Friday, October 24, 2014

Wanafunzi Taasisi ya Mufunzo Uanasheria kupata mikopo - Dkt. Migiro

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro akikagua Jengo la Mahakama ya Mafunzo katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania leo (Ijumaa, oktoba 24, 2014) jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu wake Mhe. Angellah Jasmine Kairuki na kulia ni Mkuu wa Taasisi hiyo Jaji Dkt. Gerald Ndika.
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro akikagua Jengo la Mahakama ya Mafunzo katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania leo (Ijumaa, oktoba 24, 2014) jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu wake Mhe. Angellah Jasmine Kairuki na kulia ni Mkufunzi wa Taasisi hiyo Bw. Goodluck Chuwa.
Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania Jaji Dkt. Gerald Ndika (kulia) akiongea na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro nje ya Jengo la Mahakama ya Mafunzo katika Taasisi hiyo leo (Ijumaa, oktoba 24, 2014) jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu wake Mhe. Angellah Jasmine Kairuki na kulia ni Mkufunzi wa Taasisi hiyo Bw. Goodluck Chuwa. (Picha na Martha Komba, Wizara ya Katiba na Sheria).

Serikali inakamilisha taratibu za kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria unaolenga kurekebisha Sheria ya Bodi ya Mikopo ili kuwawezesha wanafunzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) kupata mikopo kwa ajili ya mafunzo yao.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Asha-Rose Migiro amewaambia wanafunzi wa taasisi hiyo jijini Dar es Salaam leo (Ijumaa, Oktoba 24, 2014) kuwa lengo la Serikali kukamilisha mchakato huo katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia sasa.

"Nafahamu kuna changamoto ya baadhi yenu kukosa mikopo, nimeambiwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Uendeshaji wa Taasisi hii Bw. George Masaju kuwa taratibu za kurekebisha Sheria ya Bodi ya Mikopo umeanza ili wanafunzi wa taasisi wapate mikopo,” amesema Dkt. Migiro.

Waziri Migiro, ambaye aliongozana na Naibu wake Mhe. Angellah Jasmine Kairuki na Bw. Masaju, amezungumza na wanafunzi wa Taasisi hiyo iliyopo nyuma ya Jengo la Mawasiliano (Mawasiliano Towers) jijini Dar es Salaam.

Katika ziara yake ambayo ni ya kwanza tangu ateuliwe na Mhe. Rais kuiongoza Wizara ya Katiba na Sheria, Waziri Migiro alikagua ujenzi wa majengo ya kudumu ya taasisi hiyo pamoja na kukutana na watumishi na wanafunzi ili kubadilishana mawazo.

Ujenzi wa majengo hayo ya kisasa ya kudumu, ulianza Mwezi Novemba, 2010 na kukamilika Agosti, 2012 na umegharimu zaidi ya Tshs 16.1/- Bilioni na umefanywa na Serikali kupitia Programu ya Maboresho ya Sekta ya Sheria (LSRP) iliyokuwa inatekelezwa chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.

Ujenzi huo umejumuisha Mahakama ya Mafunzo, Maktaba, Madarasa, Jengo la Utawala, Ukumbi wa shughuli mbalimbali na nyumba za watumishi.

Katika mazungumzo yake na wanafunzi hao, Dkt. Migiro pia aliwakumbusha wanafunzi hao kujiandaa kutoa huduma bora kwa jamii pale wanapohitimu kwa kuzingatia kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kuendesha mafunzo hayo.

“Mkumbuke ule wito wa Mwalimu Nyerere kuwa nyie ni kama yule mtu aliyetumwa na kijiji chenye njaa kwenda kutafuta chakula ili arudi kuwasaida wanakijiji wenzake,” alisema Waziri Migiro na kufafanua kuwa kuna wananchi wengi wanaohitaji huduma za kisheria nchini ambao wanawasubiri.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt. Jaji Gerald Ndika alimweleza Waziri Migiro kuwa tangu kuanza rasmi kwa mafunzo katika Taasisi hiyo mwezi Machi mwaka 2008 hadi Julai mwaka huu, jumla ya wanafunzi 4,755 wamedahiliwa katika makundi tofauti na kati yao, wanafunzi 1,715 wamefaulu mafunzo na kupata cheti cha Stashahada ya Uzamili katika Utalaam wa Sheria (Post-Graduate Diploma in Legal Practice).

“Tunafurahi kuwa katika wanafunzi wetu 1,715 waliofaulu tangu kuanzishwa kwa Taasisi hii, wahitimu 1,540 wameorodheshwa kuwa Mawakili wa Kujitegemea baada ya kukamilisha taratbu na waliobaki wanaendelea kukamilisha taratibu,” alisema Jaji Dkt. Ndika.

Pamoja na mafanikio hayo, Mkuu huyo wa Taasisi amesema kumekuwa na malalamiko kuhusu ufaulu mdogo hususan katika hatua ya kwanza (first sitting) na kufafanua kuwa Bodi ya Uendeshaji chini ya Uenyekiti wa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeunda Kamati Maalum ili kufanya utafiti kwa lengo la kubaini kiini cha matokeo hayo.

“Bodi imeunda Kamati Maalum inayoongozwa na Prof. Bonaventure Rutinwa na inajumuisha wadau wengine kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mahakama ya Tanzania, Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE) na tunatarajia taarifa yake itakuwa tayari ifikapo mwanzoni mwa mwezi ujao wa Novemba, 2014” amefafanua Mkuu huyo wa Taasisi.

Akiongea katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Uendeshaji na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju amesema lengo la kuanzishwa kwa Taasisi hiyo ni kuwanoa wahitimu wa shahada ya kwanza ya sheria ili kukabiliana na changamoto za sasa hususan katika taaluma ya sheria.

“Hapa wanafundishwa vitu vingi ikiwemo namna ya kujadiliana katika mikataba na mengineyo mengi ambayo kwa sasa ni changamoto,” amesema Bw. Masaju ambaye aliongozana na Wajumbe wa Bodi wakiwemo Mawakili Bw. Charles Rwechungura na Bi. Aisha Bade.

WARSHA YA KUHUSU AMANI NA USALAMA BARANI AFRIKA YAHITIMISHWA JIJINI ARUSHA

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Mnasa Nyerembe akitoa hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Magese Mulongo ya kufunga Warsha ya siku tatu kuhusu Amani na Usalama Barani Afrika iliyoandaliwa na Umoja wa Afrika na kufanyika katika Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha.
Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Afrika na nchini Ethiopia, Mhe. Naimi Aziz kwa pamoja na Balozi wa Ethiopia katika Umoja wa Afrika Mhe. Konjit Sinegiorgis wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Nyerembe (hayupo pichani) alipokuwa akifunga Warsha hiyo ya Amani na Usalama Barani Afrika iliyowakutanisha Mabalozi, Wataalam wa masuala ya Amani na Wasuluhishi.
Sehemu nyingine ya Wajumbe wakimsikiliza Mhe. Nyerembe (hayupo pichani) akiwemo Rais Mstaafu wa Cape Verde, Mhe. Pedro Pires (kulia)
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Zuhura Bundala akifuatilia kwa makini hotuba ya kufunga warsha ya amani na usalama iliyokuwa ikitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Nyerembe (hayupo pichani).
Wajumbe waliokuwepo wakati wa kufunga warsha ya amani na usalama.
Kamishna wa Amani na Usalama katika Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Balozi Smail Chergui akitoa neno la shukrani kwa Uongozi wa Mkoa wa Arusha na kwa Serikali ya Tanzania kwa ujumla kwa kuwa mwenyeji wa warsha hiyo ya siku tatu ambapo wajumbe wamenufaika na masuala yote yalijadiliwa pamoja na huduma nzuri.
Balozi Mstaafu, Prof. Joram Biswaro (kulia) akifuatialia hotuba  ya Balozi Chergui (hayupo pichani)
Bi. Shella Mbita, Mtoto wa Balozi Hashim Mbita nae pia alikuwa mmoja wa wajumbe waliohudhuria warsha ya amani na usalama jijini Arusha (Picha zote na Rosemary Malale) ===============================================
Na.  Ally Kondo, Arusha
Warsha ya siku tatu kuhusu Amani na Usalama Barani Afrika iliyoandaliwa na Umoja wa Afrika (AU) imehitimishwa jijini Arusha siku ya Alhamisi tarehe 23 Oktoba 2014. Warsha hiyo ambayo kaulimbiu yake ilikuwa “Silaha zisitumike kuuwa watu Barani Afrika ifikapo mwaka 2020” ilimalizika kwa wajumbe kutoa Rasimu ya Tamko la Arusha (Arusha Declaration). 
Katika Tamko hilo, kumebainishwa asili ya migogoro inayohusu nchi moja au baina ya nchi na nchi nyingine, vitu vinavyochochea migogoro na ukosefu wa utulivu Barani Afrika, wanaochochea na kudhamini migogoro pamoja na athari za maendeleo ya dunia kwa Bara la Afrika.
Aidha, Tamko hilo limeainisha juhudi zinazofanywa katika kukabiliana na vitendo vya siasa kali, uhalifu wa kimataifa na athari za mabadiliko ya tabianchi katika amani na usalama.
Tamko limebainisha pia kuwa migogoro mingi katika nchi za Afrika inasababishwa na ukosefu wa utawala bora katika Serikali, uwajibikaji, uwazi, uongozi shirikishi pamoja na kushindwa kutatua changamoto za umasikini na ukosefu wa usawa.
Kwa mujibu wa Tamko hilo, wajumbe kwa kauli moja walikubaliana na hoja kuwa ili nchi za Afrika ziondokane na matatizo hayo, hazina budi kutekeleza miongozo na maamuzi yanayotolewa na AU kuhusu amani, usalama na uongozi. Walisema kuwa maamuzi hayo yanatoa dira nzuri ya namna ya kukabiliana na changamoto za usalama Barani Afrika, isipokuwa nchi za Afrika hazina utamaduni wa kuyatekeleza.
Hivyo, wajumbe walisisitiza umuhimu kwa nchi wanachama wa AU kutekeleza maamuzi yote yanayofanywa na kuridhiwa na AU, Jumuiya za Kikanda na wadau wengine.
Aidha, walitoa wito kwa nchi wanachama wa AU, Kamisheni ya AU, Jumuiya za Kikanda, Baraza la Amani na Usalama la AU na wadau wengine kulipa kipaumbele suala la kuweka utaratibu wa kufanya tathmini ya utekelezaji wa maamuzi hayo.
Sanjari na hayo, wajumbe walipongeza mabadiliko chanya yanayotokea Barani Afrika ikiwa ni pamoja na kupungua kwa migogoro ya kutumia silaha, kuongezeka kwa chaguzi za kidemokrasia, kukua kwa uchumi na ongezeko la kasi ya kupambana na vitendo vya ufisadi katika nchi nyingi za Afrika.
Licha ya maboresho hayo, wajumbe walielezea wasiwasi wao   kuhusu tishio linalotokana na changamoto mpya katika amani na usalama wa Bara la Afrika. Walihimiza umuhimu wa kutumia mbinu za kibunifu kukabiliana na changamoto hizo ambazo ni; uhalifu wa kimataifa kama vile ugaidi, uharamia, biashara haramu ya binadamu, biashara ya silaha na dawa za kulevya na biashara ya fedha haramu.
Wakati wa kufunga warsha hiyo ambayo iliwakutanisha Mabalozi, wasuluhishi, wajumbe maalum, wawakilishi wa Jumuiya za Kimataifa na wasomi mbalimbali, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Mnasa Nyerembe alielezea matumani yake kuwa, washiriki walipata fursa nzuri ya kujadili kwa kina chanzo cha migogoro Barani Afrika na kupendekeza njia muafaka za kukabiliana nayo. Alisisitiza umuhimu wa mapendekezo hayo kuingizwa katika sera za kitaifa, kikanda na kimataifa ili yaweze kuwa na manufaa.
-Mwisho-

WIZARA YA MALIASILI YABARIKI KUANZISHWA KWA MFUKO WA KULINDA MLIMA KILIMANJARO NA MLIMA MERU

Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu akizungumza wakati wa kikao kilicho shirikisha Kamati ya Bunge ya Ardhi,Maliasili na Mazingira,Wabunge katika majimbo ya mikoa ya Arusha na Kilimanjaro,Wakuu wa wilaya zinazopakana na mlima Kilimanjaro na mlima Meru,TANAPA na Idara ya Misitu,(kulia)ni kaimu mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro ,Ibrahim Msengi.
Naibu waziri wa TAMISEMI ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Siha ,akichangia wakati wa kikao cha kuanzishwa kwa mchakato wa uanzishwaji mfumo wa kiikolojia wa mlima Kilimanjaro na Mlima Meru ambao utalinda milima yote miwili.
Makamau mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Ardhi,Maliasili na Mazingira,Abdulkarim Shah akizungumza katika kikao hicho kimetokana na wabunge wa mkoa wa Kilimanjaro kuomba kuanzishwa kwa mfuko wa kulinda mlima Kilimanjaro.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho kilichofanyika katika Hotel ya Sal salnero wakifuatilia michango mbalimbali iliyokuwa ikitolewa katika kikao hicho.
Mbunge wa Jimbo la Vunjo ,Agustino Mrema akichangia hoja katika kikao hicho.
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki ,Joshua Nassar akichangia katika uanzishwaji wa mfuko huo.
Katibu wa Mbunge wa Moshi mjini,Basil Lema akichangia jambo katika kikao hicho akiwa amemwakilisha Mbunge Philemoni Ndesamburo.
Baadhi ya washiriki katika kikao hicho.
Kaimu mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Moshi Ibrahimu Msengi akichangia katika uanzishwaji wa mfuko wa kulinda mlima Kilimanjaro na mlima Meru.
Mkuu wa wilaya ya Rombo Elinasi Palangyo akizungumza katika kikao hicho,wilaya ya Rombo ni moja ya wilaya ambazo zinapakana na mlima Kilimanjaro.
Mkuu wa wilaya ya Siha Dk ,Charles Mlingwa akizungumza katika kikao hicho,wilaya ya Siha ni moja ya wilaya ambazo zinapakana na mlima Kilimanjaro.
Mkuu wa wilaya ya Hai,Novatus Makunga akizungumza katika kikao hicho,wilaya ya Hai ni moja ya wilaya ambazo zinapakana na mlima Kilimanjaro.
Mbunge wa Arumeru Mashariki ,Joshua Nassar,akiwa pamoja na Mbunge Suzan Kiwanga na katibu wa Mbunge wa jimbo la Moshi mjini ,Basil Lema.
Mkurugenzi wa Wakala wa Misitu (TFS) Juma Mgoo akieleza namna ambavyo mfuko huo utasaidia katika kuimarisha ulinzi wa rasilimali ya misitu.
Mhifadhi mkuu wa hifadhi ya Arusha(ANAPA) Betrita Loibook akichangia katika kikao hicho.
Mhifadhi ,idara ya ujirani mwema ,Theodora Batiho akichangia jambo katika kikao hicho.
Washiriki wa kikao hicho wakifuatilia majadiliano.
Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu akihitimisha kikao cha majadiliano juu ya kuanzishwa kwa mfuko wa kulinda mlima Kilimanjaro na Mlima Meru.
Na Dixon Busagaga wa Globu ya jamii kanda ya kaskazini.

Mama Tunu Pinda Mgeni rasmi katika Mkutano wa akina mama wa Kitanzania waishio Uingereza

Mama Tunu Pinda alikuwa Mgeni rasmi katika Mkutano cha akina mama wa Kitanzania waishio Uingereza , Kilichoandaliwa na Kikundi cha Umoja wa Wanawake kiitwacho Tanzania Women Association UK (TAWA UK).

Mama Tunu Pinda alihudhuria Mkutano huo kwa mualiko wa mwenyeji wake Mrs Joyce Kallaghe Mke wa Balozi wa Tanzania Uk, Peter Kallaghe.

Mtoa mada aliyeongozana na Mama Tunu , alikuwa ni Mama Anna Matinde , mwanamke Mjasiriamali mahiri na aliyebobea ambaye ana kofia mbalimbali za Uwakilishi wa Wanamke na kibiashara katika taasisi tofauti za sekta Binafsi ikiwemo na kuwa Mkurugenzi wa Tanzania Women Chamber of Commerce.

Mama Matinde licha ya kuwatia moyo akina mama na kuwahamasisha wajikite kwenye biashara Binafsi na kubadilishana Ujuzi kutoka Tanzania na Uingereza, vilevile aliwapa somo la Uwekezaji na pamoja na kuainisha Fursa nyingi za kuwekeza zilizopo nyumbani Tanzania. Baada ya kikao wanawake wengi walioyeshwa kuridhika na ushauri wa mama Matinde.

Mgeni rasmi Mama Tunu Pinda aliwahimiza akina mama vilevile wasisahau kuwekeza nyumbani hat kama wako nje ya Nchi, na kuwahakikishia kwamba sasa hivi mwanamke wa Kitanzania anaelekea kuwa na haki sawa za umiliki ardhi na mali kama ilivyoainishwa katika Katiba Iliyopendekezwa endapo itapita kwa wananchi, Hivyo aliwasihi akina mama hao wasiwe na woga wa kuwa na mali kutokana na baadhi ya mila kwani Katiba itawalinda.

Mkutano huu uliofana ulimalizika kwa ahadi ya Uongozi wa TAWA UK walioratibu Kikao hiki kuwa watafanya Mkutano Mkubwa Zaidi wa Uwekezaji na Fursa kwa Akina Mama Muda si mrefu.
Mgeni rasmi Mama Tunu Pinda akisalimiana na Mwenyekiti wa TAWA UK Bi Mariam Kilumanga , alipowasili katika Balozi zaTanzania Uingereza. Nyuma ya Mama Tunu ni Mwenyeji wake Mama Joyce Kallaghe na pembeni Afisa Mkuu Kiongozi wa Ubalozi Caroline Chipeta.
Mama Tunu Pinda akiweka sahihi kwenye kitabu cha wageni Ubalozini , huku mama Kalaghe akiangalia.
Mama Tunu kati akiwa na Mwenyeji wake kushoto Mama Joyce Kallaghe na kulia Mtoa Mada ya fursa na Uwekezaji aliyeambatana na mama Tunu Tanzania Women Chamber of Commerce Mama Anna Matinde.
Baadhi ay Wanawake waliohudhuria wakimkaribisha Mama Tunu na Mama Matinde.
Katibu wa Tanzania Women Association Uk (TAWA UK ) Bi Mariam Mungula akiongea machache kuwakaribisha wageni.
Mama Joyce Kallaghe , ambaye pia ni Mlezi wa TAWA UK , akifungua Mkutano rasmi na kuwatambulisha wageni wake.
Mama Anna Matinde akiongea na akina mama mambp mengi ya kusisimua na kuhamasisha aliyokuwa nayo kuhusu Uwekezaji nyumbani Tanzania.
Baadhi ya akina mama wenye shauku kubwa wakimsikiliza mama Matinde kwa makini.
Mama Tunu Pinda aliposimama kuongea na akina mama na kufunga Mkutano.
baadhi ya Wakina mama washiriki wakipata picha na wageni rasmi.
Maafisa wa Ubalozi wanawake katika Picha ya upendeleo na wageni wao.
Wageni na Uongozi wa TAWA UK walioandaa Mkutano huo.

Fly Dubai yazindua rasmi safari zake nchini

Na Reginald Philip

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mhe. Samia Suluhu (Mb.) ameupongeza Uongozi wa Shirika la Flydubai la Dubai kwa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Dubai na Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mwanza na Zanzibar kwa gharama nafuu.

Akizindua huduma hiyo kwa niaba ya Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal, jijini Dar es Salaam, Jumatano tarehe 22 Oktoba, 2014, Mhe. Suluhu alimwambia Makamu Mkuu wa Shirika la Flydubai, Bw. Sudhir Sreedharan, kuwa kuja kwao Tanzania kutafungua njia za kiuchumi na nchi nyingine za Kiafrika.

