Tuesday, August 3, 2010

Matokeo zaidi kura za maoni za CCM leo

Katika jimbo la Tanga Mjini, mbunge anayemaliza muda wake Harith Mwapachu, ameangushwa na Omari Nundu
kwa kuzidiwa kura 5293 huku Kassim Kisauji akipata kura 5087.

Katika Jimbo la Muheza, mbunge anayemaliza muda wake Herbet Mntangi ameshinda kwa kura 9,142, akifuatiwa na Julius Shemwaiko (6,595) na Jonathan Mhina (629).

Korogwe Mjini Yussufu Nasiri ameshinda kwa kura 2513, akifuatiwa na Joel Bendera (2258) na Mariam Nafutalkura (428).

Jimbo la Lushoto, Mkuu wa mkoa wa Manyara, Henry Shekifu, ameshinda kwa kura 4178, akifuatiwa na Balozi Abdi Mshangama 2,450.

Katika Jimbo la Bumbuli, Januari Makamba ameshinda kwa kura 14,612 akifuatiwa na mbunge anayemaliza muda wake William Shelukindo (1,700) na Abdi Mshihiri (609).

Jimbo la Pangani limekwenda kwa Ofisa Tawala mkoa wa Ruvuma Salehe Pamba, ambaye ameongoza kwa kura 4,391 akifuatiwa na Mohamed Rished (4,442) huku Rajabu Selemani akipata kura 1,434.


Jimbo la Buchosa, Mkuu wa wilaya ya Sikonge, Dk. Charles Tizeba ameongoza kwa kupata kura 11,278 akifuatiwa na mwandishi wa riwaya Erick Shigongo (7,574) na mbunge anayemaliza muda wake Samwel Chitalilo, akishika nafasi ya tatu.


Katika Jimbo la Kibaha Vijijini, mgombea Hemed Jumaa ameibuka kidedea kwa kura 1114 akifuatiwa na Waziri wa zamani wa Afrika Mashariki, Dk Ibrahim Msabaha (987) na ya tatu ilikwenda kwa Husein Chuma (463).

Jimbo la Bagamoyo, Waziri wa Miundo Mbinu Dk. Shukuru Kawambwa, amefanikiwa kutetea nafasi yake ya ubunge kwa kupata kura 6576 na kumshinda Andrew Kasambala aliypata kura 1061.



Katika Jimbo la Mkuranga, mbunge anayemaliza muda wake, Adam Malima, ameshinda kwa kura 5805 akifuatiwa na Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Pwani, Abdalah Ulega (3763) na Mbaraka Kihame (3437).




KATIBU wa NEC (Fedha na Uchumi) wa CCM Taifa, Amos Makalla, ameibuka na ushindi wa kishindo katika Jimbo la Mvomero na kumwangusha mbunge anayemaliza muda wake, Suleiman Saddiq. Makala ameongoza kwa kura 13,479 akifuatiwa na Saddiq (6,476).

Wagombea wengine waliojitokeza ni Leoni Msimbe (1,078), Ackley Limoso (367), Albanie Mgweno (315), Hussen Sungura (137) na Mussa Mruma (139).


Katika jimbo la Mchinga mkoani Lindi, mgombea Said Mtanda amemwangusha mbunge anayemaliza muda wake Mudhihiri Mudhihiri, baada ya kuzoa kura 3,870 dhidi ya mpinzani wake aliyepata kura 1,730.

Mgombea mwingine Mayasa Mikidadi aliyepata kura 598 akifuatiwa na Faradhani Ng’uto, aliyepata kura 439, Miki Kumtungwe (345) na Yussuph Mpwatile (139).

Matokeo ya Lindi Mjini hadi sasa hayajatolewa kutokana na kugubikwa na utata unaodaiwa kusababishwa na ongezeko la kura ikilinganishwa na idadi ya wapiga kura.

Hata hivyo, inadaiwa Mohammed Aziz anaongoza kwa kata nyingi.


MAWAZIRI wawili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na naibu mawaziri watatu na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar ni miongoni mwa wagombea walioanguka katika kura za maoni zilizopigwa visiwani Zanzibar.


Aliyekuwa Mwenyekiti Umoja wa Vijana CCM (UVCCM) Hamad Masauni ameibuka kidedea, huku wabunge wa zamani wengi wakipoteza nafasi zao.

Katibu wa CCM Wilaya ya Mjini Magharibi, Fatma Shomari, alithibitisha na kusema wagombea wengi walioshindwa katika mchakato wa kura za maoni wamewasilisha malalamiko yao .

Katika jimbo la Kikwajuni, lililokuwa na upinzani mkali, Masauni aliibuka na ushindi wa kishindo baada ya kupata kura 990 na kuwashinda Mohamed Ali Mohamed kura 511, akifuatiwa na Saleh Ramadhan Ferouz kura 155 na mbunge wa sasa, Parmukhi Hoogan Singh aliyepoteza jimbo hilo.


Mwakilishi wa jimbo hilo, Burhani Saadati Haji ambaye ni Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Mazingira wa SMZ amepoteza jimbo hilo baada ya kupata kura 858, dhidi ya mfanyabiashara Mahmoud Mohamed Mussa aliyepata kura 1,028.

Burhani alionekana katika ofisi za CCM Wilaya ya Mjini ambapo aliwasilisha malalamiko yake, ikiwemo kutoridhishwa na mchakato wa kura za maoni.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Sultani Mohammed Mungheiry ameshindwa katika mchakato wa uwakilishi baada ya kupata kura 1,722 na kuangushwa na mfanyabiashara Simai Mohamed Said aliyepata kura 5,017.

Naibu mawaziri watatu wameanguka katika mchakato wa kura za maoni, akiwemo Khatib Suleiman wa jimbo la Bububu na Naibu Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Tafana Kassim Mzee wa jimbo la Uzini na Mwakilishi Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Mzee Ali Ussi wa jimbo la Chaani.

Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wametetea nafasi zao katika majimbo ya uchaguzi, akiwemo Dk. Hussein Ali Mwinyi wa jimbo la Kwahani aliyezoa kura 1,662, akifuatiwa na Jaffar Khamsi Ramadhan aliyepata kura 150.

Mwakilishi katika jimbo la Kwahani, Ali Salum Haji ameibuka mshindi kwa kupata kura 861 dhidi ya Hija Sudi Juma, aliyepata kura 371.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (Katiba na Utawala Bora) Mahadhi Juma Maalim, ameibuka na ushindi katika nafasi ya Ubunge Jimbo la Muyuni kwa kupata kura 1,940 na kumuangusha mbunge wa muda mrefu Dk. Hajji Mwita.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mohammed Seif Khatib, ametetea nafasi yake na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Seif Ali Iddi ameshinda katika jimbo la Kitope.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Haroun Ali Suleiman ameshinda katika jimbo la Makunduchi kwa kupata kura 3,479 dhidi ya mpinzani wake Vuai Ali Mwinyi aliyepata kura 377, huku nafasi ya ubunge ikichukuliwa na Samia Suluhu Hassan.

Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, ameshinda katika mchakato wa nafasi ya uwakilishi jimbo la Mwanakwerekwe baada ya kupata kura 1,239, na kumshinda mpinzani wake wa karibu Suleiman Ali Haji aliyepata kura 784, huku mbunge wa zamani wa jimbo hilo Haji Sereweji akishinda.

Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Machano Othman Said, amefanikiwa kutetea nafasi yake ya uwakilishi jimbo la Chumbuni, huku nafasi ya ubunge ikichukuliwa na Perera Ame Silima kufuatia mbunge wa sasa Omar Mussa kuamua kutogombea.

Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, Issa Haji Gavu ameibuka na ushindi baada ya kupata kura 1,195 na kuwashinda wapinzani wake, akiwemo mwakilishi wa sasa Kombo Haji Mkanga.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma, ameibuka na ushindi katika jimbo la Kwamtipura, baada ya kupata kura 1,369 na kumshinda mpinzani wake wa karibu, Kassim Juma aliyepata kura 518, wakati mbunge wa jimbo hilo Zubeir Ali Maulidi akipoteza.

Katibu wa Chama cha Mpira Mkoa wa Mjini Magharibi (ZFA), Nassor Salum Ali, ameibuka na ushindi kwa kupata kura 540 baada ya kumuangusha Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Kamal Basha Pandu katika nafasi ya uwakilishi jimbo la Rahaleo pamoja na mwandishi wa habari mkongwe Enzi Talib.

Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamuhuna amefanikiwa kutetea nafasi yake katika jimbo la Donge ambapo aliongoza kwa kura nyingi katika matawi yote.


Huko wilayani Kilombero mkoa wa Morogoro, yanaonyesha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo , Castor Ligalama ameshindwa kutetea nafasi hiyo. Katika matokeo ya kata 11 kati ya kata 23 za wilaya ya Kilombero, yanaonyesha mgombea Abdul Mteketa, anaongoza katika kata saba, akifuatiwa na Profesa Jumanne Mhoma aliyeongoza katika kata mbili, huku Ligalama akioongoza katika kata moja ya Chisano.

Katika matokeo hayo, Mteketa amepata kura 4,492 akifuatiwa na Profesa Mhoma aliyepata kura 2,266 wakati Luteni Kanali Mstaafu Haruni Kondo akishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 1,548 na kumzidi Ligalama ambaye amepata kura 445 tu.

Hata hivyo, matokeo ya awali yaliyokuwa yakitolewa kwa njia ya simu na makatibu kata wa kata zilizo mbali na makao makuu ya wilaya hiyo, yanaonyesha dalili ya kushinda kwa mgombea Mteketa, na hivyo kumpa nafasi ya kuingia katika mchakato wa uchaguzi utakaoendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Huko Moshi baadhi ya mawakala katika uchaguzi wa kura za maoni kupata mgombea ubunge wa jimbo la Moshi mjini kwa tiketi ya chama cha mapinduzi (CCM), wamepinga matokeo ya kura hizo, kwenye vituo vyao.

Mawakala hao waliokuwa wakisimamia kura za mgombea wa nafasi hiyo Thomas Ngawaiya, wameelezea dosari kadhaa zilizojitokeza na kuvuruga kura hizo.

Kwa mujibu wa taarifa mawakala hao, wamedaiwa kumwandikia barua Ngawaiya, ambaye ameshika nafasi ya pili katika matokeo hayo, kuelezea sababu za wao kupinga kusaini matokeo katika vituo vyao.

Barua hizo ambazo pia zimewasilishwa kwa katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kazidi, zimeelezea dosari hizo kuwa ni pamoja na kuwepo ongezeko la wapigakura ikilinganishwa na wale walioandikishwa kwenye daftari pamoja na baadhi ya wanachama kunyimwa haki ya kupiga kura hizo, licha ya kuwa na vigezo vyote vya kupiga kura.

Katika mtaa wa Kwakombo, kwenye kata ya Mji-mpya, msimamizi wa uchaguzi huo Jovine Samwel amebainisha kuwepo wanachama wanne, ambao waliruhusiwa kupiga kura ingawa majina yao hayakuwepo kwenye orodha.

Imedaiwa msimamizi huyo alitoa taarifa katika ofisi za chama wilaya lakini hakuna hatua zilizochukuliwa badala yake wanachama hao waliruhusiwa kupiga kura hizo za maoni.

Hata hivyo taarifa katika kituo hicho zimedai kuwa kura 16, zilionekana kupungua wakati wa kuzihesabu ikilinganishwa na idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura kwenye kituo hicho.

Kwa upande wa tawi la Kilimanjaro, katika kata hiyo ya Mji-mpya, uliokuwa ukisimamiwa na Sharifa Komba, kulizuka utata baada ya idadi ya wapiga kura kuzidi ile iliyoandikwa kwenye daftari.

Imedaiwa katika daftari waliandikishwa wapigakura 139, kwenye tawi hilo , lakini matokeo ya kura yameonyesha jumla ya wanachama 146, walipiga kura hivyo kuleta utata katika matokeo hayo.

Kutokana na dosari hizo mawakala katika vituo hivyo, wamemwandikia Ngawaiya barua ya kupinga kusaini matokeo hayo na kumtaka kuchukua hatua zaidi kwa dosari zilizojitokeza.

Akizungumza kwa njia ya simu jana jioni kuhusu suala hilo , Ngawaiya, alisema kuwa suala hilo liko mikononi mwa viongozi wa CCM katika ngazi ya wilaya na mkoa, hivyo hayuko tayari kulizungumzia.

“Suala hili liko kwa viongozi wa chama sasa ofisi ndio inajua mimi sina cha kuongea kwa sasa”, alisema Ngawaiya.

Hata hivyo wakati akitoa matokeo ya kura za maoni kwa waandishi wa habari juzi, katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kazidi, alithibitisha kupata taarifa za Ngawaiya kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

Ngawaiya ambaye ni mwenyekiti wa wazazi mkoa wa Kilimanjaro, alikuwa mmoja wa wagombea tisa wa kinyang’anyiro hicho, ambapo alipata kura 1,539, huku mshindi wa uteuzi huo Athman Ramole akishinda kwa kura 1,554.

No comments: