Katibu wa Hospitali
Mwaka 1948 Sinodi ya Kanisa ilimwomba Pd. Van Melssen kutafuta eneo sehemu za undali bila mafanikio. Mwaka 1949 eneo dogo lilipatikana mjini Tukuyu karibu na ofisi za ustawi wa jamii. Mwaka huo huo Pd. Melssen alipeleka ombi kwa uongozi wa Wilaya kuomba eneo kwenye barabara iendayo Igale umbali wa 25 Km kutoka Tukuyu Mjini. Aliomba kati ya eka 30 hadi 40. na alisema eneo hili lingekuwa zuri kwa ajili ya kulima kahawa. Ni mwaka 1952 ndipo Wakatoliki wakafanikiwa kupata eneo Igogwe lakini badala ya eka walizoomba waliambulia eka 4 tu. Pd. Poels alifungua shule ya msingi mwaka 1953, na Pd. Melssen hali akijua pingamizi kubwa la kuanzisha kilimo cha kahawa alipanda miti 1000 ya kahawa.
Baraza la Maaskofu la mwaka 1956 liliamua kujenga misioni mpya baada ya ile ya Ipinda iliyojengwa miaka 20 iliyopita. Jimbo lilikuwa na eneo Igogwe lakini Baraza halikutaka kujenga eneo hilo kwa vile ingeweza kuhudumiwa vema na Parokia ya Kisa. Waliona vema kuanzisha maeneo ya Mwakaleli. Mapadre: Van Melssen, Hoppe na Poels walienda Mwakaleli kuomba kupata eneo kutoka kwa uongozi wa mahali pale kupitia kwa mkuu wa Wilaya bila mafanikio.
Japokuwa Baraza halikuona umuhim wa kujenga maeneo ya Igogwe, parokia ilijengwa na kufunguliwa rasmi tarehe 4/6/1957. Parokia iko kati ya mito miwili igogwe na Isaka. Parokia inahudumia eneo lote la Tarafa ya Ukukwe isipokuwa maeneo ya kata ya Malindo. Kwa wakati huo maeneo yote ya Umalila (Mbeya Vijijini) eneo ambalo kwanza lilihudumiwa na parokia za Kisa na Mlowo. Wakazi wakuu wa eneo hili ni Wanyakyusa na Wamalila.
Sababu kubwa ya kwanini Wanyakyusa walitoa eneo hili kwa misheni ya Wakatoliki ni ahadi ya kujenga shule na hospitali. Shule tayari ilijengwa mwaka 1953. Pd. Maurice Garant alianzisha Zahanati kama hatua ya kujenga hospitali muda mfupi baada ya kuanzisha parokia. Watu wengi walikuja na kuhudumiwa na zahanati ikabidi Pd. Mmoja na mhudumu wawepo muda wote kuwahudumia wagonjwa. Mwaka 1957 wakatoliki walikuwa 200 tu. Mafundisho ya wakatukumeni yalianzishwa katika vijiji sita, na shule nne za misheni zilianzishwa.
Paroko wa kwanza alikuwa Pd. Moreault akisaidiwa na Bro. Wofgang ambaye muda si mrefu alibadilishwa na Bro. Theodorich ambaye alianza ujenzi wa makazi ya mapadre na kanisa. Mwaka 1958 Pd. Romand Monnier aliipanua Zahanati iliyoanzishwa na Pd. Maurice Garant.
Mwaka 1958 Masista wa Shirika la Wafranciscan wa Denekamp – Uholanzi waliombwa kuja Tanzania na kuanzisha huduma za hospitali na Baba Askofu alipokuwa likizo yake huko Ulaya. Masista walionyesha nia ya kukubali na kuja Tanzania – kuanzisha hospitali katika Jimbo la Mbeya.
Tarehe 17/7/1960 Masista Wafranciscan wa kwanza walifika Igogwe kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali. Nao ni Sr. Tarcis, Sr. Bonifacio na Sr. Gemma. Walipofika tu walianza mara moja kazi ya kuwahudumia wagonjwa. Pole pole waliipanua zahanati na na mwaka 1962 walianza ujenzi wa hospitali. Jiwe la Msingi liliwekwa tarehe 24/6/1962 na Pd. Van Melssen.
Umri wa hospitali ni sawa na umri wa Kituo cha kulelea watoto Yatima. Wakati ule watoto ambao walifiwa na wazazi wao hasa mama kutokana na matatizo ya kujifungua walilelewa na Masista kwenye nyumba yao. Mwaka 1968 nyumba ya kulelea watoto ilijengwa na kuanza kutumiwa.
Vyote hospitali na kituo cha watoto yatima vilikuwa vinaendelezwa na Masista hao kwa niaba ya Jimbo. Hospitali imekuwa na kuongezeka sana kihuduma na kimiundo mbinu. Huduma za mama na mtoto zilianza kutolewa kwenye jengo maalum mwaka 1974, nyumba ya akina mama wajawazito mwaka 1985, jengo la kutengenea maji (infusions) lilikamilika mwaka 1990, ukarabati wa hospitali kwa mara ya mwisho ikiwa pamoja na kuongeza chumba cha upasuaji, maabara ya zamani na chumba cha mionzi vilikamilika mwaka 1993. Mwaka 1997 chumba cha ultrasound kiliongezwa kwenye wodi ya watoto. Mwaka 1998 nyumba za watumishi kumi na nane ziliongezwa na nyumba ya Masista wa Jimbo ilikarabatiwa. Mwaka 2003 jengo la magonjwa ya kuambukiza lilijengwa na kukamilika. Mwaka 2004 nyumba mbili za madaktari zilijengwa na kukamilika. Mwaka 2006 jengo jipya la maabara lilikamilika. Mwaka 2007 ukarabati wa jengo la magonjwa ya kuambukizwa ulifanyika ili kutoa mwanga zaidi na hewa zaidi. Wodi ya watoto na wodi ya wajawazito vilikarabatiwa mwaka 2009.
Huduma za hospitali:
Huduma za Tiba zinajumuisha wagonjwa wa nje, kulazwa (vitanda 140), upasuaji (Mkubwa na mdogo), kliniki ya VVU, magonjwa ya akina mama wajawazito
Huduma za kinga kama vile huduma ya mama na mtoto, elimu ya afya kuhusu magonjwa mbalimbali ya kuambukizwa ukiwemo UKIMWI, TB na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa
Huduma za majumbani
Huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ikiwemo na kumiliki kituo cha kulelea watoto Yatima.
Huduma saidizi kama maabara ya kisasa, vipimo ya mionzi, vipimo vya ultrasound, moyo, na vipimo mbalimbali kwa ajili ya mtu kujua afya yake na kupata ushauri unaofaa.
Hospitali ina wataalam waliobobea katika kutoa huduma zilizotajwa hapo juu kwa wakati muafaka
Hospitali ina vifaa mbali mbali vizuri ambavyo kwa utaalam ulipo vinasaidia kugundua magonjwa na kutoa tiba inayohitajika.
Mustakabali:
Bodi ya Hospitali pamoja na kamati ilioiunda kuratibu Jubilei ya miaka 50 imeamua kuyapa kipa umbele masuala kadhaa katika kuboresha huduma kwa wagonjwa katika mpango mkakati wake. Hospitali inaandaa chakula cha hisani chakula cha hisani tarehe 4/8/2012 ili kuchangia yafuatayo yanayoambatana na adhimisho la Jubilei miaka 50 ya Hospitali. Pia Hospitali inawakaribisha Watanzania wote na wote wenye nia njema kuchangia jitihada za kuiendeleza na kuboresha Hospitali ya Igogwe.
· Kukarabati Hospitali wodi na OPD Tshs 30,000,000/=
· Kukarabati Jengo la Watoto Yatima Tshs 25,000,000/=
· Kujenga Jengo la Idara ya Mionzi Tshs 72,000,000/=
· Kukarabati Chumba cha Upasuaji Tshs 26,500,000/=
· Kujenga jengo la maiti (mortuary) Tshs 35,000,000/=
· Kukarabati nyumba za watumishi Tshs 41,400,000/=
· Kununua gari la kubebea wagonjwa Tshs 120,000,000/=
· Adhimisho la Jubilei Tshs 22,550,000/=
Jumla ya Fedha zinazohitajika ni Tshs 372,450,000/=
Akaunti za Hospitali kwa ajili ya kuchangia walio
mbali na wenye mapenzi mema
IGOGWE HOSPITAL – JUBILEE AT NBC TUKUYU BRANCH A/C = 038201127120
IGOGWE HOSPITAL – AT NMB TUKUYU BRANCH 1/C = 61403500064
2 comments:
Asante sana kwa historia nzuri sana ya Igogwe. Nashukuru pia kanisa la katoliki kwa uwezo wake wa kutunza taarifa kwa usahihi namna hii.
Mimi nilizaliwa katika hospitali hiyo mwaka 1968. NIngependa kuchangia katika ukarabati wa hospitali hiyo.
Endelezeni moyo huohuo wa kuwasaidia wazazi na kuwapa watoto maisha. Kama nisingezaliwa katika hospital hiyo labda maishja yangu yangekuwa yamekoma kama kichanga kwanni marehemu mama yangu aliniambia kuwa nilipozaliwa nilitunzwa chini ya uangalizi wa wauguzi nikiwa nimewekewa oxygen...
NIna shauku kubwa ya kujua zaidi taarifa zangu za mwanzo wa maisha yangu na ikiwa ningepata kuona reports za madaktari za kipindi hico (ikiwa bado zimetuzwa).
Nimefurahi sana kupata historia ya hospitali ya igogwe, nilikuwa sijawahi kuisoma ingawa mimi nimezaliwa hapo, mama yangu amefanya kazi kama nurse hapo kuanzia mwaka 1979 mpaka sasa yupo hapo anaitwa Anna Noah Sakajolo, pia nimesomeshwa na Sister Bonifacio mpaka hapa nilipofikia, pindi nipatapo mchango nitawasilisha. Naipenda sana hospital ya Igogwe.
Post a Comment