Alisema kuanzishwa kwa huduma hiyo pia kutatoa fursa ya ajira kwa watanzania, na akawahimiza wananchi kuchangamkia fursa hizo. Shirika hilo, ambalo ndege zake zina bei nafuu- kutokea Dar es salaam kwenda dubai na kurudi (DSM-DXD-DSM) kwa bei ya dola za Kimarekani 399 tu (budget Airline) litafanya safari zake kati ya Dar es salaam, KIA na Zanzibar. Baadae, shirika hilo litaongeza safari zao kutokea Mbeya kuelekea Dubail.

Katika hafla hiyo ya uzinduzi iliyoandaliwa na shirika la Flydubai kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere, Mhe. Suluhu aliipongeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kwa kuratibu uanzishwaji wa safari za bei nafuu kupitia kwa Balozi Mdogo wa Tanzania nchini Dubai, Mhe. Omar Mjenga, ambaye alihudhuria hafla ya uzinduzi.

Baada ya Dar es Salaam, hafla nyingine ya uzinduzi ilifanyika Zanzibar baadaye hiyo jana, Mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi. 
Ndege ya Shirika la Ndege la Fly Dubai ikiwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere ikiwa katika uzinduzi wake uliofanywa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mhe. Samia Suluhu, Ndege hiyo itafanya safari zake za moja kwa moja kutokea Dubai mpaka Dar es Salaa, Kilimanjaro, Mwanza na Zanzibar.
Watatu kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mhe. Samia Suluhu, na wapili kutoka kushoto ni Balozi mdogo wa Tanzania, Dubai Mhe. Omar Mjenga, wakwanza kushoto ni Spika wa Bunge Mstaafu Mhe. Pius Msekwa na wakwanza kulia ni Bajeti meneja wa Fly Dubai wa nchini Tanzania Bw. Riyaz Jamal wakiitazwa Ndege ya Fly Dubai ilipokuwa inawasili.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mhe. Samia Suluhu akisalimiana na Makamu wa Mkuu wa kampuni hiyo, Sudhir Screedharan mara baada ya kuwasili na Ndege hiyo katikati ni Bajeti meneja wa Fly Dubai Tanzania Bw. Riyaz Jamal.
Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati Balozi Simba Yahaya akisalimiana na Bw. Screedharan
Balozi Mdogo wa Tanzania, Dubai Mhe. Omar Mjenga akisalimiana na Bw. Screedharan
Mhe. Suluhu akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Ndege hiyo itakayoanzisha safari zake moja kwa moja kutokea Dar es salaam mpaka Dubai
Wakwanza kushoto ni Bw. Shabani Baraza akimwakilisha Balozi wa Tanzania UAE, wa pili kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Kituo cha Biashara katika Ubalozi Mdogo wa Tanzania, Dubai, Bw. Cleophas Luhumbika Watatu kutoka Kushoto ni Afisa Mambo ya Nje Bw. Hangi Mgaka pamoja na wajumbe wengine wakimsikiliza Mhe. Suluhu
Makamu Mkuu Bw. Screedhana (wakwanza kulia), wa kwanza kushoto Balozi Mdogo Mhe. Mjenga na (katikati) ni Bw. Riyaz Jamal wakimsikiliza Mhe. Waziri alipokuwa akizungumza.
Makamu wa Mkuu wa kampuni hiyo, Sudhir Screedharan akizungumza katika hafla hiyo mara baada ya uzinduzi wa safari za Ndege ya Shirika lake la Fly Dubai, alisema safari za ndege zao zinatumia ndege mpya za kisasa aina ya Boeing zipatazo 100.
Wajumbe mbalimbali wakimsikiliza Bw. Screedharan alipokuwa akizungumza
Balozi Mdogo wa Tanzania, Dubai akizungumza na kuushukuru uongozi wa Fly Dubai kwakukubali kuanzisha safari za moja kwa moja kutokea Dar es salaam mpaka dubai, Mhe. Mjenga alisema kwa kuanza kwa safari ya ndege hiyo inategemewa kuongezeka kwa idadi ya Watalii nchini kutokea Milioni 1 kwa mwaka mpaka Milioni 2, fursa za ajira kwa Watanzania.
Sehemu ya wajumbe wengine wakimsikiliza Balozi Mdogo.
Picha ya pamoja
Picha na Reginald Philip