kwa vyombo vya dola kwa kazi nzuri waifanyayo kudhibiti shughuli za biashara hii haramu hapa nchini.  Tulielewana kuwa waendelee kuimarisha udhibiti huo kwa lengo la kukomesha kabisa biashara hii.
 Niliagiza pia kwamba kikundi kazi nilichokiunda mwaka 2006 kushughulikia ujambazi sasa kielekeze sehemu ya nguvu zake kukabili tatizo hili. Aidha, kwa pamoja tulikubaliana kuwa nchi yetu ishirikiane na wenzetu wa Ethiopia, Kenya, Malawi, Msumbiji na Afrika ya Kusini kutambua mawakala na kuwabana kwa mujibu wa sheria.  Tayari nimeshaanza kufanya mawasiliano na baadhi ya Wakuu wa Nchi hizo kuhusu ushirikiano huo.  Nashukuru wote wameafiki nchi zetu zishirikiane kwa pamoja kuvunja mtandao huu mchafu na kutokomeza biashara hii haramu na inayodhalilisha utu wa mwanadamu.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wenzetu, wakazi wa vijiji vya Chitego na Mkoka kwa kazi nzuri walioifanya. Kwa kweli, wenzetu wameonesha uzalendo wa hali ya juu kwa kutoa taarifa mapema juu ya jambo lenyewe, lakini pia wameonesha utu kwa kuwajali wageni waliokumbwa na janga hili. Naushukuru pia uongozi wa Mkoa wa Dodoma na Morogoro ikiwa ni pamoja na vyombo vya ulinzi  na usalama kwa kulishughulikia tatizo hilo kwa umakini mkubwa.   Nimefurahishwa sana na ushirikiano ulioonyeshwa na vyombo na taasisi mbalimbali za Serikali katika kushughulikia suala hili.
Mgomo wa Madaktari
Ndugu Wananchi;
          Jambo la pili ni kuhusu mgomo wa Madaktari unaoendelea nchini hivi sasa.  Nilipozungumza na Wazee wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Diamond Jubilee tarehe 12 Machi, 2012, kuhusu mgomo wa Madaktari uliokuwa unaendelea wakati ule pamoja na kuelezea chimbuko la mgomo na hatua iliyokuwa imefikiwa, nilielezea mazungumzo yangu na viongozi wa Chama cha Madakari wakiwemo pia viongozi wa Jumuiya ya Madaktari.  Nilitoa taarifa kuwa tumeelewana kuwa watasitisha mgomo na watarudi kwenye meza ya majadiliano na Serikali.  Siku ile pia nilielezea matumaini yangu kuwa mgomo ule utakuwa wa mwisho katika nchi yetu.  Bahati mbaya matumaini yangu hayo hayakuwa na hivi sasa tunashuhudia tena wagonjwa wakiteseka, kuhangaika na wengine kufa kwa sababu ya kukosa huduma wanazostahili kwa vile madaktari wao wamegoma tena.
Ndugu Wananchi;
Kama walivyoniahidi, madaktari waliacha kugoma na viongozi wao walirudi kwenye mazungumzo na Serikali.  Kama ilivyoagizwa na Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi tarehe 8 Machi, 2012, kwa mujibu wa Sheria ya Mahusiano Kazini, Namba 6 ya mwaka 2004.   Chama cha Madaktari na Serikali walifika katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (Commission for Mediation and Arbitration) kwa ajili ya majadiliano.  Kwa pamoja na kwa ridhaa yao wote, pande hizo mbili ziliiomba Tume hiyo iwape fursa ya kuzungumza wao wenyewe na wakimaliza mazungumzo wataenda kusajili makubaliano yao.  Tume ikawakubalia.  Ni vizuri ikakumbukwa kuwa siku ile ya tarehe 8 Machi, 2012 Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, ilitoa zuio la mgomo pamoja na kuagiza kuwepo mazungumzo baina ya pande mbili.
Ndugu Wananchi;
Kati ya tarehe 10 Aprili, 2012 na tarehe 30 Mei, 2012, vilifanyika vikao sita vya majadiliano kati ya Serikali na Chama cha Madaktari.  Katika mazungumzo hayo hoja au madai 12 ya madaktari yalizungumzwa.  Mambo hayo ni haya yafuatayo:
1.    Posho ya kuitwa kazini (on call allowance) iwe asilimia 10 ya mshahara.
2.    Posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (Risk allowance) iwe asilimia 30 ya mshahara.
3.    Madaktari wapatiwe nyumba grade A au posho ya makazi ambayo iwe asilimia 30 ya mshahara.
4.    Posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu iwe asilimia 40 ya mshahara.
5.    Madaktari walipwe posho ya usafiri ya asilimia 10 ya mshahara au wakopeshwe magari.
6.    Madaktari wanaoanza kazi walipwe mshahara wa shilingi 3,500,00/= kwa mwezi.
7.    Madaktari wapatiwe Green Card za Bima ya afya.
8.    Hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
9.    Viongozi wa Kisiasa kulazimisha kupewa rufaa nje.
10.           Madaktari waliofukuzwa warudishwe kazini.
11.           Huduma za afya ziboreshwe nchini.
12.           Posho ya uchunguzi wa maiti iongezwe.

Ndugu Wananchi;
          Katika mambo hayo 12 pande zote mbili zilifikia muafaka na kukubaliana wa pamoja kwa mambo saba.  La kwanza, ni kuhusu usafiri wa kwenda na kurudi kazini.  Serikali ilieleza kuwa upo utaratibu kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi wa Serikali Na. 3 wa mwaka 2011 wa kuwakopesha wafanyakazi wa Serikali fedha za kununulia magari au pikipiki, samani na matengenezo ya magari.  Ilikubaliwa kuwa madaktari waitumie fursa hiyo.
          Jambo la pili, ni kuhusu madaktari kupatiwa Green Card za Bima ya Afya.  Jambo hili lilikubaliwa na Serikali na Wizara ya Afya imekwishachukua hatua za utekelezaji wake.
          Jambo la tatu, ni kuhusu hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya.  Kwa pamoja walikubaliana kuwa suala hilo liko nje ya mamlaka ya Kamati yao ya pamoja, waziachie mamlaka husika za uteuzi.  Uongozi wa juu wa Wizara umebadilishwa na sasa kuna uongozi mpya.  Lakini, jambo la kustaajanisha hata Waziri mpya wa Afya alipowataka waonane kuzungumzia hoja walikataa kumuona.  Kwanza walisema hawaoni sababu kwa vile wameyazungumza na Kamati yake kwa miezi mitatu bila ya mafanikio
          Jambo la nne walilokubaliana ni kuhusu viongozi kulazimisha kupewa rufaa ya kutibiwa nje.  Walikubaliana mambo mawili.  Kwanza, kwamba maelekezo ya Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda kuwa madaktari wazingatie maadili ya kazi zao na kukataa kutoa rufaa kwa mtu asiyestahili awe kiongozi au asiwe kiongozi. Pili, walikubaliana kuwa hospitali zilizopo ziboreshwe ili viongozi watibiwe hapa nchini.  Ukweli ni kwamba kufanya hivyo ndiyo sera ya Serikali.  Nililieleza hili mwezi Desemba 30, 2005 katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuongoza nchi yetu. 
Tumeiongeza sana bajeti ya sekta ya afya kutoka shilingi bilioni 300 2005/2006 hadi shilingi trilioni 1.2 mwaka 2011/12 na imekuwa ya tatu baada ya miundombinu na elimu.  Tumeziimarisha hospitali za Mikoa kwa vifaa tiba na wataalamu wa afya.  Kazi inaendelea katika hospitali za Wilaya. Tumewekeza katika Hospitali ya Muhimbili.  Hospitali hiyo ilivyo leo sivyo ilivyokuwa miaka sita nyuma.  Na kazi inaendelea hasa katika maeneo ambayo tunapeleka wagonjwa nje.  Matunda yake yanaanza kuonekana kwa upande wa figo, moyo, kinywa na mipango inaendelea kwa upande wa ubongo na mishipa ya fahamu.  Tunaendelea kuimarisha mafunzo ya  madaktari na madaktari bingwa, yote kwa nia hiyo hiyo.  Hivi sasa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba,Muhimbili kinachukua wanafunzi wengi zaidi ya ilivyokuwa siku za nyuma na makazi mapya ya chuo yanaendelea kuandaliwa ili kuchukua wanafunzi wengi zaid.    Mwaka 2005 tulikuwa na madaktari bingwa 46 mwaka huu tunao 520.
Ndugu Wananchi;
          Jambo la tano ambalo pande zote mbili zilikubaliana ni kuhusu madaktari waliofukuzwa.  Hawa ni wale Interns waliokuwa wamerudishwa Wizarani kutoka Muhimbili na kupangiwa hospitali za Temeke, Ilala, Mwananyamala na Lugalo.  Hili ni jambo ambalo lilikuwa limemalizika kitambo na wote walikuwa wamerudi Muhimbili.
          Jambo la sita ni kuhusu mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na madaktari kuhusu kuboresha huduma ya afya.  Mapendekezo hayo yalihusu kutathmini sera na mpango wa afya ya msingi, bajeti ya afya kuwa asilimia 15 ya bajeti ya Serikali, kuwepo na utaratibu mzuri wa kuajiri madaktari na kuboresha viwango vya ubora wa madaktari na kadhalika.  Serikali imeyaafiki mapendekezo hayo na yatafanyiwa kazi.
          Jambo la saba, ambalo pande zote walilokubaliana ni kuhusu kuongeza posho ya uchunguzi wa maiti.  Hili ni jambo jipya halikuwepo mwazoni.  Hata hivyo, Serikali imelikubali na posho hiyo imeongezwa kutoka shilingi 10,000/= hadi kufikia shilingi 100,000/= kwa daktari na shilingi 50,000/= kwa wasaidizi wake.
Ndugu Wananchi;
          Kuna masuala matatu ambayo yamekuwa na muafaka kwa kiasi fulani na kutoafikiana kwa baadhi ya mambo.  La kwanza ni suala la kufanya kazi katika mazingira hatarishi.  Serikali imekubali hoja ya kuchukua hatua ya kuwalinda madaktari wanaofanya kazi katika mazingira hatarishi.  Serikali iliwaeleza kuwa watumishi wa kada zote za afya watapatiwa chanjo dhidi ya maambukizi ya Hepatitis B na fedha zimetengwa katika bajeti ya 2012/13.
Aidha, Serikali imeeleza dhamira ya kurudisha posho ya mazingira hatarishi kwa watumishi wa umma wanaostahili.  Utekelezaji wake utafanyika baada ya uchambuzi wa kina wa kubainisha mazingira hatarishi ni yepi, viwango stahiki viwe vipi na nani hasa wahusike.  Madaktari wamekataa hili la kufanya uchambuzi, wanataka kiwango kiwe kama wanavyotaka wao, yaani asilimia 30 ya mshahara na kianze mara moja.
          Jambo la pili ambalo wamekubaliana nusu nusu ni kuhusu nyumba za kuishi.  Serikali imekiri wajibu wake wa kuwapatia madakari nyumba za kuishi.  Aidha, imeeleza mpango ulioanza wa kujenga nyumba 700 za madaktari kote nchini na kwamba hivi sasa ujenzi wa nyumba 90 unaendelea, 50 katika mkoa wa Mtwara na 40 katika mkoa wa Rukwa.
 Kwa maeneo ambayo madaktari wanalipwa posho ya pango Serikali imesema waajiri wataendelea kufanya hivyo kwa mujibu wa taratibu zilizopo kwa watumishi wa umma wenye stahili ya kupewa nyumba.  Jambo hilo limekataliwa na Madakari na kutaka lazima walipwe asilimia 30 ya mshahara kama posho ya nyumba.  Serikali kwa upande wake imeona vigumu kufanya hivyo na kuwasihi wakubali wanayotendewa wafanyakazi wengine wote wa umma.
          Jambo lingine ambalo lilikuwa na makubaliano ya nusu nusu ni kuhusu posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu.  Pande zote mbili ziliafikiana kuwa yapo baadhi ya maeneo nchini yanayo mazingira magumu kwa watumishi wa umma  hivyo hatua zichukuliwe kuwasaidia watumishi hao. Serikali imekubali wajibu wa kuweka utaratibu wa kuboresha maisha ya watumishi katika maeneo hayo.  Kwa ajili hiyo, Serikali itatoa mwongozo kwa mamlaka za ajira kuhusu namna ya kuwasaidia watumishi hao kupunguza makali ya maisha katika kila eneo badala ya kutegemea posho peke yake.
  Kuhusu posho, Serikali imeeleza kuafiki kuwepo posho ya aina hiyo ila itatekelezwa baada ya kufanya uchambuzi wa kuainisha mazingira husika, kutambua watumishi waliopo na gharama zake.
          Madaktari hawajakubali kusubiri zoezi la uchambuzi lifanyike, wanataka Serikali ilipe posho hiyo sasa.  Tofauti hapa si posho hiyo kuwepo, bali ni rai ya Serikali ya kubaini maeneo yenyewe na kupanga aina ya hatua na viwango vya posho kulingana na mazingira halisi ya maeneo.  Madaktari hawaoni haja ya kufanya hayo.
Ndugu Wananchi;
          Mambo mawili hayakuwa na muafaka kabisa kati ya pande zetu mbili.  Jambo la kwanza ni posho ya kuitwa kazini (on call allowance).  Kwanza sina budi kueleza kuwa Serikali imekubali kuongeza posho hiyo.  Tangu Februari, 2012 posho iliongezwa kutoka shilingi 10,000/= hadi shilingi 25,000/= kwa daktari bingwa (Specialist), shilingi 20,000/= kwa dakari mwenye usajili wa kudumu (Registrars) na shilingi 15,000/= kwa madaktari waliohitimu ambao wapo katika kipindi cha mafunzo kazini (Interns).  Viwango hivyo vya posho vinatumika hivi sasa. 
  Madaktari kwa upande wao hawakukubali uamuzi huo wa Serikali na kusisitiza walipwe asilimia 10 ya mshahara.  Ugumu wa kukubali pendekezo la madakari ni kuwa sharti la malipo haya ni mtu kuitwa kazini.  Ukitaka ilipwe kiwango cha mshahara ina maana kuwa hata kama daktari hakupangwa kuitwa au alipangwa na hakutokea aendelee kulipwa.  Hili haliwezi kuwa sahihi kufanya.  Linaweza kuwafanya baadhi ya madaktari kutokutimiza wajibu wao kwa vile wana hakika mwisho wa mwezi malipo yako pale pale.
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ambalo muafaka haukufikiwa baina ya Serikali na madaktari ni kuhusu mshahara wa kuanzia kazi wa daktari.  Madaktari wanataka uwe shilingi 3,500,000/= wakati Serikali inasema kiasi hicho hatukiwezi.  Serikali imeeleza utayari wake wa kuongeza mshahara kwa kati ya asilimia 15 mpaka 20 kama ambavyo itafanya kwa watumishi wote wa umma katika mwaka huu wa fedha.  Kwa kiwango cha sasa cha mshahara wao, daktari ataanzia kati ya shilingi 1,100,000/= na 1,200,000/= kutegemea kiwango kipi hatimaye kitaamuliwa.  Madaktari wamekataa katakata na wameng’ang’ania shilingi 3,500,000/=.
Ndugu Wananchi;
Huo ndiyo mlolongo wa mambo yaliyozungumzwa na pande zote mbili na matokeo ya mazungumzo yenyewe.  Katika kikao cha sita kilichofanyika tarehe 30 Mei, 2012, upande wa Chama cha Madaktari ulisema kuwa kwa vile hoja ya nyongeza ya mshahara haina mabadiliko hawakuona haja ya kuendelea na majadiliano mpaka watakapowasiliana na wenzao.  Waliahidi kutoa taarifa ndani ya wiki mbili.  Tarehe 12 Juni, 2012, Rais wa MAT aliandika barua kwa Katibu Mkuu Utumishi ambaye ndiye kiongozi wa majadiliano kwa upande wa Serikali, kuwa Madaktari wameikataa taarifa na ufafanuzi waliopewa kutoka Serikalini kwa ujumla wake.
Ndugu Wananchi;
 Baada ya majibu yale ya madaktari, tarehe 19 Juni, 2012, Serikali na Madaktari walikwenda kwa Msuluhishi (CMA) kutoa taarifa kuwa mgogoro umekosa usuluhishi kama sheria inavyotaka.  Kwa pamoja pande zote mbili zilikubaliana suala hilo lifikishwe Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi.  Wakati pande zote zinasuburi mgogoro huu kufikishwa ngazi hiyo ya juu, upande wa Madaktari ukatangaza kuwepo kwa mgomo kuanzia saa sita ya usiku tarehe 23 Juni, 2012.  Hatua hiyo haikustahili kwani suala lenyewe halijafika mwisho wa kushughulikiwa kwa mujibu wa Sheria za Mahusiano ya Kazi nchini.
Ndugu Wananchi;
Tarehe 22 Juni, 2012, Mwanasheria Mkuu wa Serikali akaenda Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi kulifikisha suala la tishio la mgomo na kuomba zuio la muda kufanywa.   Mahakama Kuu ilikubali ombi hilo na kuagiza kuwa mgomo usitishwe.  Juhudi za kumtafuta Rais wa MAT, Dkt. Namala Mkopi na viongozi wengine wa MAT hazikufanikiwa, Ofisi ya MAT ilikuwa imefungwa na simu zote za viongozi wa MAT zilikuwa zimezimwa.  Hatimaye tarehe 25 Juni, 2012, alipatikana na kupewa amri hiyo ya Mahakama.  Tarehe 26 Juni, 2012, Dkt. Mkopi alifika Mahakamani ambapo alikana kuwa yeye hahusiki na kuitisha huo mgomo lakini hakumtaja aliyehusika.  Pamoja na rai hiyo, Jaji alimuamuru Rais wa MAT akawatangazie wanachama wake kusitisha mgomo.   Dkt. Namala Mkopi hajafanya hivyo hadi leo na mgomo umekuwa unaendelea kinyume cha Sheria.
Ndugu Wananchi;
Wagonjwa wanateseka na wengine kupoteza maisha kwa mgomo huu usiokuwa halali kisheria ambao pia haustahili kuwepo hata kwa mujibu wa maadili ya udaktari.  Viongozi wa  MAT na wenzao wanawaingiza Madaktari katika mgogoro na Mahakama na waajiri wao isivyostahili.  Ni vyema viongozi wa Madaktari na madaktari wakatambua kuwa wanashiriki katika mgomo usiokuwa halali ambao pia kiongozi wao mkuu amekana Mahakamani kuwa hahusiki nao.  Madaktari lazima watambue pia kwamba ajira zao wanaziweka hatarini.  Mfanyakazi ana kinga ya kutofukuzwa kazi na mwajiri kwa kushiriki mgomo unaokubalika kisheria.  Huu siyo.  Watapoteza ajira, hawana pa kukimbilia, hawana cha kiwalinda.  Kwa madaktari interns, wanahatarisha maisha yao kwani hawatapata cheti cha kudumu wakishiriki mgomo usiokuwa halali.   Lazima watafakari sana kwa hayo wafanyayo. 
Ndugu Wananchi;
          Napenda kurudia maneno niliyoyasema tarehe 12 Machi, 2012, kuwa kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi ni Sera ya Serikali yetu kwa maelekezo ya Ilani ya Chama Tawala (CCM).  Tumeitekeleza kwa vitendo sera hiyo, hata hivyo ni ukweli ulio wazi kuwa nia yangu njema tu pekee haitoshi, lazima uwezo wa kufanya hivyo uwepo.  Kwa kulingana na uwezo uliopo, tumeendelea kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi hatua kwa hatua tangu tuingie madarakani.  Tumefanya hivyo kwa jumla kwa wafanyakazi wote na kwa kada mbalimbali za watumishi wa umma.
Miongoni mwa wafanyakazi wa umma walionufaika na hatua hizo za Serikali ni madaktari na watumishi wa kada nyingine za huduma ya afya.  Tena nadiriki kusema madaktari tumewapa upendeleo mkubwa kuliko watumishi wengine wa umma.  Upendeleo upo kwenye mafunzo ambapo wanafunzi wa udaktari wanagharimiwa na Serikali kwa asilimia mia moja wakati wanafunzi wenzao wa taaluma nyingine hawako hivyo.
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2004/2005, mshahara wa kuanzia wa daktari ulikuwa shilingi 178,700/=, mwaka 2005/ 2006 tuliupandisha na kuwa shilingi 403,120/=. Tuliendelea kuupandisha mwaka hadi mwaka mpaka kufikia shilingi 957,700/= wanazolipwa sasa.  Kiasi hicho ni mara mbili ya mishahara ya watumishi wa taaluma nyingine wenye shahada ya kwanza wanaoanza kazi ambao kwa wastani hupata shilingi 446,100/=.
Tunafanya hivyo kwa kutambua na kuthamini nafasi maalum ya madaktari katika jamii na ukweli kwamba bado tunayo safari ndefu ya kuziba pengo la madaktari nchini.  Lakini inaonekana juhudi zetu zote hizo hazithaminiwi.
Ndugu Wananchi;
Sina budi kusisitiza  kwamba tunapofanya hivyo tunaongozwa na uwezo tulio nao wa kulipa.   Kwa sasa hatuwezi kuwaahidi kuwa tunao uwezo wa kuwalipa mshahara wa kuanzia wa shilingi 3,500,000/= na posho zote zile. Tukifanya hivyo malipo ya daktari anayeanza kazi yatakuwa shilingi 7,700,000/=.  Kwa hakika kiasi hicho hatutakiweza. Si vyema kutoa ahadi hewa kwa watu tunaowaheshimu na kuwathamini kama walivyo madaktari.
Kutokana na ukweli huo basi kama daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi Serikalini bila ya kulipwa mshahara huo awe huru kuacha kazi na kwenda kwa muajiri anayeweza kumlipa kiasi hicho.  Nasi tutamtakia kila la heri.  Hana sababu ya kugoma ili ashinikize kulipwa mshahara huo. Asisumbuke, hatalipwa mshahara huo.  Isitoshe, hana sababu ya kuendelea kuwa na mgogoro na mwajiri ambaye hana uwezo wa kumlipa anachokitaka.  Huna sababu ya kumpa usumbufu mwajiri wa kukuandikia barua ya kujieleza au kukuachisha kazi.  Kwa nini upate usumbufu wa kupata barua hizo na kuzijibu. Kwa nini upate usumbufu wa kuachishwa kazi na kutakiwa kuondoka kwenye nyumba ya Serikali ndani ya saa 24.  Jiepushe na yote hayo kwa kujiondoa mwenyewe.  Usipofanya hivyo, mwajiri anakuwa hana jinsi bali kukuondoa kazini maana unakwenda kinyume na sheria za kazi na maadili ya kazi ya udaktari.
  Mamlaka za ajira zimeanza kuchukua hatua hizo na wataendelea kufanya hivyo kwa wote wanaoendelea kugoma.   Najua baada ya hatua hizo kuchukuliwa kuna manun’guniko ya kuonewa. Hivyo, mlitegemea mwajiri afanyeje? Ni bora kufanya hivyo ili ajue hana daktari aweze kufanya utaratibu wa kuziba hilo pengo na huyo ajae awe na mahali pa kuishi. Vinginevyo atakuwa anajidanganya kuwa anae daktari ambae hayupo kazini na wala hataki kufanya kazi.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwathibitishia kwamba dhamira ya Serikali ya kuboresha maslahi ya watumishi wa umma wakiwemo  madaktari iko wazi.  Tumekuwa tunafanya hivyo, na tutaendelea kufanya hivyo kulingana na uwezo wa kibajeti.  Ni vyema watumishi wa umma wakatambua kuwa hatuwezi kutumia fedha zote au kiasi kikubwa mno cha pesa za umma kulipana mishahara.  Tukifanya hivyo, Serikali itashindwa kutoa huduma muhimu kwa wananchi ambao ndiyo wengi na wanastahili kuhudumiwa.  Hata hizo huduma za afya tunazosema ni duni tuziboreshe, hatutaweza kuziboresha kama tutatumia sehemu kubwa ya pesa za Serikali kuwalipa mishahara wafanyakazi. 
Hivi sasa matumizi ya mishahara ni asilimia 48 ya bajeti ya Serikali.  Kiwango hicho ni kikubwa mno.  Uwiano mzuri ni kuwa na matumizi ya mishahara yasiyozidi asilimia 35 ya bajeti na asilimia 65 zitumike kugharimia huduma na shughuli nyingine za maendeleo ya wananchi na taifa.  Sisi tumezidi kwa asilimia 13.  Hivyo, hatuna budi tukubali kujinyima kwa manufaa ya walio wengi. 
Suala la Dkt. Steven Ulimboka
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu, napenda kuungana na Watanzania wenzangu wote kuelezea masikitiko yangu makubwa na kuhuzunishwa kwangu na kitendo cha kinyama alichofanyiwa Dkt. Steven Ulimboka usiku wa tarehe 26 Juni, 2012. Kitendo hicho ni kinyume kabisa na mila na desturi zetu. Watanzania hatujayazoea mambo hayo. Nimeelekeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane.  Nimesema kuwa ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili tuondoe wingu baya la kutiliana shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi sasa.
Natambua kuwa Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka.  Mimi nimeshangazwa sana na hisia hizo kwani siioni sababu ya Serikali kufanya hivyo.  Dkt. Ulimboka alikuwa mmoja wa kiungo muhimu katika mazungumzo baina ya Serikali na Madkatari.  Ni kweli kwamba yeye si mtumishi wa Serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano haya.  Kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo, lakini nilisema wamuache maadam Madaktari wanamuamini kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na Serikali.
Ndugu Wananchi;
Kama nilivyoeleza, mazungumzo yalienda vizuri na mafanikio makubwa yamepatikana.  Yapo maeneo machache na hasa eneo la mshahara ambalo hatukuweza kukubaliana.  Hapo tulipofikia si pabaya na tulikubaliana sote kurudi kwenye mkondo wa Sheria kusaidiwa.  Kwa nini Serikali imdhuru Dkt. Ulimboka? Na, kuhusu mgomo, Mahakama Kuu imekwishatoa amri ya kusitisha mgomo.  Anayekaidi amri ya Mahakama ananunua ugomvi na mhimili huo wa dola ambao wenyewe una mamlaka ya kumtia adabu mtu huyo.  Hivi baada ya kufika hapo Serikali iwe na ugomvi na Dkt. Steven Ulimboka kwa sababu ipi na jambo lipi hata iamue kumdhuru?  Kama kuna mtu wa Serikali kafanya, itakuwa kwa sababu zake binafsi na siyo za Serikali au kwa kutumwa na Serikali.
Ndugu Wananchi;  
Kwa niaba yangu na kwa niaba ya Serikali natoa mkono wa pole kwa Dkt. Steven Ulimboka na kumuombea apone haraka ili aungane na familia yake na Watanzania wenzake katika ujenzi wa taifa.  Kwa namna ya pekee namshukuru na kumpongeza Bwana Juma Mgaza, kwa moyo wake wa huruma na upendo na kwa hatua alizochukua za kumsaidia Dkt. Ulimboka.
Naomba kumaliza kwa kuwasihi madaktari kuacha mgomo na kurejea kazini.  Watanzania wenzenu wanateseka na kupoteza maisha.  Muwe na moyo wa huruma na upendo na msaada kwa wagonjwa kama kiapo chenu kinavyowataka.

Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.


8 comments:

Anonymous said...

ina maana Dkt. Mkopi ndio raisi wa MAT, na Dkt. Ulimboko sio mfanyakazi wa serikari? kazi yake ni kuongoza mgomo nani muajiri wa Dkt. Ulimboko? na moja ya jukumu lake ni kuchochea vurugu au mimi ndio sielewi wananchi

Anonymous said...

we ndo rais bwana mie nafurahia maamuzi yako yenye busara jaman ma dr msitusumbue kama huwezi achia ngazi wengine wenye fan kama yenu tumekaa tu nyumbn.nendeni msituharibie nchi hapa

Anonymous said...

wananchi wenye hasira kali kuhusu Doctor Ulimboko punguzeni jazba usome hotuba ya Raisi muelewe ukweli na msisikilize minongono. Historia ya migomo ya Tanzania yetu ni ya nguvu ya soda yenye mcharuko wa siku chache kisha kama machozi huenda na maji na yote hii ni sababu tunapandisha jazba na maswala ya juu juu bila kujua ukweli halisi,wananchi wengi leo ndio tumejua sababu zenu za mgomo kumbe ni posho na sivyo kama mlivyotupandisha jazba, kumekua na madhara yanayotokana na maamuzi ya juu juu wagonjwa kufa, wauguzi kutimuliwa kazi na mamilioni ya pesa yanateketea kwa mtu mmoja kupelekwa kutibiwa nje ya nchi kisa tunadai haki. pesa ambazo zingenunua panadol na penicilin kufanya wagonjwa wote muhimbili leo walale bila maumivu kwa siku moja. Ninachosema ni kuwa migomo yetu imekua ya maswala ya kibinafsi zaidi au kundi la watu wachache wakitaka kumkomoa fulani aliye juu, madhara yake tunakufa sie walala hoi. linaundwa kundi la viongozi wanapaisha habari kwenye vyombo vya habari inakua habari motomoto watu wanaandamana jazba kila kona mwisho wa siku kila mtu anarudi nyumbani kutafuta ugali wa kula na wanae na waliojitia vimbelembele hasara kwenu na familia zenu, itabaki breaking news siku chache inapita tunasahau inakuja habari nyingine, yote hayo ni kuvuruga amani, mashujaa na wapiganaji wa haki za kweli walikua ni kina Mwalimu Nyerere sababu ziko wazi na zinaeleweka kwa wananchi wote, hii migomo ya kisiku hizi ni migomo mcharuko mnawapotosha wananchi kwamba mnadai huduma za hospitali ziwe bora mheshimiwa Raisi ametoa sababu zenu za mgomo kuanzia namba moja mpaka kumi na moja ni posho tu kipengele cha kuboresha matibabu na vifaa vya matibabu mmekiweka mstari mmoja tena cha mwisho kwenye list yenu hakina hata ufafanuzi hata demand ya kuwa wodini lazima kuwe na panadol kila wakati. Kama hii migomo sio micharuko mtauita ni mgomo sahihi? tena kwa wasomi kama madakitari kwa maoni yangu msihatarishe maisha ya watu kwa siasa mcharuko kama kuna dakitari hataki kazi acheni waacheni wale madakitari wa kweli wafanye kazi kwa mioyo yao ya kutoa huduma na nyie wachache mnaotafuta attention za siasa mkajiunge na matawi ya chama mitaani mnakoishi, wengine hata sio watumishi wa serikali mmefikaje kuchochea mgomo?

Anonymous said...

watumishi wa serikali sio madakitari peke yao hata sisi walimu pia ni watumishi jee na sisi tungedai posho na marupurupu yenu na kugoma mngefika hapo mlipo? uliona wapi ukadai mshahara wako uongezwe kwa asilimia 90 na ikafanyika hapo hapo? pesa yote mkilipwa nyinyi na sisi wenzenu tulipwe nini? msijifanye kama vile kazi yenu ndio funguo wa kuingia peponi kumbukeni na nyinyi ni binadamu

Anonymous said...

serikali haina ugomvi na Dkt. Steven Ulimboka mambo ya nyumba ndogo hayo magari yamegongana, kitu cha my wife wa mtu ukitaka kujua ukweli mbona mke wako hakukutafuta ulipokosa kurudi nyumbani usiku au Dkt mwenzio uliekua naye Bar mbona hakupiga simu polisi au hapo Bar kulikua hakuna hata muhudumu alieshuhudia unachukuliwa kinguvu tueleze tu walikukuta wapi hao bandugu usisingizie serikali

Anonymous said...

Asante sana Rais kwa maamuzi yako hawa madaktari utafikifi peke yao tu ndio wamesoma katika nchi hii kaeni pembeni msiotaka kazi wapeni nafasi wengine wanaotaka. Kila mtu ana umuhimu katika sehemu yake ya kazi, kama siyo Mwalimu ungekuwa daktari wewe acheni hizo fanyenyi kazi msituharibie nchi yetu yenye Amani na Upendo.

Anonymous said...

nimependezewa na hotuba ya MH. RAIS, huo ndo msimamo wa kweli. wanataka kazi warudi wafanye kazi hawataki waondoke wakaaajiriaw plae wanapooona watapewa hizo mil.3500000, wasitusumbue kwanza wameshawaaua sana ndgu zetu waliokuwa mahospitalini, bila ya hatia yeyote, kwnza nashauri hawa ma dr. washitakiwe wanajiingiza ktk siasa na wakati fani yao haipo wala haiambatani na siasa wasitake kutuharibia nchi hawa jamaaa na wanataka nchi isitawalike, na hao wanaojifanya HAKI ZA BINADAMU NA TAMWA sijui serikali inapaswa kuwashughulika mapema mnoooooo wamekuwa ndo chamzo na migogor ya migomo hapa nchini na wa ajenda za siri tena nyma ya pazia

Anonymous said...

Nadhni hotuba sio mbaya na kwa ushauri wangu kwa kuwa tunajua madaktari wanasoma muda mrefu kwenye digrii, mastaz na phd tofauti na sisi wengine wa fani nyingine japo tuko huko huko kwenye afya, swala la "Nafuu wafukuzwe sisi tuliko nyumbani tupate nafasi ni ujinga kwa kuwa hujatafuta kazi ukokosa, mbona wengine tukipata tunachagua ndio maana hatufanyi!!! Kwa upande wa serikali wajali muda wanaotumia madaktari kusoma na huduma muhimu wanayotoa. Pili Madaktari kwa mshahara mnaoutaka ni mkubwa kupitiliza, hata watoto wenu wakitaka shule za garama kubwa mnakuwa wakali, kwa upande wenu nashauri angalau mshahara wa 1.3

Natumanini kuwa njia sahihi ya haya mambo ni kukaa mezani na kusikilizana na baadae kutoa muafaka pole pole, MADAKTARI HARAKA HARAKA HAINA BARAKA?!!! Japo msemo wa zamani lakini zingatieni na sisi wananchi tunahitaji huduma yenu, Serikali kwa mara nyingine Hospitali binafsi wanatuua kwa gharama kubwa ya matibabu, tusaidieni kwa kumaliza haya mambo mapema. Sio kila kitu kuunda tume maamuzi mengine yawe ya moja kwa moja. wewe ni Baba na mwenye final say katika nyumba.