Monday, March 26, 2018

Wakati Mwadhama Kadinali Polycarp Pengo akiukana Waraka wa Pasaka wa MAASKOFU, siri imefichuka!!


SIRI IMEFICHUKA!!!!!!
• Maaskofu waukana Ujumbe wa Pasaka.
• Maaskofu 4 wa TEC waliouandika wajulikana
Majina yao haya hapa, kwa taarifa za uhakika.
Nimeshtushwa sana na taarifa niliyoipata juu ya Ujumbe wa Kwaresima uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ulioelekezwa kwa waumini wakati huu wa toba ya Kwaresima iliyoanza Februari 14, 2018 hadi Pasaka siku ya kusherehekea ufufuko wa Bwana Yesu Kristo (Pasaka).

Mimi ni Mkatoliki wa Jimbo la Dodoma na Askofu wangu ni Mhashamu Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya.
Nikiri nilianza kupata mashaka tangu mapema ujumbe huu ulipotoka, nilijiuliza sana na hivyo nikaamua kufanya juhudi za kujua kama kweli Kanisa langu Katoliki limefikia hatua hii? Naujua utaratibu na utamaduni wa kanisa langu ndio maana nilipatwa na mashaka haya.

Kwa ambao hawajausoma ujumbe huu, ulikuwa na sura nne lakini iliyoleta tafrani ni sura ya tatu yenye ujumbe kuhusu “Dalili za nyakati zetu Tanzania” hususani katika kipengele cha siasa. Imeleta tafrani kwa sababu katika eneo hili ujumbe huu umeenda kwenye masuala ambayo siku zote yamesababisha kuwepo malumbano kuwa viongozi wa dini wanaingia mambo ya kisiasa ama wanachanganya dini na siasa.

Kwa ufupi kabisa ujumbe huu umetoa shutuma na bila shaka dhidi ya Serikali inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli kuwa shughuli za siasa kama vile uenezi, mikutano ya hadhara, maandamano, makongamano, mijadala na mikutano ya ndani zinazuiwa kwa kutumia vyombo vya dola.

Ujumbe unaendelea kushutumu kuwa vyombo vya habari vimefungiwa au kusimamishwa kwa muda, uhuru wa Mahakama na Bunge unaminywa na kwamba katika mazingira haya ni rahisi kwa jamii kufarakana na hata kujenga chuki kiasi cha kuhatarisha amani, usalama na hadhi ya uhai wa binadamu.

Ujumbe umeongeza shutuma nyingine kuwa chaguzi zinaharibiwa kwa vurugu na hivyo kuacha nyuma uchungu, hasira, tamaa ya kulipa kisasi na hata kususia chaguzi nyingine na kwamba hali hiyo ni hatari kwa mustakabali wa Taifa letu, ikiachwa izoeleke tusishangae huko mbele kujikuta katika mifarakano mikubwa zaidi itakayobomoa misingi ya amani na umoja wa kitaifa.
NIMEPATA TAARIFA ZA UHAKIKA KABISA kuwa ujumbe huu haukuandikwa na Maaskofu 35 wa Kanisa Katoliki kama ilivyotolewa na Baraza la Maaskofu (TEC).

Katika shauku yangu hii ya kutaka kujua kwa nini viongozi wangu wa Kanisa lenye heshima hapa nchini wamefikia hatua hii nimepata taarifa za uhakika kuwa Maaskofu walioshiriki kuandika ujumbe huu ni wanne (nitawataja huko mbele) na Maaskofu wengine walikataa kushiriki kikao kilichofanya kazi ya kuandika ujumbe huu.

Mniwie radhi sana nimepata mashaka makubwa sana niliposoma majina ya Maaskofu waliofanya kazi ya kuandika ujumbe huu na historia zao za mahubiri yenye uchochezi mkubwa na hata mara kadhaa wametuhumiwa kwa ukabila na uchochezi na ushahidi upo.
Maaskofu walioandika ujumbe huu ni Mhashamu Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo Kuu la Dodoma, Mhashamu Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi wa Jimbo Kuu la Mwanza, Mhashamu Askofu Augustino Shao wa Jimbo la Zanzibar na Mhashamu Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo la Rulenge-Ngara.

Maaskofu wengine hawakushiriki kuandika ujumbe huu na kwa kuwa wanatambua dosari iliyokuwa inafanyika wakatoa udhuru mbalimbali na kwa hivyo hao Maaskofu wanne wakaifanya kazi hiyo wakishirikiana na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Padre Raymond Saba na wakamchukua Dk. Kasala kama mshauri wa uandishi wa ujumbe huo.

Kwa kuangalia safu hiyo utaona ujumbe huu umeandikwa pasi kuwepo Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wala Mwadhama Polyacarp Kardinali Pengo wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Nimepata taarifa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea Mhashamu Damian Dallu aliondoka mkutanoni na kuomba udhuru baada ya kubaini mwelekeo wa ujumbe huu.

Hapo ni kujiuliza kwa nini? Na kama kuna yeyote hayaamini haya basi na awaulize viongozi hawa kama walishiriki kuandika ujumbe huo, naamini hata wao wamekwazika na kwa namna yeyote hawawezi kukubaliana na yaliyomo katika ujumbe huu hata kama watakuwa na changamoto ya kuukana hadharani kulingana na utamaduni na nidhamu ya Kanisa.

Ukiangalia Maaskofu watatu kati ya wanne walioandika ujumbe huu wanatoka Mikoa ya ama Arusha ama Kilimanjaro ambako wanasiasa wake ndio wamekuwa wakishikia bango hizo hoja walizoziandika na wao wamekuwa mara kadhaa wakipambana kutumia Ibada na shughuli za Kanisa kueneza siasa hizo.

Askofu Niwemugizi ambaye mpaka sasa ana mgogoro mkubwa na idara ya Uhamiaji kutokana na uraia wake kuwa na mashaka na yeye amekuwa akitaka kujificha kwenye kichaka cha kudai anafuatwafuatwa kwa sababu anawakosoa watawala, anafahamika kwa namna alivyojipambanua kuegemea siasa za upinzani na kuungana na wanaharakati wanaopambana na Serikali.

LAKINI kwa kungalia hizo hoja wanazozitoa kuikosoa Serikali na kutaka kujenga taharuki kwa Watanzania kuwa nchi inakwenda vibaya, mimi nimejiuliza mambo mengi sana.

Maaskofu hawa wanne wanadai shughuli za kiasiasa zimezuiliwa, hivi ni mwanasiasa gani amezuliwa kufanya siasa? Maaskofu hawa wanawasikiliza akina Freeman Mbowe, Godbless Lema, Zitto Kabwe, Tundu Lissu na genge lao linalojumuisha Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu kinachoongozwa na mwanachama wa CHADEMA Dk. Heleni Kijo-Bisimba ambao wanataka shughuli za siasa iwe ni kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya maandamano, fujo na uchochezi?

Wakawaulize wanasiasa hao ni lini wamekatazwa kufanya shughuli za siasa kwenye majimbo yao? Au kwa wao wanafurahishwa na kauli za Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe kuwa Watanzania wawe tayari kufa 100 hadi 200 kwa ajili ya yeye kwenda Ikulu? Hawataki hata kumuuliza Freeman Mbowe kwa nini kaatamia uenyekiti wa CHADEMA kwa zaidi ya miaka 20?

Maaskofu hawa wanne wanashutumu kuwa vyombo vya habari vimefungiwa na vingine vimefungiwa kwa muda na hivyo kupunguza uwigo wa wananchi kupata habari, maoni na uhuru wa kujieleza. Hivi Maaskofu hawajui kuwa uhuru huu una mipaka na ni kwa mujibu wa sheria? Maaskofu hawajui vyombo vya habari vilivyofungiwa ni kwa sababu vimevunja sheria? Nimejiuliza sana hivi hata ndani ya Kanisa Katoliki hakuna mipanga ya uhuru wa kujieleza?

Labda niwaulize Maaskofu kama mnahoji hilo, Je Kanisa Katoliki lenyewe limejihoji juu ya hatua lilizomchukua Padre Felician Nkwera? Kwa ambao hawajui Padre huyu alikuwa hodari wa mahubiri na alipendwa sana na waumini akawa tishio ndani ya vigogo wa Kanisa Katoliki, matokeo yake alipigwa fitina hadi Makao Makuu Roma Italia na mwishowe alitengwa na Kanisa.

Padre Privatus Kalugendo vivyo hivyo aliweka msimamo wake na akaamua kuoa ambayo ni haki ya mwanadamu yeyote, matokeo yake alitengwa na akafukuzwa kwa tamko la Papa, ambalo huwa halipingwi. Padre Titus Mageranga wa Iringa yalimkuta hayo hayo, na hata Askofu Jacob Koda wa Jimbo la Same Kilimanjaro naye yalimkuta hayo hayo.

Mifano ipo mingi, hivi kuna mtu anajiuliza Askofu Mkuu Norbet Wendelin Mtega yupo wapi? Askofu Mahiri kabisa aliyeliongoza Jimbo Kuu Katoliki la Mtakatifu Mathias Mulumba Kalemba kule Songea, Ruvuma. Alipigwa fitna akaondolewa kimyakimya mpaka leo haijulikani yupo wapi na Kanisa Katoliki halijatoka kwa waumini kuwaambia alikosa nini na yupo wapi?

Na hili halipo Tanzania tu, huo ndio utamaduni wa Kanisa hili kwamba katika ngazi hizo za vigogo wakubwa, ukienda tofauti na matakwa yao bila kujali una haki au huna haki unafukuzwa, unafichwa Roma ama unawekwa popote duniani ama unapotezwa kabisa maana inakuwa hakuna mawasiliano na nyumbani wala ndugu zako. Wakatoliki wanaujua ukweli huu. Nausema kwa sababu walioanzisha kufukunyua mambo ya kuvuruga nchi ni vizuri wajue kuwa hata wao sio wasafi hivyo na sisi waumini tunajua mengi ila tunaheshimu tu.

Maaskofu hawa wanne wanasema vyombo vya habari vinafungiwa, nimewaza sana na nikakumbuka jinsi viongozi hawa hawa wa Kanisa Katoliki kule nchini Rwanda walipotumia kituo cha redio kueneza chuki miongoni mwa Wanyarwanda na kusababisha mauaji ya halaiki mwaka 1994, ambapo watu takribani Milioni 1 waliuawa kikatili kwa kuchinjwa, kuchomwa moto na kupondwapondwa kwa madai kuwa ni mende.

Kwa wasiojua mauaji ya halaiki ya Rwanda yaliibukia kwenye ukabila lakini fukuto lilianza zamani na miongoni mwa waliokuwa wanatengeneza fukuto hilo ni viongozi wa Kanisa Katoliki ambalo lina mizizi mikubwa nchini Rwanda.
Askofu Rwemugizi ambaye ana mgogoro na idara ya Uhamiaji kwa madai kuwa sio raia wa Tanzania bali nchi jirani anaujua ukweli huu na anajua vizuri madhara ya mchezo anaoufanya, naamini ama anashauku ya kuona tena mauaji yale ama anafanya kwa malengo mahususi.

Maaskofu hawa wanne wanasema Mahakama na Bunge vinaingiliwa, lakini hawajasema ni wapi mihimili hii imeingiliwa.
Kwa ujumbe unaotoka kwa jina la chombo kikubwa kama Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) nilitegemea kusoma mifano na uthibitisho wa kuingiliwa kwa mihimili hii.

Hii ni hatari kubwa sana kutoa tuhuma nzito kama hizo dhidi ya mihimili ya dola halafu ukaacha zinaelea hewani. Watoke tena Maaskofu hawa wanne waseme kwa uwazi na kwa uthibitisho kuwa mihimili hii imeingiliwa hapa na hapa na hapa.
Maaskofu hawa wanne wanasema chaguzi zinafanywa kwa vurugu na zinaacha chuki kiasi cha kuhatarisha amani, usalama na hadhi ya uhai wa binadamu. Japo kuwa kauli hii imeachwa inaelea lakini kwa namna yoyote Maaskofu wanatuhumu kuwa wanaoshindwa kwenye chaguzi nyingi hapa nchini ambao ni vyama vya upinzani ndio wanaobaki na hasira na chuki.

Hapa Maaskofu wanataka kutuambia kuwa ni Tanzania peke yake ambako wanaoshindwa kwenye uchaguzi ndio wananuna? Hivi kwenye chaguzi za ndani ya CHADEMA wanaokosa huwa hawanuni? Ina maana Maaskofu huwa hawaoni vurugu ambazo hutokea kwenye mataifa mbalimbali wakiwemo jirani zetu wa Kenya hata Taifa kubwa la Marekani ambao wamefanya uchaguzi karibuni? Mimi nilidhani jukumu la maaskofu lingekuwa kuponya kwa imani makovu ya uchaguzi hasa kwa wanaoshindwa na badala yake wanataka hapa Tanzania ndio paonekane pana tatizo kubwa na wanatuma ujumbe wa kuwachochea wananchi waikasirikie Serikali.

HITIMISHO.

Kwa sisi Wakatoliki hiki kilichofanywa na Maaskofu hawa wanne ni lazima kikemewe kwa nguvu zote. Naamini Kanisa linao Maaskofu wazuri, wacha Mungu na wanaotambua umuhimu wa Kanisa katika nchi, wanatambua umuhimu wao katika kuimarisha ustawi wa jamii badala ya kuivuruga.

Na hata katika mahubiri ya leo Jumapili ya Matawi (Machi 25, 2018) tumewasikia Maaskofu na Mapadre wazuri wakihubiri Injili juu ya Mateso ya Yesu na kusulubiwa kwake kwa ajili ya wanadamu. Wanafanya kazi ya Mungu ya kuwajenga waumini kwa imani, kutubu dhambi na kushika njia iliyonyooka, wametufundisha mambo muhimu katika maisha ya ukristo na kamwe viongozi hawa hawawi na mahubiri ya mihemko na siasa zinazoleta chuki na uchochezi.

Tunajenga Taifa la wachapakazi, nchi yetu ipo nyuma sana kimaendeleo, Maaskofu na Mapadre wetu wazuri wanahubiri matumaini, wanawaombea viongozi wa Serikali kuwa watumishi bora, wenye hofu ya Mungu, wanaviombea vyombo vya haki kutenda haki na wanawaombea Watanzania na dunia nzima kupigania amani, upendo, mshikamano na udugu badala ya kushabikia kauli na uchochezi wa kuleta vita, mapigano, malumbano na fitna.

Maaskofu na Mapadre Wakatoliki wazuri wanawahimiza Watanzania kufanya kazi mashambani na makazini ili kujipatia kipato halali kwa kuwa imeandikwa asiyefanya kazi na asile, wanawahimiza Watanzania kutovunja sheria na kuheshimu mamlaka zote badala ya kuchochea watu wakeshe kwenye maandano, malumbano na mapambano na Serikali.

Naamini mtazamo huu sio wa kwangu pekee yangu, naamini wapo Wakatoliki wengi ambao wamechukizwa na sehemu ya ujumbe huu wa Kwaresima ulioandikwa na Maaskofu hawa wanne, nawaomba tusiyumbishwe na hilo, tuendelee kuipenda nchi yetu na kuungana na Serikali hasa wakati huu ambapo kiongozi wa nchi Mhe. Rais Magufuli anafanya mambo makubwa ya kimageuzi katika uchumi, ustawi wa jamii, kutetea wanyonge na kudhibiti wizi wa mali za umma.

Natambua kuwa Baraza la Maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) nao wamefanya makosa haya haya yaliyofanywa na TEC, natambua vinara wa kutoa Ujumbe wa Pasaka wa KKKT ni watu wa mlengo gani, natambua kwa nini wamekasirishwa hivyo lakini hili wacha niwaachie waumini wa KKKT wenyewe, mimi nipo na hawa wa kwangu Kanisa Katoliki.

Kwa Maaskofu wote na viongozi wengine wa dini, naomba niseme Tanzania ninayoijua mimi ina watu ambao wapo makini sana hasa linapokuja suala la nchi yao, sisi Watanzania tunapenda amani, tunapenda upendo, sisi ni ndugu sana, hatujazoea vurugu, hatupendi ukabila na ukanda, tunawapenda majirani kama Yesu alivyosema na ndio maana hao wanasiasa walioasisi haya mnayoyasema leo wameshindwa kwenye uwanja wa siasa na sasa wanataka kuwatumia nyie kwenye makanisa.

Ninachokiona kwa kuwa mmesahau kuwa Makanisani kwenu kuna waumini wenye milengo tofauti ya siasa tunakokwenda mtayavuruga Makanisa, kwa Kanisa Katoliki itakuwa ni mtihani mkubwa kwa sababu hakuna utaratibu wa Askofu kupigiwa kura ili aendelee ama asiendelee kama ilivyo kwa Makanisa mengine, kwa hiyo kitakachotokea ni kuendelea kukimbiwa na waumini kama ambavyo mmewapoteza waumini wengi kwenda kwenye makanisa ya Kilokole.

Kwa makanisa yenye uchaguzi wa Maaskofu ninachokiona ni kuendeleza mitafaruku ambayo mpaka leo inazitafuna baadhi ya Dayosisi zenu. Tena huku mlikoingia ndio kubaya zaidi maana sasa vyama vya siasa vitaanza kushindana kuweka Maaskofu wao. Inawezekana msilione hili lakini mkae mkijua kuwa litakapofika hapo hamtaweza kulidhibiti.

CHADEMA walipoanzisha kumchukua Mwana CCM Lazaro Nyalandu walidhani CCM watakaa kimya, walichokipata na wanachoendelea kukipata wote mnaona. Sasa na nyinyi mmeamua kuingia kwenye siasa za kushabikia hoja za CHADEMA na kutumwa na CHADEMA kuichokonoa Serikali ya CCM, mjiangalie siku CCM nao wakiingia huko Makanisani kwenu mjue shughuli itakuwa pevu.

Nawaombeni msituharibie Kanisa. Acheni Makanisa yafanye kazi yake ya kuhubiri Injili, siasa waachieni wanasiasa, harakati waachieni wanaharakati na vita waachieni wanajeshi.

Julius Kindonga
Mkazi wa Dodoma Machi 25, 2018

5 comments:

Anonymous said...

Shabash!
Sidhani hata kama watunzi wa waraka kwa kwaresma na waliowatuma walitegemea bomu kulipuka kwa namna hii.
Niseme tu hongera chadema kwa mikakati isiyoisha ya kutekeleza kile kiapo chenu cha "nchi haitawaliki."
Watz tunaoelewa na kutambua mwelekeo wa nchi tumeanza kupata imani ila kwa mastaajabu kuna wenzetu kwa gharama zozote wanapambana kuhakikisha mustakbali wa jamii yetu hautengemai.
Ni kazi ya ibilisi shetani hiyo, aliyelaaniwa na kufukuzwa na Mungu, na baadae kuapa kumchafulia na kumvurugia binadamu malengo yake ya maisha ya amani duniani na akhera.
Sasa amepiga hodi ndani ya nyumba za ibada, na kwa mara nyingine tena amefanikiwa kuwanunua watumishi wa Mungu kwa thamani haba kabisa.
So far Mwenyezi Mungu amewapenda watz na ndio kama hivi, amewathibitishia uzandiki na ukibaraka wa wenye nia mbaya.
Kanisa katoliki linakabili kipindi kigumu mno, kwani jamii itataka kuona response yake.
Viongozi wenye mamlaka humo ndani mna maswali ya kuwajibu watz na walimwengu kwa jumla. Tunataka kuona hatua stahiki watazochukuliwa hawa wachunga kondoo waliolivuliwa heshma yao wakatumbukia kumtumikia mwanasiasa.
Wenye mamlaka na madaraka KKKT tupeni majibu otherwise mmeporomoka na kupoteza stahili ya kuwa chombo cha imani.
Pia nyie wanne mnaoshutumiwa, jitokezeni mbele kuukabili umma muueleze ukweli juu ya tuhuma hizi.
Mtwambie nani kakutumeni, na mkikiri makosa bora tu mng'atuke muachane na viriri vya dini mjiunge na vyama vyenu vya siasa na mvitumikie.
Mwenyezi Mungu ibariki Tanzania na watu wake Ameen .
Mndengereko Ukerewe

Anonymous said...

Ama kweli Shetani hana mchezo. Anadhani anaweza kuwatumia hawa Maaskofu wanne kutudanganya watz zaidi ya million hamsini ili tupotee mwelekeo?Hii ni kazi ambayo haitazaa matunda kamwe, wala sio kazi yenye kibari machoni pa Mungu wa mbingu na nchi. Hao Maaskofu Mungu atawakanyaga na watayeyuka kama nta mbele ya moto watatawanywa kama majani makavu mbele ya upepo!na kama moshi hewani. Wakumbuke kwamba wapatanishi wataitwa wana wa MUngu na kama wao wanaona kuna mgogolo jukumu lao ilikuwa na KUPATANISHA na wala sio kutimiza na kushabikia upande mmoja. Binafsi ninawaomba hao Maaskofu wa Katoloki wajitafakari, hata wale wa KKKT.
MMESHINDWA KTK JINA LA YESU KRISTO NA MULEGEE KABISA.

Anonymous said...

Perfect!!
Hata Manabii walivyoletwa na Mungu kuwakomboa watu wao walipata vikwazo vingi sana!(Rejea kwenye vitabu) Watanzania ni watu imara na ndio maana Mungu amewapa kiongozi imara(JPM)
JPM fanya kazi yako usiwasikilize Mashetani!!
Shetani hawezi shinda nguvu za Mungu!

Mkankala said...

Mimi naachwa kwenye mataa na nashindwa kuelewa nani mkweli! Maaskofu wana haki ya kijieleza na kutoa hisia na mawazo yao kwa mujibu wa katiba ya nchi yetu, tusiwaweke pembeni kwa sababu wao ni raia wa nchi hii, achilia mbali majukumu ya dini wanazo ziongoza kuchunga Roho za watu wa nchi hii.
Ukisoma maelezo ya Kitengo cha Sheria na Haki za Binadamu, Baraza la Maaskofu Tanzania.(TEC),Baraza la Maaskofu wa KKKT,TLS nimesoma maelezo yao naona yanatoa ujumbe unao ashiria hali siyo shwari katika nchi yetu na mimi nakubaliana.
Tunao tetea, Je, tumejaribu kutafakari kujiuliza kwa nini makundi haya yanakosoa? Je, ni kweli wamekurupuka na kuandika tu ?Tukianza kuwakebehi na kuwaita mashetani n.k nakuwa na mashaka labda kuna kitu nyuma ya pazia.
Nashauri tutumie lugha njema kwa Maaskofu wapakwa mafuta, na tuenende katika kweli, tutafute njia ya kuweka sawa hali inayoelezwa na makundi yaliyotajwa.

Anonymous said...

Jambo lina nyuso mbili:
Wewe unaewatetea ni kwa sababu ni katika wao.
Nafasi yako katika jamii hutafsiri nini useme au ufanye.
Si kila unaloruhusiwa kulifanya kisheria bali waweza kulifanya hapana.
Ila inataka uelewa wa mtu kuona hayo.
Wengine hawayaoni na hakuna muda wa kuelimishana hapa.
Ila Pelicarp Pengo amezungumza vya kutosha.