Wednesday, December 12, 2012

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MGOGORO WA WAFANYAKAZI NA WANAFUNZI KATIKA CHUO KIKUU KISHIRIKI DAR ES SALAAM CHACHUO KIKUU CHA KIMATAIFA CHA KAMPALA


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA VYUO VIKUU TANZANIA

 1.         Utangulizi
Kwa takribani wiki tatu sasa kumekuwa na mvutano baina menejimenti kwa upande mmoja na wafanyakazi na wanafunzi kwa upande mwingine wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es salaam ama, kinavyojulikana kwa wengi, KIU. Mvutano huu ulisababisha baadhi ya waalimu kusitisha kufundisha na pia baadhi ya wanafunzi kujikuta katika mgomo hadi mvutano uliojitokeza utakapopatiwa ufumbuzi. Mvutano huu hatimaye ulisababisha Tume ya VyuoVikuu Tanzania kuingilia kati katika jitihada za kuupatia ufumbuzi. Mnamo tarehe 14 Novemba 2012 Tume iliunda timu ya wataalamu ambao walikwenda katika Chuo hicho na kufanya kazi kwa siku mbili kabla ya kuuanda ripoti yao. Ripoti ilibainisha maeneo mbalimbali yenye changamoto ambazo budi zipate majibu. Ripoti hiyo ilijadiliwa katika kikao cha Kamati ya Tume ya Ithibati na Chuo kupewa maelekezo katika maeneo mbalimbali na pia kutakiwa kuleta majibu katika masuala yaliyoonekana kuwa na uhitaji wa majibu. Maelekezo haya yaliwasilishwa Chuoni kwa barua ya tarehe 4 Desemba 2012 yenye kumbukumbu na TCU/A.40/69/Vol.IV/15 na kutakiwa kuleta majibu Tume kabla ya tarehe 30 Desemba 2012. Kabla majibu hayajawasilishwa mgogoro wa wafanyakazi ulianza na kufuatiwa na mgomo wa wanafunzi na hivyo tarehe 11 Desemba 2012 Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Juu walikwenda katika Chuo hicho ili kuonana hususan na wanafunzi pamoja na menejimenti. Kimsingi, kikao kilihusisha menejimenti na wanafunzi kwa kuwa suala la wafanyakazi lilikuwa limeshapatiwa muafaka wa jinsi ya kulitatua.
Kufuatia mawasiliano ya awali baina ya menejimenti ya Chuo na viongozi wa wafanyakazi kuhusu mishahara ya wafanyakazi ya mwezi wa Novemba 2012 pande zote zilikubaliana kwamba malipo hayo yawe yamefanyika ifikapo tarehe 14 Desemba 2012. Pia Chuo pamoja na waalimu wameafiki kufidia kipindi cha masomo ambacho kilipotea wakati wafanyakazi wanashughulikia mstakabali wa mishahara yao. Kufidia huko kutafanyika kati ya tarehe 7 Januari na 11 Februari 2013 ili kutokuathiri mipango mengine ya kimasomo ambayo tayari ilishapangwa kwa kipindi cha sasa hadi Januari 2013. Makubaliano haya yamewasilishwa TCU kwa barua ya Mkuu wa Chuo ya tarehe 10 Desemba 2012 yenye kumbukumbu Na. KIU/PR/Vol.30/11/12. Tume imeelekeza makubaliano haya yatekelezwe bila kukosa ifikapo tarehe 14 Desemba 2012. Ni matumaini ya Tume kwamba hali hii haitajitokeza tena ili shughuli za ufundishaji katika Chuo hicho ziende kulingana na ratiba ya kila semesta.
Ifuatayo ni taarifa ya yaliyojiri katika kikao baina na menejimenti, wanafunzi, Katibu Mtendaji wa Tume na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Juu.
2.         Kero za wanafunzi dhidi ya Menejimenti
Kwa upande wa wanafunzi jumla ya kero 21 ziliwasilishwa kimaandishi ili ziweze kupata ufumbuzi. Yafuatayo ni makubaliano na maelekezo katika kero hizo katika makundi yafuatayo.
2.1.   Ada na malipo mengine
Kumekuwa na hoja mbalimbali kuhusiana na karo pamoja na malipo mengine katika programu mbalimbali. Hoja hizi zimejikita katika ulipaji wa ada kwa dola za kimarekani na malipo mengine ambayo mchanganuo wake hauko bayana kwa maana ya kuitwa “other charges”. Tume ilishatolea maelekezo suala la kulipa ada kwa kutumia shilingi na siyo dola kwa Vyuo vyote kwa barua ya tarehe 15 Julai 2011 yenye kumbukumbu na TCU.10.1/Vol.V/266. Chuo cha KIU kilikumbushwa suala hili kupitia barua ya tarehe 16 Machi 2012 yenye kumbukumbu na. TCU/A.40/69/Vol.IV/8. Baada ya kutazama nyaraka mbalimbali zilizowasilishwa wanafunzi na menejimenti, Tume imebaini kwamba wanafunzi waliojiunga mwaka huu wamepata barua za kujiunga na Chuo ambazo zinaonyesha ada kwa fedha ya Tanzania isipokuwa kwa wanafunzi wanaotoka nje ya Tanzania ambao ada zao zilionyeshwa kwa dola wakati walipojiunga na chuo. Wanafunzi hawa wako katika miaka tofauti ya masomo na wengine wanakaribia kumaliza. Kwa mantiki hii, malipo ya ada kwa wanafunzi hawa yatazingatia viwango vilivyoonyeshwa wakati walipopata udahili. Nyongeza yoyote ya ada ni lazima iwe imejadiliwa na kuidhinishwa na Tume kabla haijaanza kutumika. Na kwa mantiki hii kiwango cha ada cha wanafunzi waliopata udahili wakati malipo yanafanyika kwa dola ya watalipa ada zao kulingana na kiwango cha ubadilishaji wa dola kwa wakati huo walipopata udahili na siyo vinginevyo.
Kwa upande wa suala la malipo mengine ambayo hayakuwa na ufafanuzi wa kutosha, malipo hayo yamesitishwa hadi yatakapopatiwa muafaka. Tume imeelekeza menejimenti kulifanyia kazi suala hili kwa kina kwa kushirikiana na viongozi wa wanafunzi ambao nao wametoa mapendekezo yao ya viwango katika maeneo mbalimbali.
2.2.   Prospectus
Kukosekana kwa Prospectus katika chuo limekuwa ni suala amabalo wanafunzi wamekuwa wakiliwasilisha kwenye menejimenti lakini ufumbuzi wake umeendelea kuwa kitendawili. Hali hii imesababisha wanafunzi kulalamika rasmi na kudai haki yao ya kupata Prospectus. Suala hili lilikuwa tayari limeshabainishwa na timu ya wataalamu iliyokwenda kukitembelea chuo tarehe  na hivyo Tume kwa barua yake ya tarehe 4 Desemba 2012 ilikielekeza chuo kuwapatia wanafunzi Prospectus hiyo kabla ya semesta hii kumalizika. Malekezo haya yanabakia palepale na pia chuo kimelekezwa kuwapatia wanafunzi nakala ya Prospectus hiyo kwa mfumo wa kielekroniki (e-copy) ifikapo tarehe 17 Desemba 2012 wakati uchapishaji wa nakala za kutosha kwa wanafunzi na wafanyakazi ukiendelea.
2.3.   Huduma za Maktaba
Kumekuwa na malalamiko kuhusu utoshelevu wa vitabu na maandiko mengine katika maktaba ya chuo. Baada ya majadiliano katika kikao Tume imeelekeza menejimenti na serikali ya wanafunzi ipitie maeneo mbalimbali yanayolalamikiwa na kuandaa tarifa ya pamoja ya mapungufu yaliyopo na mkakati wa kuyatatua. Taarifa hii iwe imekamilika ifikapo tarehe 28 Februari 2013 na nakala yake kuwasilishwa Tume. Mapungufu yote ya maktaba yawe yamefanyiwa kazi na kutatuliwa kabla ya kufikia mwisho wa mwaka wa elimu wa 2012/13. Serikali ya wanafunzi inatakiwa kulifuatilia kwa karibu suala hili na kutoa taarifa Tume endapo hakutakuwa na utekeleza kulingana na ratiba iliyokubaliwa.
2.4.   Huduma za Intenet
Kumekuwa na malalamiko pia kuhusu upatikanaji wa huduma ya internet. Mada ya mjadala katika suala hili ilionekana ni vyema menejimenti na viongozi wa wanafunzi wakaunda timu ya kulifuatilia kwa undani ili kugundua chanzo cha tatizo kwani Chuo tayari kilikuwa kimelipia huduma hiyo kwa kampuni inayohusika na huduma hiyo lakini upatikanaje wake umekuwa siyo wa kuridhisha. Chuo kimeanza mchakato wa kupata kampuni nyingine na pia kuangalia uwezekano wa kuunganishwa kwenye mkongo wa taifa. Timu itakayoundwa imeelekezwa kukamilisha kazi yake na kuwasilisha taarifa ifikapo tarehe 1 Januari 2013
2.5.   Mfumo wa mitihani ya marudio
Wanafunzi pia walipendekeza kuwa na mfumo wa supplementary examinations badala ya ule wa retake ambao unatumika sasa. Baada ya majadiliano ilibainika kwamba suala hili linahitaji utafiti zaidi kabla ya kuamua kama mfumo wa sasa ubadilike. Hii inatokana na kukubaliana kwamba kila mfumo una faida na hasara zake. Jambo la msingi ni kuhakikisha kila upande, yaani wanafunzi, waalimu na menejimenti wanaelewa kwa ufanisi mfumo unaotumika ikiwemo haki na majukumu yao katika utekelezaji wa mfumo huo. Chuo kimeelekezwa kuwasilisha taratibu zinazotumika sasa katika mfumo wa retake ili Tume nayo iweze kungalia taratibu hizo na kutoa ushauri wake ikiwa itabidi kufanya hivyo katika hili.
2.6.   Mfumo wa utafiti na maandiko kwa wanafunzi wa mwaka wa tatu
Ilionekana pia kwamba wanafunzi hawana picha kamili ya mfumo unaotumika katika masuala ya utafiti (research) na maandiko ya wanafunzi baada ya tafiti hizo. Kutokana na hali hii kujitokeza Tume ilielekeza menejimenti ya Chuo itoe ufafanuzi wa kutosha kwa wanafunzi wote kuhusu hili. Ufafanuzi huo uende sambamba na miongozo ambayo tayari imeshatolewa na tume kuhusiana na masuala ya mafunzo kwa vitendo katika ujumla wake. Kimsingi suala hili ni la utekelezaji wa mitaala iliyoidhinishwa kutumika katika Chuo hicho. Ni vyema basi pande zote zikaelewa kinachotarajiwa na mitaala hiyo na kukitekeleza huku miongozo mbalimbali iliyopo ikitiliwa maanani.
2.7.   Sifa za waalimu
Wanafunzi pia wamehoji sifa za baadhi ya waalimu. Baada ya majadiliamo Tume imelekeza ukaguzi ufanyike na menejimenti kuwasilisha Tume orodha na sifa za waalimu ambao wanafundisha masomo mbalimbali kwa hivi sasa. Orodha hii iandaliwe kwa kushirikisha viongozi wa wanafunzi na kitengo cha udhibiti wa ubora cha Chuo (KIU Quality Assurance Unit) na iwasilishwe Tume kabla ya tarehe 31 Desemba 2012. Orodha hii iambtane na nakala za vyeti vya waalimu wote.
2.8.   Serikali ya Wanafunzi na Katiba yake
Kutokana na majadiliano, imeonekana kwamba Serikali ya wanafunzi imekuwa haipati ushirikiano wa kutosha kutoka menejimenti. Pia serikali ya wanafunzi haina Katiba kama inavyoelekezwa na Sheria ya Vyuo Vikuu (Sura ya 346 ya Sheria za Tanzania) na Kanuni za Serikali za Wanafunzi za 2012 (GN.455/2012). Hili limekuwa sehemu ya mvutano baina ya serikali ya wanafunzi na menejimenti. Baada ya majadiliano, menejimenti imekubali kukaa na serikali ya wanafunzi na kukubaliana bajeti ya serikali ya wanafunzi kulingana na viwango vinavyolipwa na wanafunzi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za wanafunzi. Pia menejimenti imekubali kuwasaidia wanafunzi na wafanyakazi kukamilisha Katiba zao ili kukidhi matakwa ya Sheria ya Vyuo Vikuu kuhusu na masuala haya. Katiba hizi ziwe zimekamilishwa na kuwasilishwa Tume ifikapo tarehe 31 Januari 2013.
2.9.   Uwakilishi wa wanafunzi kwenye kamati na vyombo mbalimbali vya Chuo
Ilibainika katika majadiliano kwamba wanafunzi wamekuwa hawana uwakilishi wa kutosha katika baadhi ya kamati au vyombo vya Chuo ambavyo vinashughulikia masuala ya wanafunzi hususan ya kitaaluma. Hali hii ni kinyume na matarajio ya Sheria ya Vyuo Vikuu. Tume imeelekeza menejimenti ihakikishe wanafunzi wanapata uwakilishi katika kamati au vyombo hivyo na kuwasilisha Tume taarifa ya utekelezaji wa suala hili ifikapo tarehe 31 Desemba 2012.
2.10.                     Ufundishaji katika shahada za udaktari wa binadamu na uhandisi
Wanafunzi pia wametoa malalamiko yao kuhusu utoshelevu wa mafunzo wanayopata katika masomo ya shahada za udaktari wa binadamu na uhandisi. Baada ya kupokea malalamiko hayo Tume itaunda timu ya wataalamu itakayoshirikisha wataalamu wa Tanganyika Medical Association na Engineers Registration Board ili kufanya uchunguzi wa kina kuhusu malalamiko yaliyojitokeza na kutoa mapendekezo yake. Zoezi hili linatakiwa likamilike ifikapo tarehe 15 Januari 2013 na hatua stahiki zianze kuchukuliwa baada ya hapo. Sambamba na hili Tume inaandaa utaratibu wa kufanya tathmini ya masuala mbalimbali katika chuo hiki ili kujiridhisha kama masuala mbalimbali yanatekelezwa kwa mujibu wa sheria.
2.11.                     Wanafunzi wa kitanzania kufikiriwa kulipa ada ya chini kuliko wageni
Wanafunzi wa kitanzania walitoa ombi la kufikiriwa kulipa ada ya chini kuliko wageni. Tume iliwaarifu wanafunzi kwamba hili ni suala la kisera na kwamba litafikishwa kwenye Bodi ya Wadhamini wa Chuo. Lakini pia wanafunzi walielezwa kuhusu mchakato unaoendelea katika Jumuia ya Afrika Mashariki kuhusiana na masuala ya ada hususan mapendekezo kwamba wanafunzi wanaotoka nchi moja na kwenda kusoma nchi nyingine ndani ya jumua walipe viwango sawa na wazawa katika nchi hizo wanazokwenda kusoma. Pia serikali inafanyia kazi uandaaji wa mfumo wa kutambua ada ya mwanafunzi katika programu (student unit cost). Kwa mantiki hii suala hili linahitaji kufanyiwa kazi zaidi na vyombo vinavyohusika kabla ya muafaka kufikiwa na kutekelezwa.
2.12.                     Ratiba za vipindi pamoja na waalimu kuwa na vipindi vingi
Ilijitokeza pia kwamba baadhi ya vipindi hususan vya masomo ya Kompyuta vimekuwa na ratiba isiyokidhi mahitaji na kusababisha wanafunzi kulundikana katika darasa moja wakati madarasa yapo ambayo yangeweza kutumika katika masomo ya aina hiyo. Baada ya majadiliano Tume imeelekeza suala hili liangaliwe na menejimenti kwa kushirikiana na uongozi wa wanafunzi ili kulipatia ufumbuzi kabla ya semesta ya pili ya mwaka huu wa masomo kuanza mwezi Machi 2013.
2.13.                     Kitengo cha Udhibiti wa Ubora cha Chuo (KIU Quality Assurance Unit)
Wanafunzi, pamoja na kupongeza uwepo wa Kitengo cha Udhibiti wa Ubora cha Chuo, wamelalamikia ufanisi wa kitengo hicho na hivyo kupendekeza kiboreshwe zaidi ili kuweza kuleta tija iliyotarajiwa. Menejimenti pia imeridhia mapendekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na uongozi wa wanafunzi.
2.14.                     Mahafali
Kumetokea pia malalamiko kwa upande wa wanafunzi wanaohitimu katika fani mbalimbali kulazimishwa kulipa kiasi cha shilingi laki tatu na pia kutakiwa kwenda Uganda kwa ajili ya kushiriki katika mahafali. Suala hili lilikuwa katika masuala yaliyotolewa maelekezo natume katika barua yake ya tarehe 4 Desemba 2012 yenye kumbukumbu na. TCU/A.40/69/Vol.IV/15 . Tume imetoa maelekezo kwa Chuo kwamba mwanafunzi ana haki ya kupewa cheti, stashahada au shahada husika endapo amehitimu na kufaulu masomo yake, halazimiki kushiriki katika mahafali na hivyo halazimiki kulipa ada ya aina yoyote endapo hatashiriki katika mahafali hayo. Wakati kipindi cha mahafali kitakapowadia, chuo kinawajibika kutoa tangazo la kuwataarifu wanafunzi kuhusu mahafali hayo na wale watakaopenda kushiriki wanahiyari ya kufanya hivyo na kulipia ada ya majoho ambayo itapangwa na chuo. Pia chuo kimeelekezwa kuandaa utaratibu wa kufanya mahafali yake hapa Tanzania kuanzia mahafali ya wanafunzi watakaomaliza masomo yao katika mwaka wa masomo wa 2012/13. Mahafali hayo yataongozwa na taratibu za mahafali zinaotumika hapa nchini.
2.15.                     Mihadhara ya kielimu
Pia yalitolewa malalamiko ya wanafunzi kuhusu kufutwa kwa mihadhara katika semesta ya kwanza. Menejimenti ilieleza tatizo lililojitokeza hadi kusitisha mihadha na kuahidi kurudisha mihadhara hiyo kuanzia Januari 2013.
2.16.                     Matokeo kutolewa kwa wakati kupitia mtandao.
Wanafunzi pia walilitoa malalamiko yao kuhusu kucheleweshewa matokeo yao. Pia wakati mwingine matokeo halisi ya wanafunzi yamekuwa na utata. Kutokana na hali hii pande zote zilikubaliana kutoa matokeo kwa njia ya mtandao. Zoezi hili liwe limekamilika na mfumo kuanza kutumika katika semesta ya pili ya mwaka wa masomo wa 2012/13.
2.17.                     Utaratibu wa Wanafunzi wenye sifa za Diploma Kujiunga na Kozi mbalimbali za ngazi ya Shahada
Suala hili lilijadiliwa na kufikia muafaka kwamba taratibu zilizoainishwa katika miongozo ya Tume na ile ya Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE) zitumike. Mwanafunzi mwenye diploma inayotambuka na Tume au NACTE anaweza kujiunga na elimu ya juu ngazi ya Shahada kama ana sifa stahiki. Matokeo ya wanafunzi wote wenye Diploma sharti yawe yamewasilisha Tume au NACTE kwa wakati na kuingizwa kwenye mtandao (database) ambayo iko ili mwanafunzi husika aweze kuomba udahili kupitia CAS. Menejimenti pamoja na viongozi wa wanafunzi wamaekubaliana kulifanyia kazi hili kabla ya kuifika mwisho wa mwaka wa masomo wa 2012/13.
2.18.                     Malipo wakati wa kujiandikisha chuoni
Wanafunzi walitoa malalamiko yao kuhusu chuo kuwatoza ada wakati wa kujiandikisha (registration fee) na kwamba hili lisifanyike kwa sababu baadhi yao tayari walishalipa ada ya udahili kupitia CAS. Ufafanuzi ulitolewa kwamba ada ya udahili kupitia CAS ni tofauti na ada ya usajili chuoni na hivyo wanafunzi wanawajibika kulipa kulingana na viwango vilivyoidhinishwa na mamlaka za chuo.
3.         Hitimisho
Kutokana na kikao hiki Tume imebaini pia mapungufu katika mawasiliano baina ya wanafunzi, wafanyakazi na menejimenti hali ambayo imepelekea kwa pande husika kutoaminiana. Tume na Wizara zinashauri pande zote kuwa na mawasiliano yenye nia ya kutatua matatizo badala ya kuyalea na hivyo kuwa tatizo kubwa mbele ya safari. Hali kadhalika Tume imebaini mapungufu ya jinsi masuala mbalimbali yanavyoshughulikiwa hususan kukosekana kwa kumbukumbu za kimaandishi kuhusiana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza Chuoni na jinsi zinavyoshughulikiwa na pande zinazohusika. Kumbukumbu hizi huwa zinasaidia katika kijua kiini cha tatizo, jinsi lilivyoshughulikiwa, yaliyojitokeza na ni msaada wa aina gani unaweza kupatikana kutoka sehemu nyingine nje au ndani ya Chuo chenyewe. Ni vyema pande zote zikakumbuka kwamba “Chuo” ni vitu vingi vinavyofanya kazi kwa pamoja ikiwemo wamiliki, menejimenti, wafanyakazi na wanafunzi. Tume inashauri pande zote kufanya kazi zake kwa karibu na kuweka kumbukumbu za kimaandishi katika masuala mbalimbali.
Kikao pia kilibaini haja ya kuwa na mabadiliko katika mitizamo. Baadhi ya wanafunzi na wafanyakazi wanaamini kwamba Tume au Wizara ni lazima ifike Chuoni na kutatua matatizo yaliyopo hapo Chuoni (micro management). Kila Chuo kina vyombo mbalimbali vya kutatua changamoto mbalimbali kwa mujibu wa Sheria ya Vyuo Vikuu. Tume inapenda kuwaasa wananafunzi, wafanyakazi na menejimenti kufuata taratibu zilizopo ndani ya Chuo ili kutatua matatizo mbalimbali yanayojitokeza. Tume pia inashauri wadau wa elimu kuisoma kwa umakini Sheria ya Vyuo Vikuu ili kujua namna ya kutatua changamoto mbalimbali za elimu ya juu Vyuoni. Hili litasaidia sana katika kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali kwa wakati na kabla hazijawa kero.
Mwisho Tume inapenda kutoa wito kwa wanafunzi, wafanyakazi na menejimenti ya Chuo na Vyuo vingine nchini kuchukua hatua kurekebisha kasoro mbalimbali zinazojitokeza Vyuoni kwa wakati kabla madhara makubwa hayajajitokeza. Kinga ni bora kuliko tiba.
Imetolewa na
Katibu Mtendaji,
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania,
S.L.P. 6562, DAR ES SALAAM
Email: es@tcu.go.tz
Simu: +255 (0) 22 2772657

No comments: