Monday, August 31, 2015

STARS YAMALIZA KAMBI UTURUKI

Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro chini ya Kocha wake Mkuu Charles Boniface Mkwasa imefanya mazoezi yake ya mwisho leo asubuhi katika viwanja vya hoteli ya Green Park Kartepe – Kocaeli nchini Uturuki.
Taifa Stars ambayo imeweka kambi nchini Uturuki kwa takribani wiki moja, inajiwinda na mchezo wake dhidi ya Nigeria siku ya Jumamosi Septemba 5, 2015 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa Afrika mwaka 2017.
Kocha Mkuu wa Stars Charles Mkwasa akiongea na tovuti rasmi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) www.tff.or.tz amesema anashukuru kambi imekua na mafanikio makubwa kwani vijana wanaonyesha mabadiliko makubwa sana.
“Ukiondoa mchezaji moja tu ambaye ni majeruhi Abdi Banda, Mkwasa amesema wachezaji wengine wote wapo fit na kila mmoja atakayepata nafasi katika mchezo wa sikuya jumamosi atafanya vizuri” amesema Mkwasa.
Mkwasa amesema mazingira ya kambi yamekua mazuri, na katika mechi ya maozezi dhidi ya Libya iliyochezwa siku ya ijumaa, vijana wake walicheza vizuri kwa nguvu na kufuata maelekezo yake, makosa machache yaliyojitokeza katika mchezo huo wameyafanyia kazi na sasa anaamini wako tayari kuwakabili Nigeria.
Mwisho Mkwasa amewaomba watanzania kujitokeza kwa wingi uwanja wa Taifa siku ya jumamosi  kuishangilia timu ya Taifa, kwani uwepo wa washabiki wengi uwanjani utawaongeza morali zaidi wachezaji na kujiona wapo nyumbani wanapambana kwa ajili ya Taifa lao.
Naye nahodha wa Taifa Stars, Nadir Haroub “Cannavaro” amesema maandalizi waliyopata ni mazuri na yamewajenga vilivyo kuelekea kwenye mchezo dhidi ya Nigeria siku ya jumamosi na kuwaomba watanzania kuja kwa wingi kuwasapoti.
Nadir amesema wao kama wachezaji kila mmoja yupo fit na anahitaji  kucheza mechi hiyo, hivyo yeyote atakayepata nafasi ya kucheza ana imani atafanya vizuri katika kuipeperusha bendera ya Tanzania.
Stars ambayo iliweka kambi ya takribani siku nane katika milima ya Katrepe - Kocaeli, inatarajiwa kuodoka kesho jumanne saa 1 jioni nchini Uturuki kurejea nyumbani kwa usafiri wa shirika la Ndege la Uturuki (Turkish Airlines) na kuwasili uwanja wa JK Nyerere majira ya saa 9 kasoro usiku.
Mara baada ya kuwasili Dar es salaam timu itaendelea na kambi kwa kufanya mazoezi mepesi siku ya jumatano pamoja wa wachezaji wa kimataifa Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Mrisho Ngasa katika uwanja wa Taifa kujiandaa na mchezo wa siku ya jumamosi dhidi ya Nigeria.

No comments: