Tuesday, March 31, 2015

Waziri wa Fedha afanya ziara kwenye bandari kavu ya kampuni ya THR jijini Dar leo

Waziri wa Fedha Mhe. Saada Mkuya (katikati) akiwasili katika Bandari ya Nchi Kavu ya TRH katika ziara ya wizara hiyo leo jijini Dar es Salaam ambapo kontena mbili zilikamtwa ambapo moja ilikutwa na bidhaa za tv na nyingine biskuti huku nyingine mbili hazikuweza kupatikana mahali zilipofichwa.
Kamishna Msaidizi wa Forodha wa Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA),Bw. Tiagi Kabisi kushoto akipata maelekezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Tanzania Road Haulage (TRH) Bw. Ali Lilani katika ziara ilifanywa na Waziri wa Fedha leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha Mhe. Saada Mkuya (kushoto) akisikiliza maelekezo kutoka kwa Kamishna Msaidizi wa Forodha wa Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA),Bw. Tiagi Kabisi katika ziara ya wizara hiyo leo jijini Dar es Salaam ambapo kontena mbili zilikamtwa ambapo moja ilikutwa na bidhaa za tv na nyingine biskuti huku nyingine mbili hazikuweza kupatikana mahali zilipofichwa.
Waziri wa Fedha Mhe. Saada Mkuya (katikati) akiangalia mbidhaa za tv zilizokutwa katika mojawapo ya kontena zilizokuwepo katika Bandari ya Nchi Kavu ya TRH katika ziara ya wizara hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha Mhe. Saada Mkuya (katikati) akijadiliana jambo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha (kulia) Mhe.Dkt.Servacius Likwelile na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA Richard Kayombo(kushoto) wakati wa ziara ya wizara hiyo katika Bandari ya nchi Kavu ya Tanzania Road Haulage(TRH) leo jijini Dar es Salaam.
Kontena mbili zenye bidhaa za Tv na Biskuti zilizokamatwa katika Bandari ya Nchi Kavu ya Tanzania Road Haulage (TRH) wakati wa ziara ya Waziri wa Fedha Mhe.Saada Mkuya leo jijini Dar es Salaam.(Picha na Lorietha Laurence-Maelezo)

Na Lorietha Laurence- Maelezo

Waziri wa Fedha Mhe.Saada Mkuya amesema kuwa serikali itawashughulikia wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi kwa kuwachukulia hatua stahiki ikiwemo kunyang’anywa leseni ya biashara na kulipa faini. Aliyasema hayo leo jijini Dar es Salaam katika ziara ya kukagua bandari kavu ya kampuni ya THR ambapo ni mjumuisho wa ziara iliyoanza jana jioni kutembelea Bandari za nchi kavu.

“Tumekamata jumla ya kontena nane ambazo katika taarifa za awali zilieleza kuwa zina bidhaa za gypsum powder na gysum plasta lakini tulipozifungua tumekutana na bidhaa tofauti na kile tulichoambiwa” alisema Mhe. Mkuya Aidha aliongeza kuwa bidhaa zilizokutwa katika kontena hizo ni pamoja na spea za pikipiki,vitenge ,Tv na biskuti ambazo zilitakiwa kulipia ushuru tofauti na zile ambazo ziliandikwa katika taarifa ya kupokea mzigo.

Mhe. Mkuya alisema kutokana na udanganyifu huo takribani shilingi milioni mia tatu zimepotea na hiyo ni mojawapo ya vikwazo vinavyokwamisha shughuli za maendeleo kusonga mbele kwa ukosefu wa fedha.

Naye Kamishana Msaidizi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bw. Tiagi Kabisi ameeleza kuwa wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali wakati wa utendaji wao wa kazi ikiwemo udanganyifu unaofanywa na wafanyabiashara ikiwemo hili la kutokulipwa kodi.

“Hii ni mojawapo ya changamoto ambazo tunakutana nazo katika kazi zetu ambapo wafanyabiashara wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za udanyifu ili kukwepa kulipa kodi” alisema Bw.Kabisi Ziara hiyo ni mojawapo ya mikakati ya Wizara ya Fedha katika kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanawajibika katika suala la ulipaji wa kodi nia ni kuhakikisha nchi inaweza kujitegemea kupitia vyanzo mbalimbali vya uchumi ili kukuza na kuendeleza ustawi wa nchi.

No comments: