Friday, March 27, 2015

UJUMBE WA VIONGOZI WA SUDAN KUSINI WAVUTIWA NA UTENDAJI KAZI WA TANROADS

Mkurugenzi wa Mipango wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Eng. Jason Rwiza, akielezea namna TANROADS inavyofanya kazi za ujenzi wa barabara hapa nchini kwa ujumbe wa viongozi kutoka Sudan Kusini katika ofisi za Wakala hao jijini Dar es salaam jana.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Barabara wa Sudan Kusini Eng. Kenyata Warille, akifafanua namna Mamlaka yake inavyofanya kazi za ujenzi wa barabara nchini kwao. (Nyuma wa kwanza kulia) ni Mwakilishi wa JICA wa Sudan Kusini Tomoki Kobayashi, akifatilia kwa makini.
Naibu Waziri wa Usafirishaji, Barabara na Madaraja wa Sudan Kusini Mh. Simon Mijok (Wa kwanza kulia), akimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi wa Sudan Kusini Eng. Gabriel Makur, baadhi ya vitabu walivyopewa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kwa ajili ya kuwasaidia kuboresha taasisi zao za ujenzi.
Ujumbe wa viongozi kutoka Sudani Kusini wakiangalia namna magari yanavyopimwa uzito kwa kutumia njia ya kigitali yenye uwezo wa kurekodi taarifa zote za vipimo na kupatikana katika mtandao wa TANROADS. Mzani huo unapima gari moja kwa muda wa sekunde 30 tofauti na wa zamani.
Gari lililozidisha uzito likipimwa katika mzani mpya wa kisasa wa Vigwaza mkoani Pwani. Magari kama haya yanayozidisha uzito huharibu miundombinu ya barabara nchini.

Ujumbe wa viongozi wa sekta ya ujenzi na mazingira toka Sudan Kusini umepongeza Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), kwa namna unavyofanyakazi na kuahidi kushirikiana nao ili kuimarisha sekta ya barabara na madaraja nchini mwao.

Akizungumza katika ziara ya mafunzo inayoendelea hapa nchini Naibu Waziri wa Usafirishaji,Barabara na Madaraja wa Sudan Kusini Mhe. Simon Mijok amesema mfumo wa uendeshaji wa TANROADS ni mzuri na unaofaa kuigwa na nchi yake kwani unatoa uhuru kwa wakala kuwa na mtandao wa utendaji nchi nzima.

“Kutokana na miaka mingi ya vita nchini kwetu miundombinu mingi ya barabara na madaraja imeharibika hivyo njia nzuri ya kuifufua kwa haraka ni kuwa na taasisi yenye mfumo wa utendaji kama TANROADS na Mfuko wa Barabara”, amesisitiza Naibu Waziri Mijok.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Barabara ya Sudan Kusini (SSRA) Eng.Kenyata Warille amesema mafunzo wanayoyapata hapa nchini yatawawezesha kufanya mabadiliko muhimu katika taasisi zao za ujenzi na watawatumia watanzania kuwashauri ili watumie muda mfupi kuboresha miundombinu ya nchi yao na kwenda na kasi ya maendeleo ya nchi za Afrika Mashariki na Kati. 

Amesema Sudan Kusini licha ya kuwa nchi kubwa kwa eneo bado ina mtandao wa barabara wa Km 19,073 zinazounganisha majimbo kumi ya nchi hiyo yenye watu takriban milioni 12.

Aidha ujumbe huo umepata nafasi ya kujionea namna mizani ya kisasa ya Vigwaza mkoani Pwani inavyofanya kazi na kuahidi kujenga mizani ya namana hiyo nchini mwao kutokana na utendaji kazi wa haraka na unaozingatia teknolojia.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo wa Usafirishaji,Ujenzi na Madaraja ameishukuru Tanzania kwa hatua mbalimbali inazochukua kuipatanisha nchi yake ili amani na utulivu viwepo. Pia amesisitiza kuwa ziara za mafunzo za viongozi wa nchi hiyo zitaendelea na kuwaalika watanzania nao kwenda Sudan Kusini kujifunza.

Naye Mkurugenzi wa Mipango wa TANROADS Eng. Jasson Rwiza ameuhakikishia ujumbe huo kuwa ushirikiano uliopo baina ya taasisi zao utaendelezwa ili kubadilishana uzoefu na hivyo kuwezesha barabara za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati zipitike kwa urahisi na kukuza uchumi wa nchi zao.

No comments: