Monday, April 9, 2018

TPA YAADHIMISHA MIAKA 13 TANGU KUAZISHWA KWAKE,WAELEZEA MAFANIO YAO



Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imeadhimisha miaka 13 tangu kuanzishwa huku ikijivunia mafanikio ya kuongezeka kwa biashara kuanzia mwaka 2011.

Pia mapato yamekuwa yakiendelea kupanda na kuanzia Julai mwaka 2017 hadi mwaka 2018 shehena iliyokuwa ikiingia ilianza kupanda na meli zinazoingia kufikia takriban 3000 kwa mwezi.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TPA wakati akielezea Wiki ya Mamlaka hiyo iliyoanza jana na kilele chake kufikiwa Jumapili.Ambapo watatumia maadhimiaho hayo kueleza walikotoka tangu April 2005, walipo na wanakotarajia kwenda kwa ajili ya kuboresha zaidi huduma kwa biashara. 

Amesema TPA imekuwa ikiendelea kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza masoko huku wakikusanya Sh.bilioni 420 kwa kipindi cha miezi sita iliyopita."Mamlaka hiyo, inalenga kuboresha zaidi huduma zake, kwa kuandaa mazingira ya serikali kupata mapato yake kwa kuwa kati ya asilimia 45 hadi kufikia 55 ya kodi inayokusanywa na Mamlaka ya Mapato, hupatikana TPA," amesema.

Kakoko amesema wanatarajia kutekeleza mradi ya ujenzi wa bandari kavu katika baadhi ya mikoa ikiwemo Kigoma, Arusha, Mbeya na hata Mwanza wanalenga kuwapa unafuu wateja wao kutoka nje ya nchi wanaokuwa wakifuatilia bidhaa katika Mamlaka hiyo.

Kuhusu maadhimisho hayo ya miaka 13,amesema watatoa elimu kwa wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara namna ya utendaji wa Mamlaka hiyo.Pia, kuchangia damu kwa wagonjwa, kutoa viti vya walemavu vya magurudumu mawili na vifaa vya kisasa vya kupima joto mwilini.

“Nia ya bandari ni kuongoza katika biashara kwa utoaji huduma ya uhakika katika mtandao wa uchukuzi katika Kanda zinazozunguka."Ikiwa pamoja na kuongeza mapato kwa kusimamia bandari katika kutoa huduma bora na nafuu kwa kutumia mbinu na teknolojia kisasa Ukanda wa Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika ,”amesema Kakoko

Ameongeza Mamlaka hiyo inatekeleza miradi katika kuboresha utoaji wa huduma na katika eneo la miundombinu, wana mpango wa kuchimba lango kuu ya kuingilia bandari katika eneo la Feri, jijini Dar es Salaam.Amesema jambo hilo litasaidia kuingia kwa wingi meli kubwa pamoja na makasha mengi zaidi.

Pia amesema Mamlaka inatekeleza miradi ya maendeleo mbalimbali katika bandari ya Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na katika bandari zilizopo maziwa makuu ya Viktoria, Tanganyika na Nyasa kwa kujenga magati na kuboresha yaliyopo.Ameongeza pia ununuzi wa vifaa mbalimbali ili kuweza kuwa na bandari za kisasa zitakazokuwa na uwezo wa kuhudumia shehena kubwa zaidi.

“Uboreshwaji wa miundombinu ya bandari si tu kwa Bandari ya Dar es Salaam lakini na Mtwara na Tanga na hata katika maziwa yote makuu,” amesema.Akizungumzia usalama Kakoko amesema wameendelea kuboreshwa ulinzi na wana mpango wa kuweka mashine za kukagulia mizigo (scanning machine) katika mipaka yote na ofisi zote

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya TPA, Profesa Ignatus Rubalatuka amesema ili Mamlaka iyafikie malengo yake inatekeleza vipaumbele vitano ambavyo ni maendeleo ya rasilimali watu, uboreshwaji wa miundombinu,matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kudumisha ulinzi na usalama pamoj ana kuongeza juhudi za kimasoko.

Amesema suala la ulinzi na usalama wa mali za wateja alisema ni jambo linalopewa kipaumbele kwa kuhakikisha ipo miundombinu ya vifaa vya ulinzi vya kisasa.
Mwenyekiti wa Bodi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Profesa Ignas Rubaratuka akizungumza kuhusiana na maadhimisho ya miaka 13 ya Mamlaka usimamizi wa bandari yaliyoanza leo , jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mhandisi Deosdidit Kakoko akizungumza na waandishi kuhusiana na mafanikio ya kuanzishwa kwa mamlaka ya usimamizi wa bandari, leo jijini Dar es Salaam.

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Fransisca Muindi akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na huduma watazozitoa katika maadhimisho ya miaka 13 ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, leo jijini Dar es Salaam.

No comments: