Wednesday, June 13, 2018

MAHAKAMA YAELEZWA 'MHASIBU TAKUKURU' ALIVYOKUWA AKIFANYA MIAMALA YA UONGO KUFICHA UMILIKI WA MALI ZAKE

Na Karama Kenyunko,Globu ya jamii

UPANDE wa mashtaka katika kesi ya utakatishaji na kumiliki utajiri kuliko kipato chake inayomkabili, aliyekuwa Mhasibu wa Takukuru Godfrey Gugai na wenzake umeieleza Mahakama kuwa, uchunguzi umeonesha kuwa, Gugai alifanya miamala ya uongo ili kuficha umiliki wa mali zake.

Hayo yameelezwa leo mahakamani hapo wakati watuhumiwa hao wakisomewa maelezo ya awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo wamekubali maelezo yao binafsi na kuyakana mashtaka yote yanayowakabili.

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasini Katera.Washtakiwa wamesomewa maelezo hayo leo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi na Wakili wa serikali Awamu Mbagwa.

Akiwasomea PH washtakiwa hao, wakili Mbagwa alidai kuwa Gugai anakabiliwa na makosa mbalimbali ikiwamo kumiliki mali isiyoelezeka, kughushi na kutakatisha fedha ambayo anadaiwa kuyatenda kati ya mwaka 2005 na mwaka 2006.Alidai kuwa Gugai aliajiriwa na Takukuru kama mchunguzi daraja la tatu mwaka 2001 na baadae 2009 aliteuliwa kuwa Mhasibu Mkuu wa Takukuru kazi alïyoendelea nayo hadi Agosti 2016 alipofukuzwa kazi.

Alidai washtakiwa wenzake wote ni marafiki zake wa karibu na kwamba katika kipindi chote cha ajira Gugai hakuwa na chanzo cha mapato ambacho kingeweza kumpatia kipato zaidi ya ajira yake.Alidai kwenye mishahara ya mshtakiwa na malupulupu mengine alijipatia kipato halali cha Sh.852,183,160.46 kutoka kwa mwajiri wake.

Pia mikopo yote aliyoipata katika benki ya CRDB, NBC, benki ya Posta na saccos ya Takukuru ilikiwa ina thamani ya Sh 137 milioni.Alidai, 2009 alitakiwa kufanya matamko juu ya umiliki wa mali zake ambapo alitamka kuwa hakuwa na vyanzo vingine vya mapato zaidi ya ajira yake na kwamba hakutamka mali zote alizokuwanazo.

Alidai kuwa mwaka 2014/015, Gugai alisajiri Kampuni mbili za familia zenye majina ya Guru medical investment ltd na Agobest (T) Ltd kampuni ambazo hazikuwahi kufanya kazi yoyote wala kupata leseni ya biashara tangu ziposajiliwa. Aliendelea kudai kuwa, January 2016 baada ya kuanzishwa kwa uchunguzi mshtakiwa Gugai alisajili kampuni ya biashara kwa jina la Cheers Wine and spirit ambayo hadi mwishoni mwa mwaka huo haikuwahi kuwaingizia kipato chochote.

Alisoma, 2015/2016 katika uchunguzi ilionyesha, Gugai alijipatia utajiri wa juu zaidi ya kipato chake halali wa Sh 3, 634,961,105.02 ambapo alimiliki nyumba 19 na viwanja 37 vilivyopimwa.Utajiri ambao alishindwa kuutolea maelezo ya jinsi alivyoupata ambapo ilisomwa kuwa, Juni 2016, Gugai alifanya juhudi za makusudi kuficha mali hizo kwa kushirikiana na washtakiwa hao wenzie kwa kutengeneza mikataba ya uongo wakionesha kuwa ameuza au kuhamisha umiliki wa mali hizo kabla ya 2016 wakati wakijua si kweli.

Wakili Mbangwa alidai, uchunguzi ulibaini siyo kweli kuwa mshtakiwa Gugai aliuza ama kuhamisha umiliki wa mali hizo bali alifanya mihamala ya uongo kwa lengo la kuficha umiliki halali wa mali hizo.Kesi hiyo itaanza kusikilizwa Juni 28, 2018

Katika kesi hiyo washtakiwa hao wanaokabiliwa na mashtaka 43 yakiwemo 20 ya utakatishaji fedha haramu, kumiliki mali zisizoendana na kipato na kughushi mikataba ya mauziano ya viwanja katika maeneo mbalimbali.

No comments: