Sunday, August 7, 2016

ZANZIBAR YAADHIMISHA WIKI YA UNYONYESHAJI DUNIANI

Naibu Waziri wa Afya Arusi Said Suleiman wa kwanza (kulia) akizungumza na akinamama waliohudhuria maadhimisho ya kilele cha wiki ya unyonyeshaji duniani katika kijiji cha Mwera Wilaya ya Kati Unguja.

Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar  

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) limesisitiza umuhimu kwa Tanzania kuongeza juhudi katika kuweka mikakati ya kuboresha unyonyeshaji wa watoto mara tu baada ya kuzaliwa hadi kufikia miaka miwili.

Akitoa salamau za kilele cha wiki ya unyonyeshaji duniani iliyoadhimishwa katika kijiji cha Mwera Wilaya ya kati Unguja,  Afisa Lishe kutoka  UNICEF  Dar es Salam, Elizabeth Macha  alisema utafiti wa 2014 unaonyesha  ni mtoto mmoja kati ya wawili wenye umri hadi kufiki miezi 23 wanaonyonyeshwa mara baada ya kuzaliwa kwa Tanzania.  
       
Alisema kwa Zanzibar ni asilimia 61 tu ya watoto wenye umri kati ya miaka 0-23 wanaonyonyeshwa katika muda wa nusu saa baada ya kuzaliwa na Mkoa wa Kusini Pemba upo nyuma  zaidi ukiwa na asilimia 52.

Aliongeza kusema kuwa watoto wakicheleweshwa kunyonyeshwa kwa masaa 2 hadi 23 baada ya kuzaliwa inaongeza hatari ya kufa katika siku 28 za kwanza za maisha ya mtoto kwa asilimia 40.

Alisisitiza watoto kunyonyeshwa maziwa ya mama kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo bila kupewa chakula chengine kwa vile yanamsaidia kukua vizuri kiakili na kimwili.

Alisema watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa Zanzibar ni asilimia 20 wakati Pemba ina asilimia 10.

Afisa Lishe wa UNICEF alisema kunyonyesha ni moja ya uwekezaji muhimu ambayo nchi inaweza kufanya kwa ajili ya ustawi wa wananchi wake.

"Tunaweza kupata maendeleo ya haraka katika maendeleo yetu endelevu kwa kukuza, kulinda na kusaidia unyonyeshaji," alikumbusha afisa Lishe wa UNICEF.

Alisema iwapo mipango mizuri ya kuboresha unyonyeshaji na kutekeleza kwa vitendo Tanzania inaweza kufanya unyonyeshaji kuwa sehemu ya mwanzo katika kuimarisha afya kwa kila mtoto na jamii kwa jumla.

Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt. Fadhil Mohd Abdalla akimkaribisha mgeni rasmi katika sherehe hizo alisema asilimia kubwa ya wanawake wananyonyesha watoto lakini kasoro iliyopo ni kuwachelewa kuwanyonyesha, kuwalisha vyakula vyengine wakiwa chini ya miezi sita na kuwaachisha maziwa kabla ya miaka miwili.

Naibu Waziri wa Afya ambae alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji duniani Arusi Said Suleiman aliwahimiza akinamama kuwanyonyesha watoto wao maziwa pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo kwani ni kinga bora kwa afya zao.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo "Unyonyeshaji ni kichocheo cha Maendeleo endelevu. Dumisha unyonyeshaji kwa maslahi ya wote".
Mkuu wa Kitengo cha Lishe Wizara ya Afya Zanzibar, Asha Hassan akizungumzia umuhimu wa kunyonyesha maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo kama Lishe bora zaidi katika makuzi ya mtoto wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji yaliyofanyika Mwera Wilaya ya Kati Unguja.
Mmoja wa akinamama anaenyonyesha watoto wake maziwa pekee miezi sita ya mwanzo Raya Khamis akitoa ushuhuda na mafanikio anayopata kwenye kilele cha maadhimisho hayo.
Afisa Lishe, UNICEF Dar es salaam Elizabeth Macha akitoa salamu za Shirika hilo katika maadhimisho ya kilele cha wiki ya unyonyeshaji duniani yaliyofanyika kitaifa Mwera Wilaya ya Kati Mkoa Kusini Unguja.
Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt. Fadhil Mohd Abdalla akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Mwera Wilaya ya Kati Unguja.

No comments: