Saturday, October 6, 2012

WAZIRI MEMBE AZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MGOGORO WA MPAKA KATIKA ZIWA NYASA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) (katikati) akifafanua kwa  Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu hoja zilizotolewa na Serikali ya Malawi za kujitoa katika mazungumzo kuhusu mgogoro uliopo kati  ya Tanzania na Malawi kuhusu Ziwa Nyasa. Wengine katika picha kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John M. Haule  na Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Irene Kasyanju.
Baadhi ya Waandishi wa Habari kutoka Vyombo na Mashirika mbalimbali ya Habari hapa nchini wakimsiliza kwa makini Mhe. Waziri Membe.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikino wa Kimataifa, Bw. John M. Haule (aliyesimama) wakati akimkaribisha Mhe. Waziri Membe kuzungumza na  Waandishi wa Habari (hawapo pichani).
Mmoja wa Wanahabari  Bw. Florian Kaijage akiuliza swali wakati wa mkutano wao na Mhe. Waziri Membe.
Mhe. Waziri Membe (waliokaa kushoto) akionesha kwa Waandishi wa Habari Ramani mpya ya Tanzania. Wengine katika picha (aliyekaa kulia) ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John M. Haule akifuatiwa na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Selasie Mayunga na Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria hapa Wizarani Balozi Irene Kasyanju.
Mhe. Waziri Membe akifafanua kwa Waandishi wa Habari kuwa mpaka katika ramani ya Tanzania umepita katikati ya Ziwa Nyasa na si ufukweni kama inavyodaiwa na Malawi.
Wageni waalikwa na baadhi ya waandishi wakimsikiliza Mhe. Waziri Membe.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) amewambia waandishi wa habari kuwa Malawi haiwezi kuipeleka Tanzania katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ili iamue mgogoro wa mpaka kwenye Ziwa Nyasa unaozozaniwa baina ya nchi hizi mbili.

Mhe. Membe alibainisha hayo mbele ya Waandishi wa Habari jijini Dar es Slaam siku ya Jumamosi tarehe 06 Oktoba, 2012. “Tanzania ni mjumbe wa ICJ lakini bado haijatambua Mamlaka ya Mahakama hiyo, hivyo Malawi haiwezi kuipeleka Tanzania ICJ isipokuwa Tanzania inaweza kuipeleka Malawi”, alisema Mhe. Membe.

Mhe. Waziri aliitolea wito Malawi irudi katika meza ya majadiliano na kuiomba Serikali ya nchi hiyo kutuma wawakilishi katika kikao walichokubaliana kufanyika Dar es Salaam kuanzia tarehe 07 - 10 Oktoba, 2012. 

Kikao hicho kinakusudia kupendekeza msuluhishi ambaye atakubalika na pande zote baada ya kubainika kuwa Tanzania na Malawi zenyewe hazitaweza kusuluhisha mzozo huo.

Mhe. Waziri aliwafahamisha waandishi kuwa alipokea kwa mshtuko taarifa kwamba Malawi haitashiriki katika kikao kilichopangwa kufanyika Dar es Salaam kwa hoja kuwa lazima Serikali ya Tanzania itoe maelezo ya kina kuhusu boti ya kijeshi iliyoonekana kufanya doria kwenye Ziwa Nyasa ambayo inasemekana kuwaletea hofu kubwa wakazi wa maeneo ya Ziwa kwa upande wa Malawi. 

Aidha, Malawi inataka kupatiwa maelezo kuhusu toleo jipya la Ramani ya Tanzania lililotolewa na Mamlaka za Tanzania ambayo inaonyesha mpaka baina ya nchi hizo mbili umepita katikati ya Ziwa Nyasa.

Akitolea ufafanuzi masuala hayo, Mhe. Membe alisema kuwa toleo hilo jipya lilikuwa na lengo la kuionyesha Mikoa mipya minne na Wilaya mpya 19 katika ramani ya nchi, na kuonyesha mpaka kupita katikati ya Ziwa, hilo si jambo jipya kwani ndivyo ramani ya nchi yetu ilivyokuwa katika matoleo yote manne yaliyotolewa na Serikali kabla na baada ya uhuru.

Kuhusu boti ya kijeshi kufanya doria kwenye Ziwa Nyasa, Mhe. Waziri alisema taarifa hizo sio sahihi, ila kinachofanyika ni doria ya kawaida ambayo inaendeshwa na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kuwasaka wavuvi haramu na wale wanaotumia zana za uvuvi zilizopigwa marufuku.

Mhe. Waziri aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Tanzania inapenda kuona mgogoro huo unamalizika katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne inayongozwa na Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete na kitendo cha Malawi kutishia kugomea majadiliano hakitarudisha nyuma dhamira ya Serikali.

Alisema Serikali imejipanga vyema kuhakikisha kuwa inakuwa na hoja za kisayansi na kisheria ili ishinde katika mgogoro huo. Moja ya mikakati ya Serikali imeunda Kamati tatu ambazo zimeshaanza kazi na kazi yao inaendelea vizuri. Kamati hizo moja inahusika na utafutaji wa nyaraka kuhusu Ziwa Nyasa, ya pili inahusika na masuala ya kisheria na ya tatu inahusika na masuala ya majadiliano.

Alidokeza kuwa katika kufuatilia kesi zilizohukumiwa na ICJ hakuna nchi iliyodai umiliki wa ziwa lote au mto uliopo mpakani baina ya nchi mbili ilishinda kesi. Hivyo, aliwataka Watanzania wasiwe na wasiwasi kwani Serikali yao itaibuka mshindi katika mgogoro huo.

Alihitimisha mazungumzo yake kwa kuwataka Wananchi wanaoishi kando ya Ziwa Nyasa kufanya shughuli zao kama kawaida pasi na kuhofia chochote kwani hakuna tishio la vita kabisa baina ya Tanzania na Malawi.

No comments: