Friday, September 4, 2015

BALOZI OMBENI SEFUE AMEWATAKA WAHANDISI KUWA WAADILIFU

 Baadhi ya Wahandisi wahitimu kutoka katika vyuo na taasisi mbalimbali wakiapa kiapo cha utii kwa Taaluma yao mbele ya Kamishna wa Viapo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wahandisi yanayoendelea jijini Dar es salaam.
 Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akizungumza na Wahandisi kutoka maeneo mbalimbali nchini wakati wa ufunguzi wa Siku ya Wahandisi nchini mwaka 2015 jijini Dar es salaam. 
 Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akikabidhi vyeti na miongozo mbalimbali ya utendaji wa kazi kwa Wahandisi baada ya kuapishwa nchini leo  jijini Dar es salaam.
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini Tanzania (ERB) Mara baada ya ufunguzi wa Siku ya Wahandisi 2015 leo  jijini Dar es salaam. Picha na Lorietha Laurence Maelezo) 

Na Lorietha Laurence
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amewataka wahandisi nchini  kuwa waadilifu na kuweka bidii na maarifa katika kazi zao ili kuleta mapinduzi ya uhakika kwa taifa.

 Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa 15 wa Wahandisi wenye kauli mbiu ya “Utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 mtazamo wa Mhandisi” leo (Alhamisi 3. Septemba, 2015) Jijini Dar es Salaam, Balozi Sefue alisema  fani ya uhandisi ni muhimu kwa kuwa inagusa maisha ya kila ya jamii.
 “Mhandisi ni mtu muhimu katika  maendeleo ya nchi kwa kuwa sekta nyingi zinategemea ujuzi wake  ikiwemo Nishati ,Madini, barabara, maji, uvuvi na kilimo na nyingine nyingi” alisema Balozi sefue.

 Aliongeza kuwa kwa kutambua  umuhimu wa wahandisi katika  maendeleo ya nchi, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuweka maabara katika shule za umma ili kuwavutia wanafunzi kupenda masomo ya sayansi na baadaye kusomea uhandisi pamoja na  kuanzishwa vyuo vya umma vya uhandisi.

Kwa mujibu wa Balozi Sefue alisema Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya  mafunzo kwa njia ya  vitendo kwa wanafunzi watakaosoma masomo ya uhandishi katika ngazi mbalimbali.

Aidha Balozi Sefue aliupongeza Ubalozi wa Norway nchini kwa mchango wake kiasi cha dola milioni 2 za kimarekani zilizosaidia kuwawezesha wahandisi wa kike 217 kusajiliwa na hivyo kuongeza idadi ya wahindisi wanawake nchini.

 “Ninawaomba watoto wa kike wa Tanzania wapende masomo ya sayansi ili baadaye waweze kusomea uhandisi na hivyo kuongeza idadi ya wahandisi nchini na kuchochea maendeleo zaidi” alisema Balozi Sefue.

Naye Katibu ya Bodi ya Wahandisi Nchini, Mhandisi. Prof. Ninatibu Lema ameiomba serikali kujenga mazingira mazuri kwa wahandisi wa serikali na wa sekta binafsi ili kuleta matunda mazuri kwa nchini.

Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Wahandisi, Mhandisi Steven Mlote alisema ili dira ya maedndeleo ya mwaka 2025 iweze kukamilika ni budi udahili wa wahindisi uongezeke kwa kuwa uhitaji wake kwa sasa ni mkubwa.

“Mpaka sasa tuna wahandisi 15364 waliosajiliwa na Bodi ya Usajili nchini idadi ambayo ni ndogo ukilinganisha na uhitaji wa watu katika kuleta maendeleo kupitia sekta mbalimbali” alisema  mhansisi Mlote.

Katika Mkutano huo wahandisi 96 waliapa kiapo cha uadilifu mpango uliozinduliwa na Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt.John Magufuli wakati wa mkutano wa 13 wa wahandisi uliofanyika September 05 2013.

No comments: