Saturday, May 9, 2015

TANZANIA YAANDIKA HISTORIA NYINGINE KWA KUZIBA MATUNDU YA MOYO BILA KUFUNGUA KIFUA

Mwezi Mei tarehe 9, mwaka 2015, Tanzania imeandika historia nyingine baada ya kufanya Tiba ya moyo bila ya kufanya upasuaji kwa kuziba matundu yaliyoko kwenye moyo kwa kutumia “kifaa maalum” bila kufungua kifua kama ilivyozoeleka. 

Tiba hii inafanyika kwa mara ya kwanza nchini kupitia Idara ya Tiba na Upasuaji Moyo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili ikishirikiana na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Prince Sultan Cardiac Centre iliyoko Riyadhi nchini Saudi Arabia ambao watakuwepo Muhimbili kwa siku tisa kuanzia tarehe 9 hadi 16 Mei, mwaka huu.

 Madaktari hawa wamekuja kupitia taasisi ya Al Mutanda Islami Trust ya Uingereza. Akizungumza na wanahabari, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Hussein Kidanto amesema jumla ya wagonjwa zaidi ya 20 wanatarajiwa kupatiwa tiba hii.
Katikati ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Hussein Kidanto akizungumza na waandishi wa habari. Kushoto kwake ni Prof. Jameel Alata ambaye ni Daktari Mwelekezi wa Magonjwa ya Watoto ambaye ameongoza timu ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Prince Sultan Cardiac Centre iliyoko Riyadhi nchini Saudi Arabia ambao watakuwepo Muhimbili kwa siku tisa kuanzia tarehe 8 hadi 16 Mei, mwaka huu. Aliyepo mwisho kulia ni Sheikh Said Ahmed Abri ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Kiislam la hapa nchini liitwayo Dhi Nureyn Islamic Foundation na shirika hili ndilo lililoratibu timu hii ya madaktari kuja kutoa huduma.
Baadhi ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Prince Sultan Cardiac Centre iliyoko Riyadhi nchini Saudi Arabia wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wakati akiwakaribisha na kuzungumza na vyombo vya habari, leo Jijini Dar Es Salaam.
Baadhi ya Waandishi wa habari wakifanya kazi yao na kuelekezwa namna (Cath Lab) mtambo wa kufanya uchunguzi na kuzibua mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye moyo na pia kuziba matundu ndani ya moyo bila kufungua kifua.

Taaluma ya matibabu inabadilika kwa kasi kubwa sana duniani na ili Hospitali ya Taifa Muhimbili iweze kuenda sambamba na kasi hiyo ni muhimu na lazima kufanya ushirikiano na nchi ambazo zimepiga hatua kubwa kwenye nyanja mbalimbali za matibabu, amesema Dkt. Kidanto.

Tiba hii inafanyika kwa kutumia kifaa maalumu (device) cha kuzibia sehemu yenye tundu kwenye moyo kupitia mishapa ya damu kufika kwenye tundu liliopo kwenye moyo ambao mtoto anazaliwa nayo. Kuna faida nyingi kufanya kwa tiba hii ambapo mgonjwa hatakaa wodini muda mrefu akisubiri kupona kidonda cha upasuaji ukilinganisha na kama angefunguliwa kifua, amesema Dkt. Kidanto. Aliongeza kuwa mara baada ya mgonjwa kupata tiba hii mgonjwa anaweza kuruhusiwa ndani ya siku moja hadi mbili na kuondoka kuendelea na shughuli zake za kawaida.

Aprili mwaka huu, Tanzania iliandika historia ya kwanza kwa kuzibua mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye moyo na kuweka kifaa maalumu kinachoitwa (stent) ambapo mtambo maaluum wa Cath Lab unatumika baada ya kufanya uchunguzi wa kuangalia mishipa ya damu inayoenda kwenye moyo jinsi unavyofanya kazi, na kama kuna mshipa umeziba uweze kuzibuliwa.

Tangu kuanzishwa kwa huduma hii mwezi uliopita jumla ya wagonjwa 31 walifanyiwa uchunguzi wa mishipa ya damu ya moyo na wagonjwa wanne waliweza kuzibuliwa mishipa yao ya moyo na kuwekewa stent ambapo damu iliweza kupita vizuri katika mishipa ya moyo, wagojwa wawili walihitaji upasuaji wa moyo wa haraka kuweza kutibiwa mishipa yao ya damu ya moyo kwa njia ya upasuaji. Ifikapo julai 31 mwaka huu tunatarajia idadi ya wagonjwa mia moja watapata huduma hii.

Dkt. Kidanto amesema kasi hii ya kutoa huduma hizi inatarajia kuleta tija kwa wagonjwa wenyewe, taifa na wafanyakazi ambao wanaona maendeleo mazuri ya wagonjwa wanaowahudumia inaongezeka. Huduma hizi mbili kuanzia kwenye uchunguzi hadi tiba hazijawahi kufanyika popote hapa nchini isipokuwa hapa Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia idara yake ya Tiba na Upasuaji Moyo. “Kwa misingi hiyo, Tanzania imeandika historia ya pekee na uenda kasi ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi ikapungua kwa kiasi kikubwa kwa wale watakaohitaji huduma hii kwa vitendo”amesema Dkt. Kidanto.

“Moja wapo ya malengo yetu ni kuhakikisha tunashirikiana na taasisi za kitaaluma rafiki na kuwakaribisha kuja kufanya kazi na sisi katika mazingira yetu na hivyo kujenga uwezo hapa hapa nchini kwa watu wengi zaidi kuliko ambayo tungepeleka watalaam wetu wachache kwao kujifunza” alisema Dkt. Kidanto.

Dkt. Kidanto amesema, hadi kufikia Aprili mwaka huu jumla ya wagonjwa 453 wamefanyiwa upasuaji wa moyo ambapo wagonjwa 110 wamefanyiwa uchunguzi wa mishipa ya damu ya moyo. Utaratibu huu wa kushirikiana na wataalam mbali mbali kutoka nje utaendelea tena 16/05/2015-22/05/2015 kwa wataalam wa moyo kutoka Medical University of South Carolina chuo kikuu kabisa cha jimbo la South Carolina, Marekani kupitia Madaktari Afrika.

Tunatarajia kupokea kundi jingine liitwalo Save A Child’s Heart kutoka Israel Juni 28-Julai 5 2015. Na kama tulivyo eleza awali haya ushirikiano huu una dhumuni la kutoa huduma kwa wagonjwa wetu na mafunzo kwa wataalam wazawa hapahaoa nchini, amesema Dkt. Kidanto

No comments: