Saturday, February 10, 2018

TUME ya Taifa ya Uchaguzi yavikumbusha vyama vya siasa kwasilisha orodha ya mawakala wao


TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevikumbusha vyama vya siasa ambavyo vimesimamisha wagombea ubunge na udiwani katika majimbo mawili na kata tisa kuwa kesho (Februari 10) ndio siku ya mwisho ya kuwasilisha orodha ya mawakala wao kwa wasimamizi wa uchaguzi.

Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Bw. Ramadhan Kailima amesema hatua hiyo ni kwa mujibu wa kifungu namba 57 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (Sura ya 343) na kifungu namba 58 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa (Sura ya 292) ambazo zinabainisha kuwa majina ya mawakala  wa vyama vya siasa yanatakiwa kuwasilishwa kwa msimamizi wa uchaguzi siku saba kabla ya uchaguzi.

“Uchaguzi utafanyika tarehe 17 Februari 2018, hivyo siku saba kabla ya uchaguzi ni kesho (tarehe 10 Februari), hivyo nivisihi vyama vyote vya siasa vilivyosimamisha wagombea, kama vikitaka kuweka mawakala  kwenye uchaguzi huo, vipeleke orodha yao yaani utambulisho wa barua na kesho Jumamosi ndio siku ya mwisho.

“Ikifika tarehe 11 yaani Jumapili wasimamizi wa uchaguzi hawataruhusiwa kupokea orodha ya mawakala wa vyama vya siasa,” amesisitiza Kailima na kuongeza kuwa orodha hiyo ya mawakala kwa mujibu wa sheria iwe inaonesha jina la wakala, anuani yake na kituo ambacho chama kimependekeza wakala aende kusimamia.

Ameongeza kuwa mawakala hao wa vyama vya siasa wanatakiwa kula kiapo cha kutunza siri kwenye fomu namba 6 siku saba kabla ya uchaguzi, hivyo kesho (Jumamosi) mawakala wote wanatakiwa wale kiapo hicho na wasipofanya hivyo kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi hawataruhusiwa kuwa wakala wa vyama vya siasa katika uchaguzi huo mdogo.

Kailima amesema mawakala hao wanatakiwa wawe na barua ya utambulisho kutoka katika chama chake kwenda kwa msimamizi wa uchaguzi na pia wawe na barua ya utambulisho kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi kwenda kwa msimamizi wa kituo.

“Ili wakala akamilike lazima awe na barua kutoka kwenye chama chake, ale kiapo na awe na barua ya utambulisho kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi kwenda kwa msimamizi wa kituo, hivyo navishauri vyama vya siasa vizingatie hili,” amesema Kailima.

Pia mkurugenzi wa uchaguzi amefafanua kuwa kwa mujibu wa kifungu namba 47 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (Sura ya 343) na 49 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa (Sura ya 292), siku nane kabla ya uchaguzi Wasimamizi wa uchaguzi wanatakiwa watoe tangazo la uchaguzi, hivyo akawataka wasimamizi wa vituo kuhakikisha wanaweka matangazo hayo Februari 9, 2018.

“Tangazo hilo liwe linafafanua siku na muda wa kupiga kura, orodha ya wapiga kura na orodha ya mfano ya kupigia kura,” amesema Kailima. Ametoa wito kwa  wapiga kura waende wakaangalie jinsi majina yalivyopangwa kwenye orodha hiyo katika kila kituo ili wawezeshwe kupiga kura vizuri siku ya Jumamosi (Februari 17)

Mkurugenzi wa uchaguzi pia amevitaka vyama vya siasa viwahamize wafuasi wao waende kuangalia orodha ya majina katika vituo vyao vya kupigia kura. Pia amewataka wananchi wa kata za Kigogo, Kijitonyama na Mwananyamala ambao vituo vyao vimehamishwa waende ambako vituo vimehamishwa.

Katika Kata ya Kijitonyama vituo 6 vilivyokuwa katika shule ya Sekondari Kenton vimehamia shule ya Msingi Mapambano na vituo 5 vilivyokuwa nje ya Ofisi ya serikali ya Mtaa wa Bwawani vimehamishiwa mbele ya ofisi hiyo.

Vituo 6 vilivyokuwa nje ya soko la Makumbusho vimehamia ndani ya Ofisi ya Meneja wa Soko hilo na vituo 5 vilivyokuwa katika Ofisi ya Serikali za mitaa kijitonyama vimehamishiwa katika shule ya msingi kijitonyama.

Katika Kata ya Kigogo vituo 16 vimehamishwa ambapo vituo 5 vilivyokuwa eneo la Kiwenge kwenye Msikiti wa Shiha vimehamia Uwanja wa People na Vituo 6 vilivyokuwa kwenye Zahanati ya Kigogo vimehamishiwa katika Shule ya Kigogo na vituo 5 vilivyhokuwa katika ofisi ya serikali ya mtaa wa Mkwajuni vimehamishiwa katika shule ya Sekondari Kigogo.

Amesema Kata ya Mwananyamala ina vituo vya kupigia kura 65 na wapiga kura 27,589 na vituo nane (8) vilivyokuwa katika shule ya Sekondari Kambangwa mtaa wa msisiri A vimehamishwa. Kati ya hivyo 6 vimehamishiwa katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa ya Msolomi na 2 kuhamishiwa uwanja wa kwakopa

No comments: