Tuesday, June 21, 2016

SERIKALI YAAGIZA WAKIMBIZI WANAJESHI, WENYE SILAHA WAJISALIMISHE

Serikali ya Tanzania imewataka wakimbizi wote ambao walikuwa wanajeshi kutoka nchi walizokuwepo, kuripoti kwenye mamlaka husika ili waweze kupewa uangalizi maalum (special protection) kama wanajeshi.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali (Mstaafu) Emmanuel Maganga, wakati wa maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani yaliyofanyika kambi ya wakimbizi Nyarugusu, wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.

Alisisitiza kuwa wakimbizi ambao wako nchini wakijua ni wanajeshi ni lazima wasajiliwe na mamlaka husika.

Aidha Maganga aliwataka vile vile wakimbizi wote ambao wanamiliki silaha wazisalimishe kwa hiari yao wenyewe.

Alisema kumekuwa na matukio mengi ya ujambazi wa kutumia silaha na hivyo kuhatarisha amani na kuwaamuru wenye silaha kuzisalimisha mara moja ili waende sawa na sheria za nchi walikopata hifadhi.
Maandamano ya wakimbizi yakiingia uwanjani katika sherehe za maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani yaliyofanyika katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu, wilayani Kasulu, mkoani Kigoma. 

Mkuu huyo wa mkoa pia alitoa wito kwa mashirika ya misaada duniani kutoa misaada inayoowana na misaada inayotolewa kwa nchi zilizoendelea na kuongeza kuwa mahitaji ya binadamu ya msingi hayatofautiani iwe nchi zilizoendelea au zinazoendelea.

Alisema kuwa wakimbizi waliopo kwenye nchi zilizoendelea hupewa makazi ya kudumu na vyakula tofauti tofauti wakati waliopo kwenye nchi zinazoendelea hupewa mahema na chakula aina moja ambayo ni mahindi.

“Mwaka jana tulishindwa kuadhimisha siku ya wakimbizi duniani kwa kuwa tulikuwa tunawapokea wakimbizi kutoka Burundi,” alisema.

Alisema wakimbizi wameongezeka sana nchini na sasa hivi kuna makambi matatu yanayowahifadhi wakimbizi nchini.
Wakati huo huo Tanzania imepongezwa kwa ukarimu wake kwa kuwahifadhi wakimbizi kwa zaidi ya miongo minne sio tu kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na hata duniani.

Mwakilishi mkazi wa shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR , Chansa Kapaya alisema hayo katika sherehe za kuadhimisha siku ya wakimbizi duniani yenye kauli mbiu kuwa “Tupo Pamoja na Wakimbizi, Tafadhali ungana nasi”.

“Tanzania ni mfano wa kuigwa kwa mfano mzuri wa kuwahifadhi wakimbizi wengi duniani na pia kuwatafutia suluhu,” alisema.

Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga akizungumza na hadhira iliyokusanyika katika sherehe za maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani yaliyofanyika katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu, wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.

Alisema mwaka 2014 Tanzania iliwapa uraia wakimbizi zaidia ya 162,000 baada ya kuishi nchini kwa zaidi ya miaka 40.

Aliongeza kuwa, wakimbizi wanapaswa kuthaminiwa kama binadamu wengine kwa kuwa hakuna mtu anayechagua kuwa mkimbizi.

Kapaya alisema kuwa kwa sasa kambi ya Nyarugusu ina wakimbizi zaidi ya 131,733 ambao ni wengi zaidi na kusababisha msongamano unaohatarisha maisha yao.

Mwakilishi wa Shirika linalohudumia wakimbizi nchini (UNHCR), Chansa Kapaya akisoma risala wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani yaliyofanyika katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu, wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.
Pichani juu na chini ni baadhi ya wageni waalikwa, wafanyakazi wa Shirika la UNHCR na wadau wa maendeleo waliohudhuria sherehe hizo wakifuatilia hotuba mbalimbali.
Mwakilishi wa Shirika linalohudumia wakimbizi nchini (UNHCR), Chansa Kapaya akipitia ratiba ya maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani ambapo kitaifa yamefanyika mkoani Kigoma katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu. Kulia kwake ni mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga akifuatiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Gerald Guninita.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga (kulia) akifurahi jambo na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Gerald Guninita wakati burudani mbalimbali zikiendelea kwenye maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani ambapo kitaifa yamefanyika katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu, wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.
Mwakilishi wa Shirika linalohudumia wakimbizi nchini (UNHCR), Chansa Kapaya akiteta jambo na Ofisa wa UNHCR Tanzania anayeshughulika na mambo ya usalama kambini, David Mulbah (kulia) wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani yaliyobeba kauli mbiu "Tupo Pamoja na wakimbizi. Tafadhali ungana nasi." ambapo kitaifa yamefanyika katika kambi ya Nyarugusu, wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.
Bendi ya muziki wa Live ya vijana wakimbizi inayojulikana kama Nyota ya Asubuhi ya kambi ya Nyarugusu ikitoa burudani ya aina yake wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani.
Wanamuziki wa bendi ya Nyota ya Asubuhi wakisakata sebene kwenye maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani.
Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga na Mwakilishi wa Shirika linalohudumia wakimbizi nchini (UNHCR), Chansa Kapaya kwa pamoja wakikabidhi jezi na zawadi kwa timu wakimbizi ya vijana ya wanawake ya mpira wa miguu katika maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani ambapo kitaifa yamefanyika mkoani Kigoma katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu.
Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga na Mwakilishi wa Shirika linalohudumia wakimbizi nchini (UNHCR), Chansa Kapaya kwa pamoja wakikabidhi zawadi kwa baadhi ya watoto wakimbizi waliofanya vizuri kwenye masomo yao.

Mkuu wa ofisi ya Shirika la Umoja wa Mtaifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Kasulu, Kigoma, Amah Assiama-Hillgartner akitoa neno la kufunga sherehe za maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga akiongozwa na Mkuu wa Kambi ya Wakimbizi Nyarugusu, Sospeter Boyo (kulia) kutembelea mabanda yenye bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa kwa mikono na vikundi mbalimbali vya wakimbizi wanaoishi kwenye kambi hiyo wakati wa sherehe za maadhimisho hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga akiwa kwenye banda la kinamama wajasiriamali wa mikate.
Mabanda yenye bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa kwa mikono na vikundi mbalimbali vya wakimbizi wa Congo na Burundi walipata fursa ya kuonyesha kazi zao kwa mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Mwakilishi wa Shirika linalohudumia wakimbizi nchini (UNHCR), Chansa Kapaya (tisheti nyeusi) akipata maelezo kutoka kwa moja ya kikundi kinachojishughulisha na ufugaji wa Kuku na Kware alipowasili kwenye viwanja vya kambi ya Nyarugusu na kutembelea mabanda mbalimbali katika sherehe za maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani ambapo kitaifa yamefanyika Kigoma, kambi ya Nyarugusu.
Mkuu wa ofisi ya Shirika la Umoja wa Mtaifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Kasulu, Kigoma, Amah Assiama-Hillgartner (kushoto) akitoa maelezo ya kifaa maalum cha kutotolea vifaranga kilichotengenezwa kienyeji (incubator) na wakimbizi wa Nyarugusu kwa Mwakilishi wa Shirika linalohudumia wakimbizi nchini (UNHCR), Chansa Kapaya (kulia) wakati wa maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani.
Mabinti wa kirundi wakitoa burudani kwenye maadhimisho hayo.
Burudani ya ngoma za wakimbizi wa Congo DRC.
Pichani juu na chini ni Baadhi ya wakimbizi wa Congo na Burundi waliohudhuria sherehe za maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani ambapo kitaifa yamefanyika katika kambi ya Nyarugusu, wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.

No comments: