Friday, April 6, 2018

Makazi ya Jebel Sifah nchini Oman ni fursa za kiuchumi kwa watu wote


Balozi Mdogo wa Oman Visiwani Zanzibar, Ahmad Mohamed Al Muzaini wa nne kutoka kulia akiwa amesimama baada ya kumaliza kuzungumza kwenye maonyesho ya makazi ya Oman Visiwani Zanzibar yakiandaliwa na Kampuni ya Muriya yenye maskani yake nchini Oman. Maonyesho hayo yamefanyika katika Hoteli ya The Park Hyatt, Zanzibar. Wengine ni wadau wa ardhi na makazi waliohudhuria kwenye maonyesho hayo. Picha na Mpiga picha wetu.

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
HUKU maonyesho ya makazi ya Jebel Sifah yanayoonyeshwa na Kampuni ya Muriya yenye maskani yake nchini Oman yakiendelea visiwani Zanzibar katika Hotel ya The Park Hyatt, baada ya kumalizika jijini Dar es Salaam, wafanyabiashara wa visiwani hapa wametakiwa kupanua wigo wao wa kibiashara kwa kununua makazi yao nchini Oman ili wajiwekee vitega uchumi kwa ajili ya maendeleo yao.

Ushauri huo umetolewa leo na Meneja Mauzo wa Muriya, Ghizlane El Gouchi, wakati wa kuelimisha wakazi na wananchi wa Zanzibar juu ya utendaji kazi wao katika sekta ya ardhi na makazi waliyojikita nchini Oman, huku wakijivunia maendeleo makubwa kwenye sekta hiyo muhimu dunian kote.

Wadau wa ardhi na makazi nchini Tanzania, Ali Al Maskary kulia na Aflah Al Maskary kushoto wakifuatilia jambo na mdau wa ardhi kutoka Oman, Faisal Said Rashid Alzakwani katika maonyesho ya makazi yanayoendeshwa na kampuni ya Muriya yenye maskani yake nchini Oman kwa ajili ya kununua makazi nchini humo. Tukio hilo linafanyika leo Aprili 6, katika Hoteli ya The Park Hyatt, Zanzibar kuanzia saa nne asubuhi hadi saa moja jioni.
Faisal Said Rashid Alzakwani kushoto akipiga picha na aalozi mdogo wa Oman Visiwani Zanzibar, Ahmad Mohamed Al Muzaini.
Alisema kwamba ni vyema Watanzania wote wakiwamo wafanyabiashara wakaelewa umuhimu wa kujitanua kibiashara kwa kuangalia uanIshwaji wa biashara nje ya mipaka yao, huku Kampuni yao ikifungua milango kwa kuwauzia makazi kwa utaratibu mzuri na rahisi katika maeneo yenye solo kama vile pembeni mwa bahari ambako wanaweza kuyatumia kama fursa za kiuchumi bila kusahau hati ya kuishi nchini Oman.

Muriya ni kampuni kubwa iliyojikita katika utoaji wa huduma za makazi na utalii nchini Oman, ambao kwa wiki moja sasa wanaendelea na maonyesho yao ya kibiashara wakianzia jijini Dar es Salaam na visiwani Zanzibar kama njia ya kubadilishana mawazo na kuwajulisha Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla juu ya biashara zao.

“Umuhimu wa biashara ni kupanuka kutoka eneo dogo kwenda eneo kubwa, hivyo ni lazima wadau wa Zanzibar kutafuta fursa nyingine hususan za kuwekeza nchini Oman katika eneo la makazi ambayo tutawauzia na wao watalipa kwa awamu ndani ya kipindi cha miaka miwili, tukiamini kuwa kwa wale wenye malengo wanaweza kufanikiwa, ambapo asilimia 10 zitalipwa baada ya kujisajili, huku gharama zetu zikianzia Dola 98,000 tu,"Alisema.

Kwa mujibu wa El Gouchi, mradi wao wa Jebel Sifah ni mwendo wa dakika 40 tu kutoka Muscat, karibu na ufukweni ambayo yana ukubwa hadi wa square meter 365,000, ukiwa ni mradi mkubwa unaowahusu Watanzania wote na ni fursa nzuri za uwekezaji.

Maonyesho hayo ya kibiashara ya makazi yanayouzwa na Kampuni ya Muriya, yamefanyika jijini Dar es Salaam kwa mafanikio makubwa tangu Aprili 3 hadi 5, ambapo kwa wakazi wa Zanzibar wenyewe wamefanikiwa kufikiwa na maonyesho hayo jana Aprili 6 katika Hoteli ya The Park Hyatt kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa na elimu juu ya umuhimu wa uwekezaji kwenye sekta ya makazi.


TAFITI ZINAONESHA NI MUHIMU KUWEKEZA KATIKA UFUNDI STADI KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA-DKT MMARI


Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti ya REPOA Dk.Donald Mmari amesema kuna sababu ya kuwekeza zaidi katika kutoa elimu ya ufundi stadi nchini kwa lengo la kupika watalaamu wa fani mbalimbali ambao watashiriki kufanya kazi zenye tija na kuleta ushindani kimataifa.

Dk.Mmari ametoa kauli hiyo wakati akielezea changamoto ambazo wamezibaini kwenye warsha ya siku mbili iliyoandaliwa na REPOA kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali katika kipindi hiki cha kuelekea Tanzania ya Viwanda.

Amesema wadau walioko kwenye warsha hiyo wamejadili kwa kina mambo mengi kwa maslahi mapana ya nchi yetu na katika mjadala huo wamebaini bado kunachangamoto ambazo ni vema zikafanyiwa kazi ili kufikia malengo ya ujenzi wa viwanda na kuwa na bidhaa zenye ushindani katika soko la kimataifa.

Ametaja moja ya changamoto ambao wameijadili ni uhaba wa wataalam katika nyanja mbalimbali na hiyo inatokana na kutowekeza zaidi kwenye elimu ya Ufundi stadi ambayo inaandaa vijana kujiajiri na kuwa watalaamu wazuri."Tumekubaliana na kutoa mapendekezo kuwa ili tuingie kwenye ushindani ipo haja ya kuhakikisha watanzania wanaalindaliwa katika elimu na ujuzi unaohusu masuala ya ufundi.

"Ni vema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta za umma na binafsi kuwekeza zaidi katika kuwajengea uwezo wananchi ambao utawafanya washiriki kikamilifu katika kufanya kazi kwenye viwanda,"amesema Dk.Mmari.Amefafanua nchi nyingi ambazo zimeendelea na zenye uwezo wa kuhimili ushindani kwenye soko la kimataifa msingi wake mkubwa wamewekeza katika elimu, ujuzi na utalaam.

"Hivyo ili kushindana nao lazima Tanzania nayo ikawekeza katika elimu, ujuzi na utaalamu kwa kuandaaa vijana watakaokuwa na ujuzi.Tumekubaliana yale ambayo tumeyaona kama changamato tumeweka na mapendekezo yetu na tumekubaliana Serikali iyapate na ikiwezekana kuyafanyia kazi,"amesem Dk.Mmari.

Amesisitiza ni vema nchi ikawekeza zaidi kwenye kujenga vyuo vya VETA ambavyo jukumu litakuwa kuandaa watalaam na kwamba kuna wakati iliingia kasumba ya kuwa na vyuo vikuu vingi ili wanaohitimu wawe na Shahada lakini elimu hiyo haina ujuzi na matokeo yake kunaibuka changamoto ya uhaba wa watalaamu.

Kwa upande wa Mlkuregenzi Mtendaji wa Tanzania Horticultural 
Asspciation (TAHA) Jacqueline Mkindi amesema pamoja na kujadili mambo mengi kwenye warsha hiyo wamegundua ujuzi kwenye maeneo ya viwandani bado tatizo kubwa.Amesema ipo haja ya kuhakikisha wanaandaliwa watalaamu wenye ujuzi unaokubalika kimataifa kwa lengo la kuwa na bidhaa zenye ushindani na kufafanua jukumu ambalo TAHA wanafanya ni kuwaandaa vijana kujiajiri kwa kuwapatia mafunzo yenye ujuzi.

"TAHA tumebaini kuna tatizo la uhaba wa watalaam, kwa mfano kwetu inapofika kipindi cha kuchanganya mbegu maabara lazima utakuta wanaofanya kazi hiyo ni watalaamu kutoka nje."Sababu kubwa ni kwamba kwetu hawapo.Hivyo wakati nchi inajipanga kwenye ujenzi wa viwanda ni vema ikaenda sambamba na kuandaa watalaam ili kuondoa changamoto iliyopo,"amesema Mkindi.

Ameongeza cha msingi ni kuweka uratibu mzuri utakaosaidia vijana kuwajengea uwezo utakaosadia kuondoa changamoto ya uhaba wa watalaamu katika fani mbalimbali nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Tasisi ya Utafiti Nchini, REPOA, Dk. Donald Mmari akizungumza wakati wa kufunga Warsha ya siku mbili kwa watafiti iliyoandaliwa na tasisi yake juu ya kwanini ushindani ni muhimu kuelekea uchumi wa Viwanda.
Mlkuregenzi Mtendaji wa Tanzania Horticultural Asspciation (TAHA) Jacqueline Mkindi akizungumza jambo wakati wa mkutano huo walipjadili nafasi ya kilimo katika uchumi wa Viwanda.
Mratibu na Mtafiti wa Warsha hiyo kutoka Repoa, Dk. Blandina Kilama akizungumza jambo wakati wa Mkutano huo wakati alipokuwa akiongoza meza ya majadiliano.
Mtafiti Kutoka Repoa, Dk. Lucas Katera akizungumza jambo kaatika mjadala wa Nishati kuelekea Uchumi wa Viwanda wakati wa Warsha ya siku Mbili ya Watafiti iliyoandaliwa na Repoa.
Baadhi ya Washiriki wa Warsha ya siku mbili kwa watafiti juu ya kwanini ushindani ni Muhimu kuelekea Uchumi wa Viwanda wakifatilia mada kwa makini.

WAZIRI KIGWANGALLA AAGIZA KILA KIJIJI KUTENGA ENEO LA UHIFADHI WA MISITU, ATOA SIKU 7 KWA TFS KUWASILISHA MPANGO WA UVUNAJI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakipanda mti wa kumbukumbu wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.

Na Hamza Temba, WMU, Kishapu, Shinyanga
.......................................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amewaagiza Wakuu wa Mikoa nchini kuhakikisha Halmashauri zote nchini zinatenga maeneo katika kila kijiji kwa ajili ya uhifadhi wa misitu ikiwa ni pamoja na vijiji hivyo kuunda kanuni na taratibu zao wenyewe za kusimamia maeneo hayo. 

Ametoa agizo hilo jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wakati wa kuhitimisha kilele cha Maadhimisho ya Upandaji Miti Kitaifa yaliyofanyika mkoani humo kuanzia Aprili 03 mwaka huu.

Katika kufanikisha zoezi hilo ameuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuchagua mikoa 10 ya kuanza utekelezaji wa agizo hilo ikiwemo mikoa ya Shinyanga na Tabora ambayo inakabiliwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa misitu.

Ameugiza pia we uongozi huo wa TFS kuweka mpango wa uhifadhi wa misitu ya asili katika maeneo hayo kwa kushirikiana na vijiji kupanga maeneo yanayostahili kuhifadhiwa sambamba na kuwapa elimu ya umuhimu wa uhifadhi wa maeneo hayo.

Wakati huo huo Dk. Kigwangalla ametoa siku saba kwa uongozi huo wa Wakala wa Huduma za Misitu kuwasilisha kwake mpango wa tathmini ya uvunaji wa mazao ya misitu wa nchi nzima kwa kuzingatia kiasi cha rasilimali misitu kilichopo na kiwango halisi kitakachotakiwa kuvunwa ambacho hakitazidi robo ya rasilimali iliyopo.

"Hatuwezi kuendelea tu kutoa vibali vya kuvuna misitu hatujui tunavuna wapi, tuna rasilimali kiasi gani, wavune kiasi gani, hapana, mnitengenezee mpango laa sivyo nitasitisha uvunaji, nikisema nasitisha uvunaji nitapeleka waraka kwa Wakuu wa Mikoa, na nina uhakika kwa nguvu walinayo hawashindwi kuzuia uvunaji. 

"Kwahiyo TFS nawapa siku saba mniletee mpango wa tathmini ya namna ambavyo tuna rasilimali kwenye kila mkoa, tujue mkoa flani una miti cubic mita kadhaa ya mbao kadhaa, ya kuni kadhaa, ya mkaa kadhaa na kwa mwaka huu tutaruhusu wavune kwenye msitu fulani  kiasi kadhaa, twende kisayansi, sio Meneja wa TFS anakaa Wilayani anatoa vibali watu wanaenda kuvuna,".

Dk. Kigwangalla amesema  takwimu za uharibifu wa misitu hapa nchini zinatisha jambo ambalo likiachwa liendelee bila kuchukua hatua nchi itageuka kuwa jangwa.

"Kwa mwaka tunakata miti kwa mahitaji mbalimbali kati ya ekari 800,000 na 1,200,000.
Ili kurejesha walau nusu ya miti tunayokata kwa mwaka tunahitaji kupanda miti 3,000,000 kwa mwaka mfululizo kwa miaka 17 ili kufidia kiasi cha uharibifu tunachofanya kwa nusu mwaka" alisema Dk. Kigwangalla.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Ezekiel Mwakalukwa ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alisema kumekuwepo na jitihada za kuandaa programu kubwa za kitaifa za uhifadhi wa mazingira katika maeneo mahususi yaliyoonekana kuzidiwa na tatizo la uharibifu wa mazingira. 

Alitaja Programu hizo kuwa ni Hifadhi Ardhi Dodoma (HADO), Hifadhi Ardhi Shinyanga (HASHI), na Hifadhi Mazingira Iringa (HIMA).

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alisema mkoa wake kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Tabora umeanza kuchukua hatua za kurejesha uoto wa asili katika maeneo yao ikiwemo kuanzisha utaratibu wa kugawa miche ya miti kwa kila kaya pamoja na kuimarisha kamati za uhifadhi wa mazingira.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Taboba, Aggrey Mwanri alisema ushirikiano huo ni muhimu kwani utawezesha kukabiliana na changamoto zilizopo katika mikoa hiyo kwa kuweka mikakati ya pamoja wa kudhibiti vitendo vya uharibifu wa mazingira kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo iliyopo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakipanda mti wa kumbukumbu wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwahutubia wananchi wakati wa kuhitimisha kilele cha Maadhimisho ya Upandaji Miti Kitaifa yaliyofanyika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga jana.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakiteta jambo wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akiwahutubia wananchi wakati wa maadhimisho hayo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakiwasalimu wananchi wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
  Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Ezekiel Mwakalukwa ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo akitoa maelezo kuhusu maadhimisho hayo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakielekea eneo la tukio la kupanda miti wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akishiriki kucheza ngoma wakati wa maadhimisho hayo.