Friday, April 13, 2012

MAONI YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YAMAENDELEO YA JAMII KUHUSU MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA ZA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII, 2012 (THE SOCIAL SECURITY LAWS (AMENDMENTS) ACT), 2012

MAONI YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YAMAENDELEO YA JAMII KUHUSU MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA ZA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII, 2012 (THE SOCIAL SECURITY LAWS (AMENDMENTS) ACT), 2012



UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007, Kanuni ya 86 (5), naomba kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu, maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, 2012 (The Social Security Laws (Amendments) Act), 2012.

Mheshimiwa Spika, Kamati ilipata nafasi ya kujadili Muswada huu katika vikao vilivyofanyika katika Ofisi ndogo ya Bunge Dar es Salaam. Katika kikao cha kwanza kilichofanyika tarehe 27/03/2012, Naibu Waziri wa Wizara ya Kazi na Ajira Mheshimiwa Dkt. Milton M. Mahanga, Mb alitoa maelezo ya jumla yanayohusu madhumuni ya Muswada. Kikao hiki pia kiliwashirikisha wadau mbalimbali miongoni mwao wakiwemo:-

1. Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi -TUCTA
2. Chama cha Waajiri Tanzania -ATE
3. Chuo Kikuu Mzumbe
4. Tanzania Higher Learning Instution Trade Union - THTU
5. Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa- LAPF
6. Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma- PSPF
7. Mfuka wa Taifa wa Bima ya Afya- NHIF
8. Mfuko wa Pensheni kwa Mashirika ya Umma- PPF
9. Mfuko wa Akiba kwa Watumishi wa Serikali- GEPF
10. Mfuko wa Hifadhi za Jamii – NSSF
11. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu- LHRC

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee Kamati inawashukuru wadau wote walioshiriki na kutoa maoni ambayo yamezingatiwa na Kamati katika kuishauri Serikali ili iyazingatie katika Jedwali la marekebisho.

Mheshimiwa Spika, vikao vingine vilifanyika terehe 03/04/2012, tarehe 04/04/2012, tarehe 11/04/2012 na tarehe 12/04/2012 ambapo Waziri Kazi na Ajira pamoja na Mwakilishi kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu walifafanua na kutoa majibu ya baadhi ya hoja zilizokuwa zimejitokeza.

Mheshimiwa Spika, Muswada huu unakusudia kufanya marekebisho katika Sheria za Hifadhi za Jamii kwa madhumuni ya kuiwezesha Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi za Jamii kufanya kazi yake ya kusimamia na kudhibiti Sekta ya Hifadhi ya Jamii kikamilifu.

Mheshimiwa Spika, Muswada huu umegawanyika katika Sehemu Kuu Nane ambazo Kamati imezifanyia kazi na kutoa mapendekezo ya kuziboresha na hatimae kuwa na Sheria inayofaa kwa mazingira ya nchi yetu.

SEHEMU YA KWANZA

Mheshimiwa Spika, Sehemu hii inaelezea jina la Muswada na maudhui yanayofanya kupendekeza kutungwa kwa Sheria hii. Kamati haikuwa na tatizo lolote katika sehemu hii na imekubali mapendekezo ya Sheria hii kuanza kutumika tarehe 1 Juni 2012, kama yalivyoletwa mbele ya Kamati katika jedwali la marekebisho.

SEHEMU YA PILI

Mheshimiwa Spika, Sehemu hii inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa, Sura 407 (The Local Authorities Pensions Fund, Act, Cap.407).

Mheshimiwa Spika, Baada ya kupitia sehemu hii kwa makini, Kamati inashauri marekebisho yafuatayo yafanyike ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa Sheria hii.

(i) Kifungu cha 2 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa ambacho hakikuletwa kwenye marekebisho haya, kirekebishwe ili kuruhusu mfuko kusajili wanachama kutoka katika sekta rasmi na isiyo rasmi kama ilivyofanyika katika Muswada huu kifungu cha 79 cha Sheria ya Mfuko wa Mashirika ya Umma na kifungu cha 120 cha Sheria ya Mafao ya Hitimisho la Utumishi wa Umma.
(ii) Kifungu cha 4 cha Muswada kinachofanya marekebisho kwenye kifungu cha 3 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa, tafsiri ya neno “employee” haijitoshelezi hivyo, iongezwe tafsiri iliyopo katika kifungu cha 61 cha Sheria ya Taasisi za Kazi (Labour Institutions Act, 2004) ili kupanua tafsiri ya nani ni mfanyakazi na hivyo kupanua wigo wa wafanyakazi wengi zaidi kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii. Aidha, marekebisho haya yafanyike sehemu zote ambapo neno ‘employee’ limetafsiriwa katika Muswada huu.

Aidha, Kamati inashauri tafsiri ya neno actuarial valuation iwe moja katika mifuko yote kuliko ilivyo sasa ambapo kila mfuko una tafsiri yake.

(iii) Kifungu cha 7 cha Muswada kinakusudia kufanya marekebisho katika kifungu cha 8 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa kwa kuongeza kifungu kipya cha (3) ambacho kinaelezea muda wa Mkurugenzi Mtendaji kushika ofisi kwamba ni kipindi cha miaka mitano na anaweza kuongezewa miaka mingine mitano kama itaonekana inafaa. Kamati inashauri neno ‘shall’ lililopo kwenye mstari wa pili lifutwe na badala yake liandikwe neno ‘may’ ili uteuzi wake kwa mara ya pili utegemee utendaji wake wa kazi kwa kuzingatia Sheria zilizopo sasa na Mkataba wa ajira.

Marekebisho haya yafanyike pia kwenye vifungu vya Muswada vya 32, 42, 85, 129 na 144 ambavyo vinahusu uteuzi wa wakurugenzi wa Mifuko yote ya Hifadhi za Jamii.

(iv) Kifungu cha 13 cha Muswada kinachofanya marekebisho katika kifungu cha 27 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa kwa kuongeza kifungu kipya cha 27A kinachoongelea kuhusu kutoa ‘bonus’ kwa mtumishi ambaye amefikisha umri wa miaka sitini na anaendelea kuchangia kwenye Mfuko, Kamati imeona kifungu hiki ni kizuri na ni vema ikaangaliwa namna ya kuingizwa katika mifuko yote ya hifadhi ya jamii.

Aidha, Kifungu cha 28 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa ambacho katika Muswada huu hakijafanyiwa marekebisho kifanyiwe marekebisho kwa kufuta maneno “commuted pension” yaliyopo kwenye kifungu 1; na kuongeza maneno “subject to subsection (1)” mwanzoni mwa kifungu cha 2 na kuacha neno ‘gratuity’ ambayo ndiyo anayotakiwa kupewa mwanachama anayekufa akiwa kazini lakini amechangia kwa kipindi chini ya miezi 180.

(v) Kifungu cha 18 cha Muswada ambacho kinafanya marekebisho katika kifungu cha 38 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa, kuwezesha mfuko kurudisha fedha ambazo mwanachama atakuwa amezidishiwa (overpaid). Kamati inashauri kifungu hiki pia kizungumzie suala la mwanachama kupunjwa (underpaid) iwapo litajitokeza. Aidha, kutokana na mwanachama kupunjwa, Kamati inapendekeza Mfuko kulipa mafao yote ya mwanachama pamoja na penult ya asilimia mbili (2%) ya mafao yote ya mwanachama.

(vi) Kifungu cha 19 cha Muswada kimefanya marekebisho machache ya kifungu cha 39 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa, Kamati inakubaliana na Kifungu hiki kwakuwa kinamruhusu mwanachama aliyeacha kuchangia kwa kipindi fulani kurejea. Vilevile, kitamsaidia mwanachama kupata mafao yake kana kwamba hakuwa ameacha kuchangia.

(vii) Kifungu cha 21 cha Muswada kinachofanya marekebisho kwenye kifungu cha 49 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa, ambacho kinaongelea kuhusu mfuko kuwekeza fedha za wanachama, Kamati inashauri kwamba ni vema sasa mfuko kuanza kuwafaidisha wanachama kutokana na uwekezaji huo kuliko hivi sasa mfuko kuwekeza katika biashara mbalimbali hasa za ujenzi lakini faida kwa mwanachama haionekani.
(viii) Kifungu cha 28 cha Muswada kinachofanya marekebisho kwenye jedwali la kwanza, ambacho kinaongelea kuhusu muundo wa Bodi, Kamati hairidhishwi na Bodi kuwa na uwakilishi wa wajumbe saba tu. Kwa mujibu wa maelezo ya Serikali kuwa idadi hiyo imetokana na suala zima la kutaka kupunguza gharama za uendeshaji. Kamati inashauri badala ya kupunguza idadi ni vema suala la malipo ya wajumbe liangaliwe upya.

Aidha, Kamati inashauri idadi ya Wajumbe iwe ni kuanzia wajumbe saba hadi tisa kulingana na ukubwa wa mifuko ili kuwa na uwakilishi mzuri wa waajiri, wafanyakazi na wataalam. Aidha, marekebisho haya yafanyike kwenye muundo wa bodi zote za mifuko ya hifadhi za jamii.

Vilevile katika kifungu kidogo cha (e) yaongezwe maneno “members representing the most representative employers association” ili uwakilishi utoke kwa chama chenye wanachama wengi kwa mujibu wa Mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO). Marekebisho haya pia yafanyike katika Kifungu cha 76(1) (b), Kifungu cha 118 (1) (c) na 136 (1) (f).

(ix) Kifungu cha 31 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa, kinachozungumzia kuhusu maslahi ya mwanachama kujitoa kwenye mfuko kwa sababu ya ndoa au uzazi, hakijafanyiwa marekebisho, Kamati inapendekeza kifanyiwe marekebisho ili kutoruhusu wanachama wanawake kujitoa kwenye uanachama kwa sababu ya ndoa au uzazi ili kwenda sambamba na dhana nzima ya hifadhi ya jamii.

(x) Kifungu cha 37 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa hakijafanyiwa marekebisho, Kamati inapendekeza kufanya marekebisho ili kuwezesha wastaafu kuwa na uhuru wa kuchagua kulipwa kwa mkupuo (lump sum) iwapo haitazidi asilimia 50 (50%) ya akiba na riba yake na asilimia 50 (50%) inayosalia alipwe kwenye malipo ya kila mwezi.

SEHEMU YA TATU

Mheshimiwa Spika, Sehemu hii inakusudia kufanya marekebisho katika Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Sura 395 (The National Health Insurance Fund, Cap.395). Katika kuchambua na kupitia sehemu hii, Kamati inashauri, Kifungu cha 38 cha Muswada kinachokusudia kufanya marekebisho ya kifungu cha 43 cha Sheria ya Mfuko wa Taifa Bima ya Afya kwa kuongeza kifungu kipya cha (3), maneno yafuatayo yanamakosa ya kiuchapaji, neno ‘instate’ lifutwe badala yake liandikwe ‘instituted’ na neno ‘concert’ lifutwe badala yake liandikwe ‘consent’.

Mheshimiwa Spika, katika mabadiliko ya Sheria hii, Kamati haikuona kama kunahitajika marekebisho makubwa zaidi.

SEHEMU YA NNE

Mheshimiwa Spika, Sehemu hii inakusudia kufanya marekebisho katika Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, Sura ya 50 (The National Security Fund, Cap.50). Kamati inapendekeza yafuatayo:-

(i) Kifungu cha 48 cha Muswada kinaandika upya kifungu cha 18 cha Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, kwanza, Kamati inapendekeza kifungu cha 18 (1) kisitaje (Order Number XXXV), kwa vile (Order Number XXXV) inaweza kubadilika wakati wowote na hivyo kulazimu kurudi tena Bungeni kufanya marekebisho. Aidha, marekebisho haya yafanyike popote ilipotajwa (Order Number XXXV).

Pili, kifungu cha 18 (2) ambacho kinalazimisha Mfuko kupata idhini ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP) kabla ya kufungua mashtaka ya jinai, Kamati inashauri ili kuharakisha usikilizaji wa kesi za aina hii, DPP apewe mamlaka ya kuteua mtu atakayesimamia mashtaka haya kwa niaba yake.

(ii) Kifungu cha 68 cha Muswada kinachoandika upya kifungu cha 74 cha Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, Kamati inapendekeza kifungu kidogo cha (1) na (2) neno ‘may’ lisomeke ‘shall’ ili kuweka uzito katika jambo hili.

(iii) Kifungu cha 72 cha Muswada kinachorekebisha kifungu cha 82(3) cha Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii inapendekeza maneno ‘a’ au ‘any’ yaongezwe baada ya neno ‘where’ ili kuondoa utata.

SEHEMU YA TANO

Mheshimiwa Spika, Sehemu hii inakusudia kufanya marekebisho katika Sheria ya Mfuko wa Mashirika ya Umma, Sura 372 (The Parastatal Organisations Pensions Scheme, Cap.372). Kamati inapendekeza yafuatayo:-

(i) Kifungu cha 80 cha Muswada ambacho kinatoa tafsiri ya maneno mbalimbali yaliyotumika katika Sheria hii, Kamati inashauri maneno ‘actuarial valuation’ na ‘actuary’ yaliyopo mwishoni mwa ukurasa 44 wa Muswada yafutwe kwakuwa yameshatolewa tafsriri katika kifungu cha 80 (a).
Vilevile neno ‘member’ lililopo katika ukurasa wa 45 lifutwe kwakuwa limetolewa tafsiri katika ukurasa wa 46.

(ii) Kifungu cha 86 cha Muswada ambacho kinakusudia kufanya marekebisho katika kifungu cha 8 cha Sheria ya Mfuko wa Mashirika ya Umma, pamoja na marekebisho yaliyopendekezwa katika Muswada, Kamati inapendekeza kuongezwe marekebisho mengine ya kumlazimisha mwajiri yeyote atakayekuwa amemwajiri raia wa kigeni kupeleka michango yake kwenye mifuko ya hifadhi za jamii. Marekebisho haya yafanyike pia kwenye mifuko yote ya hifadhi jamii.

(iii) Kifungu cha 5 cha Sheria ya Mfuko wa Mashirika ya Umma ambacho kwenye Muswada huu hakijafanyiwa marekebisho, Kamati inashauri kifungu hiki pia kifanyiwe marekebisho ili kuruhusu wanachama ambao watakoma kuwa wanachama kwa sababu yoyote ile wakiwa hawajatimiza umri wa kustaafu, endapo wataajiriwa tena waruhusiwe kuwa wanachama.

(iv) Kifungu cha 21(4) cha Sheria ya Mfuko wa Mashirika ya Umma ambacho kwenye Muswada huu hakijafanyiwa marekebisho, Kamati inapendekeza kifanyiwe marekebisho kwa kukifuta kwakuwa marekebisho yaliyofanyika mwaka 2001 kwa Sheria Na.25 yaliondoa neno ‘National Insurance Corporation’ na kuweka neno ‘Fund’ kwakuwa kwa sasa hakutoweza kuwa na mgogoro kwani bodi na mfuko ni kitu kimoja.

SEHEMU YA SITA

Mheshimiwa Spika, Sehemu hii inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Mafao ya Hitimisho la Utumishi wa Umma, Sura 317 (The Public Service Retirement Benefit Act, Cap.371. Kamati inashauri, Kifungu cha 123 cha Muswada kinachofanya marekebisho kwenye kifungu cha 6 cha Sheria ya Mafao ya Hitimisho la Utumishi wa Umma kwa kukiandika upya, Kamati inashauri kuwa kifungu hiki kirekebishwe kwakuwa kimekwenda kinyume na kifungu cha 25 cha Sheria Na.8 ya mwaka 2008, ambacho kimeipa Mamlaka jukumu la kuweka viwango vya kuchangia na sio Bodi kama ilivyoandikwa kwenye Muswada.


SEHEMU YA SABA

Mheshimiwa Spika, Sehemu hii inakusudia kufanya marekebisho katika Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Sura 135 (The Social Security (Regulatory Authority) Cap.135. Kamati inashauri yafuatayo yafanyiwe marekebisho;-

(i) Kifungu cha 142 (b) cha Muswasda kinachokusudia kufanya marekebisho katika kifungu 7 cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kufuta kifungu kidogo cha (f) ambacho kinamwondoa mtaalamu wa masuala ya hifadhi ya jamii kuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi. Kamati inashauri kifungu hiki kisiondolewe kwani mjumbe huyu ni mwakilishi muhimu sana katika Bodi hii, ili kuisaidia masuala ya kitaalam yatakayokuwa yanaamuliwa na Bodi.

Vilevile, kifungu cha 142 (c) cha Muswada kinachokusudia kuongeza kifungu kipya cha 3 kwa kumfanya Mkurugenzi Mkuu kuwa Katibu wa Bodi, Kamati imekubaliana na maelezo ya Wizara kwamba huo ndio utaratibu kwa mashirika yote lakini ili kutenganisha jukumu la usimamizi na utendaji, Kamati inashauri kifungu hiki kitamke wazi kabisa kuwa Mkurugenzi huyu hatakuwa na haki ya kupiga kura kama ilivyowekwa kwenye kifungu cha 118(b) cha Muswada huu ambacho kinafanya marekebisho katika kifungu cha 6 cha Sheria ya Mfuko wa Mashirika ya Umma.

(ii) Kifungu cha 147 cha Muswada kinachofanya marekebisho katika kifungu cha 38 cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kwa kuongeza Kifungu cha 38A (2) a, Kamati inashauri Mwenyekiti wa Kamati hii awe ni afisa wa Serikali aliyestaafu au mtu yeyote ambaye hafungamani na upande wowote.

Vilevile katika Kifungu cha 38A.-(2) (d) neno ‘Commissioner for Labour’ lifutwe kwa kuwa kwa mujibu wa Sheria za Kazi hakuna cheo hicho badala yake liandikwe ‘Labour Commissioner’.

Aidha, Kifungu cha 38A.-(2) (e), Kamati inashauri kuwa idadi ya wawakilishi kutoka uwakilishi wa vyama vya wafanyakazi iongezwe kutoka mtu mmoja na kuwa watu wawili.

Vilevile Kamati inashauri kiongezwe kifungu (f) ili kuweka uwakilishi wa waajiri kwani dhana ya msingi ya utekelezaji wa Sheria hii inazingatia zaidi masuala ya utatu.

(iii) Kifungu cha 148 cha Muswada kinachokusudia kufanya marekebisho katika kifungu cha 47 (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kukifuta na kukiandika upya, Kamati inashauri ni vema kifungu cha zamani kikabaki kama kilivyo kwavile kinaendana na kifungu cha 48 ambacho kinaipa Benki mamlaka ya udhibiti na sio ushauri kama inavyofanywa na mabadiliko haya.

(iv) Kifungu cha 150 ambacho kinafanya marekebisho katika kifungu cha 49 cha Sheria Na.8 ya mwaka 2008 kwa kuongeza kifungu kipya cha 49A ili mamlaka iweze kutoza tozo kwa mifuko ya hifadhi ya jamii na pia kuwekeza kwenye hisa (share) na dhamana (securities).

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 49A.-(1)na (2), kwanza, Muswada haukueleza tozo kusudiwa litatoka wapi. Baada ya maelezo ya Serikali kuwa tozo inayopendekezwa litatokana na punguzo la fungu la fedha za matumizi ya kiutawala (administrative costs) kwenye mifuko husika na bila kuathiri michango ya wananchama, Kamati inakubaliana na marekebisho haya ya Serikali kuhusiana na dhana nzima ya tozo ili kuiwezesha mamlaka kuweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Pili, Muswada unapendekeza Waziri akishirikiana na Waziri wa Fedha na Benki ya Tanzania kuamua kiwango cha tozo kwa kutangaza kwenye Gazeti la Serikali bila kuwashirikisha wadau. Kamati inashauri kifungu hiki kifanyiwe marekebisho ili kumlazimisha Waziri kisheria kushirikisha wadau.

Tatu, kifungu cha 49A.-(5) kinachohusiana na suala la Mamlaka kupewa uwezo wa kuwekeza kwenye hisa na dhamana. Kamati inapendekeza kuwa kifungu hiki kifutwe kwa vile kinakwenda kinyume na lengo kuu la kuanzishwa kwa mamlaka na majukumu yake kama yalivyoorodheshwa kwenye kifungu cha 5 cha Sheria ya Na. 8 ya mwaka 2008 ambapo jukumu hili halipo kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Pia kuiruhusu Mamlaka kuingia kwenye uwekezaji, itakuwa inaingilia shughuli zinazofanywa na Mifuko ambayo Mamlaka ndiye mdhibiti.

SEHEMU YA NANE

Sehemu hii inakusudia kufanya marekebisho katika Sheria ya Bima, Sura ya 394 (The Insurance Act, Cap.394). Kamati imepitia sehemu hii na haikuwa na tatizo hivyo inakubaliana na mapendekezo yaliyoletwa na Serikali.

MAONI YA JUMLA

Pamoja na kutoa mapendekezo ya jumla ya Muswada, Kamati ina maoni mengine ya ziada kwa ajili ya utekelezaji bora wa Sheria za Hifadhi ya Jamii kwa manufaa ya wanachama wake.

(i) Kwakuwa mchakato wa kuiweka mifuko ya Hifadhi za Jamii chini ya Wizara moja ni wa muda mrefu na inasisitizwa pia na Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii, Kamati haikuona sababu kwa nini marekebisho ya Muswada huu hayakuja na pendekezo la kisheria la kuiwajibisha mifuko kuwa chini ya Wizara moja. Kamati inashauri ili kuwa na uendeshaji bora wa mifuko ya Hifadhi za Jamii, ni wakati muafaka sasa Mifuko hii ikawajibika chini ya Wizara Kazi na Ajira, tofauti na sasa ambapo mifuko iko katika Wizara mbalimbali.

Aidha, kwakuwa Kamati inapendekeza mifuko yote ya hifadhi ya jamii kuwajibika chini ya Wizara yenye dhamana ya Hifadhi ya Jamii ambayo kwa sasa ni Wizara ya Kazi na Ajira, ni vema ikaanzishwa Idara maalum ndani ya Wizara itakayoshughulika na Hifadhi ya Jamii ili kuweza kusimamia utekelezaji wa shughuli hizi katika ngazi ya Wizara kwa vile kwa sasa Idara hiyo haipo.

Vilevile inapendekezwa kifungu cha 5(1)(e), (f) na (i) cha Sheria Na.8 ya mwaka 2008 kinachoelezea majukumu ya Mamlaka kifanyiwe marekebisho ili majukumu haya yafanywe na Wizara ya Kazi na Ajira chini ya Idara inayopendekezwa ya Hifadhi ya Jamii kwa sababu ni ya kisera zaidi na sio la kiutendaji. Hii ni kutokana na ukweli kwamba jukumu kuu la mamlaka ni kudhibiti mifuko ya hifadhi ya jamii, masuala ya kisera ya jinsi ya kuiboresha sekta hii ni ya Wizara.

(ii) Kwakuwa fomula ya ukokotoaji wa mafao ya mwezi ni tatizo kwani kila mfuko una utaratibu wake hivyo kusababisha viwango vya pensheni kutofautiana kwa kiwango kikubwa. Kamati inashauri Mamlaka (SSRA) iliangalie suala fomula kwa kina na kwakuzingatia yafuatayo:-

 kiasi cha juu cha miaka ambayo mtumishi ametumikia,
 muda wa kuishi baada ya kustaafu (commuting factor),
 mshahara wa mwisho aliostaafu nao,
 pensheni irekebishwe kutokana na mporomoko wa thamani ya fedha na mfumuko wa bei
 uzingatie kipindi mtumishi alichokuwa kazini katika sehemu mbalimbali.
 kiwango cha pensheni kisipungue asilimia 70 ya pato la mtu kutokana na ngazi yake.

(iii) Kwakuwa Kifungu cha 30 cha Sheria Na.8 ya mwaka 2008 kinatoa uhuru wa watumishi wanaoajiriwa kwa mara ya kwanza au ambao hawajaandikishwa katika mifuko ya Hifadhi ya Jamii kujiunga na mfuko wowote wa hifadhi ya jamii, Kamati inashauri waajiri wote nchini kuwapa nafasi watumishi wao kuchagua mifuko wanayotaka kujiunga nayo kuliko ilivyo sasa ambapo mbali na kuwepo kwa kifungu hiki bado watumishi wengi hawana uelewa na hawaeleweshwi kama kuna uhuru huo.

Aidha, kwa vile sasa mifuko imeruhusiwa kupata wanachama kutoka sekta isiyorasmi basi ni vema Mifuko ikajiandaa vyema kwa kuwawekea mazingira mazuri ambayo yatawanufaisha.

(iv) Vilevile, suala la mwanachama kuruhusiwa kuhamia mfuko mwingine liruhusiwe na lisiathiri mafao yake, jumla ya vipindi alivyochangia ndiyo vitumike.

(v) Pamoja na kwamba mifuko imeruhusiwa kuwekeza lakini mpaka sasa Kamati haijaona faida inayokwenda kwa wanachama kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na mifuko hii. Hivyo basi, Kamati inashauri ni wakati muafaka sasa mifuko kujielekeza zaidi katika kuboresha maslahi ya wanachama wake kutokana na uwekezaji huo.

(vi) Iwapo Muswada huu utapita na kuwa Sheria, Kamati inapendekeza ni vema marekebisho yote haya yakachapishwa na kuingizwa kwenye Sheria husika na kutolewa upya ili kuondoa usumbufu wa kusoma sheria Mama na mabadiliko haya. Hii itasaidia uelewa wa wanachama na wadau.

(vii) Kwa vile ripoti za tathmini ya afya ya kifedha ya mifuko (actuarial reports) hupelekwa kwenye Bodi za Mifuko husika, Kamati inashauri Wajumbe wa Bodi waone wajibu wa kuwajulisha wanachama wao juu ya ripoti hizo ili wajue hali halisi ya mifuko yao.


(viii) Mafao ya kifo yanayotolewa kwa sasa kwa wategemezi, Kamati inashauri yaendelee mpaka mjane au mgane afariki na mpaka wategemezi watakapofikisha umri wa kujitegemea.

(ix) Kwa kuwa mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Na.102, umeorodhesha mafao tisa ambayo mwanachama anapaswa kupewa, Kamati inashauri kuwa ni vyema mifuko kujielekeza kwenye kutekeleza mkataba huo na vigezo vya ushindani viwe ni mafao ya ziada.

Aidha, fao la tiba ambalo lipo kwenye mkataba huo wa kazi, inashauriwa litolewe kwa wastaafu wote ambao walikuwa wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii.

(x) Utaratibu wa sasa ambapo watumishi waliopo kwenye mkataba mara wamalizapo muda wao kulipwa pensheni na wakati huo huo kuongezewa mkataba mwingine. Kamati inaona utaratibu huu unaliingizia Taifa hasara na inapendekeza mtumishi akiongezewa Mkataba asilipwe kiinua mgongo mpaka pale atakapomaliza muda alioongezewa.


Mheshimiwa Spika, Kamati inaishukuru Serikali kwani mapendekezo mengi ya Kamati yamezingatiwa katika Jedwali la Marekebisho.

MWISHO

Mheshimiwa Spika, Kamati inaamini kuwa, Muswada huu umebeba maoni mengi ya wadau, na bila shaka utakapokuwa Sheria kamili, Kamati inaishauri Serikali, Kanuni zitakazotungwa zizingatie maoni ya Wadau na endapo kuna maeneo yanayohitaji marekebisho, Serikali isisite kuleta mabadiliko mbele ya Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii naomba kukushukuru wewe binafsi kwa kunipatia nafasi ya kuwasilisha maoni ya Kamati yangu, pia namshukuru Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge. Aidha ninapenda kumshukuru Mheshimiwa Gaudentia Mugosi Kabaka, (Mb) Waziri wa Kazi na Ajira, Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Milton Makongoro Mahanga, (Mb) na wataalam wa Wizara wakiongozwa na Katibu Mkuu Ndugu Eric Francis Shitindi kwa ushirikiano walioipatia Kamati.

Mheshimiwa Spika, Kwa namna ya pekee naomba niwashukuru wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii kwa michango na mapendekezo yaliyoboresha muswada huu. Ninapenda kuwatambua Wajumbe wa Kamati hii kwa majina:-

1. Mhe. Jenista Joakim Mhagama, Mb, Mwenyekiti
2. Mhe. Juma Selemani Nkamia, Mb M/Mwenyekiti
3. Mhe. John Damian Komba, Mb Mjumbe
4. Mhe. Mch. Dkt. Getrude P. Rwakatare, Mb “
5. Mhe. Agnes Elias Hokororo, Mb, “
6. Mhe. Fatuma Abdallah Mikidadi, Mb “
7. Mhe. Mary Pius Chatanda, Mb “
8. Mhe. Moza Abedi Saidy, Mb “
9. Mhe. Donald Kevin Max, Mb “
10.Mhe. Joseph Osmund Mbilinyi, Mb “
11.Mhe. Hamad Ali Hamadi, Mb “
12. Mhe. Abdallah Sharia Ameir, Mb “
13. Mhe. Salum Khalfan Barwany, Mb “
14. Mhe. Mariam Salum Msabaha, Mb “
15. Mhe. Assumpter Nshunju Mshama, Mb “
16. Mhe. Asha Mohamed Omari, Mb “
17. Mhe. Ramadhani Haji Salehe, Mb “
18. Mhe. Rebecca Michael Mngodo, Mb “
19. Mhe. Said Mohamed Mtanda, Mb “
20. Mhe. Abdallah Haji Ally, Mb “
21. Mhe. Hussein Mussa Mzee, Mb “
22. Mhe. Livingstone Joseph Lusinde, Mb, “

Mheshimiwa Spika, namshukuru Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilillah na Ofisi yake kwa kuiwezesha Kamati wakati wote ilipokuwa inatekeleza majukumu yake. Vilevile makatibu wa Kamati Ndugu Hosiana John na Ndugu Asia Minja kwa kuratibu kazi za Kamati.

Mheshimiwa Spika, Naunga mkono Muswada na naomba kuwasilisha



Jenista Joakim Mhagama, Mb
MWENYEKITI
KAMATI YA MAENDELEO YA JAMII
13 Aprili, 2012

No comments: