Monday, May 11, 2015

DUNIA KUJADILI CHANGAMOTO NA ATHARI YA MADAWA YA KULEVYA

Bw. Sam Kutessa, Rais  wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Na  Mwandishi Maalum, 
New York 
Jumuiya ya Kimataifa  inajiaanda  kwa  mkutano maalum na  wa aina yake kufanyika, ambapo  nchi wanachama watakutana  na  kujadiliana kwa kina kuhusu  changamoto na adhari kubwa  zitokanazo na  biashara haramu na matumizi ya dawa za kulevya.
 Mapema wiki iliyopita,    wajumbe wanaoziwakilisha nchi  zao  hapa  Umoja wa Mataifa, walikuwa na mkutano wa siku moja ambao ulikuwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano huo maalum utakaofanyika mwezi Aprili  2016.
Mkutano huo wa maandalizi uliofanyika hapa  Umoja wa Mataifa na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwamo mawaziri kadhaa kutoka nchi hasa  za  Amerika ya Kati ambako   nchi nyingi zinakabiliwa  na changamoto kubwa ya  biashara hiyo, uliandaliwa na Bw. Sam Kutessa, Rais  wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Katika  majadiliano ya  mkutano huo ,  ilidhihirika wazi kwamba hakuna nchi hata moja   duniani  iwe tajiri au maskini ambayo  haijakumbwa  na  janga  la biashara na  matumizi ya dawa za kulevya.
“ Hakuna nchi ambayo imepona kutokana na biashara hii yenye thamani  ya mabilioni  ya dola. Licha ya juhudi kubwa na raslimali nyingi ambazo mataifa yanatumia   kukabiliana na janga hili, lakini tatizo  linaendelea kukua” akasema Bw. Sam Kutessa wakati akifungua mkutano huo.
Naye Naibu Katibu Mkuu Bw, Jan Eliason  naye akizugumza  kwenye  mkutano huo. Pamoja na mambo mengine alieleza kwamba, mitandao ya kihalifu inazidi kustawi kutokana na biashara hiyo na  kuongeza  kuwa  mitandao  hiyo  inaharibu mifumo  imara ya ustawi  wa kijamii, pamoja na kuyumbisha utawala wa kidemokrasia.
 Kama hiyo  haitoshi Naibu Katibu Mkuu, ameongeza kuwa biashara haramu ya  dawa za kulevya inatumika kama vyanzo vya mapato  kwa  makundi ya wanagambo wenyenye silaha na hivyo kuwa tisho kubwa katika mataifa ambayo yanamigogoro.
 Kwa sababu hizo na nyingine nyingi zilizobainishwa na wajumbe walioshirikia mkutano huo, wameshauri   na kupendekeza kwamba,  kwa kuwa tatizo la dawa za kulevya ni la dunia nzima,  basi utashi wa kisiasa,  ushirikiano, uwazi na ukweli  utahitajika sana katika mkutano huo maalum  utakaofanyika  mwakani.
Baadhi ya wachangiaji walikwenda mbali Zaidi   kwa kubainisha kuwa,   katika kulikabili tatizo la dawa za kulevya haitoshi nguvu kuelekezwa  kule zinakozalishwa dawa hizo  bali  nguvu hizo pia zinatakiwa kuelekezwa pia katika nchi ambazo zina matumizi makubwa ya dawa.

Aidha  wachangiaji  wengine walitaka pia uwazi na  uwajibikaji katika udhibiti   wa vyanzo vya  fedha chafu  ambazo zinatumika katika biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya. Ikiwa ni pamoja na  udhibiti wa magenge  ya wahalifu wanaomiliki na kuendesha biashara hiyo.
Vile vile   wazungumzaji  wengi  pia walizungumzia  namna gani  biashara na matumizi ya  dawa za kulevya inavyoendelea kushamiri licha ya  juhudi mbalimali  za kimataifa na kimataifa za kuikabili.  Na kwamba kuendelea kwa biashara hiyo  ambayo tayari imeshaathiri na kuendelea kuathiri maisha ya watu wengi hususani  vijana, wanawake na watoto ni janga  la dunia.
Wengi wamekiri  bayana kwamba si rahisi sana kumaliza tatizo na  biashara  haramu  na matumizi ya dawa hizo  kutokana na ukweli kwamba  linawashirika na wadau wengi na ni biashara yenye kubeba uzito mkubwa kiasi kwamba si rahisi kuimaliza mara moja.
Wapo baadhi ya wajumbe waliogusia kuhusu adhabu kali  zikiwamo za kuuawa kwa watu wanaokamatwa wakisafirisha  au kuuza dawa hizo, na kwamba adhabu kama za  kifo  licha ya kwamba ni ukiukwaji  ya haki ya  mtu kuishi lakini pia ni ukiukwaji wa haki za binadamu na kwamba  hukumu ya adhabu ya kifo haijapunguza kasi ya  biashara hiyo au matumizi yake.
 Wengine walielezea haja na umuhimu ya kutowanyanyapaa watu ambao wameathirika  na dawa hizo au hata kuwatenga kwa kile walichosema wanachohitaji waathirika hao ni msaada wa matibabu yatakayowawezesha kuondoka na dhahama hiyo.
Akichangia majadiliano  hayo, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako  Manongi,  alisema kama ilivyo kwa  nchi nyingine, Tanzania nayo haijapona na  janga  la  biashara na matumzi ya dawa za kulevya.
Akasema  Tanzania imekuwa njia ya kupitishia dawa hizo kutoka  nchi moja kwenda nchi nyingine, na  kwamba katika usafirishaji huo,   kiasi cha dawa hizo  hubakia nchini na hivyo kuathiri   sehemu kubwa ya jamii  ya watanzania  ambao tayari wanakabiliwa na umaskini wa kila aina.
Akaongeza  kuwa, tatizo la dawa za kulevya limekuwa kikwazo katika  jitihada za  kuwapatia watanzania maisha yenye hadhi kutokana na kwamba tatizo hilo linaathiri nguvu kazi inayohitajika katika  ujenzi na uendeshaji wa maendeleo ya jamii   na ukuaji wa uchumi.
Kama hiyo haitoshi, Balozi Manongi ameeleza kwamba,   dawa za kulevya zimekuwa kichocheo cha ongezeko la vitendo vya uhalifu ikiwa ni  pamoja na uhalifu wa wanyamapori na misitu,  ugaidi na  pia kuongeza mzigo katika  huduma za afya.
“Lengo letu ni  kuzuia uingiaji wa dawa za kulevya kwenye  ndani ya  nchi  yetu,  lakini uzoefu umetuonyesha hii ni  kazi kubwa na ngumu na hasa  kutokana na  muingiliano baina ya mataifa ni kwa sababu hii, tunashirikiana na  nchi  jirani nasi na washirika wengine katika kuboresha jitihada za kukabiliana na changamoto hii” akasema Balozi Manongi.
  Akatilia mkazo  umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa, pamoja na mipango  mbadala  inayoweza kutoa fursa kwa  jamii kufanya shughuli nyingine badala ya kutegemea biashara ya dawa za kulevya
Mkutano wa mwakani unafanyika ikiwa miaka kadhaa  imepita    tangu  ulipofanyika mkutano   mwaka 2008  huko Vienna, ambapo  kulipitishwa   Tamko la Kisiasa na Mpango wa  Utekelezaji  juu ya ushirikiano wa uwiano ili  kukabiliana na  tatizo la dawa za kulevya. Mkutano huo wa mwakani  utafanya tathmini ya tamko hilo pamoja na masuala mengine. 

No comments: