Thursday, January 12, 2012

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII




TAARIFA KWA UMMA

MSIMAMO WA WIZARA KUHUSU UGAWAJI WA

VITALU VYA UWINDAJI‏

UGAWAJI WA VITALU HAUTARUDIWA

Wizara ya Maliasili na Utalii haina mpango wa kurudia ugawaji wa vitalu. Mchakato wa ugawaji ulikamilika mwezi Septemba mwaka jana (2011) na matokeo yake kutangazwa wazi.

Mapema mwezi Septemba 2011, Wizara ilitoa orodha ya kampuni 60 zilizofanikiwa kugawiwa vitalu. Kati ya kampuni hizo, kampuni 51 ni za kizalendo na kampuni 9 za kigeni kwa kuzingatia kifungu 39(3)(b) cha sheria ya wanyamapori Na. 5, ya 2009.

Hata hivyo, kumekuwa na taarifa mbalimbali zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu kuwepo kwa harakati zinazofanywa na waombaji waliokosa vitalu zikihusisha kuchafuana baina ya kampuni zilizopata na zilizokosa kwa nia ya kuzorotesha sekta ya uwindaji wa kitalii kwa ujumla. Vyombo hivyo vimeripoti kuwa mchakato wa ugawaji wa vitalu utarudiwa.

Wizara inasisitiza kuwa mchakato wa ugawaji wa vitalu hautarudiwa na watanzania wanahakikishiwa kuwa hatua zilizochukuliwa na serikali za kuleta mabadiliko kwenye sekta hii tangu mwaka 2008, zimesaidia sana kuimarisha usimamizi wa Sekta hii.

Kuna mabadiliko zaidi ya 21 yaliyofanyika tangu wakati huo kwa kuzingatia Sheria ya Wanyamapori, hivyo kufanya isiwe rahisi kwa mtu au kikundi cha watu kufanya tofauti (yaani, the dicretionary powers of decision makers have been seriously controlled).

Aidha, Wizara imesikitishwa na taarifa zilizoripotiwa na gazeti moja la kila siku toleo la tarehe 10/1/2011 likinukuu taarifa kutoka Dallas, Marekani kwamba zoezi la ugawaji vitalu litarudiwa kwa shinikizo la Ikulu.

Madai hayo siyo kweli na kwamba Wizara haijapokea maelekezo yoyote kutoka Ikulu wala sehemu nyingine yoyote kuhusiana na suala hili la vitalu.

Wizara inasisitiza kuwa waombaji waliopata vitalu wamehakikiwa na Waziri na kuwa barua walizopokea kutoka Wizarani kuhusu kugawiwa vitalu ni nyaraka halali za Wizara.

KABLA YA SHERIA MPYA YA WANYAMAPORI

Kabla ya 2008, taratibu za uendeshaji wa tasnia ya uwindaji wa kitalii zilijumuisha vipengele vifuatavyo ambavyo vilikuwa na mapungufu:

Ukubwa (size) wa vitalu ulikuwa hauna ukomo kisayansi kuzingatia rasilimali zilizopo;
Bei ya vitalu ilikuwa moja kwa vitalu vyote;
Hayakuwepo madaraja ya ubora wa vitalu;
Vitalu vilikuwa vinatolewa na Mkurugenzi wa Wanyamapori;
Hakukuwepo ushauri wowote ambao Mkurugenzi alilazimika kupewa na mtu au kikundi chochote kinachotambulika kisheria, kabla ya kumgawia mwombaji kitalu;
Hakukuwepo uwazi juu ya uombaji, kama vile vigezo/sifa za waombaji na utaratibu wa ugawaji;
Kampuni za uwindaji ziliruhusiwa kuwa na idadi ya vitalu bila ukomo;
Kampuni za uwindaji, ambazo 95% zilikuwa za wageni kwa hazikuwa na ulazima wa kuwa na watanzania.
Kampuni za uwindaji hazikuwa na ulazima wa kuwa na wawindaji bingwa watanzania.
Kulikuwa hakuna upekuzi kujiridhisha kuhusu utendaji kazi wa kampuni kabla ya kupewa kitalu;
Kampuni ziliruhusiwa kuuza hisa zake na vitalu vilikuwa 'tradeable assets' za kampuni. Pia Serikali haikuwa na namna ya kujua mikataba kati ya kampuni zilizouziana vitalu;
Hakukuwa na ulazima kwa kampuni za uwindaji kuwa na watanzania kama wanahisa wake;
Hakukwa na ukomo wa idadi ya kampuni za kigeni kumiliki vitalu;
Bei ya nyara ilikuwa chini na ilidhibitiwa na wawindani kupitia chama chao cha TAHOA.;
Mwombaji wa Kitalu alilazimika kuwa na vifaa kabla ya kugawiwa kitalu;
Waziri au Mkurugenzi alikuwa hana mamlaka ya kuvunja mkataba kabla ya muda wa mkataba wa miaka 5 kuisha hata pale ambapo muhusika alifanya mambo kinyume na taratibu;
Kampuni za uwindaji hazikulazimika kulipa deposit yoyote kwa kila mgeni anapokuja kwa kila siku ya safari;
Haikuwa dhambi au marufuku kukodisha kitalu kwa mtu mwingine tofauti na mtu au kampuni iliyoomba na kuingia makubaliano na serikali;
Kampuni za uwindaji hazikuwekewa kiasi cha chini cha kuchangia jamii jirani na vitalu;
Rekodi ya utii wa sheria, uchangiaji jamii, uchangiaji wa shughuli za kupambana na ujangili, ulipaji kodi, uwekezaji/utunzaji wa kitalu husika haikuzingatiwa katika kufikiria maombi ya wawindaji kabla ya kugawiwa vitalu/kitalu;
Hakukuwa na vigezo vya kuhakikisha vitalu vya aina tofauti tofauti vinatolewa kwa mwombaji.

UTEKELEZAJI WA SHERIA MPYA YA WANYAMAPORI

Tangu mwaka 2008, serikali imefanya mabadiliko makubwa kwenye tasnia hii ya uwindaji wa kitalii kwa kurekebisha vipengele vyote 21 vya taratibu za awali kwa lengo la:

(i) Kuongeza wigo wa Watanzania kushiriki kwenye tasnina hii;

(ii) Kuongeza mapato ya Serikali;

(iii) Kuongeza uwazi na uwajibikaji;

Mabadiliko haya, yaliyoanzia kwenye azimio la Bunge na baadaye kuingizwa kwenye Sheria ya Wanyamapori Na. 5, ya 2009, na Kanuni zake, sasa yamekamilika na utekelezaji wa sheria kwa kuzingatia mabadiliko haya unaendelea.

Mabadiliko ya vipengele vyote 21 yamefanyika kwa kuzingatia Sheria ya Wanyamapori Na. 5, ya mwaka 2009 na Kanuni zake za mwaka 2010.

Kwa mfao, yafuatayo yamefanyika kama sehemu ya utekelezaji wa sheria hii.
Sheria ya Wanyamapori na 5 ya 2009 ilipitishwa ikiwa na mabadiliko muhimu katika sekta hii;

Tathmini ya vitalu ilifanyika na kuwekwa kwenye madaraja matano ya ubora.;

Serikali iliweka kipindi cha mpito cha mwaka 2009-2012 ili kuruhusu mabadiliko kufanyika. Ilipangwa kuwa wawindaji wa mwaka 2013 wapatikane mwaka 2010-11, ili waanze maandalizi hadi msimu wa uwindaji wa Julai 2013;

Kanuni za Uwindaji wa Kitalii za 2010 zimekamilika;
Mwezi February 2011, vitalu 156 vilitangazwa ili viweze kuombwa na wale ambao wangevihitaji;

Kamati ya watu 12 ya kumshauri Waziri juu ya ugawaji wa vitalu iliteuliwa na kufanya kazi yake. Kamati ilimshauri Waziri kuhusu Vitalu 156 na waombaji 91 ambao walijitokeza;

Kamati ilipendekeza kuwa muda uongezwe ili upekuzi wa kina ufanyike kuhusu dhamana, uraia, ulipaji kodi na uhalali wa kampuni zilizoomba ukamilike kwa kuhusisha vyombo vyenye mamlaka na uwezo wa kusemea maeneo hayo, kama vile Idara ya Uhamiaji;

Aidha, wakati kazi ya upekuzi ikiendelea, kamati ilishauri kwa vitalu 22 ambavyo havikupata waombaji wenye sifa vitangazwe tena ili zoezi la upekuzi lihusishe pia waombaji wa vitalu hivi (22) ili kuokoa fedha na muda. Waziri aliafiki mapendekezo hayo;

Muda wa kutangaza waliogawiwa vitalu uliongezwa kwa siku 90 hadi Sept 10, 2011. Aidha, vitalu 22 vilitangazwa tarehe 20 juni 2011 na waombaji kupewa hadi julai 19, 2011 wawe wamefikisha maombi panapohusika.
MAAMUZI YAMEZINGATIA SHERIA

Kufuatia sheria na kanuni mpya zilizopo, msimamo wa Wizara ni kama ifuatavyo:

Wizara inaamini kuwa vielelezo vilivyowasilishwa na waombaji na taarifa ya ukaguzi na upekuzi uliofanywa na kamati ya ushauri kwa waombaji wote kwa zaidi ya siku 180 ni sahihi na zilifanyika kwa mujibu wa sheria;
Maamuzi ya Waziri yamezingatia sheria na mipaka ya madaraka yake kama Waziri mwenye dhamana ya sekta husika. Wizara inawasihi wahusika wote wafuate utaratibu wa kisheria katika kuwasilisha malalamiko na vielelezo vyao;
Mabadiliko yaliyofanyika ni sahihi. Wizara inawasihi wadau wote wa tasnia ya uwindaji wa kitalii, kuunga mkono mabadiliko yaliyofanyika maana yamefanyika kwa kuzingatia sheria;
Baada ya matokeo ya mchakato wa ugawaji kutangazwa, kampuni zikizofanikiwa kupata vitalu ziliandikiwa barua kuarifiwa kuhusu uamuzi huo na vitalu walivyopewa kwa mujibu wa sheria;

Matokeo hayo yalipokelewa kwa furaha na waombaji watanzania ambao walipata fursa ya kutumia utajiri wa nchi yao kama mtaji wao;

Maamuzi haya pia yalipongezwa kwa kuzingatia azimio la Bunge kuhusu hoja Binafsi ya Mzindakaya ya 2008 na baadaye sheria ya Wanyamapori Na. 5, 2009;

Vilevile, matokeo hayo yalipongezwa na kuungwa mkono na Chama cha wawindaji TAHOA maana yalizingatia sheria.

HITIMISHO

Wizara inasisitiza kuwa wadau wote watapaswa kuzingatia sheria katika kuvitumia vitalu walivyopewa kwa kuwa sheria inatambua kuwa vitalu ni mali ya serikali kwa dhamana ya Waziri. Kama kuna malalamiko yoyote ni vema yafuate taratibui za kisheria.

Hadi sasa Kampuni kadhaa zimetumia fursa za kisheria kuomba mapitio ya maamuzi ya Waziri (administrative review). Kwa mujibu wa sheria, maombi haya ya administrative review hupelekwa kwa Kamati ya Ushauri kuhusu Vitalu kwa maoni kabla ya Waziri kutoa uamuzi wa mwisho. Sheria haijaweka ukomo wa kupokea malalamiko wala ukomo wa muda wa kushughulikia malalamiko hayo. Kazi ya kupitia malalamiko hayo inaendelea.

Hata hivyo, zoezi la administrative review ni la kawaida na husaidia kufanyika marekebisho madogo kadiri ushahidi utakavyowasilishwa wala halilengi KUBATILISHA MAAMUZI YOTE ya awali.

Pia, kama itaonekana kuwa Wizara imetafsiri vibaya sheria, hivyo kutomtendea haki mwombaji ni vema mhusika aende Mahakamani.

Wizara anakumbusha pia kuwa mtumiaji wa kitalu ni kama mpangaji tu, hivyo dhana kwamba kampuni fulani imekuwa na kitalu fulani kwa muda mrefu hivyo kujijengea imani kwamba kitalu husika ni cha kampuni hiyo siyo sahihi. Vitalu vyote ni mali ya Serikali.

Vilevile, kumekuwepo tuhuma kupitia vyombo vya habari kwamba baadhi ya waombaji waliokosa vitalu wanafanya njama za kughushi baadhi ya nyaraka ili kubadili sura za maombi yao ya awali.

Wizara inatahadharisha kuwa vitendo hivyo, kama vinafanyika ni kinyume na sheria, na Wizara ikijiridhisha kwamba nyaraka zozote zilizowasilishwa siyo sahihi au ni za kugushi, itawachukulia hatua za kisheria wahusika. Hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na kuwafutia watuhumiwa ugawaji waliokwishapata, hata kwenye vitalu vingine kama wanavyo na kuwashitaki mahakamani.

Mwisho, Waziri wa Maliasili na Utalii ataunda Kamati ya Kutathmini Matumizi ya Vitalu 'blocks utilization monitoring comittee'. Kamati hii itakuwa inafanya ukaguzi na uperembaji wa matumizi ya vitalu vilivyokodishwa kwa kuzingatia sheria kwa muda wote wa ukodishaji na kumshauri Waziri kuhusu hatua za kuchukua kwa waombaji watakaovunja sheria.

George Matiko

MSEMAJI

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

12 Januari 2012

No comments: