Tuesday, May 10, 2016

KILIMO HIFADHI CHA NYANYA KATIKATI YA JIJI LA DAR ES SALAAM.




Dk. Sophia Mlote, mkazi wa Kinyerezi Zimbili jijini Dar es Salaam akiweka sawa vifaa mbalimbali kwenye banda lake la kilimo ambamo amepanda nyanya. Dk. Mlote anatekeleza kilimo hai kupitia mradi wa Green Voices unaofadhiliwa na taasisi ya Foundation for Women of Africa ambayo inaongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, María Teresa Fernández de la Vega. (Makala na Picha zimeandaliwa na www.brotherdanny.com).

Bw. Abdon Hamaro, Ofisa Kilimo kutoka TAHA na mwezeshaji wa mafunzo ya akinamama wa kikundi cha ‘Green Voices  Kinyerezi’, akiendelea kuwaelekeza wanakikundi (hawapo pichani) namna ya kuendesha kilimo hai cha nyanya. Mafunzo hayo yalifanyika hivi karibuni Kinyerezi, jijini Dar es Salaam.


Mratibu wa mradi wa Green Voices, Bi. Secelela Balisidya (kulia), akiwa makini kuangalia Bw. Hamaro akiandaa mambo mbalimbali kwa ajili ya kuwaelekeza wanakikundi namna bora ya kuendesha kilimo hai cha nyanya.


Wanakikundi cha Green Vocies Kinyerezi wakifuatilia mafunzo hayo.


Christina Lwiza (kushoto) akipokea pakiti ya mbegu ya nyanya kutoka kwa Dk. Sophia Mlote tayari kwa kuwatika ili kuanzisha kilimo hai cha nyanya.


Bw. Hamaro akiandaa tray maalum kwa ajili ya kuwapa wanakikundi kupandikiza mbegu kabla ya kupeleka kwenye vitalu vyao. Hii ilikuwa ni sehemu ya mafunzo ya vitendo.


Wanakikundi wakijaza udongo maalum kwenye tray kabla ya kuanza kupandikiza mbegu.


Bw. Hamaro akiwaelekeza kwa vitendo wanakikundi namna ya kupandikiza mbegu hizo.
Hapa wanakikundi wakiendelea kupandikiza mbegu kwenye tray.


10. Banda maalum ambalo ni shamba muhimu kwa ajili ya kilimo hai (green house) ambamo ndani yake nyanya zimestawi.


Picha ya pamoja ya wanakikundi cha Green Voices Kinyerezi.

NDANI ya banda kubwa lililoezekwa na kuzungushiwa plastiki maalum katika Mtaa wa Kinyerezi Zimbili jijini Dar es Salaam, Dk. Sophia Mlote akiwa ameongozana na mtaalamu wa kilimo, Bw. Abdon Hamaro, anaonekana akipanga vizuri vifaa vya kilimo pembeni ya matuta yaliyostawisha vizuri nyanya.

Pembeni ya banda hili lenye ukubwa unaokadiriwa kuwa wa meta 8 kwa 12, akinamama kadhaa wamezunguka wakitazama ustawi wa zao hilo huku Bw. Hamaro akiendelea kutoa maelekezo ya namna ya kuendesha kilimo hai  kinacholimwa katika mabanda maalum yajulikanayo kama green houses ikiwa ni sehemu ya mafunzo ya vitendo ya akinamama hao katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuongeza kipato.

Tofauti na nyanya ambazo watu wamezoea kuziona zikilimwa katika mashamba makubwa na bustani za wazi, nyanya hizi zinalimwa ndani ya banda ambao ukubwa wake utategemea pia na eneo lililopo pamoja na uwezo wa mhusika katika kulijenga banda hilo.

Hiki ni kilimo hifadhi ambacho kinahimizwa kwa sasa ulimwenguni kote ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji.

“Mtu yeyote anaweza kuendesha kilimo cha mazao mbalimbali kwa kutumia Green house hata katikati ya Jiji la Dar es Salaam kama tunavyoona, ni rahisi na rafiki wa mazingira kwa sababu unaweza kuendesha hata kwenye uwa wa nyumba yako kama hivi,” Bw. Hamaro anaendelea kuwaeleza akinamama hao, ambao ni wanakikundi wa mradi wa  ‘Green Voices’ unaofadhiliwa na taasisi ya Foundation for Women of Africa yenye makao yake katika mji wa Madrid, nchini Hispania.

Mbali ya kutunza mazingira, Bw. Hamaro kutoka Chama cha Wakulima wa Bustani Tanzania (TAHA) anasema, kilimo hai kinasaidia kuzalisha vyakula visivyo na kemikali ambavyo ni rafiki wa afya ya binadamu.

Katikati ya Jiji la Dar es Salaam watu wamekuwa wakishuhudia kilimo cha mboga mboga kwenye mabonde ya mito midogo, ambacho kinatumia umwagiliaji wa maji machafu na yenye kemikali za kutoka viwandani, ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu.

“Mbegu zinazotumika zimetengenezwa maalum na hazifanani za zile GMO zinazopigiwa kelele, lakini pia unatakiwa kutumia mbolea za asili kama mboji na samadi, kwa sababu ukitumia kemikali nyingi kwenye udongo, mimea inanyonya na kemikali hizo zinabaki kwenye vyakula na hatimaye kuingia miilini mwetu,” anafafanua Hamaro.

Vile vile, Hamaro anasema kilimo cha Green house kinaweza kutumika hata kwa matunda na kwamba kinatumia maji kidogo huku pia kikimpunguzia gharama mkulima hasa kwa kuepukana na magonjwa mbalimbali ambayo yanasababishwa na wadudu.

“Kwa kuwa banda limefunikwa na kukingwa, hakuna wadudu waenezao magonjwa ya mimea wanaoweza kuingia, lakini faida nyingine ni kwamba, unaweza kudhibiti hali ya hewa kwa kupunguza ama kuongeza joto ili kuifanya mimea kukua vizuri,” anaongeza.

Dk. Mlote mwenyewe, ambaye ni Ofisa Mwandamizi katika Wizara ya Kilimo, Chakula na Mifugo, ni mshiriki wa mradi wa Green Voices ambaye baada ya mafunzo aliyoyapata, sasa anaieneza elimu hiyo kwa wanawake wenzake majirani wa mtaa huo.

Yeyé ni miongoni mwa wanawake 15 waliopatiwa mafunzo ya kuongeza ujuzi wa jinsi ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yaliendeshwa nchini Hispania chini ya ufadhili mkubwa wa taasisi ya Foundation for Women of Africa inayojihusisha na maendeleo ya wanawake wa Afrika, ambayo inaongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, María Teresa Fernández de la Vega.

“Niliamua kuchagua mradi huu kwa sababu, kwanza ni rahisi kuuendesha kwa kuwa shughuli zote zipo hapa nyumbani na hata kama nitarudi usiku kutoka kazini, bado ninaweza kuingia humu shambani na kuhudumia mimea kwa kuwa banda hili lina taa,” anaeleza.

Aidha, anasema, kwa kuwa anakaribia kustaafu, na kwa elimu ya kilimo na uchumi aliyonayo pamoja na utaalamu alioupata, ameona ni vyema aanzishe mradi ambao siyo tu utampatia kipato, lakini pia utasaidia kutunza mazingira pamoja na kuwa msaada kwa jamii kutokana na mazao yatakayovunwa.

“Niliamua kuwaelimisha wanawake wenzangu katika mtaa huu na kuwashawishi waunde kikundi hiki na tayari wamekwishapata mafunzo ya kutosha ambapo kila mmoja amekuja na wazo la kuanzisha bustani ndogo nyumbani kwake ya mtindo huu kwa mazao ambayo anaona yanafaa,” anaongeza Dk. Mlote, ambaye ameeleza kwamba, anakusudia kupanua kilimo hicho kwa kupanda hata miti ya matunda.

Kikundi hicho cha ‘Green Voices Kinyerezi’ kinaundwa na wanawake 10, ambapo mbali ya kujifunza kwa nadharia namna ya kuendesha kilimo hai kwa njia ya green house, walipata fursa ya kufanya kwa vitendo kwa kupandikiza mbegu za mazao mbalimbali ya mboga mboga kama nyanya, kabichi, hoho, matango na matikiti maji kwenye bando hilo ambapo yatakapoota kila mmoja atakwenda kupanda nyumbani kwake.

Christina Lwiza, mmoja wa wanakikundi hicho ambaye anajishughulisha na biashara ya uuzaji vinywaji kwenye grocery yake mwenyewe, anasema ameshawishika kuanzisha kilimo cha nyanya nyumbani kwake ambacho kinaweza kumpatia mapato ya nyongeza pamoja na kukidhi mahitaji ya nyumbani.

“Sijawahi kulima nyanya, lakini kwa mafunzo niliyoyapata, hakika naweza kuendesha kilimo hicho bila shida,” anasema Christina.

Karibu wanakikundi wote wamehamasika, ambapo kila mmoja ameamua kubuni zao ambalo linaweza kumfaa.

Mratibu wa mradi huo, Bi. Secelela Balisidya, anasema mradi huo wa kilimo hai cha nyanya kwa kutumia green house ni sehemu ya miradi 10 inayoendeshwa nchini Tanzania kupitia Green Voices ambapo inaendeshwa katika mikoa sita ya Tanzania Bara.

Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Pwani, Mwanza, Kigoma, Morogoro na Kilimanjaro ambapo inahusisha kilimo, usindikaji, ufugaji na utafiti.

“Miradi hiyo ni kilimo cha miti ya matunda mkoani Kigoma, kilimo cha viazi lishe visiwani Ukerewe mkoani Mwanza, Ufugaji Nyuki mkoani Morogoro na Pwani, ukaushaji wa mbogamboga kwa kutumia nishati ya jua mkoani Morogoro, usindikaji wa vyakula mbalimbali kutokana na muhogo mkoani Pwani, kilimo hai cha mbogamboga, kilimo cha uyoga mkoani Dar es Salaam, mradi wa majiko banifu mkoani Pwani na mradi wa utafiti wa jiko linalotumia nishati ya jua mkoani Kilimanajro,” amefafanua Secelela Balisidya.

Aidha, amesema kwamba, lengo kubwa la mradi wa Green Voices ni kupaza sauti za akinamama kueneza ujuzi wao wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi ili jamii nzima ya Kitanzania iweze kujifunza zaidi na kuzitumia mbinu hizo katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Mradi huo unatarajiwa kutelekezwa kwa mwaka mmoja ili kutoa fursa kwa akinamama kutoa ujuzi wao wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi na sauti zao kusikika, kwa sababu kazi wanazozifanya kila siku za kilimo na utunzaji wa familia zinahusiana moja kwa moja na mazingira hivyo kuyaelewa zaidi mazingira na jinsi ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Malengo ya dunia.
Kilimo hai kinaendana na masuala mtambuka ya mazingira pamoja na kukabiliana na uhaba wa chakula na kupunguza umaskini kama inavyoelezwa kwenye Malengo Endelevu ya Dunia yaliyopitishwa mwaka 2015.

Kwa mujibu wa malengo hayo, mataifa mbalimbali yamekubaliana kuhakikisha yanatokomeza umaskini kwa namna zote pamoja na kukomesha njaa na kupata uhakika wa usalama wa chakula na kuboresha lishe kwa kuhimiza kilimo endelevu.

“Kilimo hai ni endelevu kwa sababu unaweza kulima wakati wowote hivyo kinaweza kukabiliana na njaa na uhakika wa chakula ni mkubwa, lakini pia kitasaidia familia kuongeza kipato kwa kuuza ziada ya chakula kitakachozalishwa,” anasema Hamaro.

Lakini pia kwa kutumia kilimo hai, lengo namba sita la dunia linaweza kutimia, kwani ni kilimo ambacho kinatumia maji kidogo, hivyo kuhakikisha utunzaji mzuri wa vyanzo vya maji na matumizi sahihi ya maji yaliyopo.

Aidha, kilimo hai pia kinaweza kukidhi lengo namba 13 la dunia linalohimiza kupambana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake.

Sera ya Kilimo
Kilimo hai ni sehemu ya mapendekezo yanayotajwa kwenye Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2013 ambayo inaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea mwaka 2025 kwa kuhimiza kilimo chenye tija pamoja na utumiaji mzuri wa rasilimali zilizopo, hususan ardhi na maji.


Kwa maana nyingine, kuhamasisha kilimo hai ni sehemu ya utekelezaji wa malengo, dhima na dira ya sera hiyo hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, ambayo serikali pia imeainisha mikakati yake katika Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2007.

No comments: