Tuesday, December 20, 2011

MAKALA ILIYOZAA KESI YA KIBANDA, TAMKO LA JUKWAA LA WAHARIRI JUU YA KESI HIYO


Na Samson Mwigamba

MAKALA hii ilikuwa itoke Jumatano ya wiki iliyopita lakini kwa sababu za kiufundi ikashindikana. Imekuwa ni bahati nzuri kwamba inapotoka leo, ijibu swali la askari polisi dereva wa gari la maji ya kuwasha.

Askari huyo alimweleza Mwalimu Mkuu wa watu jinsi roho inavyomuuma pale anapowamwagia Watanzania wenzake maji hayo ya kuwasha wakati wakidai haki yao. Askari uliyeuliza na wenzako wote someni makala hii kwa utulivu. Huu ni waraka maalumu kwa askari wote wa majeshi yote vikosi vyote Tanzania Bara na Visiwani.

Kwa lugha ya wazi zaidi nazungumza na askari wa Jeshi la Polisi Tanzania, Askari wa Jeshi la Kujenga Taifa, askari wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM),  askari wa Jeshi la Magereza na wale wa Jeshi la Wananchi (JWTZ).
Kuwa mwanajeshi lolote kati ya hayo niliyoyataja si dhambi na si kweli kwamba kuwa mwanajeshi kunakuondolea uwezo wa kufikiri na badala yake ukawa unafikiriwa na watu wengine.

Wala haimaanishi kuwa askari kuwa kama robot ndio nidhamu bora kuliko zote duniani. La hasha! Mimi nilikataa utumwa huo!

Mwaka 1999 nilihitimu elimu ya cheti cha ufundi mchundo, yaani Full Technician Certificate (FTC) katika uhandisi wa Elektroniki na Mawasiliano ya Anga, yaani Electronics & Telecommunications Engineering kutoka Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT).

Nikiwa bado sijapata kazi ya maana, mwezi Aprili mwaka 2000 niliona tangazo la kazi ya Radio Technician katika Jeshi la Magereza. Nikatuma maombi na kuitwa kwenye usaili uliofanyika Chuo cha Maofisa wa Jeshi la Magereza Ukonga, Dar es Salaam mwezi Juni 2000.

Wote tuliofaulu usaili tulipangiwa siku ya kuripoti Chuo cha Magereza Kiwira kule Tukuyu, Mbeya.

Kufika kule nilishuhudia mambo ya ajabu. Ingawa wao hufurahia na kusema eti wanakutoa uraiani na kuwa mwanajeshi lakini baadhi ya matendo yanayofanyika wakati wa mafunzo ya jeshi ni ya kuwapumbaza askari wetu ili baadaye wakiwa kazini, watawala wawatumie watakavyo.

Nilishindwa kuvumilia kaulimbiu ya wakufunzi wa jeshi pale walipoelekeza kwamba chochote kruta (askari mpya mafunzoni) unachoambiwa lazima uitikie “ndiyo afande”. Nilishindwa kuitikia kwa mfano pale mkufunzi mmoja mwenye cheo cha koplo alipotutamkia mfululizo wa sentensi zifuatazo:
Mkufunzi: Nyinyi makruta mbona wote hamkuja na majembe?
Makruta: Ndiyo afande!
Mkufunzi: Hamkuambiwa makao makuu ya jeshi kwamba lazima mje na majembe?
Makruta: Ndiyo afande!
Mkufunzi: Kwa hiyo kwa kuwa hamkuambiwa na nyinyi hamkuyabeba?
Makruta: Ndiyo afande!
Mkufunzi:  Wote ni wapumbavu pamoja na mama zenu waliowazaa.
Makruta: Ndiyo afande!

Ni hayo pamoja na mambo mengine ya kulazimishwa kwenda kwenye kile kinachoitwa disko, ambapo pamoja na uchovu wa kutwa nzima wa kazi ngumu na nyingi bado ni lazima ukae hapo mpaka saa 4 usiku tena ukinyooshewa kidole tu na mwenzako lazima usimame na kuimbisha wimbo tena kwa tabasamu, wimbo mmoja wapo ukisema “Magereza ninavyokupenda nitakunywa sumu juu yako”, ndiyo yaliyonifanya nikakataa kazi ya jeshi baada ya wiki moja tu ya mafunzo.

Siku niliyokataa jeshi ilikuwa ni Jumatano asubuhi ambapo sikwenda mchakamchaka na wakati wenzako wanatawanyika kufanya usafi wa nje maeneo mbalimbali, mimi nilibeba begi langu na kuanza kuondoka chuoni majira ya saa moja na nusu hivi asubuhi.

Nilikamatwa na mkufunzi mmoja wa jeshi na kupelekwa pamoja na begi langu kwa Ofisa Mafunzo wa chuo. Aliponiuliza sababu nilimtajia mbili, kwanza kwamba sifurahii mambo ya jeshi na kubwa zaidi kwamba mimi ni Msabato na nimeambiwa na wenzangu kwamba hapa hakuna kwenda kusali, siku zote za juma ni kazi.

Kitu ambacho sitaweza maana Sabato takatifu lazima nipumzike! Bila kuuliza zaidi aliconclude kwa kuniambia kwamba, “Sijawahi kuona mtu anaacha kazi kwa ajili ya mambo ya dini.

”Ni dhahiri wewe ulikuja kutupeleleza na hivyo kazi yako imeisha sasa unataka kurudi. Tutakuweka rumande, tena ile ya polisi kwa wiki mbili wakati tunafanya upelelezi juu yako.”

Askari aliyenileta alianza kunivuta ili kunipeleka rumande lakini nilikataa huku nikiendelea kujieleza kwa ofisa mafunzo ili ajue kwamba sikuwa na mpango huo aliousema.

Baada ya kuelemewa na hoja zangu alinipeleka kwa makamu mkuu wa chuo ambaye yeye alitumia zaidi Biblia kunihubiri kwamba nakaidi amri ya mamlaka wakati hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu.

Jibu langu lilikuwa fupi na lenye msimamo mzito kwamba ikiwa mamlaka ya wanadamu inafika mahali inanena tofauti na Mungu, Mtume Petro ametuandikia kwamba katika hali ya namna hiyo, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko mwanadamu”.

Na yeye alinishindwa akanipeleka kwa mkuu wa chuo na wao wote wakiwapo. Ushauri waliokuwa wakimpa mkuu wa chuo ni kwamba mimi niwekwe rumande kwanza ili wafanye upelelezi. Lakini sikuyumba katika msimamo wangu.

Nilimweleza  mkuu wa chuo kwamba mimi ni raia  na si mpelelezi. Nilizirudia rudia sababu zangu za kuacha jeshi tena kwa ujasiri mkubwa na kumhakikishia mkuu wa chuo kwamba akinipa hayo ninayoyataka niko tayari kubaki jeshini.
Hatimaye kauli ya mwisho ya mkuu wa chuo ilikuwa ni hii: “Jeshi ni wito. Tunaweza kumlazimisha huyu kijana kuwa mwanajeshi lakini baadaye ikatuletea madhara makubwa sana.” Akamalizia kwa kusema, “chukueni maelezo yake kwa maandishi kisha arudishe vifaa vya jeshi.”

Wakati naondoka nilimsikia ofisa mafunzo akitoa maelekezo kwa walio chini yake kwamba mwanafunzi mwingine wa jeshi akija kuripoti na kwenye daftari akajaza kwamba ni Msabato, msimsajili kwanza mpaka aje kwangu! Sijui kama Wasabato wameendelea kupokewa kwenye hicho chuo cha magereza lakini ninachotaka askari wote wa majeshi yetu yote na vikosi vyote, ni kwamba askari unaweza kusimama kwa miguu yako na kufikiri kwa akili yako mwenyewe!
Ndugu zangu askari, nchi imefika mahali ambapo Waingereza hupenda kupaita ‘critical point’. Ni mahali ambapo wananchi wako tayari kwa mabadiliko na watawala wako tayari kwa mapambano ili kubaki madarakani.

Katika point hii askari wetu wanakuwa na nafasi kubwa ya aidha kuwezesha mabadiliko hayo kutokea kwa wakati wanaoutaka wananchi, tena kwa amani ama kuyachelewesha (si kuyazuia) na kusababisha yatokee baadaye kidogo kuliko wananchi walivyotaka, tena baada ya kumwaga damu nyingi ya Watanzania wasio na hatia!

Napenda kurudia kwamba hakuna jeshi lolote duniani hata kama tungekusanya majeshi yote ya dunia hii na kuyaleta Tanzania hawataweza kuizuia nguvu ya umma pale inapokuwa imeamua kufanya mabadiliko.

Napenda tena kurudia kwamba si lazima askari mfanye kile ambacho wakubwa wenu wanataka na kuwaamuru kufanya. Tunaweza kusimama imara na kutetea haki za Watanzania tukiwamo na sisi askari.  Niliwahi kugoma kutii amri ya kukamatwa na kuwekwa rumande.
Lakini pia mifano ni mingi na nisingependa kuchukua mifano kutoka nchi za Ulaya kama Uingereza ambako tulishuhudia wananchi wakiandamana mitaani na askari wao hawakuwahi hata kumpiga kofi tu mwandamanaji hata mmoja.
Walipohojiwa na vyombo vya habari walisema dhahiri kwamba waandamanaji ni raia halali  wenye haki ya kufanya kile wanachokifanya kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi yao. Katiba ya Tanzania na sheria za nchi hii zinatoa haki kama zile za Uingereza. Tofauti ni utekelezaji wa matakwa hayo ya kikatiba na kisheria. Watawala wa Uingereza wako tayari  hata kung’oka madarakani ili kutekeleza matakwa ya nguvu ya umma.

Lakini wale wa Tanzania wako tayari kung’oa uhai wa raia wengi ili mradi  kuzuia nguvu ya umma inayodai  haki na   wananya hivyo kwa sababu ya hofu ya kung’oka madarakani, jambo ambalo hawataki kabisa kulisikia. Na  ndugu zangu askari napenda kuwaambia kwamba yote yanafanywa na watawala wetu kwa kuwategemea nyinyi.

Wanaminya haki zenu nyinyi wenyewe, haki za wazazi wenu, dada na ndugu zenu,  marafiki zenu, jamaa zenu na majirani zenu. Chukulia mfano rafiki zangu Mtaki na Edwin. Tumesoma wote shule ya msingi pale Magu.

Nilichaguliwa kujiunga na Mazengo Sekondari, shule kubwa na ya muda  mrefu ambayo sasa imegeuzwa kuwa chuo kikuu bila mabadiliko ya majengo.

Shule iliyokuwa na maabara nne kwa maana ya maabara ya baiolojia, kemia, fizikia na  jiografia. Ilikuwa ni sekondari ya ufundi na hakuna karakana ambayo haikuwapo.

Shule iliyokuwa na walimu wa kutosha, vyumba vya kutosha vya madarasa na vya kulala mabwenini.
Katika bweni la Ujamaa kwa mfano, nilikokuwa naishi mimi, kuna vyumba kadhaa havikuwa na watu. Darasa la Form IVA ambalo nilikuwamo lilikuwa na wanafunzi 21 tu darasani.

Na mazingira mengine mengi ambayo sitaweza kuyataja hapa ambayo yanafanya wanafunzi wa leo wa Chuo Kikuu cha Mt. John wajiulize kama kweli ile ilikuwa ni shule ambayo haina maktaba wala vitabu vya kutosha, na mengineyo mengi mnayoyafahmu.

Nikafaulu kwa kiwango cha daraja la juu lililoniwezesha kuendelea mpaka chuo kikuu na kupata kazi nzuri kwenye Umoja wa Mataiifa.

Rafiki zangu nakumbuka mlivyoamua kujiunga na Jeshi la Polisi si kwa sababu mlipenda kazi hiyo ama kwamba mlikuwa na wito wa kuwa polisi kama mnavyodanganywa kwamba jeshi ni wito.

Nakumbuka mlijiunga huku mkilalamika kwamba mnalazimika kujiunga huko kwa sababu kiwango chenu cha ufaulu hakiwapi fursa ya kazi bora zaidi ya hiyo. Lakini mimi nawafahamu vizuri. Najua uwezo wenu wa darasani. Mliathiriwa na mazingira ya hovyo ya shule mlizosoma.

Rafiki zangu nyinyi wote leo ni wakuu wa vituo vikuu vya polisi vya wilaya katika wilaya za Mbozi na Igunga.
Leo hii mimi nimeacha kazi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kushiriki vema katika mapambano ya kutafuta ukombozi wa taifa hili.

Wadogo zenu na wadogo zangu mnawajua wako katika juhudi za kutafuta maisha lakini ni magumu. Wengine walikosa kabisa nafasi ya kujiunga hata na hiyo Magu Day.

Wakaishia Bulima na Kinango, ambako hali ilikuwa mbaya zaidi. Wakafeli kabisa na leo wanahangaika hapa na pale lakini watawala wanawawekea mazingira magumu mno ya kuendesha maisha.

Na sasa chukulia nao wametambua hali yao duni inasababishwa na watawala walafi na walaghai. Wamejaribu kutumia njia za kidiplomasia kudai haki zao wanakutana na watu wanaitwa wakuu wa wilaya na mikoa.

Wanaamua kuandamana, mnashiriki kuamrisha askari walio chini yenu kuwapiga na kuwaweka rumande na hatimaye kuwafungulia kesi za kubumba!

Askari wetu igeni mfano wa askari wa Misri! Pale wananchi walipoamua kuandamana kukomesha utawala wa kidhalimu wa miaka 30 chini ya  Hosni Mubarak, askari waliwalinda badala ya kuwapiga.

Walikataa kwa sababu hata wao walikuwa wakiumizwa na Mubarak lakini zaidi ya hayo, waliokuwa wakiandamana walikuwa ni dada zao na ndugu zao na marafiki zao.

Hivi sasa nchi iko njia panda. Ugumu wa maisha umeongezeka mara nne na zaidi. Watawala hawalioni hilo wala hawajishughulishi kurekebisha hali ya mambo hususan hali ya uchumi.

Wako busy na kujiandaa kwa uchaguzi wa 2015. Mawaziri wako busy na kampeni za kuteuliwa kuwa wagombea wa urais kupitia chama tawala hapo 2015 na rais naye yuko busy kuandaa mtu wake ambaye anadhani akimrithisha jumba jeupe la pale Magogoni atasema mwacheni Ndugu Kikwete apumzike kwa amani.

Taifa limeamua kuandika katiba mpya, rais na serikali yake na chama chake wameamua kuuteka mchakato ingawa haikuwemo kwenye ilani yao ya uchaguzi ili tu waturudishie katiba ya mwaka 1977 na kuipa jina juu ya jalada KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YA MWAKA 2014.

Natambua juhudi zinazoendelea hasa zikiongozwa na CHADEMA kujaribu kumkumbusha rais kwamba katiba iko juu yake na katiba ni mali ya wananchi na yeye anaajiriwa kwa katiba hiyo na si yeye kujiandalia katiba ili atawale kwa ulaini.

Lakini juhudi za kidiplomasia zikishindikana hapo ndipo itabidi haki ya watu idaiwe kwa maandamano na hapo askari wote tuungane na kuwa kama Misri, kwa kuwa Katiba mpya ni kwa masilahi yenu pia! Jaribuni kutafakari!





KUHOJIWA KIBANDA: TAARIFA YA JUKWAA LA WAHARIRI


UTANGULIZI

1. Ijumaa iliyopita, Mhariri Mtendaji wa Free Media Ltd, wazalishaji wa magazeti ya Tanzania Daima na Sayari, Absalom Kibanda alishikiliwa na kuhojiwa kwa saa kadhaa katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini.

2. Kiini cha tukio hili ni makala iliyochapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumatano, Novemba 30, 2011 ikiwa na kichwa kisemacho "Waraka maalum kwa askari wote".

3. Mwandishi wa makala hiyo, Samson Mwigamba ambaye tayari amekamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uchochezi analalamikia hulka ya polisi wa chini kutii amri hata kama amri hizo zina madhara kwa nchi na kwa mtizamo wake anasema hali hiyo inaweza kuifikisha nchi pabaya siku zijazo.

UTENDAJI WA VYOMBO VYA HABARI NCHINI

4. Umekuwa ni utamaduni kwa Msajili wa Magazeti ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) kuchukua hatua za kuvibana vyombo vya habari, hususan magazeti ambayo yamekuwa yakionekana kukiuka sheria za nchi katika uandishi wake.

5. Chini ya utaratibu huu ambao hata hivyo umekuwa ukilalamikiwa na wadau wa habari, Maelezo humwandikia barua Mhariri husika kuhusu kosa linalodaiwa kufanywa katika gazeti lake, na kutaka atoe maelezo au afike katika ofisi hizo kwa ajili ya kuhojiwa.

6. Kupitia Maelezo, hatua mbalimbali zimechukuliwa na pande husika ikiwa ni pamoja na magazeti kupewa barua za onyo, kupewa fursa ya kusahihisha taarifa husika na katika matukio machache yasiyopendeza baadhi yamewahi kufungiwa na mengine kufutwa kabisa.

7. Licha ya kasoro zake, jambo la msingi ni kwamba utaratibu wa Msajili wa Magazeti walau umekuwa ukitoa fursa watendaji wa magazeti yanayolalamikiwa kutoa maelezo ya upande wa pili lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba Uhuru wa Habari hauminywi kiasi cha kuukosesha umma taarifa muhimu za nchi na mambo yanayofanyika nchini.

KUKAMATWA KWA KIBANDA

Jukwaa la Wahariri limefuatilia kwa karibu sana tangu kukamatwa kwa Kibanda na mtindo uliotumiwa na Polisi katika kushughulikia suala hilo na kubaini yafuatayo:

8. Kwanza Makala ambayo ni chimbuko la kukamatwa kwa Mwigamba na baadaye Kibanda haikuwahi kulalamikiwa na Ofisi ya Msajili wa Magazeti kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwa taarifa nyingine nyingi, si kwa gazeti la Tanzania Daima tu, bali hata kwa magazeti mengine.

9. Kwa maana hiyo hakuna barua yoyote kutoka Maelezo ambayo iliwasilishwa Tanzania Daima ikimtaka Mhariri Mtendaji kutoa maelezo ya kimaandishi au kufika kwa msajili kujibu tuhuma za ukiukwaji wa maadili ama sheria katika makala hiyo ya Novemba 30, 2011.

10. Hakuna taarifa zozote za mtiririko wa kimatukio katika Idara ya Habari (Maelezo) au kwingineko Serikalini ambazo zinabainisha iwapo kulikuwa na onyo lolote kwa Tanzania Daima kuhusu mwenendo wake au kuhusu makala za Samson Mwigamba.

MTIZAMO NA MSIMAMO WA TEF

11. Kutokana na hali hiyo, TEF inaona kwamba kuna msukumo usio wa kawaida nyuma ya hatua ya Polisi ya kumhoji Kibanda na kwamba mwelekeo ni kuminya uhuru wa Habari na Uhuru wa kujieleza ambao umetolwa chini ya misingi ya Katiba ya nchi.

12. Msukumo huu unatokana na kuibuka ghafla kwa vyombo vya dola na zamu hii Polisi wakitumia muda mrefu katika kile walichokiita kuwa ni uchochezi, hivyo kuwafungulia wahusika KESI ZA JINAI.

13. Mashtaka haya dhidi ya Kibada na Mwigamba yanatushawishi kuamini taarifa zisizo rasmi juu ya kuwapo kwa mpango wa kuwashughulikia baadhi ya Wahariri na Waandishi wa Habari ambao wamekuwa msitari wa mbele kukosoa waziwazi miendendo ya watawala.

14. Sisi tunasema hali hii haikubaliki kwani inalenga kurejesha demokrasia ya Taifa hili nyuma zaidi ya miaka 50 iliyopita, kwa kuminya uhuru wa kujieleza na haki ya kutoa na kupata habari.

15. Mwenendo wa aina hii wa kuamu kuwashati wahariri kwa makosa ya jinai ni hatari kwa mustakabali wa nchi yetu, hasa pale vyombo vya dola vinapotumika kwa mtindo ambao umetumiwa kuwashughulikia Kibada na Mwigamba.

16. Ikumbukwe kwamba dhamira ya kupambana na wakosoaji wa utendaji Serikalini siyo tu kwamba inaathiri dhana nzima ya utawala bora wa nchi, bali inaliweka Taifa katika hatari ya kutumbukia katika uovu uliokithiri hasa pale wenye dhamana watakapofanya wapendavyo kwa kuwa tu vyombo vya habari vitakuwa vibezibwa midomo.

17. Kwa kuwa hii inaonekana kuwa dhamira rasmi ya Serikali kutumia dola kudhibiti uhuru wa habari, tunatoa mwito kwa watawala wetu kutafakari upya na ikiwezekana kuachana kabisa na dhamira hiyo.

NEVILLE MEENA,
KATIBU MKUU – TEF
KWA NIABA YA BODI YA JUKWAA LA WAHARIRI


4 comments:

Anonymous said...

MWANAMUZIKI WA NIGERIA, FELA LELA ANIKULAPO KUTI NAYE ALIJIKUTA KATIKA WAKATI MGUMU ALIPOWAKOSOA ASKARI KATIKA WIMBO WAKE WA 'ZOMBIE' AMBAPO ALIWAKUMBUSHA KUTUMIA AKILI WALIZO NAZO BADALA YA KUTEKELEZA TU YALE WANAYOAMBIWA NA WAKUBWA ZAO.WATAWALA HAWAPENDI KUKOSOLEWA JAMANI

Anonymous said...

Kuhusu hizo taarifa zisizo rasmi juu ya mkakati wa kuvimaliza vyombo vya habari na waandishi wenye mwelekeo wa kupenda kukosoakosoa 'system', jambo hili halikuanza leo.

Wakati wa vuguvugu la mageuzi 1991, 92, 93 hadi maeneo ya 1994, palikwapo waandishi waliowekea lebo hiyo. Katika orodha alikuwepo Kajubi Mukajanga, Stanley Katabalo, Stanley Kamana na waandishi wawili watu wadogowadogo.

System ya Tanzania ina vipaji vingi sana vya jinsi ya kumaliza watu.

Kajubi Mukajanga alichapisha waraka katika jarida lake lililoitwa WAKATi, ambao iliaminika kuwa ndio mkakati wa kuwamaliza waandishi (na wanasiasa)walio nje ya 'system wanaopinga establishment. Mkakati huo ulikuwa unaitwa OPERESHENI CHAKAZA.

Nini kilitokea?


System ilimshawishi Mwenye gazeti la Family Mirror Aminieli Macha kumfuta kazi mhariri wake Stanley Kamama. Kwa bahati mbaya Kamana alikuwa na human flaws nyingi kisingizio kilipatikana kwa urahisi. Kamana alifutwa kazi Family Mirror, gazeti lile pinzani la serikali likayumba sana na hatimaye kufa.

Stanley Katabalo alikufa katika mazingira tatanishi ambayo yalihusishwa na makala zake zilizokuwa zikipinga umilikishwaji wa eneo la Uwinda la Loliondo kwa Mtawala mmoja kutoka katika mojawapo ya vile viinchi vidogo vya kiarabu vyenye fedha nyingi za mafuta.

Sijaelewa vizuri mazingira ya gazeti la Kajubi Mukajanga kufa lakini najua kuwa lilikuwa gazeti huru ambalo halikupendwa na system.

Waandishi wadogodwadogo huwa system haipati shida kuwamaliza. Anafuatwa mwenye mali, zinatolewa sifa mbayambaya bili tatu za huyo mwandishi kwa mwenye mali anatafuta tu namna ya kujaza nafasi ya huyo mwandisi. Anakosa pa kusemea, basi!

Pana kitabu mtu wantu, tena best seller, kama mtu angetaka kuandika story ya free media katika nchi hii. Jaston

Anonymous said...

Lets c wat kiwete is goin to do with his corrupt fuckin mind

Anonymous said...

y evrytime i send a comment u delete is tanzania dont have free dom of speech anymo o just u bein a coward