Monday, March 19, 2018

MWAKILISHI BENKI YA DUNIA AFANYA MAZUNGUMZO NA JAJI MKUU,ARIDHISHWA UTEKELEZAJI MRADI MABORESHO WA HUDUMA ZA KIMAHAKAMA

Na Mary Gwera, Mahakama

Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Miradi ya Utawala Bora kutoka Benki ya Dunia (WB), Bi. Nicola Smithers ameipongeza Mahakama kwa utekelezaji wake wa Mradi wa Maboresho wa huduma za Kimahakama.

Bi. Smithers aliyasema hayo mapema Machi 19, alipokutana na Mhe. Jaji Mkuu ofisini kwake Mahakama ya Rufani-Dar es Salaam ambapo alipata nafasi ya kuongea na Mhe. Jaji Mkuu na Viongozi wengine wa Mahakama akiwemo Mtendaji Mkuu na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.

“Nimefurahishwa na maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya huduma za Mahakama unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, hususani katika eneo la uondoshaji wa mlundikano wa mashauri,” alisema Bi. Smithers

Akimkaribisha ofisini kwake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahimu Juma alimueleza Bi. Smithers juu ya maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanyika ndani ya Mahakama ya Tanzania yote yakiwalenga wananchi ambao ndio wateja wa Mahakama.

“Miongoni mwa maeneo ambayo tunayoendelea kupambana nayo ili kurejesha imani ya wananchi kwa Mahakama ni pamoja na Rushwa, katika hili tmefanya jitihada kadhaa ikiwa ni pamoja na kusambaza mabango ‘posters’ yenye ujumbe wa kupinga rushwa na kuyasambaza katika ofisi za Mahakama kote nchini pamoja na kusambaza simu za kuwawezesha wananchi wenye malalamiko kutuma meseji ili malalamiko yao yaweze kufanyiwa kazi,” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.

Aidha, Mhe. Jaji Mkuu alizungumzia pia juu ya uamuzi wa utoaji wa nakala za hukumu bure kwa wananchi wenye kesi ili kuwarahisishia wananchi wenye kipato cha chini kupata haki zao pia.

Mhe. Jaji Mkuu aliongelea pia juu ya huduma ya Mahakama za Mwanzo, huku akisema kuwa wananchi wengi wanahitaji huduma za Mahakama za Mwanzo, hivyo kuna haja ya kusogeza huduma hii karibu zaidi na wananchi.

“Mfano hivi karibuni nilifanya ziara Mkoani Tabora, miongoni mwa maeneo ambayo yapo mbali kufikika kutokana na Jiografia yaki ni pamoja na Wilaya ya Uyui, hivyo basi maeneo kama haya yanatakiwa kuwa na huduma ya Mahakama inayotembea ‘Mobile Court’,” alisema Mhe. Jaji Mkuu huku akiongeza juu ya umuhimu wa Mahakama kushirikiana kwa karibu na Mabaraza ya Kata katika ufanyaji kazi wake.

Miongoni mwa maeneo ambayo Viongozi wa Mahakama i.e Mtendaji Mkuu na Msajili Mkuu wa Mahakama walizungumzia katika mazungumzo kati ya Meneja huyo kutoka Benki ya Dunia na Mhe. Jaji Mkuu, ni pamoja na ufanyaji kazi wa Mahakama wenye kuzingatia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (5), ushirikiano kati ya Wadau

Bi. Smithers ambaye amewasili nchini kutokea Washington D.C zilipo ofisi cha Benki ya Dunia amefanya ziara yake Mahakama kwa lengo la kuangalia maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama ambao unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Benki ya Dunia (WB).

Maeneo muhimu yanaotekelezwa na Mradi wa Benki ya Dunia (WB) ni pamoja na; Mapambano dhidi ya Rushwa; ni kwa jinsi gani Mahakama pamoja na wadau wengine wanaweza kushirikiana katika kupiga vita vitendo vya rushwa.Maeneo mengine ni ushirikishaji wa wadau katika masuala yote ya utoaji haki na kusogeza huduma ya utoaji haki karibu na wananchi.

Meneja huyo wa Miradi ya Utawala Bora kutoka Benki ya Dunia (WB), Bi. Smithers anatarajia pia kutembelea katika Ofisi za Maboresho ya Mahakama, Kituo cha Mafunzo-Kisutu pamoja na Mahakama ya Wilaya Kigamboni.
Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Miradi ya Utawala Bora kutoka Benki ya Dunia (WB), Bi. Nicola Smithers akisaini Kitabu cha Wageni pindi alipowasili ofisini kwa Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania, Mahakama ya Rufani-Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Juma akiongea jambo na Mgeni wake Bi. Nicola Smithers ambaye ni Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Miradi ya Utawala Bora kutoka Benki ya Dunia (WB).
Mtendaji Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hussein Kattanga (wa pili kushoto) akichangia jambo katika Mazungumzo hayo, wa kwanza kushoto ni Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revokati, wa pili kulia ni Meneja kutoka Benki ya Dunia-Tanzania, Bw. Dennis Biseko.
Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revokati (wa kwanza kushoto) akichangia jambo
Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Miradi ya Utawala Bora kutoka Benki ya Dunia (WB), Bi. Nicola Smithers akizungumza jambo.
Mkuu wa Kitengo cha Maboresho-Mahakama, Mhe. Zahra Maruma akiwa katika mazungumzo hayo.


Picha ya pamoja.

No comments: