Tarehe 9 Aprili, 2011
DAR ES SALAAM
Uundwaji wa Chama cha Wanasheria cha Tanzania Bara na Majukumu yake
Chama cha Wanasheria cha Tanzania Bara (“TLS”) ni Taasisi ya Wanasheria wa
Tanzania Bara iliyoanzishwa kwa Sheria ya Chama cha Wanasheria cha Tanganyika,
Sura ya 307 Toleo la 2002. Kwa mujibu wa Sheria hii, Chama kina, pamoja na mambo
mengine, jukumu la kuisaidia Serikali katika mashauri yanayohusu utungaji wa sheria
na utekelezaji na matumizi ya sheria, na pia kulinda na kusaidia umma katika masuala
yote yanayohusika na kadhia za sheria.
Chama cha Wanasheria kinatoa taarifa hii kwa mujibu wa mamlaka mahsusi ya sheria .
Mazingira ya Muswada wa Sheria ya Marejeo ya Katiba, 2011
Tarehe 11 Machi, Muswada wa Sheria ya Marejeo ya Katiba, 2011 (kwa kifupi
“Muswada”) ulitangazwa katika Gazeti la Serikali la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Toleo Namba 1 Jarida Na.2. Chama kilipata nakala ya Muswada huo Jumanne, tarehe 30
Machi, na kilisambaza hizo taarifa kwa wanachama wake siku ya Alhamisi tarehe 31
Machi ili kupata maoni yao. Siku ya Jumamosi tarehe 2 Aprili, Chama cha Wakufunzi wa
Chuo cha Dar es Salaam (UDASA) waliendesha mjadala wazi kuhusu Muswada, mjadala
ambao uliripotiwa kwa mapana katika vyombo vya habari. Siku ya Jumanne, tarehe 5
Aprili, Chama chetu kilialikwa kupitia Kurugenzi ya Kamati za Bunge (“Kurugenzi”)
kushiriki katika mjadala juu ya Muswada ambao ulipangwa kujadiliwa na Kamati ya
Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge (kwa kifupi “Kamati”) tarehe 7 Aprili Dodoma, kama
ilivyopangwa awali. Mnamo mwisho wa siku hiyo Chama chetu kiliulizia maendeleo
kuhusu mijadala bayana, na kikahabarishwa kwamba sasa sehemu mpya tatu (3)
zimetajwa kwa ajili ya mijadala bayana, yaani Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar;
aidha taarifa tulizopata ni kwamba mijadala itafanyika tarehe 7 na 8 Aprili, na ikibidi
tarehe 9 Aprili. Kutokana na uthibitisho huu,Chama chetu kikaahidi kushiriki kikao cha
Dar es Salaam.
Jumanne tarehe 5 Aprili Muswada uliwakilishwa Bunge ni kwa Hati ya Dharura isomwe
mara ya kwanza. Tarehe 7 Aprili, Rais wa Chama chetu aliipelekea Kamati - kwa
maandishi - maoni na mapendekezo ya wanachama wa Chama cha TLS kuhusu
Muswada. Tarehe 8 Aprili, Rais wa Chama cha TLS alitoa mapendekezo kwa mdomo.
Baada ya kushiriki katika mijadala ya umma, Chama kilitiisha mdahalo kuhusu
Muswada kwa wanachama ili kuhakikisha mawazo ya wanachama wengi iwezekanavyo
yanakusanywa kuthibitisha msimamo wa wengi katika C hama.
Hoja na Maoni
UTANGULIZI
Kwa kuwa Chama cha TLS kimejizatiti kwa dhati kuimarisha na kuendeleza
utawala wa sheria nchini Tanzania, kwa kujua kwamba sheria inapozingatiwa
ipasavyo, utawala wa sheria huwalinda wananchi dhidi ya matumizi ya kibabe ya
mamlaka ya Serikali; kwa kuwa tunaafiki dhana kwamba sheria zote lazima
zitungwe kwa shabaha ya kuenzi Utawala wa Sheria, utawala bora na nyanja ya
demokrasia ambayo imejengewa misingi imara katika falsafa ya haki ya nchi yetu
na ambayo inashabihiana na viwango vya kimataifa na vyenye ubora maridhawa;
kwa kuwa Chama kinaamini kwa dhati kwamba hatima na mchakato mzima
kuhusu marejeo na utungaji wa Katiba mpya unapaswa kupata uhalali muafaka
kwa njia ya ushirikishwaji wa wananchi; na kwa kusisitiza kwamba haki haitakiwi
tu ifanyike, bali pia ionekane kwamba inafanyika, Chama kinaeleza msimamo
wake mintarafu ya Muswada kama ifuatavyo:
1. Kuhusu lugha ya Muswada: Chama kinapendekeza kwa msisitizo kwamba
Muswada utangazwe katika lugha ya Kiswahili, kwa kuzingatia dhana ya haki
kupatikana (jambo ambalo linamaanisha mtu wa kawaida kupata nakala na
uelewa) kwa Watanzania wote (wanaoishi vijijini na mijini, wananchi wa
kawaida, wenye mapato ya kati na wa matabaka ya juu), ikiwa ni sambamba na
lugha inayotambulika ya toleo rasmi la Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya
Tanzania, 1977 (kwa kifupi “Katiba”);
2. Kuhusu jina la Muswada: Chama kinashauri kwa dhati kwamba jina la
Muswada lisomeke ‘Muswada wa Kutunga Katiba Mpya, 011’ ili kuonyesha
dhahiri nia ya wananchi (kwamba wanataka Katiba mpya, siyo marekebisho
yake) katika mchakato mzima;
3. Kuhusu maelezo ya awali la Muswada: Chama kinapendekeza kwamba tamko
la awali lirekebishwe na lioneshe wazi madhumuni: MUSWADA wa Sheria
itakayoweka mfumo wa kutunga/kuweka Katiba mpya inayokidhi vigezo
vinavyokubalika kimataifa vya demokrasia na utawala bora’;
4. Kuhusu ukomo wa Katiba na utungaji wa rasimu ya Katiba mpya: Chama
kinatoa tahadhari kwamba Katiba ya sasa haisemi lolote kuhusu ukomo wa
Katiba na utungaji wa katiba mpya; kwa mujibu wa Ibara ya 98, ni utaratibu
pekee unaotajwa wa kufanya marekebisho. Kutokuwepo kwa vipengele vya suala
hili kutafanya michakato yoyote ya kuunda Katiba mpya kuwa batili.
Hivyo basi kama jambo la lazima, Chama kinapendekeza kwa dhati yafanywe
marekebisho ya Katiba, kuwekwe vipengele vitakavyoruhusu utaratibu wa ukomo
wa Katiba iliyopo na utungaji wa Katiba mpya.
5. Kuhusu kifungu cha 5 cha Muswada - Uundwaji wa Tume: Chama kinashauri
kwa dhati kwamba Tume iundwe moja kwa moja na Sheria hii. Lugha
inayotumika katika Muswada inakasimu kwa Rais wa Jamhuri ya Tanzania
mamlaka ya kuunda Tume ambapo Rais atakuwa na uhuru wa utendaji. Aidha
Rais analazimika kuunda Tume hiyo baada ya tarehe 1 Juni 2011 (tarehe ambapo
sheria hii itaanza kutumika), lakini hakuna kikomo kinachotajwa cha jukumu
hili.
Ili kurekebisha kasoro hizi, kifungu hiki kisomeke, “Tume ya Katiba inaundwa
kwa Sheria hii.”
6. Kuhusu kifungu cha 6 cha Muswada - Uteuzi wa wajumbe wa Tume: Chama
kinatoa maoni na mapendekezo yafuatayo:
*Uwakilishi katika Tume:
Muswada unapendekeza Tume iwe na
uwakilishi wa Tanzania Bara na Visiwani kwa idadi sawa. Lakini kifungu
hiki hakizingatii hata kidogo tofauti ya ukubwa wa idadi ya watu na
kwamba Katiba ya Muungano inahusika na Zanzibar pale tu masuala ya
Muungano yanapotajwa. Hivyo basi, ili kuhakikisha kuna uwiano stahiki
katika Tume (yaani unaozingatia sura halisi ya mambo), idadi ya
wajumbe kutoka Tanzania Bara na kutoka Visiwani izingatie idadi ya
watu.
*Muundo wa Tume:
Tume iwe Jopo la Wataalamu watakaoteuliwa
kutoka mchanganyiko wa kada za taaluma, mashirika na jumuiya
mbalimbali kwa kuzingatia jinsia, dini na ngazi za utaalamu. Aidha kif.
6(2)(e) kinampa Rais mamlaka ya kuteua kwa hiari yake wajumbe wa
Tume wasiokuwa katika makundi ya watu waliotajwa katika fasili (a)
hadi (d)- jambo ambalo linaweka mwanya wa matumizi mabaya ya
madaraka.
7. Kuhusu Kifungu cha 8 cha Muswada - Hadidu za Rejea (kwa kifupi
“hadidu”) za Tume: kwa ajili ya uwazi na uwajibikaji, Chama kinapendekeza
kwamba hadidu ziandikwe na chombo huru na ziidhinishwe na Bunge la
Tanzania, badala ya Rais.
8. Kuhusu Kifung cha 14 cha Muswada – Gharama za Tume: Muswada
unadhihirisha dhamira ya Serikali kwamba matumizi ya Tume yatalipwa kutoka
Mfuko Mkuu wa Serikali. Chama kinapendekeza kwa msisitizo kwamba kuwe na
mfumo wazi, bayana na wa uwajibikaji katika kuidhinisha na kutoa taarifa za
matumizi.
9. Kuhusu Kifung cha 16 cha Muswada – Kutoa taarifa kwa Rais: ili pawe na
mfumo wazi na bayana, Chama kinapendekeza kwamba Taarifa ya Tume iweze
kupatikana kwa umma, yaani wananchi waione na waruhusiwe kutoa maoni yao
juu yake, hata kama taarifa inapelekwa kwa Rais.
10. Utekelezaji: ili kuhakikisha kwamba Watanzania hawaachwi nje ya mchakato
huu, Chama kinapendekeza kwa msisitizo kwamba shughuli ya Tume – kwa
mtizamo wa kawaida – zifanyike mikoa yote 26 ya Tanzania, na siyo katika
baadhi tu ya mikoa, kama msimamo ulivyojitokeza kwenye mijadala bayana
iliyoendeshwa na Kamati ya Bunge.
11. Kuhusu vipengele visivyoruhusiwa kuguswa – Kifungu cha 9 (2) na 20 (1):
Muswada unafanya vipengele vya msingi vinavyohusu ibara za msingi za Katiba
visiguswe. Kwa mfano, kif. 9 (2) kinataka mambo ya Muungano na suala la ofisi
ya Rais, mambo yote mawili ambayo yaliyowekwa na Ka tiba, yasiguswe. Kif. 20
(1) kinakinzana na Ibara 26(2) ya Katiba ambayo inalinda haki ya mwananchi
kupinga uhalali wa kikatiba wa sheria za nchi. Kuviacha vifungu vibaki pia ni
kukiuka utekelezaji wa Utawala wa Sheria.
12. Kuhusu kasoro za uchapishaji zimebainika, lazima ziepukwe kwa
uangalifu: Usahihi wa Muswada unategemea uandishi na rejea sahihi. Kwa
mfano, kif. 19 kinatakiwa kurejea kif. 18 na siyo kif.19; na kif. 20 (3) kirejee kif.
20(2) na siyo kif. 20 (1). Athari ya hili la pili, kwa mfano, ni kumtwika tuhuma ya
jinai mtu yeyote anayeamua kufungua shauri mahakama ni kupinga Sheria hii –
jambo ambalo ni kinyume na Katiba, na ni ukiukwaji wa haki na wajibu wa
msingi.
13. Kuhusu Kifungu cha 21 cha Muswada - Kutangazwa Baraza la Kutunga
Katiba: Muswada unatamka kwamba Rais ana mamlaka ya kuunda Baraza la
Kutunga Katiba na kwamba anaweza kutamka Bunge lijigeuze kuwa Baraza la
Kutunga Katiba.
Chama kinapendekeza kwamba Rais asiwe na mamlaka ya kuligeuza Bunge
kuwa Baraza la Kutunga Katiba, na kwamba muundo wa Baraza uamuliwe na
wananchi watakaoteuliwa kutoka kada mbalimbali (yaani taaluma na uzoefu,
mashirika, taasisi za kidini na makundi mbalimbali).
14. Kuhusu Kifungu 26 cha Muswada – Kusimamia kura ya maoni
(referendum): inaonekana kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi si mahala pake
kuratibu suala la uhalalishaji wa Katiba. Chama kinapendekeza kwamba taasisi
za jamii, vyama vya siasa na watu binafsi na makundi mengine waruhusiwe
kushiriki kwa uhuru uelimishaji wa umma kuhusu upigaji wa kura ya maoni.
Hatimaye Tume ya Katiba idhibiti uenendeshaji wa upigaji kura ya maoni.
15. Kuhusu sehemu ya VI – Uhalalishaji wa Katiba : Chama kinapendekeza
kwamba mchakato wa uhalalishaji uendeshwe na Tume, siyo Tume ya Taifa ya
Uchaguzi, kwa kuwa imeundwa na Katiba.
Mpango wa Chama wa Hitimisho:
a. Chama kinashauri kwa dhati kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano ya
Tanzania, Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, aiondoe Hati ya Dharura
iliyoambatanishwa na Muswada uliowasilishwa Bungeni. Kwa ushauri wa Chama
Muswada ufuate utaratibu wa kawaida ili Wabunge na umma wote upate fursa
ya kutosha kujadili na kutoa maoni kuhusu Muswada.
Hali halisi, Halmashauri ya Chama cha Wanasheria kimeamua
kumtembelea Mtukufu Rais ili kumfikishia yeye binafsi ujumbe huu.
b. Chama kinaisihi Serikali isitafute kugundua upya gurudumu katika mchakato
huu – kwa kadiri inavyowezekana, Serikali ijifunze kutoka uzoefu wa nchi
nyingine, kama vile Kenya na Uganda.
c. Chama chetu kiko mbioni kuunda Kamati ya Katiba, ambayo- pamoja na mambo
mengine- itaishauri Halmashauri yetu juu ya maendeleo ya mchakato
unaoendeshwa na Serikali, itatoa msaada wa kitaalamu na utatoa mapendekezo
stahiki kwa Halmashauri yetu, umma na vyombo vinavyohusika na mchakato wa
kutunga Katiba.
Kama hapana budi, Halmashauri ya Chama itapanua majukumu ya Kamati hii
ili iweze kuwa msemaji kwa niaba yake kuhusu mijadala, ambayo yaweza
kuhitaji hatua zaidi.
Imewakilishwa kwa niaba ya Chama cha Mawakili Tanzania Bara
grancis K. Stolla
RAIS
No comments:
Post a Comment