Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Anastazia Wambura akikabidhi bendera kwa nahodha wa timu ya Taifa ya Kuogelea, Hilal Hemed Hilal
Timu ya Taifa ya mchezo wa kuogelea, imetamba kufanya vyema katika mashindano ya Dunia yaliyopangwa kuanza Desemba 6 mjini Windsor, Canada.
Tanzania itawakilishwa na jumla ya wogeleaji sita ambao wamepatikana kutokana na michujo mbalimbali ikiwa pamoja na mashindano ya Taifa yaliyofanyika mwezi Machi mwaka huu kwenye bwawa la kuogelea la Hopac.
Waogeleaji hao ni Hilal Hilal ambaye ni nahodha, Adil Bharma, Denis Mhini na Joseph Sumari ambao ni wanaume ambapo kwa wanawake ni pamoja na muogeleaji namba moja nchini, Sonia Tumiotto na Catherine Mason.
Akizungumza leo, Hilal alisema kuwa wamejiandaa vizuri chini ya kocha wao, John Belela na morali ipo juu kutokana na mafanikio waliyopata hivi karibuni katika mashindano ya kanda ya tatu yaliyofanyika Kigali, Rwanda na Tanzania kushika nafasi ya kwanza.
Hilal alisema kuwa lengo lao ni kupigia taifa lao na wanaamini watafanya vyema na hasa baada ya kuwaongeza wigo wa waogeleaji.
"Tumejiandaa kufanya vizuri, kama mjuavyo kwenye mashindano ya Afrika ya kanda ya tatu Tanzania ndiyo ilikuwa bingwa, tulipata medali 99, ushindani huu tutakwenda kuuendeleza Canada," alisema Hilal.
Waogeleaji hao leo walikabidhiwa Bendera ya Taifa na Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Anastazia Wambura katika hafla fupi iliyofanyika Wizarani na kuhudhuliwa na Balozi wa Italia hapa nchini, Roberto Mengoni sambamba na mwakilishi wa kampuni ya kutengeneza vifaa vya Michezo ya Errea yenye makao makuu nchini Italia.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri Wambura aliwataka waogeleaji hao kupambana huku akimuomba Balozi Roberto na kampuni ya Errea kuendelea kuisapoti Tanzania.
"Ushirikiano wenu isiishie kwa timu yetu teule ya kuogelea, tunaomba muendelee kutusapoti hata kwenye miundo mbinu kwa kujenga mabwawa ya kuogelea hapa nchini na ikiwezekana hata kufungua viwanda vya vifaa vya Michezo," alisema Naibu Waziri huku Balozi Roberto akiahidi kushirikiana nao.
No comments:
Post a Comment