Sunday, January 21, 2018

FIGISU FIGISU KAMA HIZI KWENYE SOKA LETU,MPAKA LINI.!?

 Na Hafidh Kido, Moshi.

KWA nafasi yangu ya msemaji wa timu ya Coastal Union 'Wagosi wa Kaya' ninatakiwa kusafiri na timu popote iendapo lakini kutokana na majukumu mengine nashindwa kutenda haya.

Lakini nilijiapiza mechi baina ya Wagosi na Polisi Tanzania iliyochezwa mjini Moshi katika uwanja wa Chuo cha Ushirika lazima niende. Kwa bahati ikatokea dharura ya kifamilia nikapata ruhusa kibaruani nami nikahudhuria.

Kwa wiki kadhaa sasa kumekuwepo na maneno kuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), anaikingia kifua Coastal Union kwa sababu ni mwenyeji wa Tanga lakini pia aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za kiuongozi kwenye klabu hiyo kongwe ya jijini Tanga iliyoanzishwa mwaka 1948.

Kama hiyo haitoshi ikaelezwa kuwa kikosi cha Coastal Union kinacheza soka kwa kubebwa waamuzi ambao wanapokea maagizo kutoka TFF.

Yamezungumzwa mengi, itoshe tu kusema baadhi ya klabu zinazoshiriki Ligi ya soka Daraja la kwanza wamekuwa na malalamiko ya mara kwa mara kudai Coastal Union inabebwa.

Nimeamua kuja kushuhudia 'kubebwa' kwa Coastal Union. Naomba nitangaze maslahi kabla sijaendelea na andiko hili nililoliandika saa nane usiku wa kuamkia Jumapili Januari 21, 2018 nikiwa chumba cha hoteli Mjini Moshi Mkoa wa Kilimanjaro.

Mimi ni shabiki wa Coastal Union lakini pia ni mwanahabari. Hivyo naandika kwa jicho la kihabari lakini naweza kuteleza nikaweka unazi katika andiko hili. Nipo tayari kukosolewa na hata kuzodolewa ikiwa nitaandika uongo au kuongeza chumvi.

Hadi naandika haya msimamo wa kundi B inayojumuisha timu nane yaani Coastal Union, Polisi Tanzania, JKT Mlale, Kinondoni Manicipal (KMC), Mbeya Kwanza, Mufindi United, Mawenzi Market na Polisi Dar es Salaam.

Coastal Union ilikuwa inaongoza kundi kwa jumla ya alama 22, ikifuatiwa na Polisi Tanzania (21), JKT Mlale (21), KMC (19), Mbeya Kwanza (16), Mufindi Utd (12), Mawenzi Market (7) na Polisi DSM (3).

Kwa namna yoyote ile Polisi Tanzania wameumizwa na suluhu tuliyowalazimisha katika uwanja wao. Hivyo walijiandaa kwa hali yoyote iwayo kuhakikisha tunawaachia alama tatu muhimu kwao ili kujihakikishia kupanda Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.

Hata hivyo, mbinu walizotumia nje ya uwanja hazikuwa sahihi. Nasema nje ya uwanja kwa sababu ndani ya uwanja soka lililochezwa ni la uhakika na wala mwamuzi hakuwa na upendeleo wa aina yoyote ile. Na wachezaji pia walicheza 'Fair Game' ya kuheshimiana.

Tatizo lilianza siku moja kabla ya mechi, yaani Ijumaa ya Januari 19, 2018. Baada ya Katibu wa Coastal Union Bwana Kibabedi kukamatwa na askari polisi kwa kosa ambalo hata hao waliomkamata hawakumudu kulieleza.

Nilipowasiliana na askari ninaowafahamu hapa Moshi kuwauliza sababu za kukamatwa kiongozi wangu hakuna hata mmoja aliyekuwa tayari kunipa ushirikiano.

Askari Polisi wanadai wamemkamata kwa kosa la kutishia kumuua mtu kwa kisu. Kwanza sidhani kama kosa hilo lipo bali ni kosa la kumdhuru au kumshambulia au kutishia mtu kwa silaha au kitu chenye ncha kali. Sheria hazitambui kisu. Wanasheria watanisaidia.

Mwenyewe Kibabedi anasemaje: "Wallah Wabillah hapa mfukoni hata wembe wa kukatia kucha sina halafu naambiwa nataka kumuua mtu kwa kisu? Maajabu haya.

"Ninachokumbuka nilikua nimekaa sehemu nazungumza na simu ghafla naona watu wanakuja wananikamata wananiambia twende kituoni umetishia kutaka kumuua mtu kwa kisu."

Kwa bahati hakulala ndani bali juhudi zilifanyika akatoka salama kwa dhamana. Lakini si dhamana bali alitoka moja kwa moja. Ajabu kidogo mtu aliyetishia kuua anatoka tu hivihivi.

Tuachane na hilo. Niliingia uwanjani na Bus la timu nikiwa na wachezaji. Uwanja ulikua mtupu tukajiandaa kwa mechi. Baada ya kusikiliza mawili matatu ya kocha Juma Mgunda nikaamua niungane na mashabiki wenzangu jukwaani.

Tukiwa tumestarehe tukasikia ving'ora vikali vikiingia uwanjani. Lilikua basi la Jeshi la Polisi, ndani kuna maofisa wa polisi likazunguka uwanja mara tatu na kutimua vumbi huku wanapiga kelele za shangwe. Kisha geti likafunguliwa wakatoka nje.

Hatujakaa sawa likaingia gari la wazi lenye askari takriban 40 wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) ambao kimsingi wapo chini ya Jeshi la Polisi, wamevalia kimapambano. Wapo waliobeba mitutu ya bunduki na wapo waliobeba zana za kufyatulia mabomu ya machozi.

Baadhi ya askari walikua wananin'ginia kwenye gari wengine wanachupa huku gari inaenda kasi na kupanda tena. Nayo ilizunguka uwanja mara tatu ikamkosakosa kumgonga Meneja wetu wa timu Bwana Hilal. Lakini hatukujali wala kutishika nayo ikatoka nje ya uwanja kwa shangwe.

Baada ya rabsha hizo kuisha neno la kwanza kusikia baada ya kukaa ni maofisa wa polisi waliovalia fulana za timu ya Polisi Tanzania kutoa agizo kwa mlinzi wa mlangoni kuwa asiruhusu mtu yeyote kuingia na ngoma uwanjani.

Alisema ngoma ni silaha hatari sana, hivyo zisiingie ndani kwa kulinda usalama wa raia na mali zao. 

Niliona ajabu sana kwa sababu ikiwa Old Trafford ya Uingereza ngoma zinaruhusiwa kuingia pamoja Uwanja wa Taifa Dar es Salaam zinaruhusiwa vilevile; itakua uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi?

Zogo la mashabiki wa Coastal Union kupinga hili lilikua kubwa. Amani ikaanza kupotea na dalili za vurugu zikanukia. Nikaona askari waliovalia kijeshi tayari kwa lolote wakianza kusogea karibu tayari kwa mapambano au kudhibiti 'vurugu'.

Nilipoona hivyo nikawaza akilini kuwa hawa wanatumia mbinu za kijeshi kutuchokoza ili tuonekane wakorofi. Ghafla tukakubaliana tuachane na hilo suala tusubiri hatma ya Mungu.

Mungu yupo na yu hai daima. Kabla vurugu hazijaisha wakaingia mashabiki wa Polisi Tanzania huku wamebeba ngoma wanapiga kwa kelele. Yule afisa aliyetuzuia ngoma alikua amesimama palepale mlangoni anawatazama huku akitabasamu.

Tukamuuliza je ile si silaha inaingia uwanjani? Hakujibu kitu. Akaondoka na kupotea machoni mwetu. Watu wa Tanga tunasema alitahayari.

Ngoma zetu zikaingizwa na kuanza kupigwa kwa madaha. Uwanja mzima ulilipuka kwa shangwe, ngoma haina uadui. Moyo ndio unaopenda. Hata baadhi ya askari nikawaona wanafuatisha midundo huku wakicheka kwa pumbao.

Timu zikaingia uwanjani na mechi ikaanza. Hafla nyuma ya mgongo wangu nikasikia vurugu. Kutazama nyuma ni kijana wa makamo ameshikilia sumu ya kuua mbu. Ni ya kupulizia.

Lengo lake alitaka kumdhuru shabiki wa Coastal Union katika jukwaa letu. Ameshika chupa ya sumu hiyo huku ameshika kibiriti. Kimsingi hilo ni bomu. Lakini askari wakawa wanamwangalia na kusema mwacheni huyo ni mwendawazimu.

Tukamuuliza mwendawazimu ambaye ni shabiki wa timu pinzani anafanya nini jukwaa letu, kama hiyo haitoshi ameshika silaha mkononi ambayo muda wowote atamdhuru mtu. Katika hali ya kawaida naye atashambuliwa na pengine apoteze maisha. Kwanini wasimuondoe?

Utaona kama nasema uongo. Suala la kumuondoa pia ulikua ubishani baina ya polisi na mashabiki. Polisi wanasema mwacheni huyu kijana hana neno huku mashabiki wakisema muondoeni. Zaidi ya nusu saa tunalumbana hatimaye akaondolewa. Ajabu sana hii.

Tukiwa bado kwenye taharuki hiyo nikasikia mpira ni mapumziko. Hata sikuufaidi lakini waliofuatilia wanasema mechi ilikua ngumu ya piga nikupige.

Ikiwa imebaki dakika mbili kipindi cha pili kianze nikasikia mchezaji wetu Abubakar Kinanda, beki wa kulia ameshambuliwa na shabiki wa Polisi Tanzania tena mbele ya askari waliovalia kimapambano, kuzuia ghasia.

Kwa macho yangu nimemshuhudia Abuu akilalamika huku amefunika uso wako wakati askari wanamwangalia miguu 10 kutoka alipo. Halafu huyo aliyemshambulia kwa sumu ya mbu anaondoka taratibu bila kukimbia akizunguka uwanja watu wanamnyooshea kidole. Yuko peke yake.

Askari wamejaa uwanja mzima wanashindwa kulinda wachezaji 22 uwanjani. Je wangeweza kutulinda mashabiki 3000 tuliohudhuria?

Kama hiyo haitoshi tukiwa jukwaani ambapo pia ilikua ajabu mashabuki wa Polisi Tanzania walikuja jukwaani kwetu kukaa na sisi wanashangilia kwenye migongo yetu. Mmoja wa mashabiki hao akachana fedha halali ya Tanzania. Noti ya Sh 1000/- ya Benki Kuu.

Zikaanza kupigwa kelele. Kwa macho yangu nilimuona askari kanzu akienda kumkamata. Lakini wakatokea watu wakamwambia muache. Akamuacha.

Askari waliovalia sare walikuja kuangalia kelele hizi ni za nini? Shabiki mmoja wa Coastal Union akamweleza kuna mtu amechana pesa. Akamuuliza anatoka wapi akamjibu ni shabiki wa Polisi Tanzania. Askari yule akatabasamu na kuondoka huku anawaelezea wenzie ambao nao walikuja kusikiliza huo 'umbea'.

Hadi mpira unaisha dakika 90 mabao hayakupatikana ilikua Polisi Tanzania 0-0 Coastal Union.

Haya ndiyo waliyofanyiwa Coastal Union timu iliyobatizwa kumilikiwa na Rais wa TFF, Wallace Karia. Je hizo zisizojulikana zinafanyiwa vipi.

HAFIDH 
Moshi, Kilimanjaro Tanzania

No comments: