Wednesday, March 28, 2018

MAANDALIZI YA MFUMO WA PAMOJA WA KIELEKTRONIKI WA UONDOSHAJI SHEHENA YAANZA



Na Veronica Kazimoto,Dar es Salaam,
Serikali imeanza maadalizi ya kutengeneza Mfumo wa Pamoja wa Kielektroniki wa Uondoshaji Shehena Bandarini, Viwanja vya Ndege vya Kimataifa na Mipakani kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na ufanisi.

Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Wakuu wa Taasisi za Serikali wanaohusika na udhibiti wa mizigo katika maeneo hayo na wadau mbalimbali wa sekta binafsi, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere amesema lengo la kuwashirikisha wakuu hao ni kujenga uelewa wa pamoja wa utekelezaji wa mfumo huo.

“Uwepo wenu katika mkutano huu ni muhimu sana kwasababu mtaweza kupitia mahitaji yote ya mfumo yaliyoandaliwa na watalaamu wetu ikiwa ni pamoja na maeneo ya kisheria, kiufundi na kibiashara ili muweze kuuboresha zaidi”, alisema Kichere.

Kichere alieleza kuwa, uwepo wa wakuu hao na wadau wa sekta binafsi katika mkutano huo ni kiashiria cha kuunga mkono adhma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga mazingira bora ya kufanya biashara ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Kamishna huyo Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania aliongeza kuwa, Serikali imelenga kuwawezesha wadau wote wanaohusika na biashara za kimataifa na usafirishaji wa mizigo kutumia Mfumo wa Pamoja wa Kielektroniki wa Uondoshaji Shehena kwa lengo la kuwezesha uwasilishaji wa nyaraka mahali pamoja ili wadau wote waweze kushughulikia nyaraka hizo kwa wakati.

Naye Mratibu wa Mfumo wa Uondoshaji Shehena kutoka TRA Felix Tinka amezitaja faida za mfumo huo  kuwa ni pamoja na kurahisisha na kuwezesha biashara, kuongeza ufanisi wa matumizi bora ya rasilimali na kuongeza uhiari wa ulipaji ushuru na tozo mbalimbali kwa waingizaji na waondoshaji wa mizigo.

“Mfumo huu una faida nyingi, mbali na hizo nilizozitaja awali, pia kuna kuimarisha usalama, kuimarisha uadilifu na uwazi katika utendaji kazi, kupunguza biashara haramu, kupunguza gharama, kupunguza muda wa uondoshaji mizigo katika vituo vya forodha pamoja na kurahisisha ufuatiliaji wa mizigo kwa wakati”, Alisema Tinka.

Utekelezaji wa Mfumo wa Pamoja wa Kielektroniki wa Uondoshaji Shehena Bandarini, Viwanja vya Ndege vya Kimataifa na Mipakani umegawanyika katika maeneo makuu matano ambayo ni eneo la usimamizi wa mapato, uwezeshaji wa usafiri na uchukuzi, utekelezaji wa sera na biashara, pamoja na usimamizi wa afya na usalama wa umma, usalama wa uchumi pamoja na ugawaji.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Wakuu wa Taasisi za Serikali wanaohusika na udhibiti wa mizigo Bandarini, Viwanja vya Ndege vya Kimataifa na Mipakani pamoja na wadau mbalimbali wa sekta binafsi kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na ufanisi. Pamoja nae ni Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Mussa Shilla. (Imeandaliwa na Robert Okanda Blogs)
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga  (TCAA), Hamza Johari akitoa mchango wake wakati wa mkutano huo. 
Mwakilishi wa Mkemia Mkuu wa Serikali Daniel Ndiyo akichangia hoja leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Wakuu wa Taasisi za Serikali wanaohusika na udhibiti wa mizigo Bandarini, Viwanja vya Ndege vya Kimataifa na Mipakani pamoja na wadau mbalimbali wa sekta binafsi kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na ufanisi.
Katibu Mtendaji wa Chama cha Wakala wa Meli Tanzania (TASAA), Abel Urono akitoa mchango wake katika mkutno huo. 
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere (kulia) akibadilishana mawazo na Nibu Kamishna wa TRA, Zanzibar Mcha Hassan baada ya kuhudhuria mkutano huo. 
Mshauri wa Tehama, Abdulrahman Mbamba akitoa mada kwa washiriki wa Mkutano huo. 
Sehemu ya washiriki wa mkutano huo wakifuatilia mijadala kwenye mkutano huo. 

DK. KIGWANGALLA APOKEA WAWEKEZAJI KUTOKA CHINA WANAOTAKA KUWEKEZA KATIKA SEKTA YA UTALII

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwa kwenye picha ya pamoja na wawekezaji wa Kampuni ya Kimataifa ya Tibet Dexin Financia Leasing kutoka nchini China ofisini kwake mjini Dodoma jana wakati kampuni hiyo ilipowasilisha mpango wake wa kuwekeza apa nchini katika ujenzi wa  mahoteli na huduma za utalii zenye ladha na mandhari ya kichina.

Na Hamza Temba - WMU-Dodoma
...........................................................................
Kufuatia jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kutafuta wawekezaji wa Kimataifa kwa ajili ya kuwekeza katika sekta utalii hapa nchini, Kampuni ya Kimataifa ya Tibet Dexin Financia Leasing kutoka nchini China imejitokeza kwa lengo la kuwekeza katika utoaji wa huduma za kitalii zenye ladha na mandhari ya Kichina.

Mwenyekiti wa Kampuni hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Tony, amesema kampuni hiyo imepanga kujenga hoteli za kitalii za kichina katika mji wa Karatu jijini Arusha na Serengeti mkoani Mara.

Akizungumza na Waziri wa Maliasil na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ofisini kwake mjini hapa jana kwa ajili ya kutambulisha mradi huo, Tony alisema mradi huo ni mahsusi kwa ajili ya kutoa huduma kwa watalii wa China wanaotembelea Tanzania.

Alisema kupitia mradi huo jumla ya magari 500 ya safari  za utalii yatanunuliwa (Safari Cars) kwa ajili ya kutoa huduma kwa watalii hao wakati wa kutembelea maeneo ya vivutio hapa nchini.

Pamoja na magari hayo alisema kampuni hiyo pia imepanga kuanzisha safari za moja kwa moja za ndege kutoka China hadi Tanzania ili kupunguza muda wa usafiri na gharama.

"Kupitia mradi huu, tunategemea kuhudumia watalii 200,000 kwa mwaka kutoka nchini China na kutengeneza ajira zaidi ya 200 kwa Watanzania" alisema Tony.

Alisema kwa sasa ni watalii 35,000 tu kutoka China wanaotembelea Tanzania kwa mwaka, na kwamba kupitia mradi huo idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla alisema mradi huo umekuja wakati muafaka  wakati huu Serikali kupitia Wizara yake imeshaweka mikakati mahususi ya kupanua wigo wa soko la utalii nchini China.

Alisema miongoni mwa mikakati hiyo inayolenga kuvutia watalii zaidi ya 200,000 kwa mwaka katika kipindi cha muda mfupi wa miaka mitatu, ni kuwakaribisha wachina wenyewe kuja kuwekeza kwenye mahoteli na huduma zenye ladha na mandhari ya kikwao. Mataifa mengine ni Israel, Urusi na Oman.

Alisema kwa sasa ni idadi ndogo tu ya watalii wa China wanaotembelea Tanzania ukilinganisha na ukubwa wa soko la nchi hiyo.

Aliahidi kuwapa ushirikiano wawekezaji hao ikiwa ni pamoja na kuwapa maeneo kwa ajili ujenzi wa hoteli hizo za kitalii ndani ya maeneo ya hifadhi ili kuwezesha ongezeko la watalii kutoka nchini humo.

"Kwa yale maeneo mtakayohitaji ambayo yapo nje na maeneo yetu ya hifadhi tunayoyasimamia, tutawasiliana na mamlaka husika ili muweze kuapatiwa maeneo ya kuanzisha uwekezaji huo muhimu kwa taifa" alisema Dk. Kigwangalla.

Aliwataka pia wawekezaji hao kupitia taratibu zote za kuwekeza hapa nchini ikiwa ni pamoja na kujisajili katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Kusajili kampuni ya utalii hapa nchini na kuwasilisha andiko la mradi na namna ya utekelezaji wake.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wawekezaji wa Kampuni ya Kimataifa ya Tibet Dexin Financia Leasing kutoka nchini China ofisini kwake mjini Dodoma jana wakati kampuni hiyo ilipowasilisha mpango wake wa kuwekeza apa nchini katika ujenzi wa  mahoteli na huduma za utalii zenye ladha na mandhari ya kichina.
 Wawekezaji wa Kampuni ya Kimataifa ya Tibet Dexin Financia Leasing kutoka nchini China wakiwa kwenye mazungumzo na Waziri Kigwangalla ofisini kwake mjini Dodoma.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akimkabidhi flash yenye picha za wanyamapori wa Tanzania Mwenyekiti wa Kampuni ya Kimataifa ya Tibet Dexin Financia Leasing, aliyefahamika kwa jina moja la Tony kutoka nchini China ofisini kwake mjini Dodoma jana wakati kampuni hiyo ilipowasilisha mpango wake wa kuwekeza hapa nchini katika ujenzi wa  mahoteli na huduma za utalii zenye ladha na mandhari ya kichina.
 Waziri Kigwangalla akiendelea na mazungumzo na wakezaji hao.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wawekezaji wa Kampuni ya Kimataifa ya Tibet Dexin Financia Leasing kutoka nchini China ofisini kwake mjini Dodoma jana wakati kampuni hiyo ilipowasilisha mpango wake wa kuwekeza apa nchini katika ujenzi wa  mahoteli na huduma za utalii zenye ladha na mandhari ya kichina.
   Mazungumzo yakiwa yanaendelea.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiagana na wawekezaji wa Kampuni ya Kimataifa ya Tibet Dexin Financia Leasing kutoka nchini China ofisini kwake mjini Dodoma jana baada ya kampuni hiyo kuwasilisha mpango wake wa kuwekeza apa nchini katika ujenzi wa  mahoteli na huduma za utalii zenye ladha na mandhari ya kichina.

BancABC YATEKELEZA SERA YA FEDHA YA BoT

 Mkurugenzi mtendaji wa BancABC Dana Botha akizungumza na waandishi wa habali katika ofisi zao Leo Jijini Dar es Salaam,kuhusu punguzo la tozo  ya mikopo mbali mbali kwa wateja wao.
Mkurugenzi Mtendaji wa BancABC Dana Botha kulia,kushoto ni Mkuu wa kitengo cha Hazina BancABC Barton Mwasamengo pamoja na Mkurugenzi wa kitengo cha wateja binafsi na wafanyabiashara wa BancABC Joyce  Malai katikati wakishika bango linaloonyesha punguzo la tozo za Mikopo.


BENKI ya BancABC  imesema imetekeleza Sera ya fedha  ya Benki  Kuu ya Tanzania(BoT) kwa kutangaza kutoa punguzo kwa wateja  wake wapya kuwezesha  kukopa kuanzia Aprili 1 mwaka huu.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji was BancABC Dana Botha amesema benki hiyo ni  sehemu ya Atlasi Mara iliyosajiliwa  katika soko la hisa la Londan ikiwa na lengo la kujitanua ili kuwa kinara katika masuala ya kifedha katika ukanda wa Sahara kwa kutumia uzoefu wake na uwezo wa kukuza mitaji.

Hivyo Botha amesema watapungunza riba kwa wateja wao katika mikopo ya masharti ambayo itakuwa ni huduma ya Over draft pamoja na  ya nyumba na kufafanua mwaka jana benki nyingi zilipita katika wakati mgumu wa ukwasi.

"Hivyo kufanya uwezo wa kukopesha kuwa mdogo.Kwa miezi kadhaa sasa,Serikali kupitia BoT imekuwa ikisisitiza kuhusu punguzo la riba hiyo kwa kupunguza masharti kama vile kiwango cha  chini cha fedha kwa mabenki,"amesema Botha.

Ameongezea viwango vya punguzo,hati fungani za hazina na kukopesha 
mabenki kwa viwango vya chini na hiyo imewezesha ukopeshaji kwa watu binafsi na kampuni mbalimbali ili kuimarisha biashara zao na hatimaye kuboresha uchumi. "Na tunajivunia kuwa kati ya benki za kwanza kutangaza wazi kuhusu punguzo hili."

Aidha Mkuu wa kitengo cha Hazina BancABC Barton Mwasamengo amesema kuwa benki hiyo inahudumia wateja zaidi ya 60,000 ambao wanamiliki bidhaa tofauti za kibenki

Mwasomengo amesema fursa hiyo itawawezesha kuwashawishi wateja kupata mikopo ya Nyumba ambayo ilikuwa changamoto kubwa hasa kwa wananchi wa Daraja la kati na chini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kitengo cha wateja binafsi na wafanyabiashara wa BancABC Joyce Mlai amemalizia kwa kusema katika kujenga nyumba wanaungana na Serikali kuwapa fursa ya kuwapatia mikopo ya Nyumba  wafanyakazi wa aina zote sekta binafsi,serikalini pmoja na wafanya biashara.

TAMASHA LA PASAKA KUTIKISA KANDA YA ZIWA,KUANZIA NDANI YA CCM KIRUMBA APRIL MOSI JIJINI LA MWANZA



Mkurugenzi wa kampuni ya Msama Promotion inayoandaa Tamasha la Pasaka akizungumza katika moja ya mikutano yake na waandishi wa habari kuelezea maandalizi ya Tamasha hilo litakalofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza Aprili 1 na Kwenye uwanja wa Halmashauri mjini Bariadi mkoani Simiyu.
Mwimbaji Jesca Honore akithibitisha kushiriki katika tamasha hilo kushoto ni Chrstopher Mwahangila mwimbaji mwingine ambaye atashiriki katika tamasha hilo mkoani Mwanza na Simiyu na katikati ni Jimmy Charles mmoja wa waratibu wa tamasha hilo. 
Mwimbaji Upendo Nkone akithibitisha kushiriki katika tamasha hilo kushoto ni Mwimbaji Joshua Mlelwa ambaye pia atakuwepo katika tamasha hilo katikati ni Ufo Saro mmoja wa waratibu wa Tamasha hilo.
Mwimbaji Martha Baraka akitibitisha kushiriki katika tamasha hilo kutoka kushoto ni Jimmy Charles mmoja wa waratibu wa Tamasha hilo na katikati ni Mzee Rainfred Masako mmoja wa Viongozi wa Dira TV. 
Mwimbaji Paul Clement akizungumza kuhusu maandalizi yake na kuthibitisha kwamba yuko tayari kwa ajili ya kutumbuiza katika Tamasha a Pasaka Kanda ya Ziwa kushoto ni Mwimbaji mwenzake Beatrice Mwaipaja .
Mwimbaji Christopher Mwahangila akifanya vitu vyake katika moja ya video zake alizowahi kurekodi.

.................................................................................................

Ni siku nne zimebaki kengele ya Tamasha la Pasaka zinahesabika. Ni Aprili Mosi, kwenye Uwanja  wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Mara nyingi Tamasha la Pasaka limekuwa likifanyika jijini Dar es Salaam safari hii Msama Promotion imeamua kulifanya tamasha hilo Kanda ya Ziwa. Hivyo Pasaka hii, wapenda muziki wa injili wa Kanda ya Ziwa na viunga vyake watapata burudani ya nyimbo za kumsifu na kumtukuza Mungu huku wakipata mahubiri kwa njia ya uinjilisti wa nyimbo.

Aprili Mosi ni CCM Kirumba, Aprili Pili Tamasha la Pasaka litachukua nafasi Uwanja wa Halmashauri, mkoani Simiyu ambako nako watasheherekea kwa nyimbo za injili.

Wakati siku zikikaribia kuelekea Tamasha la Pasaka kwa mkazi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa jumla ni kuendelea kumuomba Mungu ili aendelee kukupa uzima na afya njema.Waandaaji wa tamasha hilo, Kampuni ya Msama Promotion, mwaka huu wameamua kuweka vionjo tofauti ili kuhakikisha tamasha hilo linafanyika na kuacha historia kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa.

Kila mwanamuziki aliye kwenye chati, nyimbo zake za kumsifu na kumtukuza Mungu zikiwa zinatamba na kusikika, atakuwemo kuburudisha mashabiki wake na kubwa zaidi ni kwamba kuna baadhi ya waimbaji wataimba wakipiga vyombo vya muziki Live ili kuleta ladha na burudani zaidi katika tamasha hilo..

Kwa mujibu wa waandaji wa Tamasha la Pasaka, mwimbaji Rose Muhando atazindua albam yake mpya “Usivunjike Moyo” kati ya waimbaji wengi kutoka hapa nchini Tanzania na nje watakaofanya mambo makubwa katika tamasha hilo. 

Inafahamika kuwa Rose Muhando huwa hahitaji utambulisho. Ni mwanamuziki mkubwa kati ya waimbaji wa muziki wa injili ambaye Muumba wa Mbingu na Ardhi amenyanyua kipaji cha kuimba kilichoambatana na sauti maridadi. Muziki wa Rose Mhando unapopigwa wapo ambao wanasimamisha shughuli zao kwa muda ili kumsikiliza kwanza.

Kwa Rose Mhando mwenyewe anajua ukubwa wa Tamasha la Pasaka. Wakati anazungumzia tamasha hilo ameeleza wazi amejiandaa vya kutosha. Hivyo atakuwa Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kuonesha kile ambacho amewaandalia. ambapo pia atazindua albamu yake mpya inayoitwa 

Imekuwa kawaida kwa matamasha ya Pasaka kuleta wanamuziki kutoka nje ya nchi. Kwa taarifa tu ni kwamba atakuwepo Ephrem Sekereti kutoka Zambia. Mashabiki wa muziki wa Injili wanamfahamu vema Sekeleti na ubora wa kazi zake.

Wakazi wa Mwanza na Simiyu ni zamu yenu mwaka huu kupitia Tamasha la Pasaka kuweka historia ya kumshuhudia mwanamuziki Sekereti akitoa burudani tena ndani ya ardhi ya Tanzania. Karibu Sekereti wakazi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa wanakusubir.

MGALU AWATAADHARISHA WAKANDARASI/WATUMISHI WANAOHAMASISHA MAANDAMANO

Mbunge wa jimbo la Kibaha Mjini ,Silvestry Koka na Naibu waziri wa nishati Subira Mgalu wakibonyeza kiwashio ikiwa ni sehemu ya kuuwasha umeme umeme mtaa wa Mbwawa Mkoleni,wilayani Kibaha.
Picha na Mwamvua Mwinyi

Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha

SERIKALI imetoa tahadhari kwa watumishi ,wakandarasi na wadau wa sekta ya Nishati wanao husika na miradi wasitikise kiberiti kwa kuhamasisha maandamano kupitia shida za wananchi.

Aidha wizara ya Nishati imesema itatumia kiasi cha shilingi trilioni sita kwa ajili ya kuyafikia maeneo 7,873 nchi nzima ili yaunganishwe na huduma ya umeme kupitia miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

Hayo yalisemwa kwenye mtaa wa Sagale Magengeni kata ya Viziwaziwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alipokuwa akitembelea maeneo yaliyoko kwenye miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

Alisema kuwa ole wake anayetumia tumia shida za wananchi kuhamasisha maandamano kwani akibainika chamoto atakiona.

Mgalu alieleza hayo baada ya kauli ya mwananchi mmoja ambaye alikuwa akitaka umeme na kuambiwa kama anataka umeme aandamane maandamano ya Mange Kimambi.

“Serikali imeshtushwa tena inatokea maeneo haya kwa watu waliopewa dhamana mkandarasi ni dhamana huwezi kuleta jeuri kama unazo fedha usingeomba kazi hizi ni fedha za Rais Dk. Magufuli usilete jeuri,” alisema Mgalu.

Alisema kuwa, hawezi kuamini kama ni watumishi wa serikali wanaweza kufanya hivyo lakini kutokana na kauli hiyo ya mwananchi kujibiwa hivyo watavituma vyombo vinavyohusika vifanye kazi kumbana aliyetoa kauli hiyo kwani watawatafuta kwa udi na uvumba hadi wapatikane.

“Kama hatapatikana itabidi tuitishe gwaride la utambulisho kuweza kumbaini mtumishi aliyetoa kauli hiyo mbaya ambayo inawakatisha tamaa wananchi wakati kupata huduma ni haki yao ndo maana sisi tuko huku ingukuwa hivyo tusingekuja tungekaa lakini tunawatumikia wananchi hivyo hao wakamatwe wajieleze,” alisema Mgalu.

Alisema kuwa tanesco mkoa wa Pwani itabidi wahakikishe mtu au watu waliohusika na kutoa kauli hiyo wanabainika ambao walikuwa wakifuatilia masuala ya mita huko eneo la Viziwaziwa.

Alibainisha kuwa maandamano hayo hayapo na hakuna mtu atakayethubutu kufanya hivyo wananchi hawapaswi kushughulika na suala hilo watu waendelee na kazi zao waachane na watu wasiyoitakia nchi mema.

Akizungumza mbele ya naibu Waziri mwananchi huyo jina tunalo alisema kuwa waliambiwa waweke mfumo wa umeme kwenye nyumba zao ili waunganishiwe umeme.

Alisema kuwa walijibana lakini chaajabu nguzo za umeme zikapelekwa watu ambao wanaviwanja tu hakuna hata nyumba wao waliojenga na kuweka mfumo wa umeme hawakuwekewa nguzo.

“Tuliambiwa kuwa huu ni umeme wa msaada umefikia kilometa moja tu tukafuatilia hadi tanesco kwani tunajua umuhimu wa umeme lakini wakati wale wasomaji wa mita walivyokuja tulipouliza majibu yalikuwa kama tunataka tuandamane na maandamano ya Mange Kimambi,” alisema kwa masikitiko mwananchi huyo.

Aidha mwananchi huyo alisema kuwa kama umeme huo wa REA hautakuwepo basi wapewe wa Tanesco ambapo naibu Waziri alisema kuwa atafuatilia suala hilo ili waliohusika wachukuliwe hatua kama ni wa Tanesco au ni upande wa mkandarasi.

Wakati huo huo Mgalu akiwa Mbwawa alieleza kwenye awamu ya kwanza kupitia REA awamu ya kwanza waliyafikia maeneo 3,559 awamu ya pili wameyafikia 4,314 na kwa sasa bado maeneo 7,873 nchi nzima ili kufikisha huduma hiyo kwa wananchi wengi ambapo kwa mkoa wa Pwani kwa miradi hiyo imetumia kiasi cha shilingi bilioni sita.

“Tunatarajia kuhakikisha watu wanahiotaji umeme kwa wale wa vijijini ambapo zinatakiwa trilioni sita kuhakikisha tunawafikia wananchi pia tunataka kutekeleza agizo la Rais ifikapo Juni 2021 nchi nzima watu wawe wamepata huduma ya umeme,” alisema Mgalu.

Suala la ujazilizi tumeomba awamu ya pili baada ya awamu ya kwanza na tayari tumeomba fedha kwenye bajeti ya mwaka 2018/2019 kutotimia kwenye maeneo

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema serikali iko pamoja na wananchi katika kuhakikisha wanapata huduma hiyo muhimu ya nishati ya umeme kwani ni sehemu ya maendeleo ya nchi.

Alisema serikali ya awamu ya tano imejipanga kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kama ilivyoahidi ambapo inaendelea kutekeleza ahadi zake na kumshukuru Rais kwa jitihada zake za utekelezaji miradi ya umeme.

Koka alibainisha kutokana na umuhimu wa suala la nishati rais aliamua kuifanya wizara hiyo kujitegemea na imeonyesha matumaini kwani sasa mawaziri wanashuka hadi kwa wananchi.

Milioni 260 za Tatumzuka kunyakuliwa katika ‘Jackpot’ ya Pasaka

Tatu Mzuka, mchezo wa namba unaongoza hapa nchini unawapa fursa Watanzania kushinda kitita cha Shilingi milioni 260 katika droo itakayofanyika jumapili ya pasaka na kuonyeshwa moja kwa moja saa 3:30 usiku

 Taifa linapojiandaa na sherehe za Pasaka, Tatumzuka imeungana na wateja wake kwa kutangaza fursa ya kushinda kitita cha shilingi 260 ambacho lazima kitolewe jumapili ya Pasaka.

Kitita hicho kinono cha milioni 260 ambacho hakijawahi kutolewa kwa mtu katika historia ya nchi hii sasa kitatolewa kwa mshindi mmoja atakayebahatika kwenye ‘PasakaMzukaJackpot’ siku ya tarehe 31/3/2018.

Bwana Sebastian Maganga, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa Tatumzuka, ameuelezea umma namna ilivyo rahisi kuingia katika droo. “Wiki hii ukiwa na shilingi 500 tu, kwa kutumia; Mpesa, Tigo pesa au Airtel Money, ingiza namba ya kampuni ambayo ni 555111, kisha weka namba zako tatu za bahati na hapo utakuwa umeingia rasmi kwenye droo ya milioni 260 za PasakaMzukaJackpot” alielezea Maganga

Hicho sio kitu pekee ambacho Tatumzuka inatoa msimu huu wa sikukuu, pia una nafasi ya kushinda milioni 10 kila siku na milioni 6 kila saa.“Ukinunua tiketi moja ya shilingi 500, Tatumzuka inakupa nafasi ya kuingia katika droo 3 tofauti na hivyo kukuongezea nafasi za kushinda tofauti na michezo mingine ya namba” Maganga alisisitiza

Tatu Mzuka pia imetumia fursa hiyo kuwatambulisha washindi wa wiki iliyopita ambao walitokana na droo ya 34 ya Tatumzuka jackpot.Bi Hanifa kutoka Magomeni, Dar es Salaam alijishindia milioni 5. Bwana Juma Mkombozi kutoka Magomeni, Kagera alijishindia milioni 7. Bwana Prosper Munuo kutoka Bunju A alijinyakulia milioni 5 na Magreth Nkwabi wa Kahama, Shinyanga alipata milioni 3.

Washindi wote wakiwa wenye furaha baada ya ushindi walisisitiza kwamba wataendelea kucheza kujaribu bahati zao kwenye dau la kihistoria la milioni 260 jumapili hii.‘Droo hii ya kihistoria itaonyeshwa moja kwa moja kupitia ITV, Clouds TV na TV1 jumapili hii saa 3:30 usiku’ Bwana Maganga aliufafanulia umma. 
 Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano  Sebastian Maganga akizungumza na Waandishi wa Habari mapema leo jijini Dar akielezea kuhusu Tatumzuka kuungana na wateja wake kwa kutangaza fursa ya kushinda kitita cha shilingi 260 ambacho lazima kitolewe jumapili ya Pasaka.
 Mmoja ya washindi akikabidhiwa mfano wa Hundi yake yenye thamani ya shilingi milioni tano na la  Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Sebastian Maganga.



 Washindi wa Tatu Mzuka Jackpot wa wiki iliyopita kwa pamoja wakifurahi

KENYA NA TANZANIA WAHAKIKI MPAKA WA KIMATAIFA TANZANIA NA KENYA

Na Rehema Isango, Tarime, Mara

Timu za watalaamu wa upimaji ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Tanzania na taasisi za usimamizi wa Ardhi nchini Kenya zimekutana wilayani Tarime mkoani Mara kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa kazi ya kuhakiki na kuimarisha mpaka wa Kimataifa baina ya nchi hizi mbili.

Mapema mwezi Machi, Naibu Waziri wa Adhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula alitangaza azma ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanza kuimarisha mipaka yake kwa nchi jirani za Kenya na Uganda baada ya ziara yake ya kukagua mpaka wa Tanzania na Kenya katika Mbuga ya Wanyama ya Taifa ya Serengeti iliyopo mkoani Mara.

Hatua ya uhakiki na uimarishaji wa alama za mipaka ya mikataifa inatokana na mpaka huu kuwa wa siku nyingi na haukuwa wazi katika maeneo mengi pia baadhi ya alama hizo kuharibiwa, kung’olewa au kuchakaa na hivyo kusababisha Serikali pande zote kushindwa kusimamia kwa ufanisi shughuli za mipakani, rasilimali za nchi pamoja na ulinzi na usalama.

Katika uimarishaji wa alama hizo za mipaka hivi sasa, kutaongezwa alama mpya ndogo zinazoonana kwa umbali wa mita 100 pamoja na kubainisha eneo la ardhi huru kwa kila upande wa nchi (buffer zone).

Mpaka kati ya Tanzania na Kenya una jumla ya urefu wa Kilommita 760 kuelekea bahari ya Hindi ambapo awamu ya kwanza ya kazi ya uimarishaji mpaka inayofanyika hivi sasa itahusisha urefu wa Kilomita 238 kutoka kando ya Ziwa Victoria mkoani Mara hadi Ziwa Natron mkoani Arusha.

Baadaye, kazi ya uhakiki na uimarishaji wa mipaka itaendelea katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga na kisha itafanyika katika maeneo yote yanayohusika na mipaka ya kimataifa nchini.

Uimarishaji wa mipaka ya kimataifa nchini umefanyika mara ya mwisho mwaka 1975 kwa kurudishia alama ambazo ziliondolewa na kuongeza nyingine mpya kwa kuzingatia alama zilizopo.

Mbali na Kenya nchi nyingine zinazopakana na Tanzania ni; Msumbiji, Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Burundi, Rwanda, Uganda pamoja na visiwa vya Komoro na Shelisheli.
Wataalam wa masuala ya upimaji ardhi pamoja na maafisa mbalimbali kutoka katika ofisi za Serikali za nchi zote mbili waliojumuika pamoja wilayani Tarime mkoani Mara kupanga namna ya kutekeleza kazi ya uhakiki na uimarishaji wa mipaka ya kimataifa kwa pamoja. Wa tatu kutoka kulia (walioketi) ni Mkuu wa Msafara wa wataalam kutoka Tanzania Bw. Huruma Lugala na kulia kwake ni Mkuu wa Msafara kutoka Kenya Bw. Julius Rotich.
Mkuu wa zoezi la Uhamasihaji katika kazi ya kuhakiki na kuimarisha mipaka ya Kimataifa kati ya Tanzania na Kenya Bw. Raymond Bagenda kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi akizungumza wakati wa kikao cha pamoja cha wataalam wa masuala ya upimaji ardhi kutoka katika ofisi za Serikali za nchi zote mbili. Kikao hiko kilichofanyika wilayani Tarime mkoani Mara kinapanga namna ya kutekeleza kazi hiyo kwa pamoja. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais nchini Kenya inayohusika na Usimamizi wa Mipaka ya Kimataifa (KIBO) Bw. Joseph Rotich.
Baadhi ya Wataalam wa masuala ya upimaji ardhi pamoja na maafisa mbalimbali kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na katika ofisi zingine za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakifuatilia mazungumzo kuhusu namna ya kutekeleza kazi ya uhakiki na uimarishaji wa mipaka ya kimataifa kati ya Kenya na Tanzania.

MAGAZETI YA LEO JUMATANO MARCH 28,2018