Tuesday, August 16, 2011

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA ARDHI NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI MHE. HALIMA JAMES MDEE (MB) KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2010/2011 NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI MWAKA WA FEDHA 2011/2012

UTANGULIZI


 Mheshimiwa Spika , napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwepo hapa leo kuwasilisha maoni ya Kambi ya upinzani kuhusu Wizara ya Ardhi, Nyumba Na Maendeleo ya Makazi.


Mheshimiwa Spika, pia nikushukuru wewe kwa kuniruhusu kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Wizara hii kwa mujibu wa Kanuni ya 99 kanuni ndogo ya (7) , ya Kanuni za Bunge Toleo la Mwaka 2007.


Mheshimiwa Spika, pili ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) na wananchi wa Jimbo la Kawe kwa imani yao kwangu, Makamanda wote (vijana, wazee na akina mama wa vyama vyote) walioshiriki katika harakati zote za Kampeni na hatimaye kukesha na mgombea wao, Shule ya Msingi Oysterbay kulinda ushindi wetu. Mungu pekee ndiye anayejua shukrani yangu kwao! Ahadi yangu kwao, ni kuwatumikia kwa uwezo wangu wote kwa kadiri Mwenyezi Mungu atakavyoniwezesha!


Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa shukrani za dhati kwa aliyekuwa mgombea Urais kupitia CHADEMA, Dkt. Wilbroad Peter Slaa. Hakika wabunge wengi tuliofanikiwa kushinda, sehemu ya ushindi ilipatikana kutokana na utumishi wake uliotukuka katika Taifa hili! Mungu akupe uhai,naamini ipo siku tutaifikia Nchi ya Ahadi!


Mheshimiwa Spika, sina budi kumshukuru Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Mhe. Freemani Aikaeli Mbowe, kwa kuniamini na kuniteua kuwa Msemaji Mkuu wa kambi ya Upinzani katika Wizara hii. Shukrani pia ziende kwa wasaidizi wa Kiongozi wa Kambi, Kabwe Zitto (Naibu Kiongozi wa Kambi) na Tundu Lissu (Mnadhimu wa Kambi) kwa kutuongoza vyema katika shughuli hii ngumu ya kuwatetea wanyonge. Shukrani pia ziwafikie wabunge wenzangu wote wa Kambi kwa ushirikiano wao kwangu.


Mheshimiwa Spika, sina budi pia kuishukuru sana familia yangu yote,wazazi wangu Prof. James Salehe Mdee na Theresia Kisenga Ngowi kwa upendo wao na kwa upekee nimshukuru kaka yangu Joseph James Mdee, ambaye alikuwa sambaba na mimi, na timu yangu ya kampeni iliyoongozwa na uongozi wa Jimbo la Kawe usiku na mchana mpaka kikaeleweka!


Mheshimiwa Spika, mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa kaka yangu na rafiki yangu mkubwa Mhe. Zitto Zuberi Kabwe, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini. Kwa yeyote anayemuona Halima Mdee,na mafanikio yake, afahamu kwamba safari yangu ya mafanikio ya kisiasa yalianzia mbali sana! Na katika safari hii, tokea hatua za awali kabisa, kaka yangu huyu alikuwa mhimili mkubwa. Asante sana.


Mheshimiwa Spika, ardhi ya Tanzania ina ukubwa wa kilomita za mraba 942,600 sawa na hekta milioni 94.26, kati yake kilomita za mraba 888,200 sawa na hekta milioni 88.82 ni eneo la nchi kavu. Ili ardhi hii iwe na maana katika kuleta maendeleo ni lazima kila kipande kitambiliwe kupimwe, kimilikishwe na kupangiwe matumizi, lakini hadi sasa ardhi iliyopimwa na kumilikishwa inakadiriwa kuwa ni asilimia moja tu. Jambo hili ndilo limepelekea migogoro isiyoisha baina ya watumiaji mbalimbali wa ardhi. Aidha, Serikali kwa makusudi wanapindisha matumizi ya ardhi kwa kuwamilikisha viongozi wa nchi na wafanyabiashara wakubwa kama itakavyojionyesha katika hotuba hii.


Mheshimiwa Spika, asilimia hii finyu ya utambuzi wa ardhi haina maana kuwa ardhi iliyobaki haitumiki au haina mwenyewe, kwani wananchi kwa miaka mingi wamekuwa wakiitumia katika kuendesha maisha yao, hivyo utaratibu wowote unaofanywa na Serikali kuimilikisha kwa mtu yoyote bila kwanza kuhusisha wale watumizi wa awali ni chanzo na kichocheo cha migogoro. Hivyo ardhi iskikodishwe kabla ya kuwafikiria watumiaji wa ardhi hiyo kwenye maeneo husika (wakulima na wafugaji).


MAMLAKA YA USIMAMIZI WA ARDHI


Mheshimiwa Spika, Wizara ya ardhi ni wizara mtambuka, chini ya Taasisi yake ya Tume ya Taifa ya Mipango wizara ina wajibu wa kuratibu utayarishaji na utekelezaji wa mipango na matumizi ya ardhi ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo ya uwekezaji, kilimo (ikiwa ni pamoja na kusaidia kupatikana kwa kwa ardhi kwa ajili ya utekelezaji wa Kilimo kwanza), makazi, malisho (ufugaji), wanyamapori, misitu, vyanzo vya maji na shughuli zote zinazotumia ardhi.


Mheshimiwa Spika, Ardhi ndio nchi, Ardhi ndio msingi wa maendeleo. Kwa hiyo hakuna amani,ustawi wala maendeleo kwa wanadamu bila matumizi bora na endelevu ya ardhi. Kwa bahati mbaya, baada ya kukumbatia sera ya uchumi huria ambalo limegeuzwa kuwa holela, uongozi wa nchi yetu umetelekeza kabisa wajibu wa kusimamia matumizi yenye tija ya ardhi kwa nchi yetu na watu wake.


Mheshimiwa Spika, kushindwa huko kumejidhihirisha katika maeneo makuu mawili. Moja, masuala ya usimamizi wa ardhi yamewekwa chini ya Wizara zaidi ya moja hivyo hivyo kuleta mkanganyiko kwenye suala la uwajibikaji. Kuna muingiliano mkubwa sana wa majukumu baina ya Wizara ya ardhi nyumba na maendeleo ya makazi na ofisi ya waziri Mkuu Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa ( TAMISEMI). Pili, usimamizi wa maafisa za ngazi za kati na za juu umedhoofika kwa sababu ya kuwajibika kwa zaidi ya mamlaka moja. Mfano halisi ni maafisa ardhi wa halmashauri ya miji na wilaya ambao wanategemewa kuwa chini ya wakurugenzi wa halmashauri na wakati huo huo kuwajibika kwa Kamishna wa Ardhi na Waziri wa Ardhi. Hali hii imesababisha kuongezeka kwa migogoro ya ardhi kutokana na kukosekana kwa usimamizi thabiti wa Maafisa Ardhi.


Mheshimiwa Spika, takwimu za Serikali zinaonyesha kuwa halmashauri za wilaya zinaupungufu mkubwa wa wataalam wa ardhi kwa asilimia 74, ikiwa ni sababu mojawapo ya kukua kwa kasi ya ajabu kwa vyombo visivyo na mamlaka kisheria kushiriki katika usimamizi, utawala na kutengeneza matumizi bora ya ardhi ya vijiji kama vile mkuu wa wilaya, mbunge, kamati za ulinzi na usalama na mkuu wa mkoa. Kwa mujibu wa sheria za ardhi namba 4 na 5 za mwaka 1999 na ile ya serikali za mitaa namba 7 ya mwaka 1982, hawa hawahusiki na usimamizi wa ardhi za vijiji.


Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza mkakati ilionao wa kuviimarisha vyuo vya ardhi vya Tabora na Morogoro ili viweze kutoa wahitimu wengi ili kupambana na upungufu uliopo?


Mheshimiwa Spika, Kutokana na kila taasisi/idara/wizara kujifanyia mambo yake, tumeshuhudia kutupiana mpira baina ya Wizara ya Ardhi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) na Wizara ya Nishati na Madini juu ya mgogoro wa ardhi unaowahusisha wakulima wa kijiji cha Nzasa wakipinga kuondolewa katika makazi yao halali.Katika mgogoro huu Wizara ya Maliasili na utalii wanataka kuwaondoa wananchi katika ardhi yao halali kwa madai kwamba wanaishi ndani ya hifadhi ya Msitu wa Kazimzumbwi.


Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Msitu ya wa Kazimzumbwi ilianzishwa na Gavana E.F Twinig kwa Tangazo la serikali Na. 306/1954 la tarehe 24/9/1954. Tangazo hili liliweka mipaka ya Hifadhi ya Misitu wa Kazimzumbwi. Kwa mujibu wa mipaka husika, eneo lililo katika mgogoro halimo katika hifadhi hiyo. Na hata kama lingekuwepo, kwa mujibu wa hukumu za Mahakama utaratibu wa kisheria wa kutangaza eneo kugeuzwa kuwa na hifadhi haukufuatwa hivyo kubatilisha zoezi zima!


Mheshimiwa Spika, kufuatia malalamiko hayo Ikulu ilimwandikia barua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi barua yenye Kumb. Na. CEA 110/302/IV/01 ya tarehe 10/6/2008 ikitaka wizara ikapime eneo la Nzasa- Chanika kujiridhisha kama kweli wakulima hao walikuwa ndani ya msitu wa Kazimzumbwi au la. Barua ambayo haijapatiwa majibu mpaka leo.


Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Wizara, iliambie Bunge hili tukufu ni kwa namna gani walifanyia kazi barua toka Ikulu zenye kumbukumbu namba CEA 110 /302/IV/01 ya tarehe 10/Juni 2008 na barua yenye kumbukumbu namba CEA 110/302/IV/01 ya tarehe 18 Septemba 2009 hasa ikizingatiwa kwamba kuna tuhuma kutoka kwa wanakijiji kwenda kuwa viongozi wa serikali ya CCM wanatumia Idara ya Maliasili kama Gamba kutaka kunyang’anya ardhi ya kijiji kwa manufaa yao binafsi.


MIGOGORO YA ARDHI


Mheshimiwa Spika,migogoro ya ardhi hapa nchini hivi sasa imekithiri kufikia hatua ya uvunjifu wa amani na kufikia hadi umwagaji damu na pengine vifo kutokea katika maeneo kadhaa. Hali hii imeondoa utamaduni wetu wa asili wa kuvumiliana na kumaliza matatizo yetu kwa njia mwafaka za mazungumzo. Ni muhimu serikali ikaelewa kwamba kupuuzamigogoro hii ya ardhi nchini ni sawa na kuatamia bomu, hivyo ni lazima hatua za haraka zichukuliwe!


UWEKEZAJI, UBINAFISHAJI NA HATMA YA ARDHI YA TANZANIA


Mheshimiwa Spika, Migogoro, hasa ya wananchi na wawekezaji inakua kwa kasi na kuchukua sura mpya. Anapokuja‘mgeni’, kwa jina la ‘Mwekezaji’ matendo ya Serikali yetu, yanapingana na usemi usemao ‘mgeni njoo mwenyeji apone’ bali imekuwa ‘mgeni njoo mwenyeji asulubike’ .


Mheshimiwa Spika, wakati Serikali inawapa matumaini makubwa wakulima wa Tanzania , kwa mipango kabambe ya kilimo cha kisasa, pamoja na uwekezaji mkubwa wa kilimo utakaogharimu mabilioni za dola la kimarekani kutoka kwa wanaoitwa wafadhili, hoja za msingi ni kama kilimo hicho kina malengo ya kumnuufaisha mkulima wa Tanzania , au malengo yake ni kupokonya ardhi ya wazawa na kisha kuwageuza vibarua /manamba ndani ya ardhi yao!


Mheshimiwa Spika,Utafiti uliofanya na HakiArdhi juu ya hali ya maeneo yaliyokuwa ya Nafco, NARCO na Mashamba yaliyotelekezwa wamebainisha yafuatayo:


1) Ubinafsishwaji wa mashamba ulitawaliwa na utata na udanganyifu mkubwa hali iliyopelekea uadui baina ya wawekezaji na wakulima wadogo wadogo kwa upande mmoja na mgogoro kati ya wakulima wadogo na wafugaji kwa upande mwingine


2) Katika maeneo ya yaliyokuwa mashamba ya Ngano, Hanang (Hanang Wheat Complex (HWC)) na Dakawa Ranch iligundulika kwamba wakati wananchi wanaozunguka mashamba hayo wana mahitaji makubwa sana ya ardhi wawekezaji na vigogo wenye fedha wamejilimbikizia maeneo makubwa ambayo hawayaendelezi kwa kwa ukamilifu[1].


Kambi ya upinzani inaitaka serikali ilieleze Bunge hili tukufu na watanzania kwa ujumla nini kilichojiri katika ugawaji wa ardhi ya iliyokuwa Dakawa Ranch na ni wanakijiji wangapi walinufaika na mgao huo!


3) Wawekezaji kuwakodisha wananchi wenyeji mashamba kwa ajili ya kilimo na kuwatoza fedha. Haya yalitokea katika Mashamba yanayomilikiwa na Rai Group ambapo wananchi walikuwa wanakodisha $ 10 kwa ekari. Hali kama hii pia inafanyika katika Shamba la mpunga Mbarali na Kapunga, yote yakiwa wilaya ya Mbarali.[2]
4) Mashamba yaliyotakiwa kurejeshwa kwa wananchi lakini hayajarejeshwa , kati ya mashamba hayo ni shamba la Gawal na Warret ,lililopo Hanang lenye ukubwa wa hekta 4,000. Maamuzi ya kuyarejesha mashamba kwa wananchi yalifanyika toka mwaka 2004/05.[3] Kambi ya upinzani inataka kauli ya serikali kuhusiana na mustakabali wa mashamba haya! Kambi ya upinzani inaitaka pia serikali itoe tamko juu ya mustakabali wa shamba la Bassotu.


KIJIJI CHA CHASIMBA- BOKO – DSM
Mheshimiwa Spika,Hivi karibuni kumekuwa na matamko mbali kutoka kwa kampuni ya Saruji, (Tanzania Portland Cement Co. Ltd), ikitishia kufunga kiwanda, kwa madai kwamba hawana eneo la kutosha . Hoja yao kubwa ni kwamba wananchi wa kijiji cha Chasimba wamevamia eneo lao! Na kwamba wanashindwa kujipanua kama kiwanda.


Mheshimiwa Spika,Nimeona nilizungumze hili ili kuondoa upotoshwaji unaotaka kufanywa na kiwanda husika. Ni muhimu bunge hili tukufu likafahamu kwamba , Chasimba iko ndani ya ,Kijiji cha Boko, kijiji ambacho kiliandikishwa kama kijiji kwa mujibu wa sheria ya kuandikisha vijiji,kutambuliwa kwa Vijiji vya Ujamaa na Uongozi wa Vijiji ,1975 na hati kutolewa 25/2/1976[4]. Na hakuna mazingira yoyote yanayoonyesha kwamba kijiji hicho kilifutwa ama kubatilishwa.Lakini kama ilivyo kawaida yetu, kuendekeza wawekezaji dhidi ya wenyeji, wanakijiji waliuzwa wakiwa ndani ya ardhi yao, ndipo likaja suala la kujalidiana kuhusu fidia! Zoezi ambazo liliendeshwa kihuni hasa ikizingatiwa kwamba mwekezaji alikuwa na hati tayari!


Mheshimiwa Spika,Wakati mwekezaji akidai anamiliki eneo lote la viwanja 1,4 na 7 kuna nyaraka za Serikali zinazoonyesha kwamba mwekezaji husika hakupewa umiliki wa eneo lote, kuna eneo ambalo lilibaki serikalini na mchakato wa kutengeneza hati mbili ulikuwa umefanyika na kufikia hatua za mwisho kabisa na nyaraka zipo!


Mheshimiwa Spika,Hoja ya kiwanda kushindwa kujitanua kwa sababu haina eneo la kutosha ,hazina mashiko hata kidogo. Kwa mujibu wa barua kutoka kwa Mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni ya tarehe 30/5/2002 kwenda kwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya makazi, Wizara ya ardhi na Maendeleo ya Makazi. Barua husika inaelezea ombi ambalo manispaa ya Kinondoni ililipata kutoka kwa M/S Tanzania Portland cement company Ltd la kutaka kugawanywa kiwanja na 1,4 & 7.


Mheshimiwa Spika, barua husika inabainisha kwamba kikao cha kamati ya Mipangomiji na Mazingira kilichofanyika 22/5/2002 kililijadili suala hilo na kulikubali kutokana na wawekezaji katika kiwanda hicho kutokuwa tayari kulipia eneo ambalo si la uzalishaji na wala si la malighafi! Kwa ujumla eneo lote lina ukubwa wa hekta 922.22, eneo linalohusika na uzalishaji na malighafi lina ukubwa wa hekta 685. Eneo ambalo halitumiki na mwekezaji ni hekta236.63. Ni eneo hili ambalo ndilo lina makazi ya wananchi ,ambao wengi wao walidhulumiwa kwa kulazimishwa kumpisha mwekezaji! pasipo utaratibu wa kisheria kufuatwa!


Mheshimiwa Spika, tumekuwa tunaishauri Serikali, ambayo inataka kuwaondoa wananchi kwa nguvu, kuliangalia hili suala kwa busara ya hali ya juu. Tofauti na maeneo mengine ambayo kuna uvamizi wa maeneo ya watu, wananchi eneo hili, wengi wao ni watu wazima, ambao wana kila ushahidi wa kuonyesha kwamba pale ni asili yao na kilichofanyika ni dhuluma dhidi yao kupisha wenye fedha. Na hawako tayari kuacha makazi yao, wakiungwa mkono na Mbunge wao na madiwani wao wa Kata za Wazo na Bunju (CCM)! Tumeweka itikadi pembeni!
UFISADI WA ARDHI NA MUSTAKABALI WA MTANZANIA MASIKINI


MKOA WA MBEYA


Mheshimiwa Spika, katika wilaya ya Mbarali, shamba la Mpunga la Mbarali (Mbarali Rice Farm- ekari 14437) na shamba la mpunga la Kapunga (ukubwa ekari 18425) yalikuwa ndio chanzo cha mapato cha wananchi wa eneo husika. Mashamba haya yalikuwa yanahudumia watu zaid ya 30,000 na vijiji kumi . Ardhi hiyo pia ilikuwa inahudumia watu wa Iringa na wilaya nyingine za Mbeya. Mipango ya awali ya Serikali , mwaka 2003/2004 kama ilivyobainishwa na na aliyekuwa Waziri wa Kilimo ilikuwa ni kuyabinafsisha mashamba hayo kwa wakulima wadogo wadogo, mpango ambao ungejumuisha mashamba ya Ruvu na Dakawa.


Mheshimiwa Spika,Kutokana na nguvu ya mafisadi kuizidi hekma ya serikali , na licha ya kilio cha aliyekuwa mbunge wa Mbarali kipindi hicho , Mhe . Esterina Kilasi , serikali iliamua kuuza eneo husika kwa kampuni ya Highland estates Ltd . Mmiliki wa sasa Bwana Nawab Mulla ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Mbeya. Wananchi wamegeuka wapangaji kwa kukodisha maeneo ili waweze kulima na kujipatia kipato!


Mheshimiwa Spika, wakati Shamba la Mbarali akipewa kwa bei ya kutupa Mwenyekiti wa CCM, shamba la kapunga[5] lilibinafsishwa na kukabidhiwa kwa kampuni ya Export Co. Ltd kwa bei ya kutupa ya shilingi bilioni 2.3, mmiliki akiwa bwana JEETU Patel ( Jina halisi Jayantkumar Chandubhai Patel).


Mheshimiwa Spika, hii ndio Tanzania ambayo, wazawa wananyang’anywa ardhi, maeneo yote muhimu na yakimkakati na kukabidhiwa wageni, au watu wenye mamlaka na fedha, huku ikiwaacha wazawa kubaki vibarua au wakulima wadogo wanaotegemea hisani ya mabeberu!


Mheshimiwa Spika, bado mustakabali wa shamba la mahindi Mbozi haujajulikana, serikali inataka kumpa mwekezaji, wakati wananchi wana uhaba wa ardhi kwa matumizi yao! Kambi ya upinzani inaitaka serikali itoe majibu kuhusiana na hatma ya shamba la mahindi mbozi. Halikadhalika, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali iliambie Bunge hili tukufu, ni vigezo gani vilivyotumika kupata wanunuzi wa shamba la Mpunga la Mbarali , shamba la Kapunga, na mashamba husika yaligawiwa kwa maslahi ya nani?


MKOA WA MARA
Mheshimiwa Spika, Musoma mjini kumekuwa na mtafaruku mkubwa kati Jeshi la wananchi JWTZ na wananchi wa Bukanga na Buhare (Mgaranjabo) kutokana na jeshi kujimilikisha maeneo yao ya asili, waliyokuwa wakitumia kwa ajili ya matambiko kwa Kabila ya Wakwaya. Hivi sasa wananchi hao hawaruhusiwi kuingia katika eneo hilo, jambo hilo limezusha chuki kubwa sana kati ya Jeshi na jamii ya Wakwaya wakazi wa Musoma Mjini.


MKOA WA MOROGORO
Mheshimiwa Spika,Matatizo ya ardhi,kwa wakubwa kunyang’anya wanyonge ardhi imeikumba pia Halmashauri ya wilaya ya Mvomero. Mgogoro huu unahusu shamba namba 299 (iliyokuwa NARCO Ranches),lenye ukubwa wa hekta 49,981.


Mheshimiwa Spika, katika shamba hili, taarifa zinaonyesha kwamba 30,007 hektas walipewa Mtibwa sugar licha ya malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba eneo walilopewa ni kubwa sana. Taarifa za kiuchunguzi, zinaonyesha kwamba, maeneo ambayo yalikuwa yamepangwa kugawiwa wanakijiji, wa kijiji cha Wami, yamegawiwa ’wananchi’ wafuatao:


1) Bwana Philip Mangula, aliyekuwa katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, ndio anaongoza kwa kuwa ’mwanakijiji’ mwenye eneo kubwa, alipewa hekta 2000.
2) Bwana John Malecela, Waziri Mkuu Mstaafu na Makamu Mwenyekiti wa CCM alipewa hekta 100,
3) Jenerali mstaafu Ngwilizi, ambaye pia alikuwa waziri wa serikali za mitaa awamu ya tatu alipewa hekta 100 kati ya hekta 5000, zilizosemwa wamepewa wakulima wadogowadogo wa kijiji.
4) Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, anamiliki hekta 2000, ambazo hazijaendelezwa,
5) Waziri Mkuu Mstaafu wa awamu ya tatu, Mhe. Frederick Sumaye hekta 500 na
6) Rais wa awamu ya tatu Mhe. Benjamin William Mkapa, hekta 1000 (ila tofauti na wengine shamba hili limeendelezwa).


Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inahoji, kama hawa watajwa hapo juu ni wakazi wa kijiji cha Wami- Dakawa? Na ni vigezo gani vilitumika kuwanyima ardhi wanakijiji na kuwapa wakubwa hawa? Serikali haioni kwamba mgao huu wa ardhi uliojaaa dhuluma na upendeleo unahatarisha maisha ya watanzania na usalama wa nchi kwa ujumla?


Mheshimiwa Spika, Wananchi wa maeneo haya wana hasira na serikali yao kwa kuwa wameshaambiwa hakuna tena eneo la kugawa, wakati walitozwa shilingi 20,000 kila mmoja kwa madai kwamba wangepewa hekta 5. Ahadi ya hekta 10019 kwa wakulima na wafugaji, imegeuka hewa! Tunakwenda wapi kama nchi? Mheshimiwa Spika Kambi ya upinzani , inaitaka serikali kuangalia upya zoezi la ugawaji wa ardhi katika maeneo yote yenye utata! Ambayo yalitawaliwa na rushwa,ubabe na udanganyifu.


MKOA WA PWANI -SIMBA MOTORS VS WAKAKIJIJI KITONGOJI CHA UNDINDIVU, MAPINGA – BAGAMOYO


Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kijiji cha Mapinga, kitongoji cha Undindivu chenye idadi ya watu zaidi 1400 wamekuwa wakimiliki eneo la Undindivu kwa ajili ya kilimo na ufugaji toka mwaka 1960. Kama ilivyo kawaida yetu ,kampuni ya Simba Motors (T) Ltd ilimilikishwa eneo lote la kitongoji cha undindivu bila wananchi au serikali ya kitongoji na kijiji kujulishwa. Kampuni hiyo ilipima kwa kutumia mpimaji binafsi na ilimilikishwa shamba hilo lenye hecta 322. Baada ya kampuni husika kupima na kumilikishwa bila kufuata sheria, takriban miaka 17 imepita kampuni hiyo haijawahi kuendeleza shamba hilo,kampuni haijawahi kuliendeleza eneo hilo, si kwa kilimo au ufugaji.


Mheshimiwa Spika, mpaka sasa, kuna mgogoro mkubwa baina ya Simba Motors na wananchi wa kitongoji cha undindivu, na kutokana na shamba husika kumilikishwa kwa tajiri mmoja , wakati wakazi wa maeneo hayo wamekosa;1)Maeneo kwa ajili ya huduma muhimu za jamii. 2) Maeneo kwa ajili ya kupanua makazi yao ya kuishi,kwa sababu robo tatu ya eneo la kijiji limamilikiwa na tajiri huyo.


Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inaitaka serikali, kuutafutia mgogoro huu ufumbuzi wa kudumu. Hatuwezi kuendelea kukaa kimya , na kuacha wananchi wetu masikini wakipokonywa maeneo yao kwa faida ya matajiri wachache! Mheshimiwa waziri , Kambi ya upinzani inajua kwamba ofisi yako ilishaletewa taarifa kwa barua ya tarehe 15/12/2010,hakuna kilichofanyika mpaka sasa. Tunataka majibu!


MKOA WA RUKWA – AGRISOIL , KILIMO KWANZA NA HATMA YA TANZANIA


Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imefika hapa ilipo, kutokana na watu wenye dhamana kuingia mikataba mibovu ambayo badala la kuisaidia nchi imekuwa ni msalaba mkubwa ! na kuwaacha watanzania katika limbwi la umasikini. Hivi karibuni kampuni ya Agri- Sol Energy LLC na Kampuni ya Serengeti advisors Ltd , inayoongozwa na Bwana Iddi Simba (aliyekuwa Waziri wa viwanda na Biashara, awamu ya tatu) na Betram Eyakuze kwa pamoja wameunda kampuni ya Agrisol Energy Tanzania , wameingia mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda. Mkataba ambao unatarajia kuipa kampuni husika miliki ya miaka 99 ya maeneo ya lugufu, Hekta 80,317 na Mishamo hekta 219,800.
Mheshimiwa Spika, Masharti ya Msingi katika makubaliano baina ya Halmashauri husika na wawekezaji ni yafuatayo;
a) Kodi ya ardhi ( Land rent) ambayo ni Tshs. 200 kwa hekta
b) Ushuru wa kisheria wa Halmashauri ,
c) ada itakayolipwa halmashauri ni Tsh 500 kwa hekta.
d) Na sharti la mwisho, kama mgogoro utatokea baina ya pande zote mbili, busara itatumika kutatua mgogoro, ikishindikana chemba ya Biashara ya Kimataifa ( ICC) ndio atakuwa msuluhishi!


Mheshimiwa Spika, tunakwenda wapi? Umasikini ndio utufanye tuwe mambumbu wa kufikiri? Hivi kwa nini hatujifunzi ?


Mheshimiwa Spika, Katika hatua za awali,madiwani wa Halmashauri husika walikataa kutoa maeneo yote mawili,waliagiza mwekezaji apewe eneo moja na kwa kipindi cha miaka 20. Kama ataonekana kufanya vizuri,wangefikiria kumwongezea muda na eneo! Kama kawaida, walioonekana kuwa wakali wakapelekwa Marekani, kwa siku nne! Baada ya kurejea, Nchi ikaingizwa kwenye mkataba mwingine ambao utaigharimu nchi miaka mingine 99 kuweza kujinasua!


Mheshimiwa Spika, Si dhamira ya kambi ya upinzani kudhihaki ama kukatisha tamaa uwekezaji , tunafahamu kwamba serikali inaichukulia Agri Sol Energy kama sehemu ya mkakati wake wa Kilimo Kwanza, lakini hawa wawekezaji ambao wanaitwa wakubwa, mashamba ambayo wanayaendesha ,haswa yale yaliyoko Marekani na yaliyotembelewa na maafisa wa serikali ,wakiongozwa na ofisi ya Waziri Mkuu yana ukubwa wa ekari 17,900, (ambapo ekari 13,195 ni za mahindi na ekari 4705 ni maharage). Na shamba hilo limeajiri watu 13, hivi hawa ni wakulima kweli?


Mheshimiwa Spika,Itakumbukwa kwamba kulikuwa na mkakati uliokuwa ukiendeshwa kwa usiri mkubwa na kwa kasi ya hali ya juu kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI wa kuwasambaza wakimbizi wanaokadiriwa kufikia 162,000 nchi nzima, katika mikoa mbali mbali. Mchakato ambao ulipata upinzani mkubwa hapa Bungeni na kutoka mikoa husika. Huu ulikuwa ni mkakati wa makusudi ili maeneo husika yawe wazi kwa wawekezaji hao kukabidhiwa, na mbaya zaidi wakimbizi waliambiwa bayana kwamba sharti la kupewa uraia wa Tanzania ni kuondoka maeneo hayo!


Mheshimiwa Spika, Ni muhimu ikaeleweka kwamba, huu mtindo wa kuwageuzwa watanzania manamba ndani ya nchi yao kwa kutoa ardhi kwa wageni utakuja kusababisha machafuko hapo baadae....ieleweke hoja hapa sio kulisha taifa na kupata ziada kusafirisha nje ya nchi, hoja hapa ni kumnufaisha mtanzania katika mipango yote endelevu ya matumizi ya ardhi! Na kama ni suala la chakula na kusafirisha nje ya nchi chakula hicho kipo tatizo ni kukitoa kwa wakulima na kufikisha sokoni, ushahidi huo upo kuwa mahindi ni mengi kuliko uwezo wa wananuni (Rukwa, Songea, Iringa-Ludewa n.k.)


UKIUKWAJI WA SHERIA YA ARDHI, NO. 4 YA MWAKA 1999


Mheshimiwa Spika, Vifungu vya 19(2) ,20 (1), 20 (2), 20(3) na 20(4) vya Sheria ya Ardhi vinatoa masharti ya umiliki wa ardhi kwa watu ambao sio watanzania. Kwa ujumla wake vifungu husika vinapiga marufuku ardhi kupewa kwa wageni, isipokuwa tu kwa madhumuni ya uwekezaji chini ya Sheria ya uwekezaji , No. 26 ya mwaka 1997. Na ili ardhi husika iweze kupatikana lazima kwanza itambuliwe ,itangazwe kwenye gazeti la serikali na iwe ‘ allocated’ kwa Kituo Cha Uwekezaji, ambacho ndicho kitakuwa na jukumu la kumpatia Mwekezaji.
Mheshimiwa Spika, Haya yote hayajafanyika, na kinachotaka kufanyika kwa kutumia vibaraka wa kitanzania , ni kuhakikisha kwamba wabia ‘vibaraka’ wa kitanzania wana kuwa na hisa nyingi katika umiliki wa ardhi ili kuepuka kikwazo cha kupitia katika Kituo cha uwekezaji.


Mheshimiwa Spika, kuhusu mamlaka ya kuingia ubia (joint venture) na mwekezaji ambaye si Mtanzania kama ambavyo inaonekana ni kamchezo ambako kanataka kuchezwa na Serengeti Advisers Limited, Mabadiliko ya Sheria ya Ardhi yaliyofanyika mwaka 2004, Sheria Na. 2/2004 The Land (Amendment ) Act 2004 Kifungu 19 (1), (2) (c) kinasema ili kufanikisha masharti ya uendelezaji wa ardhi, raia wa Tanzania anayemiliki ardhi anaweza kuingia ‘joint venture’ na mwekezaji ambaye si raia wa Tanzania kwa madhumuni ya uwekezaji chini ya Sheria ya Uwekezaji , Sura ya 38.


Kwa mujibu wa Kifungu hicho ubia unafanywa na mzawa na mgeni. Kwa mujibu wa Sheria ya Uraia ‘ The Tanzanian Citizenship Act’, Cap 357. Shirika la umma au Kampuni au halmashauri haiwezi kuwa na sifa za kuwa raia. Hivyo kwa mujibu wa kifungu 19 (2) (c) si halmashauri ya wilaya ya Mpanda wala kampuni ya Serengeti Advisers yenye uwezo wa kutoa ardhi yake kwa mtu ambaye si raia ili kuwekeza kwa pamoja.


Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maelezo ya vifungu nilivyovitaja hapo juu(isipokuwa kama kuna mabadiliko ya sheria ambayo hadi sasa haifahamiki), Halmashauri ya wilaya ya Mpanda na kampuni ya Serengeti Advisers haina uwezo wa kuwekeza kwa pamoja ‘ joint venture ‘ na wawekezaji ambao si watanzania mpaka hapo sheria zitakapofanyiwa marekebisho.


Kambi ya upinzani inaitaka Serikali ituambie, ilitumia utaratibu gani wa kisheria kuingia Mkataba huo wa kifedhuli na usio na maslahi hata kidogo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda na Taifa kwa ujumla? Nani aliwatuma?


MIGOGORO YA ARDHI BAINA YA WAKULIMA NA WAFUGAJI


Mheshimiwa Spika, Kilimo na ufugaji ni ya sekta zinazoongoza kwa kutoa mchango mkubwa sana katika pato la Taifa, halikadhalika ndizo zinazoongoza kwa kutoa ajira kwani zaidi ya 80% ya Watanzania wamejiajiri katika sekta hii,haswa vijijini. Hivyo basi kuboresha hizi sekta mbili, maana yake ni kwamba tutakuwa tumeboresha 80 % ya maisha ya watanzania, kwa kuwa na uhakika wa kipato, usalama wa chakula na kuongezeka kwa pato la Taifa.


Mheshimiwa Spika, Imekuwa ni jambo la kawaida kwa nchi yetu kutokea kwa migogoro baina ya wakulima na wafugaji, chanzo cha migogoro hiyo ni kutokana na kutokuwa na mipango thabiti ya serikali ili kubainisha /kutenganisha maeneo maalum kwa ajili ya wakulima , halikadhalika wafugaji.


Mheshimiwa Spika, Sheria yetu ya ardhi , No. 4 na No. 5 ya mwaka 1999 imeainisha utaratibu ambao miliki ya ardhi ya mtu mmoja mmoja ama kikundi inavyotambulika kisheria mijini na vijijini kisheria ama kimila. Hata hivyo utaratibu wa utwaaji na umiliki ardhi hasa vijijini kwa matumizi ya wafugaji , wachungaji na wawindaji haujaainishwa ipasavyo !Mikakati ya kutenga ardhi hasa ya wafugaji imekuwa finyu mno kiasi kwamba wakulima na wawekezaji wameendelea kuhodhi/kuvamia ardhi ya wafugaji kwa msaada wa mawakala wa serikali.[6] Na wakati mwingine wafugaji wamekuwa wakivamia maeneo ya wakulima kutokana na kukosa maeneo mwafaka kwa ajili ya malisho.


Mheshimiwa Spika,Tafiti pia zimeonyesha kwamba ardhi ya wafugaji imekuwa ikichukuliwa kwa ajili ya matumizi ya wawekezaji , kugeuzwa kuwa hifadhi za taifa au game reserves! Matokeo yake wafugaji wanageuka watu wa kutangatanga! Wakati serikali imekuwa ikiwataka wafugaji waondokane na njia za kizamani za kufuga, bado haijaonyesha njia mbadala za ufugaji wa kisasa!






Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inaitaka serikali , itueleze ina mikakati gani katika kuhakikisha kwamba maeneo rasmi ya wafugaji yanabainishwa ili kuepusha umwagaji damu na migogoro isiyo na tiba huko mbeleni.


Halikadhalika, kambi ya upinzani inaitaka serikali itoe tamko juu ya tatizo la mpaka na mgogoro wa wakulima na wafugaji wa jamii ya Wamasai katika eneo la vijiji vya Izava (Chamwino) na Chitego (Kongwa). Mgogoro ambao kwa kiasi kikubwa ulisababishwa na maamuzi ya kibabe yaliyofanywa na wakuu wa wilaya hizi mbili (mwaka 2006) , wakishirikiana na Mwenyekiti wa Halmashauri kipindi hicho!
Mheshimiwa Spika, Wakulima wa maeno haya wanalalamikia wafugaji ambao waliingizwa kibabe katika maeneo yao, bila kuwashirikisha kwa nguvu za ’kigogo mmoja’, matokeo yake mashamba yao ndio yamegeuka malisho ya mifugo hiyo! Kumekuwa na tuhuma ya ushiriki wa skari wa Kongwa katika zoezi hili kandamizi! Kambi ya upinzani inaitaka Serikali ifuatilie mgogoro huu ili kuepusha maafa yanayoweza kutokea, hasa ikizingatiwa kwamba matukio ya kushambuliana ,kujeruhi na kutishia maisha imekuwa ni jambo la kawaida baina ya pande mbili.


MATATIZO YA TATHMINI NA MALIPO YA FIDIA


Mheshimiwa Spika, imekuwa ni jambo la kawaida kwa wananchi kulalamika kupunjwa ama kutokulipwa kabisa fidia pale ambapo wanatakiwa na serikali kuhama maeneo yao ili kupisha matumizi mapya ya ardhi. Mheshimiwa Spika sheria zetu zinatamka bayana kwamba, pale ambapo mwananchi anapochukuliwa eneo lake na serikali kwa mamtumizi mengine na hivyo kutakiwa kuhama anatakiwa kulipwa fidia inayojumuisha, thamani ya ardhi, usumbufu, usafiri na hasara ambayo muathirika ataipata kutokana na kuchukuliwa eneo lake.


Mheshimiwa Spika, hata hivyo kumekuwa na malalamiko kila pahala ambapo wananchi wanatakiwa wasimamishe shughuli zao kupisha matumizi mapya ya ardhi. Serikali hailipi fidia ya kutosha na hata wananchi wakilalamika serikali inaendelea miradi. Badala ya fidia kumwacha mwananchi awe katika hali aliyokuwa mwanzo,mfumo wa fidia wa nchi yetu ,haswa maeneo yanapochukuliwa na serikali (ambayo ndio hiyo hiyo inafanya tathmini na kuamua kiasi gani kilipwe) unamwacha mwathirika fukara zaidi!


a) Kambi ya upinzani inaitaka serikali itoe maelezo juu ya hatma ya wananchi wa Kurasini Mabwawani ambao tangu nyumba zao zifanyiwe tathmini miaka miwili iliyopita ili kupisha upanuzi wa bandari, kumekuwa na kimya kingi na wakiuliza kuhusu hatma yao, hawajibiwi kitu!kuna kundi ambalo limelipwa, kuna kundi lingine halielewe nini kinachoendelea na wanashindwa kuendeleza maeneo yao


b) Kambi ya upinzani inaitaka wizara ya ardhi itoe maelezo juu ya hatma ya wananchi wa kijiji cha Mabwepande, kata ya Mabwepande Jimbo la Kawe ambao miaka minne iliyopita serikali ilikwenda kufanya tahmini na kuwaagiza wananchi kutokufanya maendeleo yoyote ili kupisha upanuzi wa chuo cha IFM. Hakuna kilichofanyika mpaka sasa, wananchi waliokuwa wanategemea kilimo, wamezidi kufukarishwa, serikali ikiulizwa haina majibu. Matokeo yake maeneo ambayo waliambiwa wayaache sasa yamevamiwa na genge la wavamizi, si wizara, halmashauri ya manispaa ya kinondoni ama vyombo vya usalama vinavyochukua hatua licha ya kupewa taarifa ya uvamizi huu!


c) Kambi ya Upinzani inaitaka serikali ieleze hatma ya wananchi wa Kigamboni (ambao wengi walikuwa wanafanya kazi za kilimo) ambao wanalalamikia zoezi la kuchukua maeneo yao kupisha ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni kutawaliwa na rushwa, maeneo kuthaminishwa bei ndogo, wakati huo huo serikali baada ya kulipa fidia kiduchu wanauza maeneo husika kwa bei ya kutupwa,bei ambayo mwananchi wa kawaida hawezi kuimudu!




d) Kambi ya upinzani inaitaka serikali ieleze hatma ya wananchi wapatao 1600 wa wilaya ya Mbarali waliotakiwa waondoke maeneo yao ili kupisha upanuzi mbuga ya Taifa ya Ruaha? Serikali ilitoa shilingi bilioni 6.5 tu kwa wakazi wote. Kwa tathmini ya kawaida kila mwananchi alipewa shilingi milioni 4.5. Hivi kwa maisha ya sasa kuna nyumba inayoweza kujengwa na kukamilika kwa kiasi hicho cha fedha? Huu ni unyonyaji na udhalimu ulio dhahiri.


e) Kambi ya Upinzani inaitaka serikali ieleze hatma ya fidia ya wananchi wa Jimbo la Ubungo Kata ya Kwembe wanaopaswa kuhama kupitisha ujenzi wa majengo wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba ya Afya (MUHAS) Mloganzila. Wakati wa kuhitimishwa kwa bajeti ya Waziri Mkuu katika mkutano huu wa bunge serikali ilieza kwamba tathmini ya fidia inaendelea na kwamba wapo wananchi ambao tayari wamelipwa fidia na wengine bado hawajalipwa mpaka sasa. Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuzingatia kwamba fidia iliyolipwa kwa wananchi wachache ni ya mali na mazao; hata hivyo wananchi hawajalipwa fidia ya ardhi. Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa maelekezo kwa wizara zinazohusika kuhakikisha fidia stahiki inalipwa. Mwaka 2010 Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ilifanya mkutano na wananchi na kuwaahidi kulipa fidia ya ardhi kwa mujibu wa sheria; kambi ya upinzani inataka serikali ieleze malipo hayo yatatoka kwenye fungu lipi na yatalipwa lini?


MALALAMIKO DHIDI YA MAMLAKA YA USTAWISHAJI MAKAO MAKUU (CDA)


Mheshimiwa Spika, Mwaka 2004 , Serikali kupitia wakala wa majengo mkoani Dodoma, waliwauzia wananchi, nyumba zilizokuwa zinamilikiwa na lililokuwa Shirika la Reli Tanzania (TRC). Malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi hawa wa Tambukareli,ni kunyimwa hati za nyumba zao na CDA ilhali wameshalipia nyumba hizo kwa ukamilifu. Sababu zinazotolewa na CDA, zisizo na mashiko ni kwamba eti Serikali ilitoa uamuzi wa kuuza nyumba bila kuwahusisha CDA , hivyo hawatambui uuzwaji wa nyumba hizo!


Mheshimiwa Spika,Kambi ya upinzani inaitaka serikali kutoa maelekezo kwa CDA kutoa hati husika, ni suala la kibri na jeuri kwa taasisi ya serikali kuhoji maamuzi ya serikali, au leo tuelezwe kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano inafanya kazi chini ya CDA? Kama kulikuwa na uzembe ndani ya Serikali kwa nini Wananchi hawa masikini waliodunduliza vihela vyao wapate makazi waumizwe? Kambi ya upinzani inataka kauli thabiti ya serikali kuhusiana na hili!


SHERIA NA. 5 YA ARDHI YA VIJIJI NA MUSTAKABALI WA TAIFA
Mheshimiwa Spika,Sheria ya Ardhi ya Kijiji inatoa mamlaka kwa Halmashauri ya kijiji kusimamia ardhi yote ya kijiji. Halikadhalika Halmashauri ya kijiji imepewa mamlaka ya kugawa ardhi baada ya kuruhusiwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji. Uzoefu umeonyesha kwamba kutokana na kutokuwa na ufahamu mpana wa sheria, watu wenye fedha wamekuwa wakitumia fursa hii ya kisheria vibaya kwa kuwarubuni viongozi wa vijiji, na hatimaye kugawa maeneo ya kijiji kwa wageni wenye fedha wachache, huku ikiwaacha wanakijiji bila ardhi yoyote.


Mheshimiwa Spika,Hali inakuwa mbaya zaidi pale ambapo watu ambao sio watanzania wanatumia upenyo huu wa kisheria, na kumilikishwa maeneo makubwa ya kijiji kinyemela! Kambi ya upinzani imepata malalamiko kutoka kwa wanakijiji wa kijiji cha Orngadida, Kata ya Qash, Babati ( taarifa ambayo Waziri wa Ardhi, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi Mtendaji –Halmashauri wanayo). Wanakijiji hao wanawatuhumu viongozi wa serikali ya kijiji wakishirikiana na diwani kuuza Ardhi kwa wageni pasipo kuwashirikisha, wanakijiji wamemwandikia Mkuu wa wilaya ya Babati barua mbili ambazo nazo hazijajibiwa!


Mheshimiwa Spika, Hakuna ubishi kwamba kuna wageni wengi waliopata maeneo ya vijiji kinyemela kwa kutumia upenyo huo, wakati sheria ya Ardhi No.4 , kifungu na 20 kinakataza wageni kumiliki ardhi nchini isipokuwa kwa malengo ya uwekezaji tu, na ambao umiliki wake lazima upitie Kituo cha uwekezaji Tanzania , na si vinginevyo.


Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inaitaka serikali iliambie Bunge lako tukufu,ni lini imefanya tathmini katika vijiji vyetu ili kuweza kubainisha ardhi zilizotolewa na Halmashauri za kijiji na uhalali wake. Ni maoni ya Kambi ya upinzani kwamba sheria hii isipoangaliwa kwa umakini itasababisha umwagaji damu mkubwa hasa pale wananchi watakapohisi kunyang’anywa ardhi yao kifisadi au vinginevyo. Na mbaya zaidi Mheshimiwa Spika,zoezi hili linafanywa hata mijini, na serikali za mitaa ambazo hazina mamlaka ya kugawa ardhi. Mchezo ambao wanafanya kwa kushirikiana na watendaji wa manispaa, na baadhi ya maafisa wa Wizara!
UVAMIZI WA MAENEO YA WAZI MKOA WA DAR ES SALAAM
Mheshimiwa Spika; kutokana na malalamiko ya wananchi mbalimbali kuhusu uvamimizi wa maeneo ya wazi ya umma katika mkoa wa Dar es salaam, Serikali iliunda kamati ya kufanya uchunguzi kuhusu uvamizi katika maeneo husika. Kamati ilikamilisha kazi yake tarehe 13 Julai 2010. Pamoja na majibu ya Waziri wa Ardhi na maendeleo ya makazi aliyoyatoa tarehe 1 Julai 2011 wakati akijibu maswali bungeni kuhusu hatua ambazo serikali imechukua toka mamlaka husika zilipokabidhiwa ripoti husika; kambi ya upinzani inataka maelezo zaidi kutoka kwa serikali kwa kuwa mwaka mmoja umepita toka uchunguzi huo ufanyike na sehemu kubwa ya viwanja bado vipo mikononi mwa wavamizi.


Mheshimiwa Spika; kambi ya upinzani inaitaka serikali ieleze: Ni viwanja vingapi vimerudishwa na vingapi bado vipo mikononi mwa wavamizi? Ni lini serikali itarejesha viwanja vyote vilivyobaki kwenye matumizi yake kwa mujibu wa sheria kwa kurejea mapendekezo ya kamati? Ni hatua gani zimechukuliwa kwa wahusika Wizarani na kwenye halmashauri walioshiriki kusababisha hali hiyo ukiondoa maafisa wachache ambao wamefikishwa mahakamani kutokana na kesi ya kiwanja kimoja hivi karibuni? Kwa kuwa sasa Wizara ina kada ya askari (land rangers) ni lini askari hao watatembelea maeneo yote yaliyotajwa kuvamiwa kwa mujibu wa taarifa ya kamati ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa?


Mheshimiwa Spika; athari za uvamizi wa viwanja vya wazi ni kubwa katika mipango miji na maendeleo ya wananchi kwa ujumla. Mathalani katika Manispaa ya Kinondoni kwenye kiwanja na. 856 Msasani beach ambacho kwa mujibu wa Ramani ya upimaji iliyosajiliwa namba 29331 ilikuwa ni kwa matumzi ya wazi, lakini baadae kilimilikishwa kwa mtu binafsi. Athari yake ni kuzibwa kwa njia ya mkondo kuelekea baharini yamezibwa na hivyo kuleta mafuriko katika barabara na makazi ya watu wa eneo husika; hali hiyo ipo pia katika majengo ya May Fair na Markham. Kambi ya Upinzani inataka Serikali ieleze hatua zipi itachukua ili kuepusha wananchi wa maeneo ya Msasani, Mikocheni na maeneo mengine katika jiji la Dar es salaam yaliyojengwa majengo kinyume cha sheria na mipango miji na hivyo kuleta athari kubwa kwa maisha ya wananchi.


SEKTA YA NYUMBA


Mheshimiwa Spika, sekta hii ni sekta pekee inayoweza kuleta na kutekelezwa kwa dhana nzima ya maisha bora kwa kila mtanzania. Nchi yetu na watanzania kwa ujumla bado tuna matatizo makubwa ya nyumba bora na za bei nafuu kutokana na bei kubwa ya cement na bati bidhaa muhimu katika kutimiza azma ya ujenzi.


Mheshimiwa Spika, tulisema na tunasema kuwa bei ya simenti na bati inaweza kuwa chini ya shilingi elfu saba, kama serikali itakuwa na utashi wa kuwahudumia wananchi kwa dhati, Wakati ukinunua simenti Uturuki, na Paksitani ukinunua tani 600,000 bei ya tani moja ni dola za Marekani 70 hadi bandarini. Guangzhou –China tani moja ni dola za marekani 26. Kwa hesabu za kawaida kwa mfuko mmoja ni dola 3.5 sawa na shilingi 5,250 kama ukinunua Pakstani au Uturuki, Ukinunua China bei itakuwa dola 1.3.


Mheshimiwa Spika, Kambi bado inasisitiza kuwa kama Serikali inadhamira ya kweli mfuko wa simenti hauwezi kuuzwa zaidi ya shilingi 7,500. Hivyo basi tunaitaka Serikali itueleze kwanini bei ya simenti inauzwa zaidi ya shilingi 14000 kwa Dar es salaam na kwa nje ya Dar es Salaam bei ni zaidi ya hapo, wakati malighafi zinapatikana hapa hapa nchini na kiwanda kikubwa cha simenti kinatumia gesi asili ili kupunguza gharama za umeme.


Mheshimiwa Spika, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza gharama hizi na ni faida kiasi katika kodi tunayopata kwa kuwalangua watanzania. Serikali haioni kwamba ina wajibu wa kuondoa hizi kero wananchi wajenge nyumba bora na kwa bei nafuu?


SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA-(NHC)


Mheshimiwa Spika,Shirika la Nyumba la Taifa, lilipoanzishwa mwaka 1962 , moja kati malengo yake ilikuwa ni kujenga nyumba za bei nafuu kwa ajili ya watanzania wafanyao kazi mijini . Hata hivyo kwa kadiri siku zilivyosonga mbele, shirika hili liligeuka kutoka kuwahudumia masikini na watu wenye kipato cha kati na badala yake kuwahudumia watu wa kipato cha juu.


Mheshimiwa Spika, Shirika la Nyumba la Taifa linahudumia asilimia 0.5 tu ya watanzania wote wa nchi hii, swali la msingi ni je Serikali imeweka mikakati gani ya kuhakikisha kuwa shirika hili linahudumia watanzania wengi zaidi kwa kuwapatia nyumba za bei nafuu.


Mheshimiwa Spika,Kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari, mwezi Juni 2010, Katibu Mkuu wa wizara ya ardhi, akikerwa na hali ilivyokuwa katika Shirika la Nyumba, alisema kwa sasa NHC ndilo shirika la umma linaloongozwa kwa rushwa nchini Tanzania, na kwamba baadhi ya watumishi waandamizi wameligeuza shirika hilo kuwa ni ng’ombe wao wa kukamua fedha chafu!.[7] Katibu Mkuu alikwenda mbele zaidi, kwa kutolea mfano wa nyumba iitwayo Victoria house iliyopo kando ya Barabara ya Ali hassan Mwinyi ambayo pesa ya pango ilikuwa ikiingia kwenye akaunti ya mtumishi wa shirika.


Mheshimiwa Spika, kumekuwa na malalamiko pia ya kutokuwa na uaminifu baina ya wapangaji, wakishirikiana na washirika wao walioko kwenye utumishi wa shirika, kulikopelekea shirika kupata hasara ya mabilioni ya shilingi kwa kuingia mikataba tata! Kwa mujibu wa vyanzo vya taarifa hizi, mikataba tata imekuwa ikifanyika huku ikiwashirikisha wapangaji wa asili ya kihindi kwa kiasi kikubwa ambao wanatuhumiwa kuligeuza shirika hilo kama mali yao binafsi.


Mheshimiwa Spika, mwaka mmoja ukiwa umepita tangu kauli hii nzito toka kwa mtendaji wa ngazi ya juu wa wizara,Kambi ya Upinzani inaitaka serikali ilieleze Bunge hili tukufu , ni hatua gani zimechukuliwa dhidi ya watumishi hawa , na ni hatua gani zimechukuliwa dhidi ya wapangaji wasio waaminifu!




SERIKALI NA TAASISI ZAKE KUTOLIPA KODI ZA PANGO KWA WAKATI


Mheshimiwa Spika,Katika kipindi cha julai 2011 shirika lilikusanya kodi za pango pamoja na malimbikizo kiasi cha shilingi bilioni 31.


Pamoja na na jitihada za kukusanya kodi na malimbikizo na hasa yale yanayodaiwa serikali na taasisi zake, malimbikizo bado ni makubwa . Hadi machi 2011, serikali na taasisi zake ilikuwa ikidaiwa kiasi cha shilingi bilioni 1.543, baada ya kupunguza malimbikizo kwa kiasi cha shilingi milioni 115, sawa na asilimia 8 tu!Kambi ya upinzani inataka serikali ieleze ni kwa nini imekuwa ni mdaiwa sugu, na kwa nini hailipi madeni ya shirika la nyumba?


MIKOPO YA UNUNUZI NA UJENZI WA NYUMBA


Mheshimiwa Spika, Pamoja na kuwepo kwa sheria ya Mikopo ya nyumba (mortgage financing act) ya mwaka 2008 na sheria ya umiliki wa sehemu ya majengo ( unit titles act) ya mwaka 2008, masharti ya mikopo hii bado ni magumu. Mfano, kwa sasa benki zanazotoa mikopo ya nyumba masharti yake ni pamoja na muda wa marejesho ya kati ya miaka 6 mpaka 15 na riba kati ya asilimia 17 mpaka 22 kwa mwaka .




Mheshimiwa Spika, Iwapo hali hii haitabadilika , itakuwa vigumu kwa wananchi, halikadhalika shirika letu la nyumba kujenga nyumba za gharama nafuu na kwa wananchi walio wengi kuweza kumudu mikopo ya ununuzi wa nyumba.


Kambi ya upinzani, inaitaka Serikali itueleze ni kwa namna gani imejipanga kuweza kutatua tatizo hili ! Lazima Serikali iweke Mazingira ya kuziwezesha Benki kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wawekezaji na wanunuzi wa nyumba.!!!!


KODI YA ONGEZEKO LA THAMANI (VAT) NA ONGEZEKO LA MTAJI (CAPITAL GAIN TAX) KWENYE MAUZO YA NYUMBA ZINAZOJENGWA NA SHIRIKA


Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa inyowakabili watanzania wengi ni kuweza kupata nyumba za bei nafuu. Kwa sheria zetu za kodi, nyumba mpya iliyojengwa kwa ajili ya kuuzwa inapaswa kutozwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) pale inapouzwa, na anayelipa kodi hiyo ni mnunuzi!


Mheshimiwa Spika, suala la msingi ni kuwa nyumba hiyo wakati inajengwa vifaa vyote vya ujenzi ulipiwa kodi hiyo, hivyo kitendo cha mnunuzi kulipa kodi ya VAT wakati wa kununua nyumba hiyo ni kulipia kodi mara mbili (DOUBLE TAXATION). Je, serikali haioni kama haimsaidii mwananchi kuweza kuishi kwenye nyumba nzuri na kwa gharama iliyonafuu?


Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuangalia upya mkakati wake wa kuwanyang’anya watanzania hata kile kidogo walichonacho badala ya kuwaongezea umasikini iwe ni kuwapa maisha bora kama kauli mbiu yenu inavyosema. Mfano dhahiri, kwa mwaka wa fedha 2010/11 shirika lilitarajia kujenga nyumba 49 , zenye jumla ya thamani ya shilingi bilioni 4.08. Kwa gharama iliyotumika, wastani wa nyumba moja ililigharimu shirika shilingi milioni 83.4.


Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya utekelezaji wa Kazi za Shirika la Nyumba la Taifa kuanzia Julai 2010 hadi Mei 2011 wanatarajia kupata shilingi bilioni 6.3 kutokana na mauzo ya nyumba hizo , yaani faida ya shilingi bilioni1.9 Kwa tafsiri nyingine nyumba moja itauzwa na shirika la nyumba kwa shilingi milioni 129.2, wakati gharama halisi za ujenzi ni shilingi milioni 83. Kwa kila nyumba iliyounzwa shirika limepata faida ya shilingi milioni 46.


MUSTAKABALI WA NYUMBA ZA SHIRIKA LA NYUMBA


Mheshimiwa Spika, Hivi karibuni kumekuwa na sintofahamu nyingi kuhusiana na nyumba za shirika. Wapangaji (hususan katika maeneo ya katikati ya miji) wamekuwa wakilitaka shirika liwauzie nyumba. Kambi ya upinzani inaitaka serikali itoe kauli, nini msimamo wake kuhusiana na suala hili,[8] lakini sisi tunaona kuwa hakuna haja yeyote ya shirika hili kuuza nyumba hizo na badala yake iweke mkazo katika kujenga nyumba ambazo zitapangishwa kwa bei nafuu.


Mheshimiwa Spika, Sheria ya mikopo yaani "Government Loans, Guarantees and Grants Act 1974 and amendments 2003" inalifanya shirika la nyumba la taifa kulazimika kupata kibali kutoka Wizara ya Fedha hata pale ambapo halihitaji kupata dhamana ya serikali na pia hata kwa mikopo ya ndani ya nchi. Wote tunafahamu rasilimali ambazo shirika hili linazo. Pamoja na kufahamu yote, bado tumeamua kuliweka shirika hili katika urasimu mkubwa wa kiserikali wa kupata vibali kutoka wizara ya fedha bila ya sababu za lazima. Je, serikali imedhamiria ya kutekeleza ahadi zake katika ujenzi wa nyumba na kuliwezesha shirika kujiendesha kibiashara kama sheria yake inavyolitaka? Kambi ya Upinzani inaitaka serikali itoe ufafanuzi ni lini inatarajia kuanzisha mchakato wa kurekebisha sheria hiyo?






MPANGO WA UENDELEZAJI ENEO LA KIGAMBONI
Mheshimiwa Spika, tangu mwaka 2007, Wizara ilianza hatua za awali za kuendeleza mji mpya wa Kigamboni. Mradi huu unahusisha hekta 6500 linaloshirikisha kata 5 za Kigamboni, Tungi,Mjimwema,Vijibweni, Kibada na mitaa miwili ya Mbwamaji na Kizani kwenye Kata ya Somangila.


Mheshimiwa Spika, Miaka minne imepita,Kambi ya upinzani inaitaka serikali ibainishe ni lini hasa mradi huu utaanza, na michakato ya fidia kwa wananchi imefikia wapi,na ni utaratibu upi unaotumika kulipa fidia husika. Halikadhalika Kambi ya upinzani inaitaka serikali kuhakikisha kwamba kunakuwepo kwa utaratibu ulio wa uwazi, pasi na upendeleo kuhakikisha kwamba wananchi waishio ndani ya eneo la mpango ( yaani wakazi wa kata zote tano) wanabaki kwenye eneo hilo, kama ambavyo madhumuni ya mpango unavyoainisha.


Mheshimiwa Spika,Kambi ya upinzani ina taarifa juu ya mchakato unaofanyika baina ya serikali na shirika la nyumba la taifa unaohusiana na uendelezaji wa eneo la Tanganyika Pakers-Kawe, kama ilivyobainishwa na naibu waziri wa viwanda na biashara, wakati akijibu swali namba 246, ambapo pamoja na mambo mengine alikiri kwamba katika eneo la kawe kuna heka 180, ambalo ni eneo la makazi na ambalo halikuuzwa na Serikali kwa mwekezaji.Kambi ya upinzani inaitaka serikali ifahamu kwamba , eneo husika bado lina wakazi ambao walikuwa ni wafanyakazi wa Kiwanda cha Tanganyika Pakers, na hatua zozote za kuliendeleza eneo husika,lazima uhakikishe unawahusisha kikamilifu wananchi hao! Ambao wameishi eneo hilo maisha yao yote.


MAMLAKA YA/WAKALA WA KURATIBU BEI ZA PANGO LA NYUMBA
Mheshimiwa Spika, kutokana na ongezeko kubwa la watu mijini, mahitaji ya nyumba za kupanga yamekuwa ni makubwa sana . Imekuwa ni jambo ka kawaida kwa wenye nyumba kujipangia bei za kodi ya nyumba kwa kadiri wanavyoona inafaa wao, kwa kuwa hakuna chombo cha kuwathibiti. Matokeo yake kodi ya nyumba imegeuka mzigo mkubwa sana kwa wananchi wa kawaida. Kambi ya upinzani inaitaka serikali, iweke utaratibu utakaotambulika kisheria utakaoweka mwongozo na kuweza kuwadhibiti gharama za kodi za nyumba kwa ujumla wake. Kwa maana nyingine ni kuanzisha mamlaka ya udhibiti itakayoitwa ”Real Estate Regulatory Authority”.


WAKALA WA TAIFA WA UTAFITI WA NYUMBA BORA NA VIFAA VYA UJENZI- (NHBRA)
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA), jukumu la Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (National Housing and Building Research Agency - NHBRA) ni kufanya tafiti, kuelimisha, kukuza, kushauri, kuhamasisha na kusambaza matokeo ya utafiti na utaalam wa ujenzi wa nyumba bora na za gharama nafuu. Lengo la Wakala ni kuinua na kuboresha viwango vya nyumba kwa kutumia vifaa vilivyotafitiwa na vipatikanavyo hapa hapa nchini jambo ambalo litaongeza ubora wa maisha ya wananchi mijini na vijijini ili kutimiza malengo ya MKUKUTA.


Mheshimiwa Spika, kambi ya upinzani inataka ipewe taarifa ni kwa namna na kiasi gani wakala huu umefanikiwa kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake kwani ujenzi wa nyumba za matope, fito na nyasi bado uko pale pale jambo ambalo linasababisha maisha bora kwa kila mtanzania kuwa ni kitendawili kwa miaka mingi ijayo!


MUHSTASARI WA MATUMIZI YA FEDHA ZA KAWAIDA NA MAENDELEO KWA MWAKA WA FEDHA 2010/2011


Mheshimiwa Spika,Katika mwaka wa fedha 2010/11 , Wizara iliidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 53,848,061,000. Kati ya fedha hizo shilingi 6,423,295,000 zilitengwa kwa ajili ya mishahara, shilingi 25,159,688,000 kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi 22,265,078,000 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.




Mheshimiwa Spika, Hadi Mei , 2011 Wizara ilipokea jumla ya shilingi 27,787,178,679 (Bilioni 27.7)sawa na asilimia 51.5 ya tengeo la bajeti kwa mwaka. Kati ya fedha hizo, shilingi 25,658,017,495 sawa na asilimia 92.5 ya fedha zilizopokelewa , shilingi 13,226,897,075 zilitumika kwa ajili ya matumizi mengineyo, shilingi 8,499,539,334 zilitumika kulipa mishahara na shilingi 3,931,581,086 zilitumika kutekeleza miradi ya maendeleo.Kambi ya upinzani inaitaka serikali itueleze ni kwa sababu gani kati fedha za maendeleo zilizotengwa ( Tshs.22,265,078,000), zilizoweza kutumika ni Tshs. Bilioni 3.9 tu? Ni miradi mingapi iliyokuwa itekelezwe katika mwaka wa fedha 2010/2011 imeshindwa kutekelezwa kutokana na kukosekana huko kwa fedha?


POSHO NA MARUPURUPU VS FEDHA ZA MIRADI YA MAENDELEO


Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tulikuja na hoja ya kuitaka serikali iangalie upya mfumo wake wa ulipaji posho na marupurupu , lengo likiwa na kuisaidia serikali kuokoa matumizi yasiyo ya lazima na hatimaye fedha ambazo tunazitumia kulipana posho tuzielekeze kwenye matumizi yenye tija kwa wananchi. Tunashukuru kwamba hatimaye tulichokuwa tukikipigia kelele na kubezwa, kimeanza kutekelezwa na Serikali hii hii . Mhe. Waziri Mkuu wakati akiliomba Bunge kuahirisha hoja ya Wizara ya Nishati na Madini ili waende kujipanga upya alitamka yafuatayo , naomba kunukuu:“Mheshimiwa Spika, ushauri mlioutoa ni wa msingi sana. Moja mmesema Serikali nunueni mtambo na tusitafute visingizio vya fedha. Kwamba tafuteni kila mbinu huko,tafuteni,kateni posho zenu,kateni vitu gani,nendeni mkatazame magari mnayotumia haya, punguza huko. Tazameni OC yenu kikamilifu,mtaona kule ndani yako matumizi mengine ambayo mkiamua kwa dhati mnaweza kabisa mkayaondoa huko, yakaenda yakanunua mitambo ya uhakika,yakawasaidia hata kuongeza uwezo wa mafuta kwa ajili ya mitambo inayotumia mafuta” Mwisho wa kunukuu.


Mheshimiwa Spika,Kumbe inawezekana!Tukiamua kupunguza anasa na starehe na kuwekeza kwa wananchi wetu,inawezekana! Hakika Inawezekana!Katika Wizara hii zaidi ya shilingi bilioni moja, zimetengwa kwa ajili ya posho(wakati ni bilioni 3.9 tu zilitumika kwa shughuli za maendeleo). Cha kusikitisha zaidi hadi karne hii,kuna posho zinatengwa kwa ajili ya kuwalipia baadhi ya maafisa bili za maji na umeme ‘kwa maofisa wanaostahili’. Mfumo huu umesambaa mpaka kwenye Halmashauri zetu.


Mheshimiwa Spika, ni wajibu wa serikali kuagalia upya mfumo huu wa kimwinyi, na kuacha huduma hizi ‘BINAFSI’ zigharamiwe kwa viongozi wa waandamizi (wakuu) tu, wa mihimili mitatu ya dola! Tatizo kubwa linalotukumba kama nchi, ni kuendesha mambo kwa mazoea. Lazima tubadilike! Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
.................................................. ......
Halima James Mdee(Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani-Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
15.08.2011




[1] Tathmini iliyofanywa na Consolidated Holding Corporation imegundua kwamba mwekezaji, RAI Group anayemiliki mashamba ya Setchet, Murjanda na Gidagamowd kati ya mashamba yanayolalamikiwa mwekezaji alikuwa amelima 53% tu ya shamba


[2] Tarehe 29/1/2008 , akijibu swali Bungeni, aliyekuwa waziri wa kilimo kipindi hicho, Mhe. Wassira aliliambia Bunge kwamba jumla ya hekta 2500 zilikodishwa kwa vikundi vya ushirika vya wakulima wadogo 884Wassira aliliambia Bunge kwamba jumla ya hekta 2500 zilikodishwa kwa vikundi vya ushirika vya wakulima wadogo 884.


[3] Mwaka 2004 kupitia barua zenye kumbukumbu namba CAE/426/449/01 ya tarehe 14 Januari 2004 na barua yenye kumbukumbu namba GC.118/426/01 ya tarehe 22/7/2004 Wizara Chakula na kilimo iliiandikia Halmashauri ya wilaya ya Hanang ikiitaarifu juu ya uamuzi wa kamati ya Baraza la Mawaziri namba 8/2003 kilichofanyika Dodoma ,tarehe 10 Novemba 2003. Ambapo moja ya maamuzi ya hiko kikao ni kugawa mashamba ya warret na Gawal kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo kwa shughuli za kilimo na ufugaji.


[4] Hati ya kuandikishwa kwa Kijiji , na DSM VIJ. 7


[5] Akijibu maswali tarehe 29/1/2008 , akielezea moja ya mafanikio ya mwekezaji huyu ni kukodisha jumla ya hekta 573 na 786 kwa vikundi vya wakulima wadogo 39 na 59 katika mwaka 2006/2007 na 2007/2008 na kwamba hekta 174 zilitarajiwa kukodishwa mwaka 2008.


[6] Improving Land Sector Governance in Africa : The Case of Tanzania. Paper prepared for the “ Workshop on “ Land Governance in support of the MDGs: Responding to New Challenges” Washington DC March 9 -10 2009, J.M Lusugga Kironde , Ardhi University , Dar es Salaam, Tanzania.


[7] Tanzania Corruption Tracker System


[8] Majibu pia yajumuishe msimamo juu ya maombi ya kuuziwa nyumba Block ‘A’ na ‘B’ Iringa Flats, Iringa Road Hazina ‘ X’ Dodoma.

No comments: