Monday, April 25, 2016

NSSF YAWAKWAMUA WANANCHI WA KIGAMBONI.


 Hivi juzi tumeshuhudia ufunguzi wa daraja la Kigamboni ambalo Mh. Rais Dr. John Pombe Mgufuli alilipa jina la daraja la Nyerere. Daraja hili ni matunda ya uwekezaji wenye tija unaofanywa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii la NSSF.

Shirika hilo kwa kushirikiana na serikali limeweza kujenga daraja lenye urefu wa mita 680 likiwa na barabara sita; tatu zikielekea Kigamboni na tatu zikitokea Kigamboni.  Daraja hili lina njia ya watembea kwa miguu yenye upana wa mita 2.5 kila upande.

Daraja hilo limejengwa kisasa na kampuni ya  China Railway Construction Engineering Group iliyotekeleza mradi huo kwa kushirikiana na kampuni ya China Railway Major Bridge Group kutoka nchini China.


 Kukamilika kwa ujenzi wa daraja hili, kumejumuisha barabara za kufika katika daraja hili zenye jumla ya urefu wa kilomita 2.5. Katika ujenzi wa daraja hili, Shirika la NSSF limetoa asilimia 60 ya gharama za Ujenzi na Serikali asilimia 40 ya gharama hizo.

 Akizungumza na waandishi wa habari waliotembela daraja hilo hivi karibuni, Meneja wa Mradi huo kutoka NSSF, Muhandisi Karim Mattaka alisema daraja la Kigamboni limejengwa ili kuondoa kero ya siku nyingi ya usafiri kwa wakazi wa Kigamboni na wakazi wa Dar es Salaam kwa ujumla, kuimarisha hali ya uchumi wa Mkoa huu wa Dar es Salaam, mikoa ya jirani na nchi kwa ujumla pamoja na kuimarisha hali ya uchumi wa shirika, kuliwezesha shirika kuboresha na kulipa mafao kwa kutunza thamani ya fedha kupitia kitega uchumi hiki.

Faida zitokanazo na uwekezaji huo kwa mujibu wa Muhandisi Mattaka ni faida ya moja kwa moja kwa wanachama kwani huingizwa katika akaunti zao pindi wanapochukua mafao yao pamoja na kulipia matibabu yatolewayo bure kwa wanachama.

“Daraja hili linadhihirisha uwezo wa shirika katika nyanja za uwekezaje na kuwapa wanachama uhakika kuwa pesa zao ziko salama,’’.

 “Ni dhahiri kuwa daraja litaondoa usumbufu mkubwa ambao wananchi walikuwa wanaupata na hata wakati mwingine kupoteza maisha, kwani vivuko vya Kigamboni vikiwa vimeharibika wananchi walikuwa wanatumia mitumbwi ambayo wakati mwingine sio salama,.’’ Alisema  

> Kukamilika kwa daraja hilo kunaelezwa kuwa kutachangia sana katika kusukuma maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Kigamboni, Jijini Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.

 Inaelezwa kuwa daraja hilo sasa limefungua fursa  kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kukamilisha utaratibu wa kujenga mji wa kisasa (Kigamboni Elite City) utakaokuwa na nyumba za kisasa,   kuongeza  ufanisi katika utalii kwa kujenga mahoteli ya kitalii katika fukwe zilizopo eneo la Kigamboni, kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoa ya kusini mwa nchi yetu na hata nchi jirani zetu, kupanua kilimo cha matunda, mboga na mazao mengineyo yanayozalishwa  katika eneo hili.

 “Wakulima sasa wataweza kufikisha bidhaa zao sokoni kwa urahisi zaidi na hivyo kuongeza kipato chao,’’ aliongeza.

 Kwa mujibu wa Muhandisi Mattaka daraja hilo vilevile  litarahisisha uwezekano wa upanuzi wa bandari upande wa Kigamboni.

 “Kwa ujumla Daraja la Kigamboni litaboresha sana usafiri ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari unaolikabili Jiji la Dar es Salaam hasa baada ya ujenzi wa barabara ya Dar es Salaam – Chalinze kwa kiwango cha “Expressway” ambayo itaunganishwa na Bandari ya Dar es Salaam kupitia Daraja la Kigamboni.,’’ alisema

 Muhandisi Mattaka alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wadau wa shirika hilo kuhusu usalama wa fedha zao na kuahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa kiwango cha kimataifa.

 Kwa upande Muhandisi wa Mradi huo kutoka kampuni ya  China Railway Construction Engineering Group iliyotekeleza mradi huo kwa kushirikiana na kampuni ya China Railway Major Bridge Group kutoka nchini China, Muhandisi Jamal Mruma alitumia fursa hiyo kuwatoa hofu watumiaji wa daraja hilo kwa kuwa limetengenezwa katika ubora na teknolojia ya hali juu kabisa.

 “Ni aina ya mradi bora kabisa kuwezeshwa na NSSF pamoja serikali na hatimaye kutekelezwa kampuni bora katika masuala ya ujenzi kutoka China.Niwatoe hofu watumiaji wa daraja pamoja na wanachama wa NSSF kuwa wajivunie mradi huu unafaida kubwa sana kwao na taifa kwa ujumla...waulinde na wajivunie haya ni matunda ya pesa zao,’’ alisema.

 Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa daraja, Naibu waziri wa kazi, ajira, vijana na walemavu aliwaasa waajiri wasiopeleka michango yao katika mifuko ya hifadhi ya jamii kutekeleza sheria kwa kuchangia kwa wakati ili kuepuka usumbufu wakati wanachama watakapokua wanahitaji mafao yao.

No comments: