Sunday, July 10, 2016

CCM ZANZIBAR YATAKA MIKATABA YA MALI ZAKE KUSIMAMIWA NA WANASHERIA

Na Is-haka Omar, Zanzibar.

CHAMA cha Mapinduzi  (CCM)  Zanzibar kimewataka viongozi na watendaji wa chama hicho kuhakikisha mikataba ya kibiashara wanayofunga inapitiwa na kuwashirikisha wanasheria ili kuepuka vitendo vya utapeli.

Kimesema kuwashirikisha wanasheria wakati wa kufunga mikataba ya aina mbali mbali ya kukodisha Mali za Chama hicho kutasaidia kumaliza kero na migogoro ya matumizi mabaya ya Rasilimali za CCM.

Hayo aliyasema  Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai katika mwendelezo wa ziara ya  kukagua na kuhakiki mali za Chama hicho huko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema matatizo ya matumizi mabaya ya Mali za chama hicho yanayojitokeza katika maeneo nchini ni kutokana  na baadhi ya viongozi na watendaji kufunga mikataba ama makubaliano na wafanyabiashara bila ya kuwashirikisha wanasheria ama kupata ushauri kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu  hali inayopelekea baadhi ya watu kutumia nafasi hiyo kujinufaisha wenyewe badala ya kuangalia maslahi ya CCM.

Vuai alieleza kwamba njia pekee ya kuziweka salama mali mbali mbali za chama hicho ni uwepo wa maridhiano na makubaliano yanayojali na kuzingatia matakwa ya kisheria.

“ Naendelea kusisitiza kwamba mali za CCM hazipo kwa ajili ya kuwanufaisha watu wachache, bali zipo kwa ajili ya kukinufaisha chama ambacho ni taasisi halali ya watu wengi na jambo lolote la umiliki wa Rasilimali zake lazima liendeshwe kwa misingi ya uwazi na usawa kupitia utaratibu halali wa kisheria.

Pia Mali zote kwa sasa ni lazima zitumike ipasavyo kwa mujibu wa matakwa ya sera ya CCM ya siasa kwenda sambamba na ukuaji wa uchumi ndani ya chama chetu.”, alisisitiza Vuai na kuongeza kuwa CCM kwa sasa inaendelea na mipango ya kuhakikisha Rasilimali zake zinatumika vizuri kuimarisha uchumi wa Chama hicho badala ya watu wachache wanaojimilikisha mali hizo kinyume na taratibu.

Alisema lengo la ziara hiyo ni kuhakiki mali za Chama hicho pamoja na kuwakumbusha  Viongozi na Watendaji wa Chama na Jumuiya kwamba chombo pekee kinachomiliki mali zote ni Baraza la Wadhamini la Chama hicho hivyo hakuna chombo kingine  tofauti na baraza hilo kinachoweza kutoa maamuzi ya kuuza mali za Chama.

Aliwaagiza Viongozi wa Mkoa huo kupitia upya mikataba yote waliyofunga na wafanyabiashara katika eneo linalomilikiwa na CCM ili kuhakikisha maslahi yanayopatikana yanaendana na mahitaji ya wakati uliopo sasa kibiashara.

Aliwasihi Wana CCM kuendelea na utamaduni wa kuwashirikisha viongozi wa ngazi mbali mbali za chama hicho pindi panapotokea kasoro za kiutendaji ili ziweze kutatuliwa kwa kufuata utaratibu wa kinanuni na kimaadili kwa lengo la kuepuka kauli na malalamiko yasiyofaa ndani ya Chama hicho.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kazi iliyopo sasa mbele ya CCM ni kuendelea kujiimarisha kisiasa huku ikitekeleza ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015/2020 kwa kasi na kwa ufanisi zaidi ili wananchi waendelee kuiunga mkono na hatimaye Chama hicho kiweze kuandika historia mpya ya ushindi wa mwaka 2020.

Alisema maeneo ya CCM yaliyopo Nungwi ni Rasilimali kubwa kwani yapo katika ukanda wa Utalii hivyo yanatakiwa kulindwa na kuangaliwa vizuri na wahusika yasije yakaangukiwa mikononi kwa watu ambalo ni matapeli na wapinga maendeleo na  wakatumia fursa hiyo kupandikiza migogoro na mipasuko isiyokuwa ya lazima ndani ya Chama.

Pamoja na hayo alisema endapo uongozi wa Mkoa huo utahitaji msaada wa kisheria Afisi kuu ipo tayari kuwaunga mkono kwa kuwapa mwanasheria wake ili aweze kuwashauri na kuwaelekeza njia bora ya kufunga mikataba rasmi inayotambulikana kisheria. 

Nao Viongozi wa Mkoa huo wameahidi kuzifanyia kazi kwa haraka changamoto zilizojitokeza katika maeneo yanayomilikiwa na chama hicho ili kwenda sambamba na matakwa ya sera ya ukuaji wa uchumi ya CCM.

Walisema licha ya CCM ndani ya mkoa huo kuendelea na harakati za kuimarisha shughuli za kisiasa, bado wana fursa ya kuhakikisha rasilimali za chama hicho hasa zilizopo katika maeneo ya uwekezaji katika sekta ya utalii zinakinufaisha chama badala ya watu wachache wanaojali maslahi binafsi.

No comments: