Tuesday, May 10, 2016

MGODI WA GGM YAKUBALI KUTOA MAGWANGALA

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter  Muhongo (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, baadhi ya Wabunge na  Wakuu wa Wilaya za mkoa huo, Wawakilishi wa Wachimbaji Wadogo na Watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) mara baada ya kumaliza kikao kilichofanyika mjini Geita. Wa Pili kulia ni Mkuu  wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Wa Pili kulia) akiwa na baadhi ya wananchi wa mkoa wa Geita, waliohudhuria kikao baina ya Waziri na Watendaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, baadhi ya Wabunge na  Wakuu wa Wilaya za mkoa huo, Wawakilishi wa Wachimbaji Wadogo na Watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) mara baada ya kumaliza kikao kilichofanyika mjini Geita. Kikao kililenga katika kujadili suala la magwangala na maeneo ya wachimbaji wadogo nchini.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter  Muhongo (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, baadhi ya Wabunge na  Wakuu wa Wilaya za mkoa huo, Wawakilishi wa Wachimbaji Wadogo na Watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) mara baada ya kumaliza kikao kilichofanyika mjini Geita. Wa Pili kulia ni Mkuu  wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga.

Na Teresia Mhagama, Geita.
MGODI wa Dhahabu wa Geita (GGM) uliopo mkoani Geita umeridhia ombi la Serikali la kutoa mabaki ya mawe ya  dhahabu kwa wananchi ili kuweza kuyachenjua na kupata dhahabu.

Hayo yameelezwa mjini Geita na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo mara baada ya kumaliza vikao vya majadiliano kati ya watendaji wa GGM, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, baadhi ya Wabunge na Wakuu wa Wilaya za mkoa huo, Wawakilishi wa Wachimbaji Wadogo na Watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

“Tatizo la Magwangala sasa limetatuliwa kwani Mgodi umekubali kuyatoa kwa wananchi ila kinachotakiwa kufanywa kabla ya kuyatoa magwangala hayo ni Serikali ya Mkoa huu kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa kwanza wanapata eneo ambalo uchenjuaji wa magwangala utafanyika,” alisema Profesa Muhongo.

Aidha aliongeza kuwa eneo hilo litakalotengwa na Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Geita lazima lifanyiwe tathmini ya mazingira na Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ili kuweza kuthibitika kama eneo hilo linafaa kwa shughuli hizo bila kuleta athari kwa wananchi na mazingira.

Profesa Muhongo alitoa agizo kuwa  kazi hizo zinatakiwa kukamilika tarehe 30 Juni, mwaka huu ambapo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itafanya kikao kitakachohudhuriwa na watendaji wa  Mgodi na Wabunge wa mkoa huo na kutoa uthibitisho wa kimaandishi kuhusu eneo lililotengwa kwa shughuli hiyo pamoja na Cheti kutoka NEMC cha uthibitisho kuwa eneo hilo linafaa au halifai kwa shughuli za uchenjuaji madini kufanyika.

Aidha alieleza kuwa katika kikao hicho cha tarehe 30 Juni GGM itapaswa pia kutoa uthibitisho wa kimaandishi kuwa imekubali kutoa magwangala hayo kwa wananchi.

“Baada ya Eneo hilo na Cheti cha mazingira kupatikana,  sasa katika kikao hicho mtaweza kujadiliana kuhusu  usafirishaji wa magwangala  hayo kutoka eneo la Mgodi hadi eneo lililotengwa, hapo mtakubaliana nani atachukua jukumu la kusafirisha magwangala hayo,”alisema Profesa Muhongo.

Aliongeza kuwa Leseni za uchenjuaji madini zitakazotolewa mara baada ya eneo  hilo kupatikana, zitakuwa katika vikundi na si mtu mmoja mmoja  ambapo  Ofisi ya Mkuu wa mkoa ndiyo itakayoratibu suala hilo huku jukumu la Wizara likiwa ni kutoa Leseni hizo.

“Ni vizuri pia mkashirikiana na viongozi wa Wachimbaji Wadogo katika kuratibu uundaji wa vikundi hivyo na lazima vikundi hivyo vielezwe kuwa ni lazima walipe kodi stahiki kwa Serikali kama ilivyo kwa shughuli nyingine za uchenjuaji madini,” alisema Profesa Muhongo.

Kwa nyakati tofauti Wabunge wa mkoa huo walieleza kuwa utoaji wa Magwangala hayo kwa wananchi, utasaidia wanachi hao kujiajiri, kujiongezea kipato na kuwaepusha katika kushiriki matendo ya uhalifu.

No comments: