Monday, June 25, 2012

Wanafunzi walemavu washindana Maadhimisho ya Mtoto wa Afrika


 Baadhi ya wanafunzi wenye ulemavu wakijiandaa kuanza kutimua mbio walipokuwa mashindanoni
 Hapa wakitimua mbio tayari kumsaka kinara wa kufukuza upepo
 Mpambano wa netiboli
Kikosi cha Kandanda kutoka Shule ya Mtwivila kikiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kwa pambano
kwaya kutoka Shule ya Makalala wakitumbuiza 
 Kikosi cha Mpira wa Miguu kutoka Shule ya Msingi Njombe katika picha ya pamoja.
 Mgeni rasmi Farida Mwasumilwe, ambaye ni Ofisa Elimu Msingi akikagua timu za mpira wa miguu kabla ya pambano.
 Salamu kwa watanzamaji zikitolewa na timu za netibali kabla ya kuanza kwa pambano.
 Vijana wa Njombe wakipasha viungo moto
Waamuzi na waratibu wa michezo hiyo wakijadiliana jambo


Na Mwandishi wa Thehabari.com, Mafinga
WANAFUNZI wenye ulemavu anuai wilayani Mafinga wameadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika kwa kufanya mashindano katika michezo mbalimbali ili kujenga ushirikiano na makundi mengine ya jamii.

Mashindano hayo ambayo yaliwaleta pamoja wanafunzi wenye ulemavu anuai yaliyofanyika hivi karibuni wilayani Mafinga yaliandaliwa na mashirika na taasisi zinazofanya kazi na kundi hilo maalumu pamoja na kushirikiana na Serikali ya Tanzania idara husika.

Katika mashindano hayo yaliyofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Makalala mjini Mafinga, mkoani Iringa, Shule ya Msingi Mtwivila ndiyo iliyoibuka mshindi wa jumla baada ya kufanikiwa kunyakuwa ubingwa wa mpira wa miguu na mpira wa pete kwa wanafunzi walemavu.

Shule ya Mtwivila ilifanikiwa kutwaa ushindi katika mpira wa miguu baada ya kuifunga Shule ya Msingi Njombe kwa mikwaju ya penati 3-2, baada ya kumalizika kwa dakika 90 za muda wa kawaida huku timu zote zikitoka sare ya magoli 1-1.

Akina dada wa Shule ya Mtwivila nao waliibuka msindi kwa mpira wa pete (netibali) baada ya kuwafunga bila huruma wenzao wa Njombe na kufanikiwa kutwaa saa ya kisasa ya ukutani na mipira ya mchezo huo.

Kwa upande wa riadha shule ya Msingi Makalala ndiyo iliyoibuka kidedea baada ya kushinda kwa wavulana na wasichana huku wakifuatiwa na Shule za Njombe, Mtwivila na Kidamali. Hata hivyo Shule Maalumu ya Makalala iliendelea kuwa mwiba katika michezo hiyo baada ya kutwaa mataji ya nyimbo za kwaya na zile za kizazi kipya (Hip Hop), huku taji la nidhamu michezoni likienda kwa wanafunzi wa Njombe baada ya kuonesha nidhamu ya hali ya juu.

Washindi wa michezo yote kwa nafasi za kwanza na za pili walipewa mataji pamoja na saa za kisasa za ukutani. Miongoni mwa mashirika na asasi zilizofanikisha tamasha hilo ni pamoja Kituo cha Habari Kuhusu Ulemavu nchini (ICD), Chama cha Wasioona Tanzania (TLB), Sightsavers, CCBRT, INUKA, SHIVYAWATA na Serikali ya Tanzania.

*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com 

kwa kushirikiana na Kituo cha Habari Kuhusu Ulemavu Tanzania (ICD).

No comments: