Sunday, January 25, 2015

Halmashauri ya Wilaya ya Chunya yachangia Shilingi Milioni 210 katika Mfuko wa Vijana na Wanawake kwa kipindi cha miaka miwili

Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Bibi Ester Makalili akizungumza na ujumbe kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo walipomtembelea ofisini kwake kabla ya kukutana na vijana wa Wilaya hiyo kutoa mafunzo ya Ujasiriamali, Stadi za Maisha, Ujuzi na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana jana katika Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya. Kushoto ni Mwenzeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa na kushoto ni Mkuu wa Kituo cha Vijana Sasanda Mbeya Bw. Laurean Masele.
Mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa akitoa mada ya Ujuzi kwa vijana wakati wa semina ya Ujasiriamali, Stadi za Maisha, Ujuzi na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana jana katika Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya.
Afisa Ushirika kutoka Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya Bw. Mwanyi Magambo akiwaelimisha vijana wa Wilaya ya Chunya umuhimu wa kuunda Saccoss ya Vijana itakayowawezesha vijana kuweka akiba na kukopeshana wakati wa semina ya Ujasiriamali, Stadi za Maisha, Ujuzi na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana jana katika Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya.
Afisa Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Amina Sanga kushoto akizungumza na wanakikundi wa Ngozi group wanaosindika ngozi kwa njia ya asili na kutengeneza bidhaa za ngozi kwa kutumia ngozi walizosindika walipowatembelea kukagua mradi wao jana katika kijiji cha Mkwajini Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya. Wa pili kulia ni Mkuu wa Kituo cha Vijana Sasanda Mbeya Bw. Laurean Masele.
Kijana Meshaki Ngailo kushoto kutoka kikundi cha Vijana Bush Man Works kinachofanya kazi ya kuunga vyuma akizungumza na maafisa waliofika kukagua mradi wa kikundi chake wakati wa ziara ya kukagua miradi ya vijana wa Mkoa wa Mbeya. (Picha zote na: Genofeva Matemu – Maelezo. Chunya, Mbeya).

Na: Genofeva Matemu – Maelezo, Mbeya

Halmashauri ya Wilaya ya Chunya iliyopo katika Mkoa wa Mbeya imefanikiwa kuchangia shilingi milioni 210 katika mfuko wa Vijana na wanawake kwa mwaka wa fedha 2013/2014 na 2014/2015.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Bibi Ester Makalili jana alipotembelewa ofisini kwake na ujumbe kutoka Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo kabla ya kukutana na vijana wa Wilaya hiyo kwa ajili ya kutoa mafunzo ya Ujasiriamali, Stadi za Maisha, Ujuzi na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.

Bibi Makalili amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya imefanikiwa kutimiza maagizo yanayotolewa na serikali katika kila Halmashauri kwani kwa sasa Halmashauri imeshatenga maeneo yakutosha kwa vijana na inasubiri vijana wa Halmashauri hiyo kuandika maombi ya kupatiwa maeneo hayo ili iweze kuwapatia.

Aidha Afisa Michezo na Vijana kutoka Mkoa wa Mbeya Bw. George Mbijima amesema kuwa semina ya Ujasiriamali, Stadi za Maisha, Ujuzi na Mfuko wa Maendeleo kwa Vijana wa mkoa wa Mbeya imetoa hamasa kubwa kwa vijana hasa katika upande wa vijana kujitambua na kufahamu taratibu zinazotumika kuwawezesha vijana katika vikundi kwani serikali haiwezi kumfikia kijana mmoja mmoja.

Bw. Mbijima amesema kuwa Halmashauri za Wilaya zilizopo katika Mkoa wa Mbeya zimekua na changamoto kubwa ya utengaji na utoaji wa asilimia tano katika mfuko wa vijana kutokana na mapato yanayokusanywa kuwa kidogo ukilinganisha na kundi kubwa la vijana wanaoishi katika wilaya hizo hivyo kushinda kuwafikia vijana wote.

Akizungumza na vijana wakati wa semina hiyo Afisa Ushirika kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Bw. Mwayi Magambo amewataka vijana wa Wilaya ya Chunya kushirikiana kuunda Saccoss ya Vijana ya Wilaya watakayoitumia kujiwekea akiba na kukopeshana huku serikali ikitumiwa kama nyongeza katika kuchangia Saccoss hiyo.

Kwa upande wake kijana Abubakari Sokolo amesema kuwa semina ya Ujasiriamali waliyoipata ni chachu ya maendeleo kwa vijana wa Chunya hivyo kutumia ujuzi walioupata kuleta mafanikio katika vikundi vyao na kusambaza elimu waliyoipata kwa vijana wengine.

No comments: