Saturday, September 17, 2016

Kujitoa katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ni sawa na Mkulima kula Mbegu :Mambo 10 muhimu ya kuyaelewa kuhusu Hifadhi ya Jamii

Na Kibaja Kariongo

Upo mjadala unaoendelea na kufukuta kuhusu uamuzi wa Serikali kupeleka Muswada wa Sheria Bungeni kufanya marekebisho katika Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Muswada huo sijauona na haujawekwa hadharani. Hata hivyo, lililopenyezeka katika vyombo vya habari ni taarifa ya azma hiyo ya Serikali iliyotamkwa katika kikao cha Serikali na wadau kuwa Muswada huo utafuta FAO LA KUJITOA.
Nimefuatilia mjadala huo na kuisoma barua ya wazi ya vyama vya wafanyakazi kwa umma ikilaani vikali nia hiyo ya Serikali na muswada. Nikasikia na kusoma tena kauli mbalimbali za Serikali na Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kuhusu azma hiyo na mambo mengine mengi yanayoambatana na muswada unaondaliwa. Kwa maelezo hayo, muswada huo una mambo mengi zaidi ya kinachoitwa fao la kujitoa. Aidha, maelezo yao ni kuwa muswada wenyewe haujakamilika isipokuwa ni hatua ya maoni tu.
 Ninachokiona kwa haraka haraka ni kuwepo kwa ombwe la taarifa katika suala hili jambo linalofanya mjadala wenyewe kwenda harijojo. Ombwe hili litafanya hata muswada wenyewe ukitolewa tushindwe kuujadili vizuri  na kwa nafasi. Kwa sababu hiyo, nimejitolea kuchokoza mjadala kwa kuyaweka bayana mambo 10 ya msingi ya kuyaelewa kuhusu hifadhi ya jamii kama ninavyoyainisha hapa chini.
1. Ipo tofauti kati ya dhana mbili  'AKIBA YA WAFANYAKAZI' na 'HIFADHI YA JAMII'  yaani Provident Scheme na Social Security. Provident Scheme inakupa tu jumla ya fedha wewe na mwajiri mliyochangia siku ya kustaafu na mnaachana kimoja. Social Security inahusisha mnyumbuliko wa mafao ikiwemo malipo ya kila mwezi baada ya kustaafu, matibabu kwa mtu na mwenza, gharama za maziko na malipo kwa mjane na kusomeshewa watoto. Kutokana na uchanga wa mifuko hii, mafao bado yanatofautiana kati ya mfuko na mfuko hatimaye mbeleni mafao yanapaswa kufanana katika mifuko yote.
2. Hifadhi ya Jamii ni Haki ya Kikatiba na si suala la hiyari. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kuwa kila mtu anahaki ya kupata hifadhi. Aidha Hifadhi ni Haki ya Binadamu katika Tamko la Haki za Binadamu na Mikataba ya Shirika la Kazi Duniani. Haki hiyo inaambatana na wajibu kwa Serikali, Mwajiri na Mfanyakazi. Serikali kusimamia na kuhakikisha Haki hiyo inatolewa na kupatikana, Mwajiri kumchangia Mfanyakazi na Mfanyakazi kuchangia kwa mujibu wa Sheria.

3. Hakuna kitu kinachoitwa FAO LA KUJITOA kulikuwepo na KUJITOA KWENYE MAFAO. Kwa kuwa mifuko iliyopo iliundwa kwa sheria tofauti kwa nyakati tofauti, baadhi ya mifuko ilikuwa bubu kuhusu kipengele cha kukataza kujitoa hali iliyofanya watu kujitoa bila kukataliwa. Hivyo hakuna FAO LA KUJITOA lililofutwa na hakuna Mfuko wowote wenye fao hilo. Kilichofanyika ni kuoanisha Sheria mbali mbali za Mfuko na kuwa na Sheria moja kurahisisha udhibiti na usimamizi ambapo katika Sheria hiyo ya 2012 imetamka bayana kutokuwepo na kujitoa kuziba ombwe lililoachwa na sheria mbalimbali.
4.. Hifadhi ya Jamii ni KINGA si AKIBA. Hifadhi ya Jamii ni sawa na bima ya kumkinga mfanyakazi na mwanachama dhidi ya majanga yanayoweza kumpata na kumpotezea uwezo wake wa kuzalisha na kujikimu. Majanga hayo ni kama kustaafu,kupata vilema na kamwe si mfuko wa akiba na mikopo, chama cha kuweka na kukopa au upatu. Hivyo michango yako katika hifadhi ya jamii haiwezi kuwa mbadala wa wewe kujiwekea akiba na kuwekeza sehemu ya kipato chako inayobaki kwako baada ya kukatwa  mchango wako usiovuka asilimia 10 ya mshahara wako(kwa wale wafanyakazi). Kushindwa kwako kuweka akiba hakuhalalishi kugeuza Mfuko wako wa Hifadhi ya Jamii kuwa ni Benki. Hoja ni kuongeza tija na hatimaye mishahara/kipato na kujenga utamaduni wa kuweka akiba (culture of saving).
5. Michango yetu kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ni MBEGU ambayo mavuno yake yanatokana namna tunavyoendelea kuyapalilia na kunyunyuzia dawa kwa kuendelea kuchangia. Huwezi kupanda leo na kuvuna kabla ya mazao kukomaa au msimu wa mavuno kufika. KUJITOA KWENYE MAFAO NI SAWA NA MKULIMA KULA MBEGU.

6. Unapostaafu au kwa sababu yoyote unapolazimika kuhifadhiwa na jamii kwa kupewa kinga una uwezo wa kutumia zaidi ya ulichochangia. Hifadhi ya jamii hutoa kinga kwa kadiri ya uhitaji na si kwa kadiri ya mchango pekee. Hii inatokana na uwekezaji unaofanywa na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa upande mmoja na muendelezo wa mitiririko ya michango kwa wale ambao bado wako katika umri wa kuchangia. Mafao yako wewe baada ya kuchukua kiinua mgongo yataendelea kulipwa na wale ambao bado wanachangia. Hivyo, kuruhusu watu kujitoa ni kumomonyoa nguzo ya Hifadhi ya Jamii ya vijana na wanaojiweza kuwafaa wazee na wasiojiweza. Ndivyo ilivyo duniani kote.
7.Skimu za Hifadhi ya Jamii tofauti na iliyokuwa skimu ya mifuko ya Akiba ya Wafanyakazi inapaswa kugusa wananchi wote kwa kuwa ni haki ya kikatiba na si wafanyakazi pekee. Inapaswa kugusa wasiojiweza,wasio na ajira, waliojiajiri,wakulima, wanamichezo na wengine walioko kwenye sekta isiyo rasmi. Tuendako kila mtanzania anapaswa kuwa mwanachama wa hifadhi ya jamii kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea ambako namba yako ya uanachama wa hifadhi ya jamii ndio kitambulisho chako kikuu. Hivyo hoja ya kujitoa katika mfuko ulipwe ukajiajiri haijitoshelezi. Huko tuendako hata ukijiajiri hatimaye itakuwa ni lazima uchangie hifadhi ya jamii kama ilivyo lazima sasa kulipa kodi alimradi una kipato kiwe cha kuajiriwa au kujiajiri. Kujiunga katika hifadhi ya jamii kwa wasio waajiriwa katika sekta rasmi ni hiyari tu kwa sasa katika kipindi cha mpito.
8. Tanzania imeingia katika skimu hii mwanzoni mwa miaka ya 2000 tulipobadilisha mifuko iliyokuwapo. Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi (NPF) ukawa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na uliokuwa Mfuko wa Pensheni kwa Mashirika ya Umma  (PPF) ukabadilika kutoka kuwa mfuko wa Mashirika ya Umma tu na kuwa mfuko wa kila mtu, na Serikali kuunda PSPF, LAPF nk. Sisi Tanzania ndio tumeianza safari ya kuelekea kwenye hifadhi ya jamii na bado hatujafikia huko.  Katika muda mfupi manufaa yameanza kuonekana kadri uwezo wa mifuko unavyoongezeka na kupata faida. Leo tuna bima ya afya, fao la ulemavu kazini, fao la kujifungua, fao la elimu, fao la afya vijijini nk.  Huko tuendako, mafao haya yatafanana katika mifuko yote  na upo uwezekano wa mifuko yote ya sasa kuunganishwa na kuwa mmoja. Hatuwezi kufika huko ikiwa wanachama wataruhusiwa kujitoa kila wanapojisikia kufanya hivyo maana itaathiri uimara wa mifuko.

9. Kama ilivyo kanuni ya msingi kwa sheria yoyote, katika kila sheria lazima kuwepo na mazingatio (exceptions). Zipo aina ya sekta au kazi ambazo kwa mazingira yake ya asili ya shuruba zake hakuna mfanyakazi anayeweza kuhimili kuwa na uwezo wa kufanya kazi hizo hadi miaka 55. Aina hizi za kazi humfanya mfanyakazi apoteze uwezo wake wa kufanya kazi na kuchangia kutokana na sababu za kiafya (na)au ulemavu. Lazima sheria itambue watu wa aina hii na kazi za aina hii ili kuwawezesha hawa kuanza kunufaika na hifadhi ya jamii kabla ya umri wa kisheria uliowekwa wa kuchangia kwa miaka 15 au kupata mafao ya kiinua mgongo kabla ya miaka 55 kwa hiyari na 60 kwa lazima. Hawa  wanahitajika kuwekewa FAO lao (si kujitoa) mahsusi la kuwahifadhi, kuwasitiri na kuwakinga dhidi ya kudhalilika na kufadhaika katika jamii. Hawa wanahitaji hifadhi. Mjadala wetu wafaa kuelekezwa hapo tunapojadili kuhusu marekebisho ya Sheria. Pia tujadili pendekezo la fao la kukosa ajira na ikiwezekana kama tunaweza kutumia michango yetu kama dhamana kukopea nyumba, kujisomesha nk na si kujitoa. Tusipoteze lengo kwa kile alichokisema Mwl. Nyerere, 'Tukipoteza muda mwingi kugawana KIBABA tutapoteza wasaa wa kugawana PISHI'.
10. Mimi na wewe hatuiujui kesho yetu wala hatuna uhakika wa msaada wa ndugu zetu na rafiki zetu pale  tutakapofikwa na uzee au janga. Hifadhi ya Jamii ndio mbeleko yetu ya kujishikizia. Mimi na wewe na wengi wetu ambao ndio wafanyakazi wengi wa Tanzania ambao hatujachangia mifuko kwa zaidi ya miaka 15 kuweza kustahili mafao ya pensheni tuna maslahi gani na kujitoa kwenye mafao? Hao viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wanaotutia hamasa mbona wote umri wao umeshakwenda na wamekaa mkao wa kufaidika na pensheni? Tukumbuke Ujana Ukuta na Fainali Uzeeni.


Inawezekana kabisa sijatoa majawabu na ieleweke haikuwa lengo langu. Lengo langu ni kuchokoza tu mjadala. Tujadili.

*Ndugu Kibaja Kariongo ni 
mdau wa harakati za wafanyakazi











No comments: