Wednesday, July 1, 2015

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI , UTALII NA MICHEZO ZANZIBAR AZINDUA HOTELI TAUSI Palace, MJI MKONGWE ZANZIBAR.

Mwenyekiti wa Makampuni ya Hoteli ya Mark and High Class Group Tanzania Rustam Merani akimuonesha moja ya vyumba cha Hoteli hiyo Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Saidi Ali Mbarouk mara baada ya kuizundua rasmi.

Na Faki Mjaka
Maelezo Zanzibar  
Upatikanaji wa huduma bora za Kiutalii ikiwemo Hoteli za kisasa ni miongoni mwa Vivutio muhimu vya Watalii kuja kuitembelea Zanzibar.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari,Utamaduni,Utalii na Michezo Zanzibar ,Said Ali Mbarouk katika uzinduzi wa  Hoteli ijulikanayo kama TAUSI Palace iliyopo Mji Mkongwe mjini, Zanzibar.
Amesema Utalii imara huambatana na huduma bora na kwamba uwepo wa Tausi Palace utasaidia ongezeko la Watalii na kupelekea kuimarika zaidi Sekta hiyo.
Waziri Mbarouk amesema kwa sasa Sekta hiyo inaajiri zaidi ya watu Elfu 20, na kuchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la Pato la taifa.
 Amefahamisha kuwa Serikali itaendelea na juhudi zake za kuwahamasisha Wawekezaji kuwekeza katika Sekta hiyo ili kuzidi kuimarisha Uchumi wa Zanzibar.
Amesema Zanzibar ina vivutio Vingi vya Utalii na mazingira salama ya kiuwekezaji na kuwaomba Wawekezaji hao kuendelea kutumia fursa hiyo ili iweze kuwanufaisha wao na Jamii kwa ujumla.
Waziri Mbarouk amesema anaamini Ubora wa Hoteli hiyo utapelekea Watalii mbalimbali wanaofika Zanzibar kufika katika Hoteli hiyo na kujionea Ubora wa huduma zake.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kampuni ya Hoteli za “Mark and High Class Group” inayomiliki Hoteli mbalimbali Zanzibar na Tanzania Bara amesema lengo lao ni kutoa huduma bora za kiutalii ili ziwanufaishe na kuisaidia jamii ya Zanzibar.
Amesema Kampuni yao imevutika na Vivutio vingi vya kiutalii Zanzibar sambamba na hali ya utulivu na amani iliyopo jambo ambalo litapelekea Sekta hiyo kupiga hatua siku hadi siku.
Aidha amesema wapo njiani kujenga Hoteli bora ya Nyota tano katika Eneo la Mbweni ifikapo June mwakani.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Hoteli hiyo John Kiruthi amesema ubora wa huduma zao na kujitangaza vyema katika Soko la Utalii la Dunia ndiko kutakakopelekea kupata wageni wengi katika Hoteli hiyo.
Aidha amesisitiza kuwa watahakikisha agizo la kuajiri Asilimia 30 ya Wafanyakazi kutoka Zanzibar linatekelezwa ili kuisaidia Serikali kupunguza tatizo la Ajira kwa Vijana.
Miongoni mwa mambo ya upekee ya Hoteli hiyo ni pamoja na kuwepo kwa Vyumba Vikubwa, Ukumbi mkubwa wa Mikutano na Wahudumu wakarimu.

No comments: